Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

96. SURAT AL-A'LAQ

(Imeteremka Makka)

Katika Sura hii upo wito wa kusoma na kujifunza, na kwamba aliye weza kumuumba mtu kutokana na asli nyonge ni Mweza wa kumfunza kuandika kwa kudhibitia ilimu na kutimizia kufahamu, na amfunze aliyo kuwa hayajui. Kwani Yeye Subhanahu ndiye Mwenye kummiminia ilimu mwanaadamu. Na Sura  inanabihisha kwamba utajiri na nguvu huenda zikampelekea mtu kupindukia mipaka ya Mwenyezi Mungu, lakini marejeo ya wote ni kwa Mwenyezi Mungu mwishoni. Na mazungumzo yanamwelekea kila mwenye kusilihi kusemezwa kuwaonya hao majeuri wanao pinga kheri, kuwaonya kuwa watakuja kushikwa kwa nywele zao za utosi wakibururwa Motoni; na hawatofaliwa na wasaidizi wowote. Na Sura inakhitimisha kwa kuwataka wasikivu wende kinyume na hao wenye inda wanao kadhibisha, na wajijongeze kwa ut'iifu kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, *

2. Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, *

3. Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! *

4. Ambaye amefundisha kwa kalamu. *

5. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui. *

6. Kwani! Hakika mtu bila ya shaka huwa jeuri *

7. Akijiona katajirika. *

8. Hakika kwa Mola wako Mlezi ndio marejeo. *

9. Umemwona yule anaye mkataza *

10. Mja anapo sali? *

11. Umeona kama yeye yuko juu ya uwongofu? *

12. Au anaamrisha uchamngu? *

13. Umeona kama yeye akikanusha na anarudi nyuma? *

14. Hajui ya kwamba Mwenyezi Mungu anaona? *

15. Kwani! Kama haachi, tutamkokota kwa shungi la nywele! *

16. Shungi la uwongo, lenye makosa! *

17. Basi na awaite wenzake! *

18. Nasi tutawaita Mazabania! *

19. Hasha! Usimt'ii! Nawe sujudu na ujongee!  *  


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright © 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani