1. Ewe Muhammad! Soma unayo funuliwa kwa kufunguliwa
kwa Jina la Mola wako Mlezi ambaye ni Yeye tu peke yake ndiye Mwenye uweza
wa kuumba.
2. Amemuumba mtu kwa ukamilifu wa mwili wake na ilimu kutokana na
kipande cha damu ambacho hakina chochote cha kupelekea kujiona bora.
3. Endelea na kusoma, na Mola wako Mlezi aliye Karimu kushinda wote,
atakutukuza wala hatakudharau.
4. Yeye ndiye ambaye aliye mfunza mtu kuandika kwa kalamu, na wala
kwanza hakuwa anajua hayo.
5. Amemfunza mtu yasiyo kuwa yanampitia katika mawazo yake.
6,7. Ni hakika kweli mtu hupindukia mpaka na hupanda kiburi mbele
ya Mola wake Mlezi anapo jiona si mhitaji, katajirika.
8. Ewe Muhammad! Hakika ni kwa Mola wako Mlezi peke yake ndiyo yako
marejeo ya wote kwa kufufuliwa na kulipwa.
9,10. Je! Umemwona huyu jeuri anaye mzuia mja asisali anapo taka
kusali?
11,12. Hebu niambie khabari za jeuri huyu kama yeye yumo katika uwongofu
katika huku kuzuia kwake, au kwamba ndio anaamrisha uchamngu katika hayo
anayo amrisha!
13. Niambie khabari za huyu mwenye kukataza anapo yakadhibisha aliyo
kuja nayo Mtume, na akapuuza Imani na vitendo vyema!
14. Hivyo hajui kwamba Mwenyezi Mungu anazijua vyema hali zake, naye
atamlipa kwazo?
15. Kwa kumkemea huyu mwenye kuzuia, anaambiwa kama hakuacha hayo
anayo yafanya, basi hapana shaka tutamkokota kwa nguvu tukimshika kwa shungi
lake la nywele mpaka Motoni!
16. Hilo shungi lilio juu ya uso wake mwenye kuropokwa uwongo na
mwenye athari za ukosefu!
17. Basi yeye awaite wenziwe na watu wa baraza lake wawe ndio wasaidizi
duniani au Akhera.
18. Sisi tutawaita askari wetu wamsaidie Muhammad na walio pamoja
naye, na wapambane na huyo mwenye kukanya na wasaidizi wawasukume kwenye
Jahannamu!
19. Kumnyamazisha huyu mwenye kuzuia, wewe usimkubalie kwa hayo anayo kukataza nayo, na dumu juu ya Sala zako, na endelea na sijida zako, na jijongeze kwa Mola wako Mlezi kwa hivyo.