Sura hii imeanzia kwa kiapo cha kuashiria dalili za kudra ya Mwenyezi Mungu, na inatilia mkazo kuwa kila nafsi ina mlinzi wake na muangalizi, na inamtaka mtu ajifikirie kuumbwa kwake, na ya kwamba yeye kaumbwa na maji yenye kutoka kwa kasi, ili ipatikane hoja kwamba Mwenye kuumba hivi ni Mweza wa kumrejeza tena baada ya kufa kwake.Tena ikaapa mara ya pili kwamba Qur'ani ni kauli ya kufafanua wala si maneno ya maskhara. Na juu ya kuwa hivyo makafiri bila ya shaka wameshughulika kuikanya na kuipangia njama. Na Mwenyezi Mungu amezirudi njama zao kwa njama kali kuliko zao. Kisha Sura imekhitimisha kwa kutaka wapewe muhula makafiri.
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
1. Naapa kwa mbingu na Kinacho kuja usiku! *
2. Na nini kitakacho kujuulisha ni nini hicho Kinacho kuja usiku? *
3. Ni Nyota yenye mwanga mkali. *
4. Hapana nafsi ila inayo mwangalizi. *
5. Hebu naajitazame mwanaadamu ameumbwa kwa kitu gani? *
6. Ameumbwa kwa maji yatokayo kwa kuchupa, *
7. Yatokayo baina ya mifupa ya mgongo na mbavu. *
8. Hakika Yeye ana uweza wa kumrudisha. *
9. Siku zitakapo dhihirishwa siri. *
10. Basi hatakuwa na nguvu wala msaidizi. *
11. Naapa kwa mbingu yenye marejeo! *
12. Na kwa ardhi inayo pasuka! *
13. Hakika hii ni kauli ya kupambanua. *
14. Wala si mzaha. *
15. Hakika wao wanapanga mpango. *
16. Na Mimi napanga mpango. *
17. Basi wape muhula makafiri - wape muhula pole pole. *
Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka
Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com