1. Naapa kwa mbingu na nyota inayo tokeza usiku!
2,3. Na kitu gani kitakujuvya ukweli wa nyota hii? Ni hiyo inayotoa
mwanga wake katika giza.
4. Hapana nafsi ila inayo mlinzi wa kuiangalia na kudhibiti vitendo
vyake.
5. Basi naafikiri mtu, yeye kaumbwa kutokana na nini?
6. Ameumbwa mtu kutokana na maji yanayo toka kwa nguvu.
7. Maji haya yanatoka baina ya uti wa mgongo na mbavu za mwanamume
na mwanamke.
S'ULB ni sehemu za uti wa mgongo; na TARAAIB ni mafupa ya
vifua, yaani mbavu. Masomo ya watoto wanapo kuwa ndani ya matumbo ya mama
zao (Embryology). yamedhihirisha kuwa viini vya vyombo vya uzazi na mkojo
katika mtoto ndani ya tumbo la mama yake vinadhihiri baina ya khalaya (cells)
za mishipa itakayo kuwa mafupa ya uti wa mgongo, na baina ya khalaya zitakazo
kuwa mafupa ya kifua.
Mafigo hubakia pahala pake, na kokwa huteremka kwenye pahala pake
pa kawaida katika pumbu wakati wa kuzaliwa. Na juu ya kuteremka kokwa chini
mishipa inayo inywesha damu maisha yake yote inatokana na mishipa ya mafigo.
Hali kadhaalika mishipa ya Navo inayo peleka kuhisi na ikasaidia
kuzalisha vitu vya uhai na yaliyo khusiana na hayo kama maji yanayo toka
kwenye mshipa wa kifua wa kumi unao tokana na ubongo wa uti wa mgongo kwenye
kipingili cha kumi na kumi na moja.
Yaliyo wazi kutokana na hayo ni kwamba vyombo vya uzazi na vinavyo
lisha vyombo hivyo, na vyombo vya damu, vipo katika kiwiliwili baina ya
uti wa mgongo na mbavu.
8. Hakika Mwenyezi Mungu aliye muumba hivi hapo mwanzo, bila ya shaka
ni Muweza wa kumuumba tena baada ya kufa kwake.
9. Siku dhamiri zitapo fanyiwa mtihani, na zitengwe mbali mbali baina
ya ziliyo kuwa nzuri na ziliyo kuwa mbovu.
10. Basi hapana mtu wakati huo ataye kuwa na nguvu ya kujikinga nafsi
yake, wala hatakuwa na msaidizi wa kumnusuru.
11. Naapa kwa mbingu yenye mvua inayo rejea na kuja mara kwa mara!
12. Na ardhi inayo pasuka kwa kuchipuka mimea!
13,14. Hakika hii Qur'ani ni yenye kupambanua baina ya kweli na uwongo.
Wala haina nuksani yoyote ya mchezo au maskhara.
15. Hakika hao wanao ikadhibisha Qur'ani wanaipangia njama kutaka
kuiharibia, njama zenye kufikia ukomo!
16. Lakini Mimi nitawalipa, na nitavipambanisha hivyo vitimbi vyao
kwa vitimbi madhubuti ambavyo hawataweza kujikinga navyo.
17. Basi wangojee hao makafiri! Wape muhula wa karibu mpaka nikuamrishe amri gani kali ya kuwatendea.