Imeanzia Sura hii kwa kueleza kuwa kila kiliomo katika mbingu na katika
ardhi kinamtakasa Mwenyezi Mungu na kisio laiki na utukufu wake, na kwamba
Yeye ndiye Mwenye Ufalme na Mwenye sifa njema zote, na kwamba Yeye ni Muweza
wa kila kitu. Kisha hayo yakafuatilizwa na kutajwa baadhi ya dalili za
utimilivu wa uweza wake na ujuzi wake. Kisha Sura ikatupa macho kuwaangalia
makafiri walio kuwa kabla ya hawa, na wakawaasi Mitume wa Mola wao Mlezi,
na kwamba wao walionja matokeo maovu ya vitendo vyao. Na hayo yalikuwa
hivyo kwa sababu Mitume wao walipo kuwa wakiwajia kwa hoja, waliwakataa
na wakawapuuza! Sura tena ikaingia baada ya hayo kuvunja madai ya makafiri
kwamba wao ati hawatafufuliwa. Na ikawataka watu wamuamini Mwenyezi Mungu
na Mtume wake, na Nuru iliyo teremshwa juu yake. Na ikawahadharisha na
Siku ya Mkusanyo, siku kutapo dhihiri kupunjana kwa watu. Kwani wale walio
amini na wakatenda mema watapata kufuzu kukubwa, na walio kufuru ndio watakuwa
watu wa Motoni, na hayo ndiyo marudio maovu. Na hakika masaibu yatakuwa
kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, na hakika mwenye kumuamini Mwenyezi Mungu
ndio anauongoa moyo wake.
Sura inawataka watu wamt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Wakipuuza,
basi hakika Mtume hana juu yake ila kufikisha Ujumbe. Na inawaambia Waumini
kuwa mali yao na watoto wao ni fitna, majaribio. Basi isiwe kuyashughulikia
hayo kukawapelekea kuacha waliyo amrishwa. Kisha ikawaamrisha wamche Mwenyezi
Mungu kwa kadri wawezavyo. Na Sura ikakhitimisha kwa kuwakhusisha Waumini
watoe katika njia za kheri, na kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kushukuru,
Mpole, Mjuzi wa yaliyo fichikana na yanayo onekana. Basi atawalipa kwa
mali yao wanayo yatumia. Na kwamba Yeye ni Mwenye nguvu asiye shindika,
Mwenye hikima, hafanyi upuuzi.
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
1. Kinamtakasa Mwenyezi Mungu kila kilichomo katika mbingu na katika ardhi. Ufalme ni wake, na sifa njema ni zake. Na Yeye ni Mwenye uweza juu ya kila kitu. *
2. Yeye ndiye aliye kuumbeni. Miongoni mwenu yupo aliye kafiri, na yupo aliye Muumini. Na Mwenyezi Mungu anayaona mnayo yatenda. *
3. Ameziumba mbingu na ardhi kwa haki, na akakupeni sura, na akazifanya nzuri sura zenu. Na marudio ni kwake. *
4. Anajua viliomo katika mbingu na ardhi, na anajua mnayo yaficha na mnayo yatangaza. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa yaliomo vifuani. *
5. Kwani haikukujieni khabari ya walio kufuru kabla, wakaonja matokeo mabaya ya mambo yao? Na wao wana adhabu iliyo chungu. *
6. Hayo ni kwa kuwa walikuwa wakiwajia Mitume wao kwa hoja zilizo wazi, nao wakasema: Hivyo binaadamu ndio atuongoe? Basi wakakufuru, na wakageuka upande. Mwenyezi Mungu akawa hana haja nao. Na Mwenyezi Mungu ni Mkwasi, si mhitaji, naye ni Msifiwa. *
7. Walio kufuru wanadai kuwa hawatafufuliwa. Sema: Kwani? Naapa kwa Mola wangu Mlezi! Hapana shaka mtafufuliwa, na kisha hapana shaka mtaambiwa mliyo yatenda. Na hayo ni mepesi kwa Mwenyezi Mungu. *
8. Basi muaminini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na Nuru tuliyo iteremsha. Na Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayo yatenda. *
9. Siku atakayo kukusanyeni kwa ajili ya Siku ya Mkusanyiko; hiyo ni siku ya kupunjana. Na anaye muamini Mwenyezi Mungu na akatenda mema, atamfutia maovu yake, na atamuingiza katika Mabustani yenye kupitiwa kati yake na mito, watadumu humo milele. Huko ndiko kufuzu kukubwa. *
10. Na walio kufuru na wakakadhibisha Ishara zetu, hao ni watu wa Motoni, watadumu humo milele. Na hayo ndiyo marudio mabaya. *
11. Haufiki msiba wowote ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na mwenye kumuamini Mwenyezi Mungu huuongoa moyo wake. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu. *
12. Na mt'iini Mwenyezi Mungu, na mt'iini Mtume. Mkigeuka, basi hakika juu ya Mtume wetu ni kufikisha (Ujumbe wake) kwa uwazi tu. *
13. Mwenyezi Mungu, hapana mungu isipo kuwa Yeye. Na juu ya Mwenyezi Mungu nawategemee Waumini. *
14. Enyi mlio amini! Hakika miongoni mwa wake zenu na watoto wenu wamo maadui zenu. Basi tahadharini nao. Na mkisamehe, na mkapuuza, na mkaghufiria basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghfira, Mwenye kurehemu. *
15. Hakika mali yenu na watoto wenu ni jaribio. Na kwa Mwenyezi Mungu upo ujira mkubwa. *
16. Basi mcheni Mwenyezi Mungu kama mwezavyo, na sikieni, na t'iini, na toeni, itakuwa kheri kwa nafsi zenu. Na mwenye kuepushwa na uchoyo wa nafsi yake, basi hao ndio walio fanikiwa. *
17. Mkimkopesha Mwenyezi Mungu mkopo mzuri, atakuzidishieni mardufu, na atakusameheni. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa shukra, Mpole. *
18. Mwenye kujua siri na dhaahiri, Mwenye nguvu, Mwenye hikima. *
Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka
Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com