1. Vitu vyote viliomo katika mbingu na katika ardhi
vinamtakasa Mwenyezi Mungu na kila kisicho kuwa laiki na utukufu wake.
Yeye ndiye peke yake Mwenye ufalme ulio timia, na Mwenye sifa njema, na
ndiye Mwenye uweza ulio timia juu ya kila kitu.
2. Yeye peke yake ndiye aliye kuumbeni mlipo kuwa si chochote. Basi
kati yenu yupo anaye kanya Ungu wake, na miongoni mwenu yupo anaye sadiki.
Na Mwenyezi Mungu anayaona mnayo yatenda, na atakulipeni kwa mujibu wa
vitendo vyenu.
3. Mwenyezi Mungu ameziumba mbingu na ardhi kwa hikima isiyo na ukomo,
na akakuumbeni kwa sura, na akazifanya nzuri sura zenu, kwa kuwa amewafanya
wanaadamu ndio viumbe walio nyooka vizuri. Na kwake Yeye ndiyo marejeo
Siku ya Kiyama.
4. Yeye Mwenyezi Mungu anajua yote yaliomo katika mbingu na ardhi,
na anayajua mnayo yaficha, na mnayo yaeneza, ikiwa maneno au vitendo. Na
Mwenyezi Mungu ametimia ujuzi wake kwa mnayo dhamiria katika nyoyo zenu.
5. Zimekwisha wafikieni khabari za walio kufuru kabla yenu, na wao
wakameza ubaya wa matokeo wa mambo yao katika dunia. Na Akhera watapata
adhabu yenye machungu makali.
6. Masaibu hayo yaliyo wapata ni kwa sababu Mitume wao waliwajia
na miujiza iliyo dhaahiri, nao wakasema kwa kukanya: Ati atujie mtu kama
sisi kutuongoza? Wakakanya kuwa watafufuliwa. Wakaiacha Haki. Mwenyezi
Mungu akadhihirisha kuwa hana haja na imani yao kwa kuwaangamiza. Na Mwenyezi
Mungu ni Mwenye kutimia ukwasi wake (kujitosha kwake), si Mwenye kuwa na
haja na viumbe vyake. Ni Mwenye kustahiki kusifiwa na kuhimidiwa kwa uzuri
wa neema zake.
7. Makafiri wamedai kwa uwongo kwamba hawatafufuliwa baada ya kufa
kwao. Ewe Muhammad! Waambie: Mambo sio kama mnavyo dai nyinyi. Ninaapa
kwa Mola wangu Mlezi! Hapana shaka yoyote nyinyi mtafufuliwa baada ya kufa
kwenu, na hapana shaka yoyote kuwa mtaambiwa mliyo yatenda duniani. Kisha
mtalipwa kwayo. Na huko kufufuliwa, na kuhisabiwa, na kulipwa, ni jambo
sahali na jepesi kabisa kwa Mwenyezi Mungu.
8. Basi msadikini Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na ongokeni kwa kuifuata
Nuru tuliyo mteremshia hata akakufahamisheni kwa uwazi kuwa kufufuliwa
kunakuja bila ya shaka yoyote. Na Mwenyezi Mungu ana ujuzi wa kutumia kwa
yote yanayo tokana nanyi.
9. Siku atapo kukusanyeni katika Siku ya Mkusanyo wa walio tangulia
mwanzo na walio kuja mwisho, akulipeni kwa vitendo vyenu! Siku hiyo ndiyo
Siku ya Taghaabun, Kupunjana, kutapo dhihiri kupunjika kwa makafiri
kwa kuacha Imani, na kupunjika Waumini kwa kupuuza kuongeza ut'iifu. Na
mwenye kumuamini Mwenyezi Mungu, na akatenda mema atamwondolea maovu yake,
na atamtia katika Bustani zenye kupita kati yake mito, wakae humo milele.
Malipo hayo ndio kufuzu kukubwa.
10. Na walio ikataa Imani, na wakaikanusha miujiza yetu tuliyo wapa
Mitume wetu kuwaunga mkono, hao ndio watu wa Motoni. Watadumu humo. Na
marudio maovu ni hayo walio yarudia hao.
11. Mja hasibiwi na balaa ila kwa kudra ya Mwenyezi Mungu. Na mwenye
kumsadiki Mwenyezi Mungu basi humwongoa moyo wake kwendea katika yanayo
mpendeza. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kutimia ujuzi wake.
12. Na mt'iini Mwenyezi Mungu kwa aliyo kuamrisheni, na mt'iini Mtume
kwa Ujumbe aliyo kufikishieni kutoka kwa Mola wake Mlezi. Mkiupuuza ut'iifu
huu, basi Yeye hadhuriki kitu kwa mapuuza yenu. Na hakika Mtume wetu hana
jukumu juu yake ila kufikisha Utume wake tu kwa uwazi.
13. Mwenyezi Mungu, hapana wa kuabudiwa kwa haki isipo kuwa Yeye
tu peke yake. Basi Waumini nawamtegemee Yeye tu katika mambo yao yote.
14. Enyi mlio amini! Hakika miongoni mwa wake zenu na watoto wenu
wamo maadui zenu, ambao wanakuzuilieni msimt'ii Mwenyezi Mungu kwa kutaka
kuwatimizia hao matakwa yao. Basi kuweni na hadhari nao. Na mkiweza
kuyavuka makosa yao yanayo kubalika kusameheka, na mkayapuuza, na mkawafichia,
basi Mwenyezi Mungu naye atakughufirieni nyinyi. Kwani hakika Mwenyezi
Mungu ni Mkunjufu wa maghfira na rehema.
15. Hakika mali yenu na watoto wenu ni majaribio na mtihani. Na kwa
Mwenyezi Mungu upo ujira mkubwa kwa anaye pendelea kumt'ii Mwenyezi Mungu.
16. Basi tumieni juhudi zenu na nguvu zenu katika kumcha Mwenyezi
Mungu. Na sikieni mawaidha yake, na t'iini amri zake, na toeni katika alicho
kuruzukuni kwa ajili ya hicho alicho amrisha kitolewe kwa ajili yake. Na
tendeni kheri kwa sababu ya nafsi zenu. Na mwenye kuzuiliwa na Mwenyezi
Mungu ubakhili na uchoyo wa roho yake, basi watu kama hao ndio walio jaaliwa
kupata kila kheri.
17. Mkitoa katika mambo ya kheri kutoa kwa moyo safi, basi Mwenyezi
Mungu atazidisha mardufu thawabu za mlicho toa, na atakusameheni madhambi
yenu yaliyo kuponyokeni. Na Mwenyezi Mungu ni Mkuu wa shukrani, na kuwalipa
watendao mema, na ni Mpole, hafanyi haraka kuwaadhibu wanao muasi.
18. Yeye ni Mjuzi wa vilivyo fichikana na vinavyo onekana, Mwenye nguvu, Mtenda nguvu, Mwenye hikima katika mipango ya viumbe vyake, Mwenye kuweka kila kitu kwa pahala pake.