Imefunguka Sura hii kwa kutoa khabari yake Mtukufu kwamba viliomo katika
mbingu na ardhi vyote vinamsabihi Yeye. Na Mwenyezi Mungu aliye tukuka
shani yake amesema kwamba ameineemesha kaumu isio jua kuandika wala kusoma
kwa kuwaletea Mtume miongoni mwao, ambaye anawafundisha Kitabu, na hikima,
na anawatakasa. Na hakika hii ni fadhila ya Mwenyezi Mungu humpa amtakaye.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu amewakemea Mayahudi kwa kuacha kwao kutenda
yaliyo amrishwa katika Taurati, na hali wao wanajua yaliomo humo. Na amepinga
madai yao kwamba wao peke yao ndio vipenzi vya Mwenyezi Mungu, si watu
wenginewe. Na amebariziana nao kwa kuwataka watamani kufa ikiwa wao wanasema
kweli! Na Sura imekhitimisha kwa kuwaamrisha Waumini wakimbilie kwenda
sali Sala ya Ijumaa pindi wakisikia adhana, na waache biashara. Na Sala
ikisha malizika watawanyike katika nchi wende kutafuta fadhila za Mwenyezi
Mungu. Na kawakataza wasiache biashara au jambo la pumbao lolote kuwashughulisha
wasiisikilize khutba ya Ijumaa. Na Mwenyezi Mungu amewadhamini kuwaruzuku,
na Yeye ndiye mbora wa kuruzuku.
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
1. Viliomo mbinguni na viliomo katika ardhi vinamtakasa Mwenyezi Mungu, Mfalme, Mtakatifu, Mwenye nguvu, Mwenye hikima. *
2. Yeye ndiye aliye mpeleka Mtume kwenye watu wasio jua kusoma, awasomee Aya zake na awatakase, na awafunze Kitabu na hikima, ijapo kuwa kabla ya haya walikuwa katika upotofu ulio dhaahiri. *
3. Na kwa wengine ambao bado hawajaungana nao. Na Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hikima. *
4. Hiyo ni fadhila ya Mwenyezi Mungu anayo mpa amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila kubwa. *
5. Mfano wa walio bebeshwa Taurati kisha wasiibebe, ni mfano wa punda anaye beba vitabu vikubwa vikubwa. Mfano muovu mno wa watu walio kadhibisha Ishara za Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu madhaalimu. *
6. Sema: Enyi mlio Mayahudi! Ikiwa nyinyi mnadai kuwa ni vipenzi vya Mwenyezi Mungu pasipo kuwa watu wengine, basi yatamanini mauti, ikiwa mnasema kweli. *
7. Wala hawatayatamani kabisa, kwa sababu ya iliyo kwisha yatanguliza mikono yao. Na Mwenyezi Mungu anawajua walio dhulumu. *
8. Sema: Hayo mauti mnayo yakimbia, bila ya shaka yatakukuteni. Kisha mtarudishwa kwa Mwenye kuyajua yaliyo fichikana na yanayo onekana. Hapo atakwambieni mliyo kuwa mkiyatenda. *
9. Enyi mlio amini! Ikiadhiniwa Sala siku ya Ijumaa, nendeni upesi kwenye dhikri ya Mwenyezi Mungu, na wacheni biashara. Hayo ni bora kwenu, lau kama mnajua. *
10. Na itakapo kwisha Sala, tawanyikeni katika nchi mtafute fadhila za Mwenyezi Mungu, na mkumbukeni Mwenyezi Mungu kwa wingi ili mpate kufanikiwa. *
11. Na wanapo iona biashara au pumbao wanayakimbilia hayo na wakakuacha umesimama. Sema: Yaliyoko kwa Mwenyezi Mungu ni bora kuliko pumbao na biashara. Na Mwenyezi Mungu ni Mbora wa watoa riziki. *
Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka
Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com