1. Vitu vyote viliomo katika mbingu na viliomo katika
ardhi vinamsabihi na kumtakasa Mwenyezi Mungu na kila kisicho kuwa
laiki, Yeye ndiye Mfalme wa kila kitu, Mwenye kuendesha atakavyo bila ya
mpinzani, Mwenye kutakasika kwa ukamilifu na kila cha upungufu, Mwenye
kushinda kila kitu, Mwenye hikima ya kufika mwisho.
2. Mwenyezi Mungu ndiye aliye mtuma Mtume kwa watu wasio jua kuandika,
naye ni katika wao wenyewe, anawasomea Aya zake Mwenyezi Mungu, na anawasafisha
na mambo machafu ya itikadi na tabia, na anawafundisha Qur'ani na kuijua
Dini. Na wao kabla ya kuletwa yeye walikuwa wamepotoka kabisa kuiacha haki.
3. Na pia Mwenyezi Mungu amempeleka Muhammad kwa watu wenginewe,
ambao hawajaja bado, lakini watakuja. Na Mwenyezi Mungu peke yake ndiye
Mwenye kushinda kila kitu, Mwenye hikima ya kufikia ukomo katika vitendo
vyake.
4. Kuletwa Mtume huko ni fadhila inayo toka kwa Mwenyezi Mungu. Anamkirimu
kwayo aliye mkhitari katika waja wake. Na Mwenyezi Mungu peke yake, ndiye
Mwenye fadhila kubwa.
5. Mfano wa Mayahudi walio funzwa Taurati, na wakalazimishwa waifuate,
na wao hawakuifuata kwa vitendo, ni mfano wa punda aliye beba vitabu ambavyo
hajui ndani yake mna nini. Ni mbaya mno mfano wa watu wanao kadhibisha
Ishara za Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu hawasaidii kufikilia uwongofu
watu ambao kazi yao ni kudhulumu.
6. Ewe Muhammad! Sema: Enyi nyinyi mlio Mayahudi! Kama mnadai kwa
uwongo kwamba nyinyi peke yenu ati ndio vipenzi vya Mwenyezi Mungu, basi
takeni mauti kwa Mwenyezi Mungu, ikiwa nyinyi mnasema kweli katika hayo
madai ya kwamba Mwenyezi Mungu anakupendeni.
7. Mwenyezi Mungu anasema: Wala Mayahudi hawatamani mauti milele
kwa sababu ya ukafiri na vitendo viovu walio kwisha vitenda. Na Mwenyezi
Mungu anawajua vyema walio dhulumu.
8. Sema: Hayo mauti mnayo yakimbia hamwezi kuyakimbia, bila ya shaka
yatakukuteni tu. Kisha mtarudishwa kwa Mwenye kujua ya siri na ya dhaahiri.
Na Yeye atakwambieni mliyo kuwa mkiyatenda.
9. Enyi mlio amini! Ikiadhiniwa Sala siku ya Ijumaa, basi nendeni
kwa hima na hamu kumkumbuka na kumtaja Mwenyezi Mungu, na wacheni biashara.
Hayo mliyo amrishwa yana nafuu zaidi kwenu nyinyi, ikiwa mnajua.
10. Mkisha maliza kusali basi tawanyikeni katika nchi kwa ajili ya
maslaha yenu, na mtake fadhila za Mwenyezi Mungu. Na mkumbukeni Mwenyezi
Mungu kwa nyoyo zenu na ndimi zenu kwa wingi, ili asaa mkafuzu katika kheri
za duniani na Akhera.
11. Na wakiona bidhaa za biashara, au pumbao lolote hutawanyika kuendea hayo, na wakakuacha wewe umesimama unakhutubu! Waambie: Fadhila na thawabu zilioko kwa Mwenyezi Mungu zina nafuu zaidi kwenu kuliko pumbao na kuliko biashara. Na Mwenyezi Mungu ni Mbora wa wanao toa riziki. Basi itafuteni riziki yake kwa kumt'ii Yeye.