Imeanzia Sura hii kwa harufi mbili za alifbete, na ikafuatia kwa kuitaja
Qur'ani na kueleza cheo chake kwa Mwenyezi Mungu. Kisha Sura ikaingia kubainisha
msimamo wa wale wanao zifanyia maskhara Risala za Mitume wao, na ikazileta
dalili nyingi za kuthibitisha Imani ya Mwenyezi Mungu pekee. Na juu ya
hoja hizo wao wakamzulia Mwenyezi Mungu kuwa ana washirika, na wakamfanya
kuwa ana watoto wa kike, na wao wanao wa kiume. Na walipo ishiwa na hoja
wakashikilia mila za baba zao.
Kisha Sura ikasimulia kisa cha Ibrahim, na ikafuatiliza kule kuyaona
makuu makafiri wa Makka ya kwamba Qur'ani iliteremka juu ya Muhammad, wala
isiteremke juu ya mmoja katika wakuu wa miji yao miwili. Hayo ni kama kwamba
wao ndio wanao zigawanya fadhila za Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu alikwisha
wagawia maisha yao ya duniani, kwa kuwa wao wenyewe wameshindwa hayo. Kisha
Sura ikathibitisha kwamba lau kuwa si kuchukia wasije watu wote wakakufuru
basi bila ya shaka angeli mpa kafiri starehe na mapambo na uzuri wote wa
duniani. Kadhaalika Sura imebainisha kwamba mwenye kupuuza Haki Mwenyezi
Mungu humsalitisha na Shet'ani amwongoze kwenye maangamio. Kisha Sura inasimulia
kisa cha Musa na Firauni, na alivyo ghurika Firauni na ufalme wake, na
yaliyo mteremkia Firauni na kaumu yake ya mateso ya Mwenyezi Mungu. Na
hayo akafuatiwa kutajwa Bin Maryamu, na kwamba yeye ni mja aliye
neemeshwa na Mwenyezi Mungu, na akawaita watu wende kwenye Njia Iliyo Nyooka.
Na baada ya kuonya kwa adhabu ya Siku ya Kiyama itayo wapata walio
dhulumu, na kubashiriwa Waumini kuwa watapata Pepo ambayo ndani yake macho
yao yatatua, Sura inakhitimisha kueleza kuwa Ufalme wa Mwenyezi Mungu umeenea
kote, na hao walio washirikisha naye hawanalo wawezalo. Basi, ewe Muhammad!
Wapuuzilie mbali, na useme: Salamu! Watakuja jua!
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA
REHEMA MWENYE KUREHEMU
1. H'a Mim *
2. Naapa kwa Kitabu kinacho bainisha. *
3. Hakika Sisi tumeifanya Qur'ani kwa Kiarabu ili mfahamu. *
4. Na hakika hiyo imo katika Asili ya Maandiko yalioko kwetu, ni tukufu na yenye hikima. *
5. Je! Tuache kukukumbusheni kabisa kwa kuwa nyinyi ni watu mlio pita mipaka kwa ukafiri? *
6. Na Manabii wangapi tuliwatuma kwa watu wa zamani! *
7. Na hawajii Nabii yeyote ila walikuwa wakimkejeli. *
8. Na tuliwaangamiza walio kuwa na nguvu kushinda wao. Na mfano wa watu wa zamani umekwisha pita. *
9. Na ukiwauliza: Nani aliye ziumba mbingu na ardhi? Bila ya shaka watasema: Kaziumba Mwenye nguvu, Mjuzi, *
10. Ambaye amekufanyieni ardhi kama tandiko, na akakufanyieni ndani yake njia mpate kuongoka. *
11. Na ambaye ndiye aliye teremsha kutoka mbinguni maji kwa kiasi, na kwa hayo tukaifufua nchi iliyo kufa. Na namna hivi ndivyo mtakavyo tolewa. *
12. Na ambaye ndiye aliye umba katika kila kitu jike na dume, na akakufanyieni marikebu na wanyama mnao wapanda. *
13. Ili mkae vizuri migongoni mwao, kisha mkumbuke neema za Mola wenu Mlezi mnapokaa sawa sawa juu yao na mseme: Ametakasika aliye mfanya huyu atutumikie, na tusingeli weza kufanya haya wenyewe. *
14. Na hakika sisi tutarudi kwa Mola wetu Mlezi. *
15. Na wanamfanyia katika waja wake fungu. Kwa hakika mwanaadamu ni mtovu wa fadhila aliye dhaahiri. *
16. Au amejichukulia watoto wanawake katika vile alivyo viumba, na akakuteulieni nyinyi watoto wanaume? *
17. Na anapo bashiriwa mmoja wao kwa yale aliyo mpigia mfano Mwenyezi Mungu, uso wake husawijika na hujaa hasira. *
18. Ati aliye lelewa katika mapambo, na katika mabishano hawezi kusema kwa bayana...? *
19. Na wakawafanya Malaika, ambao ni waja wa Mwingi wa Rehema, ni wanawake! Kwani wameshuhudia kuumbwa kwao? Ushahidi wao utaandikwa na wao watahojiwa! *
20. Nao husema: Angeli penda Mwingi wa Rehema tusingeli waabudu sisi. Hawana ujuzi wowote wa hayo! Hawana ila kusema uwongo tu! *
21. Kwani tuliwapa Kitabu kabla ya hichi, na ikawa wao wanakishikilia hicho? *
22. Bali wanasema: Hakika sisi tuliwakuta baba zetu wanashika dini makhsusi, basi na sisi tunaongoza nyayo zao. *
23. Na kadhaalika hatukumtuma mwonyaji kwenye mji wowote ila watu wake walio deka kwa starehe walisema: Hakika sisi tuliwakuta baba zetu wanashika dini makhsusi, na sisi tunafuata nyayo zao. *
24. Akasema (Mwonyaji): Hata nikikuleteeni yenye uwongofu bora kuliko mlio wakuta nao baba zenu? Wakasema: Sisi tunayakataa tu hayo mliyo tumwa. *
25. Basi tukawalipizia. Angalia ulikuwaje mwisho wa walio kadhibisha! *
26. Na pale Ibrahim alipo mwambia baba yake na kaumu yake: Hakika mimi ninajitenga mbali na hayo mnayo yaabudu, *
27. Isipo kuwa yule aliye niumba, kwani Yeye ataniongoa. *
28. Na akalifanya hili liwe neno lenye kubaki katika vizazi vyake ili warejee. *
29. Bali tuliwastarehesha hawa na baba zao mpaka ikawafikia Haki na Mtume aliye bainisha. *
30. Na ilipo wafikia Haki wakasema: Huu ni uchawi, na sisi hakika tunaukataa. *
31. Na walisema: Kwa nini Qur'ani hii haikuteremshwa kwa mtu mkubwa katika miji miwili hii? *
32. Kwani wao ndio wanao gawa rehema za Mola wako Mlezi? Sisi tumewagawanyia baina yao maisha yao katika uhai wa duniani, na tukawanyanyua baadhi yao juu ya wengine kwa daraja nyingi; kwa hivyo baadhi yao wanawafanya wenginewe wawatumikie. Na rehema za Mwenyezi Mungu ni bora kuliko hayo wanayo yakusanya. *
33. Na lau isinge kuwa watu watakuwa kundi moja tungeli wajaalia wanao mkufuru Rahmani wana nyumba zao zina dari ya fedha, na ngazi zao pia wanazo pandia, *
34. Na milango ya nyumba zao na vitanda wanavyo egemea juu yake, *
35. Na mapambo. Lakini hayo si chochote ila ni starehe ya maisha ya dunia tu, na Akhera iliyoko kwa Mola wako Mlezi ni ya wenye kumchamngu. *
36. Anaye yafanyia upofu maneno ya Rahmani tunamwekea Shet'ani kuwa ndiye rafiki yake. *
37. Na hakika wao wanawazuilia Njia na wenyewe wanadhani kuwa wameongoka. *
38. Hata atakapo tujia atasema: Laiti ungeli kuwako baina yangu na wewe kama umbali baina ya mashariki na magharibi. Rafiki mwovu mno wewe! *
39. Na kwa kuwa mlidhulumu, haitakufaeni kitu leo kwamba nyinyi mnashirikiana katika adhabu. *
40. Je! Unaweza kuwasikilizisha viziwi, au unaweza kuwaongoa vipofu na waliomo katika upotofu ulio wazi? *
41. Na hata tukikuondoa, Sisi tutalipiza kisasi chetu kwao. *
42. Au tutakuonyesha tulio waahidi. Nasi bila ya shaka tuna uweza juu yao. *
43. Basi wewe yashike yaliyo funuliwa kwako. Hakika wewe uko kwenye Njia Iliyo Nyooka. *
44. Na hakika haya ni ukumbusho kwako na kwa kaumu yako. Na mtakuja ulizwa. *
45. Na waulize Mitume wetu tulio watuma kabla yako: Je! Tulifanya miungu mingine iabudiwe badala ya Rah'mani? *
46, Na bila ya shaka tulimtuma Musa kwa Ishara zetu ende kwa Firauni na waheshimiwa wake, na akasema: Hakika mimi ni Mtume wa Mola Mlezi wa walimwengu wote! *
47. Lakini alipo wajia na Ishara zetu wakaingia kuzicheka. *
48. Na hatukuwaonyesha Ishara yoyote ila hiyo ilikuwa kubwa zaidi kuliko nyenginewe. Na tukawakamata kwa adhabu ili warejee. *
49. Na wakasema: Ewe mchawi! Tuombee kwa Mola wako Mlezi kwa ile ahadi aliyo kuahidi; hakika sisi tutakuwa wenye kuongoka. *
50. Basi tulipo waondolea adhabu hiyo, mara wakaingia kuvunja ahadi. *
51. Na Firauni alitangaza kwa watu wake, akisema: Enyi watu wangu! Kwani mimi sinao huu ufalme wa Misri, na hii mito inapita chini yangu? Je! Hamwoni? *
52. Au mimi si bora kuliko huyu aliye mnyonge, wala hawezi kusema waziwazi? *
53. Basi mbona hakuvikwa vikuku vya dhahabu, au hawakuja Malaika pamoja naye wakamwandama? *
54. Basi aliwachezea watu wake, na wakamt'ii. Kwa hakika hao walikuwa watu wapotovu. *
55. Walipo tukasirisha tuliwapatiliza tukawazamisha wote! *
56. Kisha tukawafanya kuwa watangulizi na mfano kwa wa baadaye. *
57. Na alipo pigiwa mfano Mwana wa Mariamu, watu wako waliupiga ukelele. *
58. Wakasema: Miungu yetu kwani si bora kuliko huyu? Hawakukupigia mfano huo ila kwa ubishi tu. Bali hao ni watu wagomvi! *
59. Hakuwa yeye (Isa) ila ni Mtumwa tuliye mneemesha na tukamfanya ni mfano kwa Wana wa Israili. *
60. Na tungeli penda tungeli wafanyia miongoni mwenu Malaika katika ardhi wakifuatana. *
61. Na kwa hakika yeye ni alama ya Saa ya Kiyama. Basi usiitilie shaka, na nifuateni. Hii ndiyo Njia Iliyo Nyooka. *
62. Wala asikuzuilieni Shet'ani. Hakika yeye ni adui yenu wa dhaahiri. *
63. Na alipo kuja Isa na dalili zilizo wazi, alisema: Nimekujieni na hikima, na ili nikuelezeni baadhi ya yale mliyo khitalifiana. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na mnit'ii mimi. *
64. Kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mola wangu Mlezi, na ni Mola wenu Mlezi. Basi Muabuduni Yeye tu. Hii ndiyo Njia Iliyo Nyooka. *
65. Lakini makundi kwa makundi yao yalikhitalifiana wao kwa wao. Ole wao walio dhulumu kwa adhabu ya siku chungu. *
66. Je! Nini wanangojea ila Saa iwajie kwa ghafla na wala wao hawatambui? *
67. Siku hiyo marafiki watakuwa ni maadui, wao kwa wao, isipo kuwa wachamngu. *
68. Enyi waja wangu! Hamtakuwa na khofu siku hiyo, wala hamtahuzunika. *
69. Ambao waliziamini Ishara zangu na walikuwa Waislamu. *
70. Ingieni Peponi, nyinyi na wake zenu; mtafurahishwa humo. *
71. Watakuwa wanapitishiwa sahani za dhahabu na vikombe; na vitakuwamo ambavyo nafsi zinavipenda na macho yanavifurahia, na nyinyi mtakaa humo milele. *
72. Na hiyo ni Pepo mliyo rithishwa kwa hayo mliyo kuwa mkiyafanya. *
73. Mnayo humo matunda mengi mtakayo yala. *
74. Kwa hakika wakosefu watakaa katika adhabu ya Jahannamu. *
75. Hawatapumzishwa nayo na humo watakata tamaa. *
76. Wala Sisi hatukuwadhulumu, bali wao ndio walio kuwa madhaalimu. *
77. Nao watapiga kelele waseme: Ewe Malik! Na atufishe Mola wako Mlezi! Naye aseme: Hakika nyinyi mtakaa humo humo! *
78. Kwa yakini tulikuleteeni Haki, lakini wengi katika nyinyi mlikuwa mnaichukia Haki. *
79. Au waliweza kupitisha amri yao? Bali ni Sisi ndio tunao pitisha. *
80. Au wanadhani kwamba hatusikii siri zao na minong'ono yao? Wapi! Na wajumbe wetu wapo karibu nao, wanayaandika. *
81. Sema: Ingeli kuwa Rahmani ana mwana, basi mimi ningeli kuwa wa kwanza kumuabudu. *
82. Ametakasika Mola Mlezi wa mbingu na ardhi, Mola Mlezi wa A'rshi, na hayo wanayo msifia. *
83. Basi waache wapige porojo wakicheza mpaka wakutwe na hiyo siku yao waliyo ahidiwa. *
84. Na Yeye ndiye Mungu mbinguni, na ndiye Mungu katika ardhi. Naye ndiye Mwenye hikima, Mwenye ujuzi. *
85. Na ametukuka Mwenye ufalme wa mbingu na ardhi na viliomo ndani yake. Na uko kwake ujuzi wa Saa ya Kiyama, na kwake Yeye mtarudishwa. *
86. Wala hao mnao waomba badala yake Yeye hawana uweza wa kumwombea mtu, isipo kuwa anaye shuhudia kwa haki, na wao wanajua. *
87. Na ukiwauliza ni nani aliye waumba? Bila ya shaka watasema: Mwenyezi Mungu! Basi ni wapi wanako geuziwa? *
88. Na usemi wake (Mtume) ni: Ewe Mola wangu Mlezi! Hakika hawa ni watu wasio amini. *
89. Basi wasamehe, na uwambie maneno ya salama. Watakuja jua. *
Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka
Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com