Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

89. SURAT AL-FAJR

(Imeteremka Makka)

Imeanza Sura hii kwa viapo vya mambo yanayo onekana namna mbali mbali, yanayo pelekea kuangalia athari ya kudra kwamba wanao mkanya Mwenyezi Mungu na kukanya kufufuliwa watakuja adhibiwa, kama walivyo kwisha adhibiwa walio kadhibisha kabla yao. Na Sura ikaingia kuthibitisha mwendo wa Mwenyezi Mungu wa kuwajaribu waja wake kwa kheri na shari, na kwamba kupa kwake na kunyima kwake sio dalili ya kuridhika kwake au kukasirika kwake. Tena mazungumzo yakawaelekea wanao semezwa ya kwamba hali zao zinafichua wingi wa pupa yao na choyo chao. Kisha inakhitimisha kwa kuashiria majuto ya wanao pindukia kiasi na kutamani kwao kwamba laiti wangeli tanguliza mema ya kuwaokoa na hayo wanayo teseka nayo ya vitisho vya Siku ya Kiyama, na yanayo kuwa ya kuiliwaza nafsi iliyo tua iliyo tanguliza mema wala isikiuke mipaka, na itavyo itwa iingie pamoja na walio kirimiwa miongoni mwa waja wa Mwenyezi Mungu katika Pepo ya Mwenyezi Mungu.

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Naapa kwa alfajiri, *

2. Na kwa masiku kumi, *

3. Na kwa viwili viwili na kimoja kimoja, *

4. Na kwa usiku unapo pita, *

5. Je! Hapana katika haya kiapo kwa mwenye akili? *

6. Kwani hukuona jinsi Mola wako Mlezi alivyo wafanya kina A'di? *

7. Wa Iram, wenye majumba marefu? *

8. Ambao haukuumbwa mfano wake katika nchi? *

9. Na Thamudi walio chonga majabali huko bondeni? *

10. Na Firauni mwenye vigingi? *

11. Ambao walifanya jeuri katika nchi? *

12. Wakakithirisha humo ufisadi? *

13. Basi Mola wako Mlezi aliwapiga mjeledi wa adhabu. *

14. Hakika Mola wako Mlezi yupo kwenye mavizio anawavizia. *

15. Ama mtu anapo jaribiwa na Mola wake Mlezi, akamkirimu na akamneemesha, husema: Mola wangu Mlezi amenikirimu! *

16. Na ama anapo mjaribu akampunguzia riziki yake, husema: Mola wangu Mlezi amenitia unyonge! *

17. Sivyo hivyo! Bali nyinyi hamuwakirimu mayatima, *

18. Wala hamhimizani kulisha masikini; *

19. Na mnakula urithi kwa ulaji wa pupa, *

20. Na mnapenda mali pendo la kupita kiasi. *

21. Sivyo hivyo! Itakapo vunjwa ardhi vipande vipande, *

22. Na akaja Mola wako Mlezi na Malaika safu safu, *

23. Na ikaletwa Jahannamu siku hiyo, siku hiyo mtu atakumbuka! Lakini kukumbuka huko kutamfaa nini? *

24. Atasema: Laiti ningeli jitangulizia kwa uhai wangu! *

25. Basi siku hiyo hataadhibu yeyote namna ya kuadhibu kwake. *

26. Wala hatafunga yeyote kama kufunga kwake. *

27. Ewe nafsi iliyo tua! *

28. Rejea kwa Mola wako Mlezi umeridhika, na umemridhisha. *

29. Basi ingia miongoni mwa waja wangu, *

30. Na ingia katika Pepo yangu.  *  


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright © 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani
1