Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

83. SURAT AL-MUT'AFFIFIIN

(Imeteremka Makka)

Imeanzia Sura hii kwa onyo kali kwa huyo anaye jipimia mwenyewe sawa na akampimia mtu mwingine kwa upungufu; na ikaeleza hayo kwa wayatendayo watu katika kutaka watimiziwe haki zao katika vipimo na mizani, na ikaonya mtindo kama huo kwa kuwa ipo Siku ya Hisabu, na ikathibitisha kuwa vitendo vyao vimedhibitiwa katika daftari la hisabu, ambalo halimkadhibishi ila mwenye kupindukia mipaka, mwenye dhambi aliye zuiliwa na rehema za Mola wake Mlezi, na mwisho wake ni Jahannamu.
Tena Aya zikawageukia watu wema, zikawatuza nyoyo kwa vitendo vyao, na zikataja neema zao na alama zao, zikiashiria namna moja wapo katika neema hizo, na kwa ajili ya hizo washindanie wanao shindana. Na Aya zikaeleza walio kuwa wakiyafanya makafiri wakosefu kuwafanyia Waumini wanapo waona, au wanapo kuwa Waumini wanapita mbele yao. Na Sura ikakhitimisha kwa kuwatuliza Waumini kwamba Siku ya Kiyama itawafanyia insafu, wao watakuwa katika neema wakiwacheka makafiri, nao wamekaa juu ya makochi wakiwaangalia, na makafiri watalipwa kwa waliyo kuwa wakiyatenda.

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Ole wao hao wapunjao! *

2. Ambao wanapo jipimia kwa watu hudai watimiziwe. *

3. Na wao wanapo wapimia watu kwa kipimo au mizani hupunguza. *

4. Kwani hawadhani hao kwamba watafufuliwa *

5. Katika Siku iliyo kuu, *

6. Siku watapo msimamia watu Mola Mlezi wa walimwengu wote? *

7. Hasha! Hakika maandiko ya wakosefu bila ya shaka yamo katika Sijjin. *

8. Unajua nini Sijjin? *

9. Kitabu kilicho andikwa. *

10. Ole wao siku hiyo kwa wanao kadhibisha! *

11. Ambao wanaikadhibisha Siku ya Malipo. *

12. Wala haikadhibishi ila kila mwenye kuruka mipaka, mwenye dhambi. *

13. Anapo somewa Aya zetu husema: Ni visa vya watu wa kale! *

14. Hasha! Bali yametia kutu juu ya nyoyo zao hao walio kuwa wakiyachuma. *

15. Hasha! Hakika hao siku hiyo bila ya shaka watazuiliwa na neema za Mola wao Mlezi. *

16. Kisha wataingia Motoni! *

17. Kisha waambiwe: Haya ndiyo mliyo kuwa mkiyakadhabisha. *

18. Hasha! Hakika maandiko ya watu wema bila ya shaka yamo katika I'liyyin. *

19. Na nini kitakacho kujuvya nini I'liyyin? *

20. Kitabu kilicho andikwa. *

21. Wanakishuhudia walio karibishwa. *

22. Hakika watu wema bila ya shaka watakuwa katika neema. *

23. Wakae juu ya viti vya enzi wakiangalia. *

24. Utatambua katika nyuso zao mng'aro wa neema, *

25. Watanyweshwa kinywaji safi kiliyo tiwa muhuri, *

26. Muhuri wake ni miski. Na katika hayo washindanie wenye kushindana. *

27. Na mchanganyiko wake ni Tasniim, *

28. Chemchem watakayo inywa walio kurubishwa. *

29. Kwa hakika wale walio kuwa wakosefu walikuwa wakiwacheka walio amini. *

30. Na wanapo pita karibu yao wakikonyezana. *

31. Na wanapo rudi kwa watu wao hurudi nao wamefurahi. *

32. Na wanapo waona husema: Hakika hawa ndio khasa walio potea. *

33. Na wao hawakutumwa wawe walinzi juu yao. *

34. Basi leo walio amini ndio watawacheka makafiri, *

35. Nao wako juu ya viti vya enzi wakiangalia. *

36. Je! makafiri wamelipwa malipo ya yale waliyo kuwa wakiyatenda?  *  


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright © 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani