Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

101. AL-QAARIA'H

(Imeteremka Makka)

Sura hii inaanza  kwa kitisho cha hiyo AL-QAARIA'H, yaani Inayo gonga, sauti inayo gonga katika masikio ya watu, yaani ndio Kiyama. Na Sura imetaja baadhi ya hali za hiyo sauti inayo gonga khasa kwa mintarafu ya watu na milima. Na ikashughulikia kusimulia hao ambao mizani yao itakuwa nzito kwa kuzidi mema yao, na mizani yao itayo kuwa duni kwa kuzidi maovu yao (na kupunguka mema yao).

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Inayo gonga! *

2. Nini Inayo gonga? *

3. Na nini kitacho kujuilisha nini Inayo gonga? *

4. Siku ambayo watu watakuwa kama nondo walio tawanyika; *

5. Na milima itakuwa kama sufi zilizo chambuliwa! *

6. Basi yule ambaye mizani yake itakuwa nzito, *

7. Huyo atakuwa katika maisha ya kupendeza. *

8. Na yule ambaye mizani yake itakuwa khafifu, *

9. Huyo maskani yake yatakuwa Moto wa Hawiya! *

10. Na nini kitacho kujuilisha nini hiyo? *

11. Ni Moto mkali!  *  


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright © 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani