Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

92. SURAT AL-LAYL

(Imeteremka Makka)

Mwenyezi Mungu Mtukufu ameapa kwa viapo vitatu juu ya kuwa vitendo vya watu vinakhitalifiana, baadhi yake ni vya uwongofu, na baadhi yake ni vya upotofu. Mwenye kutoa, na akamchamngu, na akawafiki tabia yenye kukusanya kheri, basi Mwenyezi Mungu atamsahilishia mambo yake kwa wepesi. Na mwenye kufanya ubakhili, na akajiona hana haja na mtu, na akakanusha tabia zenye kukusanya kheri Mwenyezi Mungu atamfanyia wepesi kuingia mashakani.  Na wala mali yake hayatamfaa kitu kumwokoa akitumbukia katika adhabu! Na Aya zikabainisha baada ya hayo kwamba hakika Mwenyezi Mungu amechukua jukumu kubainisha njia za uwongofu kwa fadhila zake, na kwake yapo mambo ya maisha mawili, ya Akhera na ya duniani. Na kwamba hakika Yeye amekwisha onya kwamba Moto watauingia waovu na watauepuka walio wema.

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Naapa kwa usiku unapo funika! *

2. Na mchana unapo dhihiri! *

3. Na kwa Aliye umba dume na jike! *

4. Hakika juhudi zenu bila ya shaka ni mbali mbali. *

5. Ama mwenye kutoa na akamchamngu, *

6. Na akaliwafiki lilio jema, *

7. Tutamsahilishia yawe mepesi. *

8. Na ama mwenye kufanya ubakhili, na asiwe na haja ya wenzake, *

9. Na akakanusha lilio jema, *

10. Tutamsahilishia yawe mazito! *

11. Na mali yake yatamfaa nini atapo kuwa anadidimia? *

12. Hakika ni juu yetu kuonyesha uwongofu. *

13. Na hakika ni yetu Sisi Akhera na dunia. *

14. Basi nakuonyeni na Moto unao waka! *

15. Hatauingia ila mwovu kabisa! *

16. Anaye kadhibisha na kupa mgongo. *

17. Na mchamngu ataepushwa nao, *

18. Ambaye hutoa mali yake kwa ajili ya kujitakasa. *

19. Na wala si kwa kuwa yupo yeyote aliye mfanyia hisani ndio anamlipa. *

20. Ila ni kutaka radhi ya Mola wake Mlezi aliye juu kabisa. *

21. Naye atakuja ridhika!  *  


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright © 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani