Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

90. SURAT AL-BALAD

(Imeteremka Makka)

Mwenyezi Mungu anaapa kwa mji mtakatifu wa Makka, mji wa kuzaliwa Muhammad s.a.w. na ndipo alipo kulia na akapapenda, na pia anaapa kwa mzazi na anacho kizaa, kwani kwa hao ndio jinsi inahifadhika na maamrisho yanabakia, na ya kwamba mtu ameumbwa kwa mashaka na shida na taabu. Tena anabainisha kwamba mtu anadanganyika kwa kudhani kuwa uweza wake haushindiki, na kwamba yeye ana mali mengi anayo yatumia kuridhisha matamanio yake na pumbao lake. Kisha Subhanahu akazitaja neema alizo mneemesha mwanaadamu na kumsahilishia njia za uwongofu na za kupitia milimani, ili awe katika watu wa Peponi, watu wa mkono wa kulia, na aikimbie njia ya kumpelekea kuwa katika watu wa kushoto ambako itawatumbukiza Motoni na kufungiwa milango.

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Naapa kwa Mji huu! *

2. Nawe unaukaa Mji huu. *

3. Na naapa kwa mzazi na alicho kizaa. *

4. Hakika tumemuumba mtu katika taabu. *

5. Ati anadhani hapana yeyote ataye muweza? *

6. Anasema: Nimeteketeza chungu ya mali. *

7. Ati anadhani ya kuwa hapana yeyote anaye mwona? *

8. Kwani hatukumpa macho mawili? *

9. Na ulimi, na midomo miwili? *

10. Na tukambainishia zote njia mbili? *

11. Lakini hakujitoma kwenye njia ya vikwazo vya milimani. *

12. Na nini kitakujuvya ni nini njia ya vikwazo vya milimani? *

13. Kumkomboa mtumwa; *

14. Au kumlisha siku ya njaa *

15. Yatima aliye jamaa, *

16. Au masikini aliye vumbini. *

17. Tena awe miongoni mwa walio amini na wakausiana kusubiri na wakausiana kuhurumiana. *

18. Hao ndio watu wa kheri wa kuliani. *

19. Lakini walio zikataa Ishara zetu, hao ndio watu wa shari wa kushotoni. *

20. Juu yao utakuwa Moto ulio fungiwa kila upande.  *  


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright © 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani