Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

81. SURAT ATTAKWIR

(Imeteremka Makka)

Katika Sura hii yanaelezwa yatakayo tokea wakati wa Saa ya Kiyama na baada yake, na yanaelezwa ya kuonyesha dalili za uweza wa Mwenyezi Mungu, na kutilia mkazo cheo cha Qur'ani tukufu, na kupinga madai ya uzushi katika Qur'ani, na kumtakasa Mtume s.a.w. na tuhuma za wazimu, na kuwatisha na kuwaonya hao wanao endelea na upotovu, na inataka yaangaliwe mazingatio yaliyomo katika Qur'ani ambayo yatawafaa watu wenye kusimama msimamo wa sawa, na inarudisha mambo yote ya watu kwenye mapenzi ya Mola Mlezi wa walimwengu wote.

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Jua litakapo kunjwa, *

2. Na nyota zikazimwa, *

3. Na milima ikaondolewa, *

4. Na ngamia wenye mimba pevu watakapo achwa wasishughulikiwe, *

5. Na wanyama wa mwituni wakakusanywa, *

6. Na bahari zikawaka moto, *

7. Na nafsi zikaunganishwa, *

8. Na msichana aliye zikwa hai atapo ulizwa, *

9. Kwa kosa gani aliuliwa? *

10. Na madaftari yatakapo enezwa, *

11. Na mbingu itapo tanduliwa, *

12. Na Jahannamu itapo chochewa, *

13. Na Pepo ikasogezwa, *

14. Kila nafsi itajua ilicho kihudhurisha. *

15. Naapa kwa nyota zinapo rejea nyuma, *

16. Zinazo kwenda, kisha zikajificha, *

17. Na kwa usiku unapo pungua, *

18. Na kwa asubuhi inapo pambazuka, *

19. Kwamba hakika bila ya shaka hii ni kauli ya Mjumbe mtukufu, *

20. Mwenye nguvu na mwenye cheo kwa huyo Mwenye Kiti cha Enzi, *

21. Anaye t'iiwa, tena muaminifu. *

22. Na wala huyu mwenzenu hana wazimu. *

23. Na hakika yeye alimwona kwenye upeo wa macho ulio safi. *

24. Wala yeye si bakhili kwa mambo ya ghaibu. *

25. Wala hii si kauli ya Shetani maluuni. *

26. Basi mnakwenda wapi? *

27. Haikuwa hii ila ni ukumbusho kwa walimwengu wote. *

28. Kwa yule miongoni mwenu anaye taka kwenda sawa. *

29. Wala nyinyi hamtataka isipo kuwa atake Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa walimwengu wote.  *  


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright © 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani