Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

80. SURAT A'BASA

(Imeteremka Makka)

Sura hii imeanza kwa kumlaumu Nabii Muhammad s.a.w. kwa kumpuuza Ibnu Ummi Maktoum alipo mjia kutafuta ilimu na uwongofu. Naye Nabii s.a.w. alikuwa kashughulika kuwalingania Dini baadhi ya mabwana wa Kikureshi kwa kutaraji watamwitikia, ili kwa kusilimu kwao wange silimu watu wengi. Kisha Sura inamkumbusha binaadamu kwa neema alizo pewa na Mwenyezi Mungu tangu kuumbwa kwake mpaka kufufuliwa kwake. Na ikakhitimisha kwa kusimulia khabari za Siku ya Kiyama, ikibainisha kwamba watu siku hiyo ni makundi mawili, kundi la Waumini lenye furaha, na kundi la makafiri wapotovu.

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Alikunja kipaji na akageuka, *

2. Kwa sababu alimjia kipofu! *

3. Na nini kitakujuulisha pengine yeye atatakasika? *

4. Au atawaidhika, na mawaidha yamfae? *

5. Ama ajionaye hana haja, *

6. Wewe ndio unamshughulikia? *

7. Na si juu yako kama hakutakasika. *

8. Ama anaye kujia kwa juhudi, *

9. Naye anaogopa, *

10. Ndio wewe unampuuza? *

11. Sivyo hivyo! Huku ni kukumbushana. *

12. Basi anaye penda akumbuke. *

13. Yamo katika kurasa zilizo hishimiwa, *

14. Zilizo inuliwa, zilizo takaswa. *

15. Zimo mikononi mwa Malaika waandishi, *

16. Watukufu, wema. *

17. Ameangamia mwanaadamu! Nini kinacho mkufurisha? *

18. Kwa kitu gani amemuumba? *

19. Kwa tone la manii, akamuumba na akamkadiria. *

20. Kisha akamsahilishia njia. *

21. Kisha akamfisha, akamtia kaburini. *

22. Kisha apendapo atamfufua. *

23. La! Hajamaliza aliyo muamuru. *

24. Hebu mtu na atazame chakula chake. *

25. Hakika Sisi tumemimina maji kwa nguvu, *

26. Tena tukaipasua pasua ardhi kwa nguvu, *

27. Kisha tukaotesha humo nafaka, *

28. Na zabibu, na mimea ya majani, *

29. Na mizaituni, na mitende, *

30. Na bustani zenye miti iliyo songana baraabara, *

31. Na matunda, na malisho ya wanyama; *

32. Kwa manufaa yenu na mifugo yenu. *

33. Basi utakapo kuja ukelele, *

34. Siku ambayo mtu atamkimbia nduguye, *

35. Na mamaye na babaye, *

36. Na mkewe na wanawe - *

37. Kila mtu miongoni mwao siku hiyo atakuwa na lake la kumtosha. *

38. Siku hiyo ziko nyuso zitazo nawiri, *

39. Zitacheka, zitachangamka; *

40. Na nyuso siku hiyo zitakuwa na mavumbi, *

41. Giza totoro litazifunika, *

42. Hao ndio makafiri watenda maovu.  *  


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright © 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani