Sura hii tukufu ina Aya 111, nayo ni Sura ya Makka ila Aya hizi:
26, 32, 33, 57 na tangu Aya 73 mpaka Aya 80. Aya zote hizi, nazo ni 12,
ni za Madina. Sura hii imeanza kwa kumsabihi, kumtakasa, Mwenyezi Mungu
Mtukufu. Kisha ikaitaja Israi, nayo ni safari ya usiku aliyo chukuliwa
Mtume s.a.w. kutoka Makka mpaka Bait Al Muqaddas (Yerusalemu), na baadae
akapelekwa mbinguni, na kurejeshwa Makka usiku ule ule.
Baadae Sura inaeleza Ujumbe wa Nabii Musa a.s., na yaliyo kuwa ya Wana
wa Israili. Kisha ikaashiria cheo cha Qur'ani Tukufu katika uwongofu, na
zikatajwa Aya za uumbaji usiku na mchana, na yatakayo watokea watu Siku
ya Kiyama katika kulipwa kwa vitendo walivyo vitenda duniani. Na Subhanahu
amebainisha sababu za kuharibika umma, na hali ya watu katika kuhangaika
kwao, na matokeo ya vitendo vyao huko Akhera. Tena zikaja Aya za kutukuzwa
wazazi, baba na mama, na hali ya watu kukhusu mali zao; na zikaja Amri
Kumi za kuunda umma ulio bora. Kisha Subhanahu akauvunja uzushi wa washirikina
kukhusu Malaika, kisha akabainisha Qur'ani inavyo eleza hoja zake.
Kisha Subhanahu akaashiria anavyo stahiki kuhimidiwa, na upinzani wa
washirikina, akawapa wasia Waumini. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu akaeleza
namna anavyo watendea makafiri duniani na Akhera. Tena akaeleza asili ya
uumbaji wa binaadamu na Shet'ani, na akawatisha washirikina kwa Aya zake.
Baada ya hayo Subhanahu alibainisha utukufu wa binaadamu, na akataja adhabu
za Siku ya Kiyama. Akataja vipi washirikina wanavyo jaribu kumzuia Nabii
asitimize Wito wake, na vipi Mwenyezi Mungu anavyo mtia nguvu. Baada ya
hayo Allahu Subhanahu wa Taa'la akamuusia Nabii kwa wasia za uwongofu,
na wito mnasaba. Kisha akaashiria cheo cha Qur'ani Tukufu, na akataja khabari
za Roho, na akaashiria siri zake. Kisha akataja umuujiza wa Qur'ani, kushindwa
majini na watu kuleta mfano wake. Na akabainisha Subhanahu uwezo wake kuleta
Ishara nyengine. Tena akataja vipi Qur'ani ilivyo kusanya Haki, na hali
za Waumini wema katika Imani zao, na inavyo takikana kuwa daima wawe wanamhimidi
Mwenyezi Mungu na wakimtukuza
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
1. SUBHANA, Ametakasika aliye mchukua mja wake usiku mmoja kutoka Msikiti Mtukufu mpaka Msikiti wa Mbali, ambao tumevibariki vilivyo uzunguka, ili tumuonyeshe baadhi ya Ishara zetu. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia na Mwenye kuona. *
2. Na tukampa Musa Kitabu, na tukakifanya uwongofu kwa Wana wa Israili. (Tukawambia): Msiwe na mtegemewa ila Mimi! *
3. Enyi kizazi tuliyo wachukua pamoja na Nuhu! Hakika yeye alikuwa mja mwenye shukrani. *
4. Na tukawahukumia Wana wa Israili katika Kitabu kwamba: Hakika nyinyi mtafanya fisadi katika nchi mara mbili, na kwa yakini mtapanda kiburi, kiburi kikubwa. *
5. Basi itapo fika ahadi ya kwanza yake tutakupelekeeni waja wetu wa kali kwa vita. Watakuingilieni ndani ya majumba. Na hii ilikuwa ahadi iliyo timizwa. *
6. Kisha tukakurudishieni nguvu zenu dhidi yao, na tukakusaidieni kwa mali na wana, na tukakujaalieni mkawa wengi zaidi. *
7. Basi mkifanya wema, mnajifanyia wema nafsi zenu. Na mkifanya ubaya, mnajifanyia wenyewe. Na ikifika ahadi ya mwisho ili waziharibu nyuso zenu, na waingie Msikitini kama walivyo ingia mara ya kwanza, na waharibu kila walicho kiteka kwa uharibifu mkubwa. *
8. Huenda Mola wenu Mlezi akakurehemuni. Na mkirudia na Sisi tutarudia. Na tumeifanya Jahannamu kuwa ni gereza kwa ajili ya makafiri. *
9. Hakika hii Qur'ani inaongoa kwenye ya yaliyo nyooka kabisa, na inawabashiria Waumini ambao wanatenda mema ya kwamba watapata malipo makubwa. *
10. Na yakwamba wale wasio iamini Akhera tumewaandalia adhabu chungu. *
11. Na mwanaadamu huomba shari kama vile aombavyo kheri, kwani mwanaadamu ni mwenye pupa. *
12. Na tumefanya usiku na mchana kuwa ishara mbili. Tena tukaifuta ishara ya usiku, na tukaifanya ishara ya mchana ni yenye mwangaza ili mtafute fadhila itokayo kwa Mola wenu Mlezi, na mpate kujua idadi ya miaka na hisabu. Na kila kitu tumekifafanua waziwazi.
13. Na kila mtu tumemfungia a'mali yake shingoni mwake. Na Siku ya Kiyama tutamtolea kitabu atakacho kikuta kiwazi kimekunjuliwa. *
14. Ataambiwa: Soma kitabu chako! Nafsi yako inakutosha leo kukuhisabu. *
15. Anaye ongoka basi anaongoka kwa ajili ya nafsi yake. Na anaye potea basi anapotea kwa khasara yake mwenyewe. Wala habebi mbebaji mzigo wa mwengine. Wala Sisi hatuadhibu mpaka tumpeleke Mtume. *
16. Na pindi tukitaka kuuteketeza mji huwaamrisha wale wenye starehe na taanusi, lakini wao huendelea kutenda maovu humo. Basi hapo kauli huthibiti juu ya mji huo, nasi tukauangamiza kwa maangamizo makubwa. *
17. Na kaumu ngapi tumeziangamiza baada ya Nuhu! Na Mola wako Mlezi anatosha kabisa kuwa ni Mwenye kuzijua na kuziona dhambi za waja wake. *
18. Anaye taka yapitayo upesi upesi, tutafanya haraka kumletea hapa hapa tunayo yataka kwa tumtakaye. Kisha tumemwekea Jahannamu; ataingia humo hali ya kuwa ni mwenye kulaumiwa na kufurushwa. *
19. Na anaye itaka Akhera, na akazifanyia juhudi a'mali zake, naye ni Muumini, basi hao juhudi yao itakuwa ni ya kushukuriwa. *
20. Wote hao tunawakunjulia - hawa na hao - katika
neema za Mola wako Mlezi. Wala neema za Mola wako Mlezi hazizuiliki.
*
21. Angalia vipi tulivyo wafadhili baadhi yao
kuliko wenginewe. Na hakika Akhera ni yenye daraja kubwa zaidi na fadhila
kubwa zaidi.
*
22. Usimfanye mungu mwengine pamoja na Mwenyezi
Mungu, usije ukawa wa kulaumiwa uliye tupika.
*
23. Na Mola wako Mlezi ameamrisha kuwa msimuabudu
yeyote ila Yeye tu, na wazazi wawili muwatendee wema. Mmoja wao akifikia
uzee, naye yuko kwako, au wote wawili, basi usimwambie hata: Ah! Wala usiwakemee.
Na sema nao kwa msemo wa hishima.
*
24. Na uwainamishie bawa la unyenyekevu kwa kuwaonea
huruma. Na useme: Mola wangu Mlezi! Warehemu kama walivyo nilea utotoni.
*
25. Mola wenu anajua kabisa yaliyo nyoyoni mwenu.
Ikiwa nyinyi mtakuwa wema, basi hakika Yeye ni Mwenye kuwaghufiria wanao
tubia kwake.
*
26. Na mpe aliye jamaa yako haki yake, na masikini,
na msafiri; wala usitumie ovyo kwa fujo.
*
27. Hakika wabadhirifu ni ndugu wa Mashet'ani.
Na Shet'ani ni mwenye kumkufuru Mola wake Mlezi.
*
28. Na ikiwa unajikurupusha nao, nawe unatafuta
rehema ya Mola wako Mlezi unayo itaraji, basi sema nao maneno laini.
*
29. Wala usiufanye mkono wako kama ulio fungwa
shingoni mwako, wala usiukunjue wote kabisa, utabaki ukilaumiwa muflisi.
*
30. Hakika Mola wako Mlezi humkunjulia riziki
amtakaye, na humpimia amtakaye. Hakika Yeye kwa waja wake ni Mwenye kuwajua
na kuwaona.
*
31. Wala msiwauwe wana wenu kwa kuogopa umasikini.
Sisi tunawaruzuku wao na nyinyi. Hakika kuwaua hao ni khatia kubwa.
*
32. Wala msikaribie uzinzi. Hakika huo ni uchafu
na njia mbaya.
*
33. Wala msiuwe nafsi ambayo Mwenyezi Mungu amekataza
isipo kuwa kwa haki. Na aliye uliwa kwa kudhulumiwa basi tumempa madaraka
mrithi wake. Lakini asipite mpaka katika kuuwa. Kwani yeye anasaidiwa.
*
34. Wala msiyakaribie mali ya yatima, isipo kuwa
kwa njia iliyo bora, mpaka afike utuuzimani. Na timizeni ahadi. Kwa hakika
ahadi itasailiwa.
*
35. Na timizeni kipimo mpimapo. Na pimeni kwa
mizani zilizo sawa. Hayo ni wema kwenu na khatimaye ndio bora.
*
36. Wala usiyafuate usiyo na ujuzi nayo. Hakika
masikio, na macho, na moyo - hivyo vyote vitasailiwa.
*
37. Wala usitembee katika ardhi kwa maringo.
Hakika wewe huwezi kuipasua ardhi wala kufikia urefu wa milima.
*
38. Haya yote ubaya wake ni wenye kuchukiza kwa
Mola wako Mlezi.
*
39. Haya ni katika hikima alizo kufunulia Mola
wako Mlezi. Wala usimweke pamoja na Mwenyezi Mungu mungu mwengine, usije
ukatupwa katika Jahannamu ukilaumiwa na kufurushwa.
*
40. Je! Mola wenu Mlezi amekuteulieni wavulana,
na Yeye akawafanya Malaika ni banati zake? Kwa hakika nyinyi mnasema usemi
mkubwa.
*
41. Na tumekwisha bainisha katika Qur'ani hii
ili wapate kukumbuka. Lakini haikuwazidisha ila kuwa mbali nayo.
*
42. Sema: Lau kuwa wangeli kuwa pamoja naye miungu
mingine kama wasemavyo, basi wangeli tafuta njia ya kumfikia Mwenye Kiti
cha Enzi.
*
43. Subhanahu Wa Taa'la, Ametakasika na Ametukuka
juu kabisa na hayo wanayo yasema.
*
44. Zinamtakasa zote mbingu saba na ardhi na
vyote viliomo ndani yake. Na hapana kitu ila kinamtakasa kwa sifa zake.
Lakini nyinyi hamfahamu kutakasa kwake. Hakika Yeye ni Mpole na Mwenye
maghfira.
*
45. Na unapo soma Qur'ani tunaweka baina yako
na wale wasio iamini Akhera pazia linalo wafunika.
*
46. Na tunaweka vifuniko juu ya nyoyo zao wasije
wakaifahamu, na tunaweka kwenye masikio yao uziwi. Na unapo mtaja katika
Qur'ani Mola wako Mlezi peke yake, basi wao hugeuka nyuma wakenda zao.
*
47. Sisi tunajua vyema kabisa sababu wanayo sikilizia
wanapo kusikiliza, na wanapo nong'ona. Wanapo sema hao madhaalimu: Nyinyi
hamumfuati isipo kuwa mtu aliye rogwa.
*
48. Tazama vipi wanavyo kupigia mifano. Basi
wamepotea. Kwa hivyo hawawezi kuipata njia.
*
49. Na walisema: Je! Tutapo kuwa mifupa na mapande
yaliyo vurugika, tutafufuliwa kwa umbo jipya?
*
50. Sema: Kuweni hata mawe na chuma.
*
51. Au umbo lolote mnalo liona kubwa katika vifua
vyenu. Watasema: Nani atakaye turudisha tena? Sema: Yule yule aliye kuumbeni
mara ya kwanza! Watakutikisia vichwa vyao, na watasema: Lini hayo? Sema:
A'saa yakawa karibu!
*
52. Siku atakapo kuiteni, na nyinyi mkamuitikia
kwa kumshukuru, na mkadhani kuwa hamkukaa ila muda mdogo tu.
*
53. Waambie waja wangu waseme maneno mazuri,
maana Shet'ani huchochea ugomvi baina yao. Hakika Shet'ani ni adui aliye
dhaahiri kwa mwanaadamu.
*
54. Mola wenu Mlezi anakujueni vilivyo. Akipenda
atakurehemuni, na akipenda atakuadhibuni. Na hatukukutuma ili uwe mlinzi
juu yao.
*
55. Na Mola wako Mlezi anawajua vilivyo waliomo
mbinguni na katika ardhi. Na hakika tumewafadhilisha baadhi ya Manabii
kuliko wengine; na Daudi tulimpa Zaburi.
*
56. Sema: Waombeni hao mnao wadaia badala yake
Yeye. Hawawezi kukuondoleeni madhara, wala kuyaweka pengine.
*
57. Hao wanao waomba, wao wenyewe wanatafuta
njia ya kwendea kwa Mola wao Mlezi - hata miongoni mwao walio karibu mno
- na wanataraji rehema zake na wanaikhofu adhabu yake. Hakika adhabu ya
Mola wako Mlezi yafaa kutahadhari nayo.
*
58. Na hapana mji wowote ila Sisi tutauteketeza
kabla ya Siku ya Kiyama, au tutaupa adhabu kali. Haya yamekwisha andikwa
katika Kitabu.
*
59. Na hapana kinacho tuzuia kupeleka miujiza
ila ni kuwa watu wa zamani waliikanusha. Na tuliwapa Wathamudi ngamia jike
kuwa ni Ishara iliyo dhaahiri, lakini walidhulumu kwaye. Nasi hatupeleki
Ishara ila kwa ajili ya kuhadharisha.
*
60. Na tulipo kwambia: Hakika Mola wako Mlezi
amekwisha wazunguka hao watu. Na hatukuifanya ndoto tulio kuonyesha ila
ni kuwajaribu watu, na mti ulio laaniwa katika Qur'ani. Na tunawahadharisha,
lakini haiwazidishii ila uasi mkubwa.
*
61. Na pale tulipo waambia Malaika: Msujudieni
Adam. Wakamsujudia isipo kuwa Iblisi. Akasema: Je! Nimsujudie uliye muumba
kwa udongo?
*
62. Akasema: Hebu nambie khabari ya huyu uliye
mtukuza juu yangu. Ukiniakhirisha mpaka Siku ya Kiyama, hapana shaka nitawaangamiza
dhuriya zake wasipo kuwa wachache tu.
*
63. Akasema Mwenyezi Mungu: Ondokelea mbali!
Atakaye kufuata katika wao, basi Jahannamu itakuwa ndiyo malipo yenu, malipo
ya kutimia.
*
64. Na wachochee uwawezao katika wao kwa sauti
yako, na wakusanyie jeshi lako la wapandao farasi na waendao kwa miguu.
Na shirikiana nao katika mali na wana, na waahidi. Na Shet'ani hawapi ahadi
ila ya udanganyifu.
*
65. Hakika wewe huna mamlaka juu ya waja wangu.
Na Mola wako Mlezi anatosha kuwa ni wa kutegemewa.
*
66. Mola wenu Mlezi ndiye anaye kuendesheeni
marikebu katika bahari ili mtafute katika fadhila zake. Hakika Yeye ni
Mwenye kukurehemuni nyinyi.
*
67. Na inapo kufikieni taabu katika bahari, hao
mnao waomba wanapotea, isipo kuwa Yeye tu. Na anapo kuvueni mkafika nchi
kavu, mnageuka. Ama mwanaadamu ni mwingi wa kukanusha.
*
68. Je! Mmeaminisha ya kuwa hatakudidimizeni
upande wowote katika nchi kavu, au kwamba hatakuleteeni tufani la kokoto?
Kisha msipate wa kumtegemea.
*
69. Au mmeaminisha ya kuwa hatakurudisheni humo
mara nyengine na kukupelekeeni kimbunga cha upepo akakuzamisheni kwa mlivyo
kufuru, na kisha msipate wa kukunusuruni nasi.
*
70. Na hakika tumewatukuza wanaadamu, na tumewapa
vya kupanda nchi kavu na baharini, na tumewaruzuku vitu vizuri vizuri,
na tumewafadhilisha kwa fadhila kubwa kuliko wengi miongoni mwa tulio waumba.
*
71. Siku tutapo waita kila kikundi cha watu kwa
mujibu wa wakifuatacho - basi atakaye pewa kitabu chake kwa mkono wake
wa kulia, basi hao watasoma kitabu chao wala hawatadhulumiwa hata chembe.
*
72. Na aliye kuwa hapa kipofu, basi atakuwa kipofu
Akhera, na atakuwa aliye ipotea zaidi Njia.
*
73. Na hakika walikaribia kukushawishi uache
tuliyo kufunulia ili utuzulie mengineyo. Na hapo ndio wangeli kufanya rafiki.
*
74. Na lau kuwa hatukukuweka imara ungeli karibia
kuwaelekea kidogo.
*
75. Hapo basi bila ya shaka tungeli kuonjesha
adhabu mardufu ya uhai, na adhabu mardufu ya kifo. Kisha usinge pata mtu
wa kukunusuru nasi.
*
76. Na walitaka kukukera ili uitoke nchi. Na
hapo wao wasingeli bakia humo ila kwa muda mchache tu.
*
77. Huo ndio mwendo kwa Mitume tulio watuma kabla
yako. Wala hupati mabadiliko katika mwendo wetu.
*
78. Shika Sala jua linapo pinduka mpaka giza
la usiku, na Qur'ani ya al fajiri. Hakika Qur'ani ya alfajiri inashuhudiwa
daima.
*
79. Na amka usiku kwa ibada; ni ziada ya sunna
khasa kwako wewe. Huenda Mola wako Mlezi akakunyanyua cheo kinacho sifika.
*
80. Na sema: Mola wangu Mlezi! Niingize muingizo
mwema, na unitoe kutoka kwema. Na unipe nguvu zinazo toka kwako zinisaidie.
*
81. Na sema: Kweli imefika, na uwongo umetoweka.
Hakika uwongo lazima utoweke!
*
82. Na tunateremsha katika Qur'ani yaliyo ni
matibabu na rehema kwa Waumini. Wala hayawazidishii madhaalimu ila khasara.
*
83. Na mwanaadamu tunapo mneemesha hugeuka na
kujitenga kando. Na inapo mgusa shari hukata tamaa.
*
84. Sema: Kila mmoja anafanya kwa namna yake.
Na Mola wenu Mlezi anajua aliye ongoka katika njia.
*
85. Na wanakuuliza khabari za Roho. Sema: Roho
ni katika mambo ya Mola wangu Mlezi. Nanyi hamkupewa katika ilimu ila kidogo
tu.
*
86. Na tungeli penda tungeli yaondoa tuliyo kufunulia.
Kisha usingeli pata mwakilishi wa kukupigania kwetu kwa haya.
*
87. Isipo kuwa iwe rehema itokayo kwa Mola wako
Mlezi. Hakika fadhila yake kwako ni kubwa.
*
88. Sema: Wangeli kusanyika watu na majini ili
walete mfano wa hii Qur'ani basi hawaleti mfano wake, hata wakisaidiana
wao kwa wao.
*
89. Na hakika tumewaeleza watu katika hii Qur'ani
kwa kila mfano. Lakini watu wengi wanakataa isipo kuwa kukanusha tu.
*
90. Na walisema: Hatutakuamini mpaka ututimbulie
chemchem katika ardhi hii.
*
91. Au uwe na kitalu cha mitende na mizabibu,
na utupitishie mito kati yake ikimiminika.
*
92. Au utuangushie mbingu vipande vipande kama
ulivyo dai; au utuletee Mwenyezi Mungu na Malaika uso kwa uso.
*
93. Au uwe na nyumba ya dhahabu, au upae mbinguni.
Wala hatutaamini kupaa kwako mpaka ututeremshie kitabu tukisome. Sema:
Subhana Rabbi, Ametakasika Mola wangu Mlezi! Kwani mimi ni nani isipo kuwa
ni mwanaadamu na Mtume?
*
94. Na nini kilicho wazuilia watu kuamini ulipo
wajia uwongofu isipo kuwa walisema: Je! Mwenyezi Mungu humtuma mwanaadamu
kuwa ni Mtume?
*
95. Sema: Ingeli kuwa duniani wapo Malaika wanatembea
kwa utulivu wao, basi bila ya shaka tungeli wateremshia Malaika kuwa ni
Mtume wao.
*
96. Sema: Mwenyezi Mungu anatosha kuwa Shahidi
baina yangu na nyinyi. Hakika Yeye anawajua vyema waja wake na anawaona.
*
97. Na anaye mhidi Mwenyezi Mungu basi huyo ndiye
aliye hidika. Na anaye wapotoa basi huto wapatia walinzi badala yake. Na
tutawakusanya Siku ya Kiyama hali wakikokotwa juu ya nyuso zao, nao ni
vipofu na mabubu na viziwi. Na makaazi yao ni Jahannamu. Kila moto ukifanya
kusinzia tutazidi kuuchochea uwake kwa nguvu.
*
98. Hayo ni malipo yao kwa sababu walizikataa
ishara zetu, na wakasema: Hivyo tukisha kuwa mifupa na mapande yaliyo vurugika
tutafufuliwa kwa umbo jipya?
*
99. Kwani hawakuona ya kwamba Mwenyezi Mungu
aliye umba mbingu na ardhi ni Mwenye kuweza kuumba mfano wao? Na Yeye amewawekea
muda usio na shaka yoyote. Lakini madhaalimu hawataki ila ukafiri.
*
100. Sema: Lau kuwa nyinyi mnazimiliki khazina
za rehema za Mola wangu Mlezi, basi hapana shaka mngeli zuia kuzitumia
kwa ajili ya kukhofu. Na mwanaadamu tangu hapo tabia yake ni mchoyo!
*
101. Na kwa yakini tulimpa Musa ishara tisa
zilizo wazi. Waulize Wana wa Israili alipo wafikia, na Firauni akawaambia:
Hakika mimi nakuona wewe Musa umerogwa!
*
102. Musa akasema: Wewe unajua bila ya shaka
kuwa haya hakuyateremsha ila Mola Mlezi wa mbingu na ardhi ili kuwa ni
ushahidi wa kuonekana. Na hakika mimi bila ya shaka nakuona wewe, Firauni,
kuwa umekwisha angamia.
*
103. Basi Firauni akataka kuwafukuza katika
nchi. Kwa hivyo tukamzamisha yeye na walio kuwa pamoja naye wote.
*
104. Na tukawaambia baada yake Wana wa Israili:
Kaeni katika nchi. Itapo kuja ahadi ya Akhera tutakuleteni nyote pamoja.
*
105. Na kwa Haki tumeiteremsha, na kwa Haki
imeteremka. Na hatukukutuma ila uwe mbashiri na mwonyaji.
*
106. Na Qur'ani tumeigawanya sehemu mbali mbali
ili uwasomee watu kwa kituo, na tumeiteremsha kidogo kidogo.
*
107. Sema: Iaminini au msiiamini. Hakika wale
walio pewa ilimu kabla yake, wanapo somewa hii, huanguka kifudifudi wanasujudu.
*
108. Na wanasema: Subhana Rabbina, Ametakasika
Mola wetu Mlezi! Hakika ahadi ya Mola wetu Mlezi lazima itimizwe!
*
109. Na huanguka kifudifudi na huku wanalia,
na inawazidisha unyenyekevu.
*
110. Sema: Mwombeni Allah (Mwenyezi Mungu),
au mwombeni Rahman (Mwingi wa Rehema), kwa jina lolote mnalo mwita. Kwani
Yeye ana majina mazuri mazuri. Wala usitangaze Sala yako kwa sauti kubwa,
wala usiifiche kwa sauti ndogo, bali shika njia ya kati na kati ya hizo.
*
111. Na sema: Alhamdulillah, Himdi zote ni za
Mwenyezi Mungu ambaye hana mwana, wala hana mshirika katika ufalme, wala
hana rafiki wa kumsaidia kwa sababu ya udhaifu wake. Na mtukuze kwa utukufu
mkubwa.
*
Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka
Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii
qurani-tukufu@geocities.com
Copyright © 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani