Sura hii iliteremka Makka kabla ya Hijra, kuhamia Mtume s.a.w. Madina.
Imeitwa Al-Faatih'a, yaani Kifungulio kwa kuwa ndiyo sura ya mwanzo katika
mpango wa Msahafu Mtukufu, nayo ni sura ya mwanzo iliyo teremka kwa utimilivu
wake. Na sura hii inakusanya jumla ya yaliyomo katika Qur'ani na kama kwamba
huu ni mukhtasari wake, na baadaye yatakuja mambo kwa tafsili, babu-babu.
Na makusudio ya Qur'ani ni: Kubainisha Tawhid, Upweke wa Mwenyezi Mungu;
na kubainisha ahadi na bishara kwa Muumini mtenda mema; na kubainisha ahadi
na onyo kwa kafiri na mtenda maovu; na kubainisha ibada; na kubainisha
njia ya kufanikiwa duniani na Akhera; na hadithi za walio mt'ii Mwenyezi
Mungu wakafuzu, na hadithi za walio muasi wakaangamia.
Sura Al-Faatih'a inakusanya kwa ufupi na kwa kuashiria makusudio
haya, na kwa hivyo ndio ikaitwa pia "Ummul Kitaab" yaani "Msingi wa Kitabu".
1. KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.1
2. Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote;2
3. Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu;3
4. Mwenye Kumiliki Siku ya Malipo. 4
5. Wewe tu tunakuabudu, na Wewe tu tunakuomba msaada.5
6. Tuongoe njia iliyo nyooka,6
7. Njia ya ulio waneemesha, siyo ya walio kasirikiwa, wala walio potea. 7
Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka
Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com