MTAZAMO WA QUR'AN

Anasema Mwenyeezi Mungu kuwa: "Na Ayubu, alipomwita Mola wake ya kwamba imenigusa dhara nawe ndiye unaye rehema zaidi kuliko wanaorehemu. Basi tukamkubalia na tukamuondolea dhara aliyokuwa nayo na tukampa watu wake na mfano wao pamoja nao, ni rehema kutoka kwetu, na ukumbusho kwa wafanya ibada." 21:83-84.

"Na mkumbuke mjawetu Ayubu, alipomwita Mola wake: Kwa hakika shetani amenifikishia udhia na taabu. Kaza mwendo, hapa mahala baridi pa kuogea na kinywaji. Na tukampa watu wake na wengine kama wao pamoja nao, kwa rehema itokayo kwetu na mawaidha kwa watu wenye akili." 38:41-43.

Imepokewa kutoka kwa Anas bin Malik, kwamba Mtume s.a.w amesema:

"Hakika Nabii wa Mwenyeezi Mungu Ayubu (a.s) alipatwa na balaa kwa muda wa miaka saba, na wengine wanasema miaka mitatu, wengine wanasema miaka kumi na minane. Jamaa na ndugu zake wote walimuepuka isipokuwa ndugu zake wawili na mkewe. Hawa ndugu zake wakawa wanapitapita kumuangalia, kisha mmoja wao akamwambia mwenzake:

Unajua! Wallahi Ayubu kwa hakika ametenda kosa kubwa ambalo hakuna yeyote katika walimwengu aliyetenda kosa (kubwa kama yeye!) mwenzake akamuuliza: Ni vipi! Akasema: (Balaa moja kwa moja) tangu miaka kumi na minane, Mwenyeezi Mungu hajamhurumia!

Taz: Tafsirut Tabari         J. 23 Uk. 107 Tafsir Ibn Kathir        J. 4 Uk. 43

Nabii Ayubu (a.s) alipoteza watoto, jamaa na ndugu walimtenga, mali yake yote ilipotea, na alipata maradhi mazito. Kwa balaa hilo nabii Ayubu (a.s) akaambiwa: "Amelaaniwa na Mwenyeezi Mungu" Nabii Ayubu, kila lilipomfikia balaa alikuwa akisema: ''Allahumma anta akhadhta wa anta a'twayta" yaani, Ee Mola! Wewe (ndiye) uliyechukua na wewe (ndiye) uliyetoa." Ndipo Mwenyeezi Mungu akasema: "Bila shaka tulimkuta ni mwenye subira, mja mwema, kwa hakika alikuwa mnyenyekevu sana." 38:44.

Anasema Mtume s.a.w kuwa: "Watu wenye kupata balaa kubwa zaidi ni:

Manabii, kisha watu wema, kisha wa mfano (wao), kisha wa mfano (wao). Mtu hujaribiwa (hupewa balaa) kwa kadiri ya dini (imani) yake, basi kama katika imani yake kuna nguvu, huongezewa balaa yake."

Taz: Ma'al Anbiyaa fyil Qur-an          Uk. 212 Alburhan fyitafsiril Qur-an    J.4  Uk. 53 Tafsirus Saafi                J.4  Uk. 303

Kwa hiyo, kwa dalili hizi, inatuonyesha kuwa: Balaa linalomfika mtu si dalili ya uovu! Kwa sababu, Manabii wa Mwenyeezi Mungu pia hawakusalimika nalo, bali wao walipatwa na balaa kubwa zaidi kuliko binadamu yeyote wa kawaida. Mwisho wa kisa cha Nabii Ayubu (a.s) Mwenyeezi Mungu anasema:

"Ni ukumbusho kwa wafanya ibada" 21:84

"Ni mawaidha kwa watu wenye akili," 38:43

Kwa ufupi, Mwenyeezi Mungu anasisitiza hapa ya kwamba:

"Kumbukumbu" na "mawaidha" haya ni kwa ajili ya "wacha Mungu" na "watu wenye akili" tu, si kwa kila mtu.