YALIYOSEMWA BAADA YA TUKIO LA MOTO

Baada ya moto kuunguza nyumba yangu kila kitu isipokuwa vitabu vya Kiislamu tu. Watu walilipokea tukio hili kwa mitazamo mbalimbali, wako walioona kuwa tukio hili ni mtihani wa Mwenyeezi Mungu, ambao huwajaribu baadhi ya waja wake. Na wengine waliona kuwa tukio hili ni laana ya Mwenyeezi Mungu, ambayo huwapata wale waliomkosea. Hili lilisemwa sana katika maeneo mbalimbali, kama Misikitini na madarasani na katika mihadhara yao. Kwa hivyo, katika mtazamo wao juu ya tukio hili la moto, wanaona kuwa: Mwenyeezi Mungu ameniadhibu kwa kunichomea nyumba yangu na vitu vyote kwa sababu ya uovu nilio nao kwake. Huu ndio mtazamo wa kundi la pili juu ya tatizo la moto uliounguza nyumba yangu na vitu vyote vilivyokuwemo ndani yake isipokuwa maktaba ya vitabu vya Kiislamu tu.

Mimi nami, ambaye ndiye niliyefikwa na tukio hili la moto, nina mtazamo wangu juu ya hili. Mimi ninaliona tukio hili ni la kawaida, na kufikiwa na balaa kama hili mmoja wa waja wake Mwenyezi Mungu si kitu kigeni. Bali waja wa Mwenyeezi Mungu, hasa waja wenye kumcha kikweli kweli, Mwenyeezi Mungu amewapa balaa kubwa za aina mbali mbali. Basi mimi ninashukuru sana kwa kuwekwa katika barabara ya watukufu hao!!!

Qur-an inatupa khabari za Manabii wa Mwenyezi Mungu ambao walipatwa na balaa kubwa kubwa "Je, hawaizingatii Qur-an? Au nyoyo zinakufuli?" 47:24.