KATIKA KIPINDI CHA KUTAFSIRI QUR-AN NILIFIKWA NA MATUKIO HAYA UANDISHI NA ATHARI ZAKE

Wadhamini wa Taasisi ya ALMALID walimpelekea Rais waraka wenye kurasa nne Ref: ALM/HQ/AD3/97 tarehe 14/7/97 kumuomba kwa makusudi kabisa Serikali ichukue hatua kali dhidi yangu, mimi binafsi pamoja na baadhi ya vitabu nilivyokwisha andika na kuvichapisha. Katika waraka huo, ukurasa wa pili wametaja vitabu hivyo ni: "Muongozi wa wasomao", Tarekh ya Kiislamu", na "Meza ya uchunguzi".

Tarehe 25/7/97 Masheikh wa Bakwata, Baraza Kuu, Ansaar Sunnah, na Maimamu wa Misikiti mbalimbali, walianza kunilaani Misikitini na madarasani mwao. Ikiwa ni utekelezaji wa azimio lao walilolipitisha katika kikao kilichofanyika karibuni katika Hoteli ya Starlight mjini Dar es Salaam.

Akizungumza katika kikao hicho Sharif Juneidy, aliwataka Masheikh na Maimam kuchukua hatua na kutoa kauli juu yangu na kitabu changu (Tarekh ya Kiislamu).

Kufuatia kauli hiyo ya Sharif Juneidy, Masheikh wakiwemo wa Bakwata, Baraza Kuu, Ansaar Sunnah, na Maimam wa Misikiti mbalimbali walipitisha azimio kwamba suala hilo lizungumzwe katika khutuba za Ijumaa kwa Misikiti yote.

Taz: An-nuur, Na. 1108 ya tarehe 25-31/7/97

Tarehe 2/9/97 Masheikh na Maimamu wa Misikiti mbalimbali walikutana katika Hoteli ya Starlight Dar es Salaam kusisitiza (tena) azimio la kunilaani, na kuwataka Waislamu wote kunitenga.

Tarehe 11/11/97 niliitwa katika Kituo cha Polisi cha Kati, kuhojiwa juu ya waraka uliopelekwa kwa Rais. Nilitakiwa kuripoti tena tarehe 13/11/97 kisha nikatakiwa kuripoti tarehe 17 /11/97 lakini mara mbili zote hizo 13/ 11/97 na 17/11/97 Masheikh waliopeleka waraka huo Ikulu, walipotakiwa kufika Kituo cha Polisi cha Kati, kwa ajili ya kuhojiwa madai yaliyomo kwenye waraka wao, walijificha hawakuonekana.

Tarehe 30/3/98 majira ya saa sita mchana nikifuatana na mwenzangu aliyenichukua katika gari lake.

Tulipita eneo la Msikiti wa Mwembechai kuelekea nyumbani kwangu. Ndipo tuliposimamishwa na kundi la polisi wa F.F.U. wakiwa pamoja na polisi wa kawaida. Ambao walikua wanalinda eneo la Msikiti huo, kufuatia mashambulio waliyoyafanya kwa Waislamu wa Msikiti wa Mwembechai tangu tarehe 12/2/98. Ambapo waliua Waislamu wengi na wengine kuwajeruhi.

Walipotuzingira, walininyang'anya karatasi za tafsiri ya Qur-an tukufu. Kisha tukapelekwa katika Kituo cha Polisi cha Magomeni na zile karatasi wakabaki nazo. Sisi tukatiwa rumande kuanzia saa sita na nusu mchana hadi saa tisa jioni, walipotutoa ili kuandikisha maelezo. Kuanzia saa tisa jioni hadi saa kumi na rnbili magharibi tukiandika maelezo, kisha tukaachiwa huru, na zile karatasi za tafsiri ya Qur-an nikarejeshewa.

Taz: Majira ISSN 0856-5082 Na. 1549

Machi 31 /98 ukurasa wa kwanza na wa tatu.