SHUKRANI

Alhamdu lillah, ninamshukuru Mwenyeezi Mungu Subhanahu Wataala kwa rehema zake nyingi juu yangu. Katika rehema hizo nyingi ni hii ya kuniwafikisha kuandika Tafsiri ya Qur'an Tukufu mwanzo wa Suuratul Faatiha mpaka mwisho wa Suuratun Naas, alhamdu lillah. Na, rehema na amani ziwashukie Mtukufu Mtume Muhammad na Aali zake Watukufu.

Ninawashukuru sana wafadhili ambao wameiwezesha leo Tafsiri hii kuwa mikononi mwa wasomaji. Bila shaka, juhudi za hali na mali walizotoa kwa ajili ya kufanikisha kazi hii hazipotei bure. Kwa hakika Mwenyezi Mungu hapotezi malipo ya wafanyao mema.

Na, ninawashukuru sana Masheikh walioupitia Muswadda wa Tafsiri hii kwa kadiri yao. Wapo ambao waliupitia robo yake, wengine nusu yake, hii ni kutokana na dhurufu walizonazo hazikuwawezesha kuupitia wote, ingawa walitaka sana kufanya hivyo.

Lakini, wapo Masheikh walioupitia Muswadda wote, alhamdu lillah. Kisha wakanipa ushauri, maelekezo nawakanizindua muhala mwingi, bila shaka, ninakiri hapa ya kuwa: Kama si wao, basi Mayunga angeliangamia. Ninashukuru sana.

Aidha, ninawashukuru sana rafiki zangu wote waliopo hapa Tanzania bara, na huko Tanzania Visiwani, kwa ushirikiano mkubwa walionipa juu ya kazi hii.

Na wale rafiki zangu waliotafsiri maudhui niliyoyahitaji, kutoka kwenye vitabu vya Kiingereza, ninawashukuru sana.

Mwishoni, ninamshukuru sana mke wangu Hamida Juma Muhammad. Ingawa ni wa mwisho kumtaja, lakini ni wa mwanzo kustahiki shukrani zangu, kwa kunilea mpaka nikamakinika kuifanya kazi hii ambayo imenichukua zaidi ya miaka mitano. Alhamdu lillah.

Ali Jumaa Mayunga

Magomeni Mapipa

Mzimni

Dar es Salaam