92 SUURATUL LAYL

Sura hii imeteremshwa Makka, na ina  Aya 21

Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

1. Naapa kwa usiku unapofunika.

2. Na kwa mchana unapoangaza.

3. Na kwa yule aliyeumba kiume na kike.

4. Hakika amali zenu ni mbali mbali.

5. Lakini anayetoa na kumcha (Mwenyeezi Mungu).

6. Na akalisadiki jambo jema.

7. Basi tutamrahisishia yawe mepesi.

8. Ama Mwenye kufanya ubakhili, akajiona hana haja.

9. Na akalikadhibisha jambo jema.

10. Basi tutamrahisishia kupata taabu.

11. Na mali yake haitamfaa atakapoangamia..

12. Hakika ni juu yetu kuongoza.

13. Na bila shaka, ni yetu sisi Akhera na ulimwengu.

14. Basi nakuhadharisheni na Moto uwakao.

15. Hatauingia ila muovu sana.

16. Ambaye amekadhibisha na kuipa mgongo (dini ya haki).

17. Na amchaye (Mwenyeezi Mungu) ataepushwa nao.

18. Ambaye hutoa mali yake (kwa) kujitakasa.

19. Na hapana yeyote aliyemfanyia hisani ili apate kulipwa.

20. Ila ni kutaka radhi ya Mola wake aliye Mtukufu mno.

21. Na hakika atakuwa radhi.