80 SUURA A'BASA

Sura hii imeteremshwa Makka, na ina Aya 42

Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

1. Alikunja uso na akageuza mgongo.

2. Kwa sababu alimjia kipofu.[1]

3. Na nini kitakujulisha huenda yeye atatakasika.

4. Au atakumbuka na ukumbusho utamfaa?

5. Ama ajionaye hana haja.

6. Wewe ndiye unayemshughulikia.

7. Na si juu yako kama hakutakasika.

8. Lakini anayekukimbilia.

9. Naye anaogopa.

10. Wewe unampuuza.

11. Sivyo, hakika (Qur'an) hii (ni) mawaidha.

12. Basi anayependa atawaidhika.

13. Katika kurasa zilizoheshimiwa.

14. Zilizotukuzwa, zilizotakaswa.

15. Zilizomo mikononi mwa waandishi.

16. Watukufu, wacha Mungu.

17. Ameangamia mtu, mbona anakufuru sana!

18. Kwa kitu gani amemuumba?

19. Kwa tole la manii, amemuumba na akamuwezesha.

20. Kisha akamfanyia njia nyepesi.

21. Kisha akamuua na akamuweka kaburini.

22. Kisha atakapotaka atamfufua.

23. Hapana, hajamaliza aliyomwamuru.

24. Basi mtu atazame chakula chake.

25. Hakika tumemimina maji kwa nguvu.

26. Tena tukaipasuapasua ardhi.

27. Kisha tukaziotesha humo mbegu.

28. Na mizabibu na mboga.

29. Na mizaituni na Mitende.

30. Na bustani zenye miti mingi.

31. Na matunda na malisho.

32. Kwa manufaa yenu na wanyama wenu.

33. Basi itakapokuja sauti ya nguvu.

34. Siku ambayo mtu atamkimbia nduguye.

35. Na Mama yake na Baba yake.

36. Na mkewe na watoto wake.

37. Kila mtu miongoni mwao siku hiyo atakuwa na jambo litakalo mtosha.

38. Siku hiyo nyuso zitanawiri.

39. Zitacheka, zitachangamka.

40. Na nyuso siku hiyo zitakuwa na mavumbi juu yao.

41. Giza zito litazifunika.

42. Hao ndio makafiri, waovu.


[1] Aya 1-2

NANI ALIYEKUNJA USO?

Imepokewa kwa Mwana Aisha anasema: Siku moja, Mtume alikuwa katika kikao na wakubwa wa Kikuraishi akiwamo: Abujahli bin Hisham, Utba bin Rabia, akiwaita katika dini ya Mwenyeezi Mungu. Mara akaja Abdullah bin Ummi Maktum, ambapo Mtume ameshughulika na Makuraishi. Abdullah bin Ummi Maktum akamuuliza (swali) Mtume: Mtume akakunja uso na akageuza mgongo. Ndipo Mwenyeezi Mungu akateremsha Aya 1-2.

Taz: Addurrul Manthur     J.6   Uk.517

Tafsirul Qurtubi J.19 Uk.211

Tafsiri Ibn Kathir J4    Uk. 502

UPEMBUZI JUU YA TUKIO HILI

Sura Abasa, imeteremshwa Makka baada ya Suratun Najmi. Ni sura ya ishirini na nne kwa kuteremshwa, na ni ya themanini kupangwa katika Msahafu.

Taz: Tafsirul Basair   J.52 Uk. 226

a) Sanad za riwaya ya tukio hili zinaongozwa na: Mwana Aisha, Anas na Ibn Abbas. Ambao, wakati zikiteremshwa hizo Aya, miongoni mwao hawajazaliwa. Na wale waliokwisha zaliwa, basi umri wao ni mdogo sana.

Taz: Alhuda ilaa dinil Mustafa    J.l   Uk. 158

 As'Sahih Minsiiratin Nabi     J.2     Uk. 78-83

b) Kukunja uso na kugeuka, si sifa wala tabia ya Mtukufu Mtume

Muhammad s.a.w Mwenyeezi Mungu anamtaja Mtume wake, akihakikisha ubora wa tabia njema aliyo nayo, anasema: "Na bila shaka, una tabia njema kabisa" Aya hii imo katika Suratul Qalam ambayo ni sura ya tatu kushuka kwa Mtume s.a.w kwa hiyo ni sura ya mwanzoni sana, ukilinganisha na sura Abasa, ambayo ni ya ishirini na nne kwa kuteremshwa.

c) Mwenyeezi Mungu anasema: "Na uwaonye jamaa zako walio karibu nn uinamishe bawa lako kwa yule anayekufuata katika Waumini 26:214-215.

Aya hii imeshuka kabla ya A'basa kwa miaka miwili, ndani ya Aya hii kuna amri ya kuinamisha BAWA kwa Waumini, maana yake: "Kuwa Mnyenyekevu."

Limetumiwa neno BAWA kwa njia ya Kinaya kwa mujibu wa elimu ya Bayaan. Kwa maadili yanayopatikana katika Aya chache tulizozitaja juu ya Mtume Muhammad s.a.w yanavunja kabisa na kutupilia mbali madai potovu ya Mwana Aisha na wenzake.

Sasa, nani aliyekunja uso na kugeuka? ni kwamba: Mtume s.a.w alipokuwa ameketi pamoja na maswahaba akiwamo Uthman bin Affan Al'Amawy, na wakubwa wa kikuraishi ambao Mtume alikuwa akiwalingania. Mara akafika Abdullah bin Ummi Maktum, ambaye jina lake kamili anaitwa Abdullah bin Shurayh bin Maalik bin Rabia Alfihry akakaa karibu na Uthman bin Affan, ndipo alipokunja Uthman uso wake na kugeuka. Pale pale Mwenyeezi Mungu akateremsha Aya hizi.

Taz:Tafsirul Basair J.52  Uk. 230

Tafsirus Saafi   J.5    Uk. 284

Almizan fyitafsiril Qur'an  J.20  Uk. 308

Majmaul Bayani fyitafsiril Qur'an  J,5    Uk. 437

 Alburhan fyitafsiril Qur'an   J.4    Uk. 427