76 SUURATUD DAHR

Sura hii imeteremshwa Madina, na ina Aya 31

Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

1. Hakika ulimfikia mtu wakati fulani wa zama ambapo hakuwa kitu kinachotajwa.

2. Kwa hakika tulimuumba mtu kutokana na mbegu ya uhai iliyochanganyika, tunamjaribu, hivyo tukamfanya ni mwenye kusikia, mwenye kuona.

3. Hakika sisi tumemuongoza njia awe mwenye kushukuru au awe mwenye kukufuru.

4.Hakika sisi tumewaandalia makafiri minyororo na mapingu na Moto uwakao.

5.Hakika watawa watakunywa katika kikombe kilichochanganyika na kafuri.

6.(Itakuwako) chemchem watakayoinywa waja wa Mwenyeezi Mungu, wataitiririsha mtiririko (mzuri).

7.Wanazitimiza nadhiri na wanaiogopa siku ambayo shari yake itaenea.

8.Na huwalisha chakula masikini na yatima na mfungwa hali ya kuwa wanakipenda.[1]

9.(Husema) Tunakulisheni kwa ajili ya radhi ya Mwenyeezi Mungu tu, hatutaki kwenu malipo wala shukurani.

10.Hakika sisi tunaogopa kutoka kwa Mola wetu siku yenye shida na taabu.

11.Basi Mwenyeezi Mungu atawalinda katika shari ya siku hiyo na kuwakutanisha na neema na furaha.

12.Na atawapa Mabustani na hariri kwa sababu walisubiri.

13.Humo wataegemea viti vya enzi humo hawataona jua (kali) wala baridi (kali).

14. Na vivuli vyake vitafikia karibu yao na matunda yataning'inia chini chini.

15. Na watapitishiwa vyombo vya fedha na vikombe vya vigae.

16. Vigae vya fedha, wamevifanya kwa vipimo.

17. Na humo watanyweshwa kikombe kilichochanganyika na tangawizi.

18. Humo mna chemchem inayoitwa salsabil.

19. Na watawazungukia wavulana wasiochakaa, utakapowaona utawafikiri ni lulu zilizotawanywa.

20. Na utakapoyaona humo utaona neema na ufalme mkubwa.

21. Juu yao (watavaa) nguo za hariri laini ya kijani kibichi na za hariri nzito, na watavikwa bangili za fedha na Mola wao atawanywesha kinywaji safi.

22. Hakika haya ni malipo yenu, na juhudi yenu imekubaliwa.

23. Hakika sisi tumekuteremshia Qur'an sehemu sehemu.

24. Basi ngojea hukumu ya Mola wako wala usimtii miongoni mwao mwenye dhambi au mwenye kufru.

25. Na litaje jina la Mola wako asubuhi na jioni.

26. Na usiku msujudie yeye, na umtukuze usiku (wakati) mrefu.

27. Kwa hakika hawa wanayapenda wayapatayo upesi, na huiacha nyuma yao siku nzito.

28. Sisi tumewaumba na tukaimarisha viungo vyao, na tutakapotaka tutawaleta wengine badala yao walio kama wao.

29. Hakika huu ni ukumbusho basi anayetaka ashike njia kwa Mola wake.

30. Wala hamuwezi kutaka asipotaka Mwenyeezi Mungu, hakika Mwenyeezi Mungu ni Mwenye elimu, Mwenye hekima.

31. Anamwingiza anayemtaka katika rehema yake, na madhalimu amewawekea dhabu yenye kuumiza.


[1] Aya 7-8

AHLUL BAYT WAMETIMIZA NADHIRI YAO

Imepokewa kwa Abdallah bin Abbas anasema:

Walipatwa na maradhi, Hasan na Husein (a.s) ikawa babu yao Mtume s.a.w anakwenda kuwaona. Imam Ali (a.s) akashauriwa aweke nadhiri kwa ajili ya watoto wake, Akasema Imam Ali (a.s): Ikiwa watapoa basi atafunga siku tatu kwa kumshukuru Mwenyeezi Mungu, Mwana Fatima (a.s) naye akasema hivyo hivyo. Mtumishi wao Fadh-dhatu akasema: Ikiwa watapoa mabwana wangu, basi nitafunga siku tatu kwa kumshukuru Mwenyeezi Mungu. Muda mfupi Mwenyeezi Mungu akawapoza, na nyumbani mwao hakuna chakula. Imam Ali (a.s) akaenda kwa Sham'un Alkhaybary, kuazima pishi tatu za ngano, Mwana Fatima (a.s) akachukua pishi moja akaiandaa, tayari mkate kwa chakula. Imam Ali (a.s) alipomaliza kuswali pamoja na Mtume s.a.w akaingia nyumbani mwake kikaandaliwa chakula, mara masikini akafika mlangoni kwao, akagonga mlango akasema: Amani juu yenu (enyi) watu wa nyumba ya Muhammad (mimi) masikini katika watoto wa Kiislamu nipeni chakula Mwenyeezi Mungu atakupeni chakula cha Peponi.

Imam Ali akamsikia, akaamrisha apewe chakula chote (kilichokuwa kimeandaliwa hapo) siku hiyo wakakaa kutwa kucha hawana walichokula isipokuwa maji. Siku ya pili, Mwana Fatima akachukua pishi moja akaiandaa, tayari mkate kwa chakula. Imam alipomaliza kuswali pamoja na Mtume s.a.w akaingia ndani kikaandaliwa chakula, mara yatima akafika mlangoni kwao, akagonga mlango akasema: Amani juu yenu (enyi) watu wa nyumba ya Mtume Muhammad (mimi ni) yatima ni katika watoto wa Muhajirina, mzazi wangu ameuliwa vitani, naomba chakula. Akapewa chakula chote. Wakabaki hiyo siku ya pili bila ya kutia chochote vinywani mwao ila maji tu.

Siku ya tatu, Mwana Fatima (a.s) akachukua pishi iliyobaki katika zile pishi tatu alizoleta mumewe. Akaiandaa, tayari mkate kwa chakula. Baada ya kumaliza kuswali Imam Ali (a.s) pamoja na Mtume s.a.w akaingia ndani, kikaandaliwa chakula. Mara mf'ungwa akafika mlangoni kwao, akagonga mlango akasema: Amani juu yenu (enyi) watu wa nyumba ya Mtume, wameniteka na kunifunga na kuninyima chakula! Nipeni chakula, wakampa chakula chote, wakashinda siku ya tatu usiku kucha na mchana kutwa, hawana chakula ila maji tu. Ndipo Mtume s.a.w alipokwenda akaikuta hali hiyo! Mwenyeezi Mungu akamteremshia Mtume wake Aya 7-8.

Taz: Tafsirul Basair J.51 Uk. 7

Tafsirul Qurtubi   J.19 Uk. 130

Shawahidut Tanzil     J.2  Uk.299

Usudul Ghaba   J.5  Uk. 530

Addurul Manthur  J.6  Uk. 485

Tafsirul Khazin   J.7  Uk. 191

Tafsirul Kabir   J.30 Uk. 243

Tafsirul kashshaf   J.4  Uk. 197