73 SUURATUL MUZZAMMIL

Sura hii imeteremshwa Makka, na ina Aya 20

Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

1. Ewe uliyejifunika nguo.

2. Simama usiku ila kidogo.

3. Nusu yake au ipunguze kidogo.

4. Au izidishe na soma Qur'an kwa vizuri.

5. Hakika sisi hivi karibuni tutakutilia kauli nzito.

6. Hakika kuamka usiku (kwa ibada) ni bora zaidi kwa kukanyaga (nafsi) na vizuri zaidi kutamka.

7. Hakika mchana una shughuli nyingi.

8. Na litaje jina la Mola wako na ujitupe kwake kwa kweli.

9. (Yeye ndiye) Mola wa mashariki na magharibi, hakuna aabudiwaye ila Yeye tu, basi mfanye kuwa mlinzi.

10. Na subiri juu ya hayo wasemayo na uwaepuke mwepuko mwema.

11. Na niache mimi na wanaokadhibisha walioneemeka na uwape muda kidogo.

12. Hakika tunazo adhabu na Moto uwakao.

13. Na chakula kikwamacho kooni na adhabu yenye kuumiza.

14. Siku ardhi na milima vitakapotetemeka, na milima itakuwa kama mkusanyiko wa mchanga.

15. Hakika sisi tumekuleteeni Mtume aliye shahidi juu yenu, kama tulivyompeleka Mtume kwa Firaun.

16. Lakini Firaun alimuasi Mtume, basi tukamtesa mateso makubwa.

17. Basi nyinyi mkikufuru, mtawezaje kujikinga na siku ambayo itawafanya watoto kuwa wazee.

18. Mbingu zitapasuka (siku) hiyo ahadi yake itakuwa imetimizwa.

19. Kwa hakika hii (Qur'an) ni mawaidha, basi anayetaka atajifanyia njia kwa Mola wake.

20. Kwa hakika Mola wako anajua kuwa wewe husimama (kumwabudu) karibu na thuluthi mbili za usiku, na (pengine) nusu yake, na (wakati mwingine) thuluthi yake, na baadhi ya watu walio pamoja nawe. Na Mwenyeezi Mungu huupima usiku na mchana, anajua kuwa hamuwezi kufanya hivyo, basi amekusameheni, kwa hiyo, someni yaliyo mepesi katika Qur'an. Anajua kuwa baadhi yenu watakuwa wagonjwa na wengine watasafiri katika ardhi wakitafuta fadhili ya Mwenyeezi Mungu, na wengine watapigana katika njia ya Mwenyeezi Mungu, kwa hiyo someni yaliyo mepesi humo, na simamisheni swala na toeni zaka, na mkopesheni Mwenyeezi Mungu mkopo mwema. Na kheri yoyote mnayoitanguliza kwa ajili ya nafsi zenu mtaipata kwa Mwenyeezi Mungu imekuwa bora zaidi na ina malipo makubwa sana. Na ombeni msamaha kwa Mwenyeezi Mungu, hakika Mwenyeezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.