71 SUURA NUUH

Sura hii imeteremshwa Makka, na ina Aya 28

Kwa jina la Mweayeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

1. Hakika sisi tulimtuma Nuhu kwa watu wake, kwamba, waonye watu wako kabla ya kuwafikia adhabu yenye kuumiza.

2. Akasema: Enyi watu wangu! kwa hakika mimi ni Muonyaji dhahiri kwenu.

3. Kuwa; Mwabuduni Mwenyeezi Mungu na mcheni na mtiini.

4. Atakusameheni madhambi yenu na atakuakhirisheni mpaka muda uliowekwa, hakika ifikapo ajali itokayo kwa Mwenyeezi Mungu haizuiliki, laiti mungejua.

5. Akasema: Ee Mola wangu! kwa hakika nimewaita watu wangu usiku na mchana.

6. Lakini mwito wangu haukuwazidishia ila kukimbia.

7. Na kila mara nilipowaita uwasamehe, waliziba masikio yao kwa vidole vyao, na walijifunika nguo zao na walizidi kuendelea na kufru na wakafanya kiburi kingine.

8. Tena niliwaita kwa sauti kubwa.

9. Kisha nikawatangazia na nikasema nao kwa siri.

10. Nikawaambia: Ombeni msamaha kwa Mola wenu, hakika yeye ni Mwingi wa kusamehe.

11. Atakuleteeni mawingu yanyeshayo mvua nyingi.

12. Na atakupeni mali na watoto, na atakupeni mabustani, na atakufanyieni mito.

13. Mmekuwaje hamuweki heshima kwa Mwenyeczi Mungu.

14. Na hali yeye amekuumbeni namna mbalimbali?

15. Je, hamuoni jinsi Mwenyeezi Mungu alivyoziumba mbingu saba tabaka tabaka.

16. Na akaufanya mwezi ndani yake uwe nuru na akalifanya jua kuwa taa?

17. Na Mwenyeezi Mungu amekuotesheni katika ardhi (kama) mimea.

18. Kisha atakurudisheni humo na atakutoeni tena.

19. Na Mwenyeezi Mungu amekufanyieni ardhi kuwa tandiko.

20. Ili mtembee humo katika njia zilizo pana.

21. Nuhu akasema: Mola wangu! hakika hao wameniasi na wamewafuata ambao mali yao na watoto wao hawakuwazidishia ila khasara tu.

22. Na wakafanya hila kubwa.

23. Na wakasema: Msiache miungu yenu, wala msimwache Waddi wala Suwaa wala Yaghutha wala Yau'ka wala Nasra.

24. Nao wamekwisha poteza (watu) wengi wala usiwazidishie madhalimu ili kupotea (zaidi).

25. Kwa ajili ya makosa yao waligharikishwa wakaingizwa Motoni, wala hawakupata wasaidizi kinyume cha Mwenyeezi Mungu.

26. Na Nuhu akasema: Mola wangu! usiache juu ya ardhi mkazi yeyote katika makafiri.

27. Hakika ukiwaacha watapoteza watu wako, wala hawatazaa ila (watoto) waovu wenye kufru.[1]

28. Mola wangu! nisamehe mimi na wazee wangu, na kila aliyeingia nyumbani mwangu hali ya kuamini, na Waumini wanaume na Waumini wanawake, wala usiwazidishie madhalimu ila maangamizo.


[1] Aya 27

 Iliposemwa: "Wala hawatazaa ila (watoto) waovu wenye kufru."

Kwa desturi, binadamu anapozaliwa hawi kafiri wala muovu, bali huwa ni kiumbe safi. Mpaka akifikia umri wa miaka ya baleghe (kwa wastani ni miaka kumi na mitano) Ndipo Sharia itamuwajibikia kwa hali zote.

Kwa hiyo, usluubu uliotumika katika Aya hii, iliposemwa: "Hawatazaa ila (watoto) waovu wenye kufru" ni katika, Majaz Mursal: litibaar Ma yakuun.