63 SUURATUL MUNAFIQUUN

Sura hii imeterecashwa Madina, na ina Aya 11

Kwa jina la Mweayeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

1. Wanapokujia wanafiki, husema: Tunashuhudia ya kuwa, kwa hakika wewe ni Mtume wa Mwenyeezi Mungu, na Mwenveezi Mungu anajua kwa hakika wewe, ni Mtume wake, na Mwenyeezi Mungu anashuhudia ya kuwa, kwa hakika wanafiki ni waongo hasa.

2. Wamevifanya viapo vyao ngao, wakaiacha njia  ya Mwenyeezi Mungu, kwa hakika ni mabaya waliyokuwa wakifanya.

3. Hayo ni kwa sababu waliamini kisha wakakufuru, kwa hiyo muhuri umepigwa juu ya nyoyo zao nao hawafahamu.

4. Na unapowaona, miili yao inakupendeza, na kama wakisema. unasikiliza usemi wao, wao ni kama boriti zilizotengenezwa, wanadhani kila kishindo ni juu yao, wao ni maadui jihadharini nao, Mwenyeezi Mungu awaangamize, vipi wanageuzwa.

5. Na wanaambiwa: Njooni, Mtume wa Mwenyeezi Mungu atakuombeeni msamaha huvigeuza vichwa vyao, na unawaona wanajizuia na wakijiona wakubwa.

6. Ni sawa kwao ukiwatakia msamaha au usiwatakie msamaha. Mwenyeezi Mungu hatawasamehe, hakika Mwenyeezi Mungu hawaongozi watu waasi.

7.Wao ndio wanaosema: Msitoe mali kwa ajili ya wale walioko kwa Mtume wa Mwenyeezi Mungu mpaka waondoke. Na khazina za mbingu na ardhi ni za Mwenyeezi Mungu lakini wanafiki hawafahamu.

8. Wanasema: Tukirudi Madina, mwcnye utukufu atamfukuza mnyonge, na utukufu hasa ni wa Mwenyeezi Mungu na Mtume wake wa Waumini lakini wanafiki hawajui.

9. Enyi mlioamini! yasikusahaulisheni mali yenu wala watoto wenu kumkumbuka Mwenyeezi Mungu, na wafanyao hayo, basi hao ndio wenye khasara.

10. Na toeni katika yale tuliyokupeni kabla mmoja wenu hayajamfikia mauti, kisha aseme: Mola wangu! mbona hukuniakhirisha muda kidogo nikatoa sadaka na nikawa miongoni mwa watendao wema?

11. Lakini Mwenyeezi Mungu hataiakhirisha nafsi yoyote inapofika ajali yake, na Mwenyeezi Mungu anazo khabari za mnayoyatenda.