60 SUURATUL MUMTAHINAH

Sura hii imeteremshwa Madina,na ina Aya 13

Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

1. Enyi mlioamini! msiwafanye adui zangu na adui zenu kuwa marafiki, mnawapelekea (khabari) kwa ajili ya urafiki hali wamekwisha kataa haki iliyokufikieni, wakamfukuza Mtume na nyinyi pia, kwa sababu mnamwamini Mwenyeezi Mungu Mola wenu. Kama mnaondoka kufanya jihadi katika njia yangu na kuitafuta radhi yangu mnawapa siri (zenu) kwa ajili ya mapenzi, nami najua sana mnayoyaficha na mnayoyadhihirisha, na anayefanya hayo miongoni mwenu, basi amekwishapotea njia iliyo sawa.

2. Kama wakikukuteni watakuwa maadui zenu, na wanakukunjulieni mikono yao na ndimi zao kwa uovu, na wanapenda kama mkikufuru.

3. Hawatakufaeni jamaa zenu wala watoto wenu siku ya Kiyama, atahukumu baina yenu, na Mwenyeezi Mungu anaona mnayoyatenda.

4. Hakika nyinyi mna mfano mzuri kwa Ibrahimu na wale waliokuwa pamoja naye, walipowaambia watu wao: Kwa hakika sisi tu mbali nanyi na hayo mnayoyaabudu kinyume cha Mwenyeezi Mungu, tunakukataeni, na umekwishadhihiri uadui na bughudha ya daima kati yenu na yetu mpaka mtakapomwamini Mwenyeezi Mungu peke yake, isipokuwa kauli ya Ibrahimu kwa baba yake. Hakika nitakuombea msamaha, wala sina uwezo wa chochote kwa ajili yako mbele ya Mwenyeezi Mungu. Mola wetu! tumetegemea kwako, na tumegeukia kwako, na kwako ni marejeo.

5. Mola wetu! usitufanye mtihani kwa waliokufuru, na tusamehe Mola wetu! hakika wewe ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima.

6. Bila shaka umekuwa mfano mzuri kwenu katika mwendo wao, kwa anayemuogopa Mwenyeezi Mungu na siku ya Mwisho na anayeyapuuza (haya) basi kwa hakika Mwenyeezi Mungu ni Mkwasi, Mwenye kusifiwa.

7. Huenda Mwenyeezi Mungu akaweka mapenzi kati yenu na wale ambao mnawaona kuwa maadui miongoni mwao, na Mwenyeezi Mungu ni Muweza, na Mwenyeezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.

8. Mwenyeezi Mungu hakukatazini kuwafanyia ihsani na uadilifu wale ambao hawakupigana nanyi kwa ajili ya dini wala hawakukufukuzeni katika nchi zenu. Hakika Mwenyeezi Mungu anawapenda wenye kufanya uadilifu.

9. Mwenyeezi Mungu anakukatazeni na wale ambao wanapigana nanyi katika dini, na kukufukuzeni katika nchi zenu, na wanasaidia katika kufukuzwa kwenu, (anakukatazeni) kuwafanya marafiki, na wawafanyao marafiki, basi hao ndio madhalimu.

10. Enyi mlioamini! watakapokufikieni wanawake walioamini wanaohama. basi wajaribuni, Mwenyeezi Mungu ndiye ajuaye zaidi imani yao, kama mkijua kuwa wao ni waumini basi msiwarudishe kwa makafiri, (wanawake) hawa si halali kwao, wala wao (wanaume makafiri) si halali kwao, na warudishieni (waume zao) mali walizotoa. Wala si hatia kwenu kuwaoa ikiwa mtawapa mahari yao, wala msiwaweke wanawake makafiri katika kifungo cha ndoa zenu, na ombeni mliyoyatoa, nao waombe walivyovitoa. Hiyo ndiyo hukumu ya Mwenyeezi Mungu anayo kuhukumuni, na Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye hekima.

11. Na kama akitoroka yeyote katika wake zenu kwenda kwa makafiri tena ikatokea bahati (ya kupata mateka) basi wapeni wale ambao wake zao wametoroka, kiasi cha mahari waliyotoa, na mcheni Mwenyeezi Mungu ambaye mnamwamini.

12. Ewe Nabii! watakapokujia wanawake Waumini wanakuahidi kuwa, hawatamshirikisha Mwenyeezi Mungu na chochote, wala hawataiba, wala hawatazini, wala hawatawaua watoto wao, wala hawataleta uzushi waliouzusha baina ya mikono yao na miguu yao, wala hawatakuasi katika jambo jema, basi peana ahadi nao na uwatakie msamaha kwa Mwenyeezi Mungu hakika Mwenyeezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.

13. Enyi mlioamini! msifanye urafiki na watu ambao Mwenyeezi Mungu amewakasirikia, maana wamekata tamaa ya Akhera kama vile makafiri walivyowakatia tamaa watu wa makaburini.