56 SUURATUL WAAQI'A

Sura hii imeteremshwa Makka,na ina  Aya 96

Kwajina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehenaa, Mwenye kurehemu.

1. (Wakumbushe) litakapotokea tokeo.

2. Hapana cha kukanusha kutokea kwake.

3. Lifedheheshalo. Litukuzalo.

4. Ardhi itakapotetemeshwa tetemesho.

5. Na milima itakaposagwasagwa.

6. Ndipo itakuwa mavumbi yanayopeperushwa.

7. Na nyinyi mtakuwa namna tatu.

8, Basi watu wenye kheri, watakuwa namna gani wenye kheri.

9. Na watu wenye shari, watakuwa namna gani wenye shari.

10. Waliotangulia ndio waliotangulia.

11. Hao ndio watakaokaribishwa.

12. Katika Bustani zenye neema.

13. Jamii kubwa ni miongoni mwa (watu) wa kwanza.

14. Na jamii ndogo ni miongoni mwa (watu) wa mwisho.

15. (Watakuwa) juu ya viti vya fahari vilivyo pangwa.

16. Wataviegemeza wakielekeana.

17. Watawazunguka zunguka wavulana wasiochakaa.

18. Kwa vikombe na mabirika na gilasi za kinywaji safi.

19. Hawataumwa na vichwa kwa kunywa (kinywaji) hicho wala hawatalewa.

20. Na matunda watakayoyapenda.

21. Na nyama ya ndege watakayoitamani.

22. Na wanawake weupe wenye macho mazuri.

23. Yatakayokuwa kama lulu zilizofichwa.

24. Ni malipo kwa hayo waliyokuwa wakiyatenda.

25. Humo hawatasikia upuuzi wala maneno ya dhambi.

26. Isipokuwa itasemwa: Amani amani.

27. Na watu wa kheri, watakuwa namna gani watu wa kheri.

28. (Watakuwa) katika mikunazi isiyo na miiba.

29. Na migomba iliyopambwa na matunda.

30. Na kivuli kilichotandazwa.

31. Na maji yanayomiminika.

32. Na matunda mengi ( ya kila aina)

33. Hayakatiki wala hayakatazwi.

34. Na wanawake watukufu.

35. Kwa hakika tumewaumba (wanawake) kwa umbo (bora).

36. Na tukawafanya ndio kwanza wanaolewa.

37. Wanaopendana na waume zao.

38. Kwa ajili ya watu wa kuliani.

39. Jamii kubwa ni miongoni mwa (watu) wa kwanza.

40. Na jamii kubwa ni miongoni mwa (watu) wa mwisho.

41. Na watu wa shari, watakuwa namna gani watu washari.

42. Watakuwa katika upepo wa moto na maji yachemkayo.

43. Na kivuli cha moshi mweusi sana.

44. Si baridi wala si starehe.

45. Bila shaka wao walikuwa kabla ya hayo wakiishi maisha ya anasa.

46. Na walikuwa wakishikilia (kufanya) dhambi kubwa.

47. Na walikuwa wakisema: Tutakapokufa na tutakuwa udongo na mifupa, je, tutafufuliwa?

48. Au baba zetu wa zamani?

49. Sema: Bila shaka wa kwanza na wa mwisho.

50. Watakusanywa kwa wakati uliowekwa katika siku maalumu.

51. Kisha nyinyi, enyi mliopotea (na) kukadhibisha.

52. Kwa hakika mtakula mti wa zakkum.

53. Na kwa huo mtajaza matumbo.

54. Na juu yake mtakunywa maji yachemkayo.

55. Tena mtakunywa kama anywavyo ngamia mwenye kiu sana.

56. Hii ni karamu yao siku ya malipo.

57. Sisi tumekuumbeni, basi mbona hamsadiki?

58. Je, mmeiona mbegu ya uzazi mnayoidondokeza?

59. Je, mnaiumba nyinyi au tunaiumba sisi?

60. Sisi tumekuwekeeni kati yenu mauti na sisi hatuwezi kushindwa.

61. Kuwaleta wengine badala yenu na kukuumbeni katika umbo msilolijua.

62. Na bila shaka nyinyi mnajua umbo la kwanza, tena mbona hamkumbuki.

63. Je, mmeiona mnayoilima?

64. Je, nyinyi mmeiotesha au tumeiotesha sisi?

65. Tungelitaka tungelivunja vunja ndipo mngenung'unika.

66. Hakika sisi tumegharamika.

67. Bali sisi tumenyimwa.

68. Je, mmeyaona maji ambayo mnayanywa?

69. Je, mmeyateremsha nyinyi mawinguni au tumeyateremsha sisi?

70. Tungelitaka tungeliyafanya makali basi mbona hamshukuru?

71. Je, mmeuona moto ambao mnauwasha?

72. Je, mti wake mmeuumba nyinyi au sisi ndio tuliouumba?

73. Sisi tumeufanya kuwa ukumbusho na manufaa kwa wenye kusafiri.

74. Basi litukuze jina la Mola wako aliye Mkuu.

75. Basi ninaapa kwa maanguko ya nyota.

76. Na hakika hicho bila shaka ni kiapo kikubwa, laiti mngelijua.

77. Bila shaka hii ni Our'an yenye heshima.

78. Katika Kitabu kinachohifadhiwa.

79. Hapana atakayeigusa ila waliotakaswa.

80. Ni uteremsho utokao kwa Mola wa walimwengu.

81. Je, mnaibeza hadithi hii?

82. Na mnafanya kuikadhibisha kuwa pato lenu.

83. Basi mbona (roho) ifikapo kooni.

84. Na nyinyi wakati huo mnatazama.

85. Nasi tunakaribiana nayo zaidi kuliko nyinyi, wala nyinyi hamuoni.

86. Kama nyinyi si katika mamlaka ya wengine.

87. Kwa nini hamuirudishi, ikiwa mnasema kweli?

88. Basi akiwa ni miongoni mwa wale waliokaribishwa.

89. Basi ni raha na manukato na Bustani yenye neema.

90. Na kama akiwa ni miongoni mwa watu wa kheri.

91. Basi (ataambiwa): Salama kwako, (ewe uliye) miongoni mwa watu wa kheri.

92. Na kama mkiwa ni miongoni mwa waliokadhibisha, wapotovu.

93. Basi karamu (yake) ni maji ya moto yachemkayo.

94. Na kuwaka Motoni.

95. Bila shaka hii ndiyo haki yenye yakini.

96. Basi litukuze jina la Mola wako Mwenye utukufu.