53 SUURATUN NAJMI

Sura hii imeteremshwa Makka, Aya 62.

Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

1. Naapa kwa nyota inapoanguka.

2. Kwamba mtu wenu hakupotea wala hakukosa.

3. Wala hasemi kwa tamaa (ya nafsi yake).

4. Hayakuwa haya ila ni Wahyi uliofunuliwa.

5. Amemfundisha Mwenye nguvu sana.

6. Mwenye uwezo, naye akastawi.

7. Naye yu katika upeo wa juu kabisa.

8. Kisha akakaribia, na akateremka.

9. Ndipo akawa umbali wa pinde mbili au karibu zaidi.

10. Na akamfunulia mja wake aliyoyafunua.

11. Moyo haukusema uongo uliyoyaona.

12. Je, mnabishana naye juu ya yale aliyoyaona?

13. Na bila shaka yeye amemuona (Jibril) kwa mara nyingine (katika sura ya kimalaika).

14. Penye mkunazi wa mwisho.

15. Karibu yake pana Bustani inayokaliwa.

16. Kilipoufunika mkunazi kilichofunika.

17. Jicho (lake) halikuhangaika wala halikuruka mpaka.

18, Kwa hakika aliona katika dalili za Mola wake zilizo kuu.

19. Je, mmewaona Lata na Uzza?

20. Na Manata, mwingine wa tatu?[1]

21. Je, nyinyi mna watoto wa kiume na yeye ana watoto wa kike?

22. Huo tena ni mgawanyo mbaya.

23. Hayakuwa haya ila ni majina mliyowapa nyinyi na baba zenu, Mwenyeezi Mungu hakuteremsha dalili juu yao. Hawafuati ila dhana na zinayoyapenda nafsi (zao) na kwa hakika muongozo umewafikia kutoka kwa Mola wao.

24. Je, mwanadamu anaweza kupata kila anachotamani?

25. Lakini mwanzo na mwisho ni wa Mwenyeezi Mungu.

26. Na wako Malaika wangapi mbinguni ambao uombezi wao hautafaa chochote isipokuwa baada ya Mwenyeezi Mungu kutoa idhini kwa amtakaye na kumridhia.

27. Hakika wale wasioamini Akhera wanawaita Malaika kwa majina ya kike.

28. Nao hawana elimu ya haya, hawafuati ila dhana, na kwa hakika dhana haisaidii chochote mbele ya haki.

29. Basi jiepushe na yule aupaye kisogo ukumbusho wetu na wala hataki ila maisha ya dunia.

30. Huo ni mwisho wao katika elimu, hakika Mola wako ndiye amjuaye sana anayepotea njia yake, na ndiye amjuaye sana anayeongoka.

31. Na ni vyake Mwenyeezi Mungu vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini, ili awalipe wale waliofanya ubaya kwa yale waliyoyatenda, na kuwalipa mema wale waliofanya mema.

32. Ambao wanajiepusha na madhambi makuu na vitendo vibaya isipokuwa makosa hafifu, bila shaka Mola wako ndiye Mwenye msamaha mkubwa. Yeye ndiye anayekujueni sana tangu alipokuumbeni katika ardhi na mlipokuwa mimba matumboni mwa mama zenu, basi msijitakase nafsi zenu, yeye anamjua sana anayetakasika.

33. Je, umemuona yule aliyegeuka?

34. Na akatoa kidogo kisha akajiziwia.

35. Je, anayo elimu ya yasioonekana na akayona?

36. Au hakuambiwa yaliyomo katika Vitabu vya Musa?

37. Na vya Ibrahimu aliyetimiza ahadi.

38. Kwamba habebi mbebaji mzigo wa mwingine.

39. Na kwamba mtu hatapata ila yale aliyoyafanya.

40. Na kwamba amali yake itaonekana.

41. Kisha atalipwa malipo yaliyo kamili.

42. Na kwamba mwisho ni kwa Mola wako.

43. Na kwamba yeye ndiye anayechekesha na kuliza.

44. Na kwamba yeye ndiye afishaye na kuhuisha.

45. Na kwamba yeye ndiye aliyeumba dume na jike.

46. Katika mbegu ya uzazi inapotiwa.

47. Na kwamba juu yake ufufuo mwingine.

48. Na kwamba yeye ndiye atajirishaye na atiaye umasikini.

49. Na kwamba yeye ndiye Mola wa (nyota) ya Shi-iraa.

50. Na kwamba yeye ndiye aliyewaangamiza Adi wa kwanza.

51. Na Thamudi, hakuwabakisha.

52. Na kabla (yao) watu wa Nuhu, hakika wao walikuwa madhalimu na waasi sana.

53. Na miji iliyopinduliwa ndiye aliyeiangusha.

54. Vikaifunika vilivyoifunika.

55. Basi neema gani ya Mola wako unayoifanyia shaka?

56. Huyu ni Muonyaji miongoni mwa Waonyaji wa zamani.

57. Tukio lililo karibu linasogea.

58. Hakuna awezaye kuliondoa ila Mwenyeezi Mungu.

59. Je, mnaistaajabia hadithi hii?

60. Na mnacheka wala hamlii?

61. Na hali nyinyi mmeghafilika?

62. Basi msujudieni Mwenyeezi Mungu na Mumuabudu.


[1] Aya 19-20

TUKIO LA GHARAANIIQ

Inasimuliwa kuwa: Waislaamu baada ya kuhamia Ithiopia kwa miezi miwili hivi, siku moja Mtume (s.a.w) alikuwa ameketi akiwa na baadhi ya maswahaba pamoia na makafiri, mara Mwenyeezi Mungu akateremsha Suuratun Najmi. Mtume (s.a.w) akaisoma, hata alipofikia Aya: Je, mmewaona Lata na Uzza na Manata mwingine wa tatu? Shetani akamnong'oneza matamko mawili, akayasema akifikiri ni sehemu ya Wahyi, nayo ni: "Hao ni waungu watukufu, na kwamba maombezi yao bila shaka yanatarajiwa." Mtume(s.a.w) akaendelea kusoma Aya katika Suuratun Najmi mpaka alipofikia Ayatus Sijda, akasujudu, na Waislamu nao wakasujudu pamoja naye. Makafiri walipoona, kwa vile Muhammad amewasifu masanamu wao kwa sifa ya uungu, nao wakaporomoka (wakasujudu) pamoja na Waislaamu. Lakini Walid bin Mughira hakuweza kusujudu, kwa hiyo, alichofanya ni kuchukua mchanga na kuweka kwenye paji lake. Wengine wanasema: aliyefanya hivyo ni Said bin Al'a's, wengine wanasema: Ni hao wote wawili. Na wengine wanasema:

Ni Umayya bin Khelef............. Madai haya yanatiliwa nguvu kwa Aya

wanayoisema kuwa imeshuka kwa mnasaba wa tukio hili. "Na hatukumtuma kabla yako Mtume wala Nabii ila anaposoma, shetani alitia (fitna) katika masomo yake. Lakini Mwenyeezi Mungu huondoa anayoyatia shetani, kisha Mwenyeezi Mungu huzimakinisha Aya zake, na Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye hekima."

MAJIBU YETU:

Dhana hii potovu inajibiwa haraka katika sura hiyo hiyo kuwa: “Wala hasemi kwa tamaa (ya nafsi yake): Hayakuwa haya (anayosema) ila ni Wahyi uliofunuliwa.”

Anasema Abdallah bin Amri:

"Nilikuwa nikiandika kila kitu ninachokisikia kwa Mtume wa Mwenyeezi Mungu ili nikihifadhi, Makuraishi wakanikataza, wakasema: Wewe unaandika kila kitu unachokisikia kwa Mtume? na Mtume ni binadamu, anazungumza (wakati mwingine) katika hali ya ghadhabu, basi nikaacha kuandika, na nikamjulisha hili Mtume (s.a.w) akasema:

Andika, namuapa ambaye nafsi yangu imo katika milki yake chochote kinachotoka kwangu ni haki tu."

Taz: Tafsir Ibn Kathir J.4  Uk. 264

 Tafsiirul Maragy       J.27 Uk. 45

Mwenyeezi Mungu anasema: "Na kama (Mtume) angelizua juu yetu baadhi ya maneno, lazima tungelimshika kwa mkono wa kulia, kisha kwa hakika tungelimkata mshipa mkubwa (wa moyo) 69:44-46.

Ama, kuhusu Aya ya 52 ya Sura 22 inayodaiwa kutia nguvu madai hayo potovu, tunasema: Suratul Hajji imeteremshwa Madina, na kisa hiki (Al'gharaaniiq) kilitokea Makka.'Katika mwaka wa tano wa Biitha (kupewa Utume) Sasa, unaweza kuona tofauti kubwa iliyoko! Mtume Muhammad (s.a.w) aliishi Makka baada ya kupewa Utume, miaka kumi na mitatu kabla ya kuhamia Madina. Kwa hiyo, baada ya tukio la Gharaaniiq, pana miaka minane kabla ya kushuka Aya iliyoko katika Suratul Hajji.

Suuratun Najmi imeteremshwa Makka katika mwaka wa tano wa Biitha, baada ya Suuratul Ikhlas na kabla ya Suura 'Abasa. Ni Sura ya ishirini na tatu kushuka, na ni Sura ya hamsini na tatu kupangwa katika Msahafu.

Taz: Tafsirul Basair   J. 42 Uk. 10

Aidha, sanadi za riwaya hiyo potovu zinadaiwa kuongozwa na:

(a)Abdullah bin 'Abbas, aliyezaliwa mwaka wa tatu kabla Mtume hajahamia Madina.

(b) Abul 'Aaliya Rafii bin Mahran, aliyesilimu baada ya kufariki Mtume (s.a.w).

(c) Abdur Rahman bin Alharithi, aliyezaliwa katika awamu ya pili (kipindi cha Umar).

(d) Abul Hajjaj Mujahid bin Jabru Al Makiyyi, aliyezaliwa mwaka 21 Hijria.

(e) Muhammad bin Saad (Yahudi) aliyezaliwa mwaka 40 Hijria.

(f ) Dhahhak bin Mazaahim, aliyezaliwa mwaka 105 Hijria.

 (g) Muhammad bin Qays, aliyezaliwa mwaka 126 Hijria.

(h) Abu Muhammad Ismail bin Abdur Rahman As Sudy, aliyezaliwa mwaka 127 Hijria.

Hawa wote, hakuna aliyeshuhudia tukio hilo.

Taz: Alquran Wariwayatul Madrasatayn  J. 2 Uk. 627-631

Kwa hiyo, kutokana na tarekh ya kushuka kwa sura hii, na uchambuzi wa sanadi za riwaya yake, madai yaliyotajwa hapo juu yanakosa mashiko. Lakini, zaidi ya hayo, laana ya Mwenyeezi Mungu imshukie yeyote anayezua uongo juu ya Mwenyeezi Mungu, na juu ya Mtume wake Muhammad s.a.w.

Ukweli ulivyo: Makafiri walimwandama Mtume ili waizime Qur'an isisomwe, wakatumia kila hila kama anavyoyaweka wazi haya Mwenyeezi Mungu. “Na walisemawaliokufuru: Msisikilize Qur'an hii na ipigieni makelele (isomwapo) huenda mtashinda.” 41:26.

1323

Kwa hiyo, Mtume( s.a.w ) aliposoma Suratun Najmi akafika katika Aya: Je, mmewaona Lata na Uzza na Manata mwingine wa tatu? mara makafiri wakasema: "Hao ni waungu watukufu, na kwamba maombezi yao bila shaka yanatarajiwa."

Kwa kuwa Aya ya mwisho ya Suratun Najmi ni Ayatus Sajda, Ambayo inatakikana kwa Mwenye kusoma Our'an, akifika katika Aya ya namna hii asujudu, basi Mtume (s.a.w ) alipoisoma akafika mwisho akasujudu.