47 SUURA MUHAMMAD

Sura hii imeteremshwa Madina, na ina Aya 38.

Kwa jina la Mwenyeezi Mung-u, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

1. Wale waliokufuru na wakazuilia (watu) njia ya Mwenyeezi Mungu, yeye ataviharibu vitendo vyao.

2. Na wale walioamini na wakatenda mema na wakaamini yaliyoteremshwa juu ya Muhammad nayo ni haki itokayo kwa Mola wao, atawafutia makosa yao na atastawisha hali yao.

3. Hayo ni kwa sababu wale waliokufuru walifuta upotovu, lakini wale walioamini wakafuata haki itokayo kwa Mola wao, hivyo ndiyo Mwenyeezi Mungu anavyowaeleza watu hali zao.

4. Basi mnapokutana (vitani) na wale waliokufuru wapigeni shingo mpaka mmewashinda, kisha wafungeni pingu, tena waacheni kwa ihsani au kwa kujikomboa mpaka vita vipoe. Ndivyo hivyo, na lau angelitaka Mwenyeezi Mungu angejilipiza kisasi kwao lakini (vita vimetokea) ili awajaribu baadhi yenu kwa wengine. Na wale waliouawa katika njia ya Mwenyeezi Mungu, basi hataviharibu vitendo vyao.

5. Karibuni atawaongoza na kustawisha hali yao.

6. Na atawaingiza katika pepo aliyowajulisha.

7. Enyi mlioamini! mkimsaidia Mwenyeezi Mungu, atakusaidieni na ataiimarisha miguu yenu.

8. Na wale waliokufuru, basi kwao ni maangamizo na atavipoteza vitendo vyao.

9. Hayo ni kwa sababu waliyachukia aliyoyateremsha Mwenyeezi Mungu, basi akaviharibu vitendo vyao.

10. Je, Hawakutembea katika ardhi wakaona umekuwaje mwisho wa wale waliowatangulia? Mwenyeezi Mungu atawaangamiza na kwa makafiri itakuwa (adhabu) kama hii.

11. Hayo ni kwa sababu Mwenyeezi Mungu ni Mlinzi wa walioamini, lakini makafiri hawana Mlinzi.

12. Kwa hakika Mwenyeezi Mungu huwaingiza walioamini nawafanyao mema katika bustani ipitayo mito chini yake lakini waliokufuru hustarehe, na Moto ndio makazi yao.

13. Na miji mingapi ilikuwa yenye nguvu zaidi kuliko mji wako uliokutoa, tuliwaangamiza wala hawakuwa na msaidizi.

14. Je, mtu mwenye kuwa na dalili zitokazo kwa Mola wake atakuwa sawa na mtu aliyepambiwa ubaya wa matendo yake? na wakafuata tamaa zao.

15. Mfano wa Pepo waliyoahidiwa wacha Mungu mna mito ya maji yasiyoharibika na mito ya maziwa yasiyogeuka utamu wake, na mito ya pombe yenye ladha kwa wanywaji, na. mito ya asali iliyosafishwa, tena humo watapata matunda ya kila namna, na msamaha kutoka kwa Mola wao. Basi je, hao watakuwa sawa na yule akaaye Motoni? Na watanyweshwa maji yachemkayo yatakayokata matumbo yao.

16. Na wako miongoni mwao wanaokusikiliza hata wanapoondoka kwako wana wauliza wale waliopewa elimu: (Mtume) amesema nini sasa? Hao ndio ambao Mwenyeezi Mungu amewapiga muhuri nyoyoni mwao na wakafuata tamaa zao.

17. Na wale walioongoka huwazidishia muongozo na huwapa ucha Mungu wao.

18. Na hawangojei ila Kiyama kiwafikie kwa ghafla, basi alama zake zimekwisha kuja. Hivyo (utawafaa) wapi ukumbusho wao kitakapowafikia (Kiyama).

19. Basi jua ya kwamba: Hakuna aabudiwaye ila Mwenyeezi Mungu tu, na omba msamaha kwa dhambi zako na za Waumini wanaume na Waumini wanawake. Na Mwenyeezi Mungu anajua mahala penu pakurudia na mahala penu pakukaa.

20. Na walioamini husema: Mbona haijateremshwa sura? Lakini inapoteremshwa sura thabiti na ndani yake inatajwa vita, utawaona wale wenye maradhi katika nyoyo zao wanakutazama mtazamo wa anayezimia kwa mauti, basi ole wao.

21. (Yanayotakiwa ni) utii na kauli njema, na amri inapoazimiwa, basi kama wakiwa wa kweli kwa Mwenyeezi Mungu bila shaka itakuwa bora kwao.

22. Na kama nyinyi mkipata utawala nikaribu mtaiharibu nchi na mtaukata ujamaa wenu.

23. Na ndio Mwenyeezi Mungu amewalaani na amewatia uziwi na amewapofusha macho yao.

24. Je hawaizingatii Our'an au nyoyo zinakufuli?

25. Kwa hakika wale wanaorudi kwa migongo yao baada ya kuwabainikia muongozo, shetani amewadanganya na kuwachelewesha.

26. Hayo ni kwa sababu wao waliwaambia wale waliochukia yale aliyoyateremsha Mwenyeezi Mungu: Tutakutiini kwa baadhi ya mambo hayo, na Mwenyeezi Mungu ndiye anayejua siri zao.

27. Basi itakuwaje Malaika watakapowafisha? watawapiga nyuso zao na migongo yao.

28. Hayo ni kwa sababu wao waliyafuata yaliyomchukiza Mwenyeezi Mungu na wakachukia yanayomridhisha, basi akaviharibu vitendo vyao.

29. Je, wale wenye maradhi nyoyoni mwao wanadhani kwamba Mwenyeezi Mungu hataidhihirisha bughudha yao?

30. Na kama tungependa tungekuonyesha hao na ungewatambua kwa alama zao, na hasa utawafahamu kwa namna ya usemi wao, na Mwenyeezi Mungu anavijua vitendo vyenu.

31. Na bila shaka tutawajaribuni mpaka tuwajue wanaopigania dini miongoni mwenu na wanaosubiri, nasi tutazifanyia mtihani khabari zenu.

32. Kwa hakika wale waliokufuru na kuzuilia (watu) njia ya Mwenyeezi Mungu na wakapingana na Mtume, baada ya kuwabainikia muongozo wao hawamdhuru Mwenyeezi Mungu chochote, na ataviharibu vitendo vyao.

33. Enyi mlioamini! Mtiini Mwenyeezi Mungu na mtiini Mtume, wala msiviharibu vitendo vyenu.

34. Hakika wale waliokufuru na kuzuilia (watu) njia ya Mwenyeezi Mungu kisha wakafa nao ni makafiri, Mwenyeezi Mungu hatawasamehe.

35. Basi msilegee na kutaka suluhu, maana nyinyi ndio mtakaoshinda, na Mwenyeezi Mungu yu pamoja nanyi, wala hatakunyimeni (thawabu za ) vitendo vyenu.

36. Hakika maisha ya dunia ni mchezo na upuuzi, na kama mkiamini na kujilinda, atakupeni malipo yenu, wala hatakuombeni mali zenu.

37. Kama akikuombeni hayo na kukushurutisheni mtafanya ubakhili, na atatoa mifundo.

38. Lo! nyinyi ndio mnaitwa ili mtoe (mali) katika njia ya Mwenyeezi Mungu lakini wengine wenu wanafanya ubakhili na afanyaye ubakhili basi hakika anafanya ubakhili kwa (kuidhuru) nafsi yake. Na Mwenyeezi Mungu ni Mkwasi nanyi mafakiri, na kama mkirudi nyuma basi Mwenyeezi Mungu ataleta watu wengine badala yenu, nao hawatakuwa mfano wenu.