42 SUURATUSH SHUURAA

Sura hii imeteremshwa Makka, na ina Aya 53

Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

1. Haa Mym.

2. A'yn Syn Qaf.

3. Hivyo ndivyo, Mwenyeezi Mungu Mwenye nguvu (na) Mwenye hekima anavyokuletea Wahyi wewe na wale waliokutangulia.

4. Ni vyake vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini, na yeye ndiye aliye juu, Mkuu.

5. Zinakaribia mbingu kupasuka juu yao, na Malaika hutukuza kwa kumsifu Mola wao na kuwaombea msamaha waliomo ardhini. Angalieni! hakika Mwenyeezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.

6. Na wale waliofanya waungu wengine badala yake (Mwenyeezi Mungu) Mwenyeezi Mungu ndiye mhifadhi wao, nawe si mlinzi juu yao.

7. Na hivyo ndivyo tumekufunulia Qur'an kwa uwazi ili uwaonye siku ya mkutano isiyo na shaka, kundi moja litakuwa Peponi na kundi (jingine) litakuwa Motoni.

8. Na Mwenyeezi Mungu angelipenda angewafanya wote kundi moja, lakini humwingiza katika rehema yake amtakaye, na madhalimu hawana mlinzi wala msaidizi.

9. Je, wamefanya waungu wengine badala yake! lakini kiongozi hasa ni Mwenyeezi Mungu na yeye ndiye atakaye wahuisha waliokufa naye ni Mwenye uwezo juu ya kila kitu.

10. Na mkikhitilafiana katika jambo lolote, basi hukumu yake ni kwa Mwenyeezi Mungu, Mola wangu nimtegemeaye, na kwake ninarejea.

11. Muumba wa mbingu na ardhi amekuumbieni wake katika jinsi yenu, na wanyama (nao akawaumbia) wake, anakuzidishieni kwa namna hii Hakuna chochote mfano wake, naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.

12. Funguo za mbingu na ardhi ziko kwake, humfungulia riziki amtakaye na hudhikisha, bila shaka yeye ndiye ajuaye kila kitu.

13. Amekupeni Sharia (njia nyoofu) ya dini aliyomuusia Nuhu na tuliyokufunulia wewe Muhammad na tuliyowausia Ibrahimu na Musa na Isa, kwamba: Simamisheni dini wala msifarakane kwayo, ni ngumu kwa washirikina (dini hii) unayowaitia, Mwenyeezi Mungu humchagua kwake amtakaye na humuongoza kwake aelekeaye.[1]

14. Na hawakutengana ila baada ya kuwafikia elimu, kwa sababu ya uasi baina yao na kama isingelikuwa kauli iliyotangulia kutoka kwa Mola wako juu ya muda uliowekwa, lazima ingelihukumiwa (sasa hivi) Na kwa hakika wale waliorithishwa Kitabu baada yao wanakitilia shaka inayowahangaisha.

15. Basi kwa ajili ya hayo waite, na uendelee kwa kudumu kama unavyoamrishwa, wala usifuate matamanio yao, na useme: Naamini aliyoyateremsha Mwenyeezi Mungu Kitabuni, na nimeamrishwa nifanye uadilifu baina yenu. Mwenyeezi Mungu ndiye Mola wetu na (pia) ni Mola wenu, vitendo vyetu ni kwa ajili yetu, na vitendo vyenu ni kwa ajili yenu, hakuna ugomvi baina yetu na yenu, Mwenyeezi Mungu atatukusanya pamoja, na marejeo ni kwake.

16. Na wale wanaohojiana juu ya Mwenyeezi Mungu baada ya kumkubali, hoja yao ni batili mbele ya Mola wao, na juu yao iko ghadhabu na itakuwa kwao adhabu kali.

17. Mwenyeezi Mungu ndiye aliyeteremsha Kitabu kwa haki na Mizani. Na ni nini kitakujulisha kwamba pengine Kiyama kimekaribia?

18. Wasioamini (Kiyama) hukuomba kifike haraka, lakini walioamini wanakiogopa na wanatambua kwamba (kuja kwake) ni haki, tahadharini! kwa hakika wanao bishana katika (khabari ya) Kiyama wamo katika upotovu wa mbali.

19. Mwenyeezi Mungu ni mpole kwa waja wake, humpa riziki amtakaye, naye ni Mwenye nguvu, Mwenye kushinda.

20. Anayetaka mapato ya Akhera tutamzidishia katika mapato yake, na anayetaka mapato ya dunia tutampa, lakini katika Akhera hana sehemu yoyote.

21. Je, wana washirika waliowawekea dini asiyoitolea idhini Mwenyeezi Mungu? Na kama lisingelikuwako neno la kupambanua hukumu ingelikatwa baina yao, Na kwa hakika watapata madhalimu adhabu iumizayo.

22. Utawaona madhalimu wakiogopa kwa sababu ya yale waliyoyachuma. nayo yatawatokea, na wale walioamini na kutendawema watakuwamo katika mabustani ya Peponi. watapata watakayoyataka kwa Mola wao, hiyo ndiyo fadhila kubwa.

23. Hiyo ndiyo khabari nzuri ambayo Mwenyeezi Mungu huwaambia waja wake walioamini na kufanya vitendo vizuri, sema; Kwa haya siombi malipo yoyote kwenu isipokuwa mapenzi katika ndugu (kizazi changu) Na anayefanya wema tutamzidishia wema, kwa hakika Mwenyeezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwingi wa shukrani.[2]

24. Au wanasema: Amemzulia Mwenyeezi Mungu uongo? Lakini kama Mwenyeezi Mungu akipenda atapiga muhuri moyoni mwako, na Mwenyeezi Mungu ataifuta batili na atahakikisha ukweli kwa maneno yake, bila shaka yeye ndiye ajuaye yaliyomo vifuani.

25. Naye ndiye anayepokea toba za waja wake, na husamehe makosa, na anayajua mnayoyatenda.

26. Na anawajibu walioamini na kutenda mema, na anawazidishia fadhila zake na makafiri watakuwa na adhabu kali.

27. Na lau kama Mwenyeezi Mungu angetoa riziki nyingi kwa waja wake, bila shaka wangeliasi ardhini, lakini huiteremsha kwa kipimo akipendacho, hakika yeye kwa waja wake ni Mwenye khabari, Mwenye kuona.

28. Naye ndiye anayeteremsha mvua baada ya wao kukata tamaa, na kueneza rehema yake, naye ndiye Mlinzi, anaye shukuriwa.

29. Na katika dalili zake ni kuumbwa mbingu na ardhi na katika vyenye uhai alivyovieneza humo tena ndiye Mwenye uwezo wa kuvikusanya

apendapo.

30. Na msiba uliokupateni ni kwa sababu ya matendo ya mikono yenu, na (pia) anasamehe mengi.

31. Na nyinyi hamuwezi kumshinda (Mwenyeezi Mungu) katika ardhi, na pasipo Mwenyeezi Mungu nyinyi hamna mlinzi wala msaidizi.

32. Na katika dalili zake ni meli baharini zilivyo kama milima.

33. Kama akitaka hutuliza upepo, nayo husimama juu yake, kwa hakika katika hayo mna mazingatio kwa kila afanyaye subira, Mwingi wa shukrani.

34. Au huwaangamiza kwa sababu ya yale waliyoyatenda na (pia) anasamehe mengi.

35. Na watajua wale wanaojadiliana katika Aya zetu (kuwa) hawana mahala pa kukimbilia.

36. Basi vyote hivi mlivyopewa ni starehe ya maisha ya dunia, lakini kilichoko kwa Mwenyeezi Mungu ni bora na cha kudumu zaidi kwa wale walioamini na wanamtegemea Mola wao.

37. Na wale wanaojiepusha na madhambi makubwa na mambo mabaya na wanapokasirika husamehe.

38. Na wale waliomwitikia Mola wao na wakasimamisha swala, na mwendo wao ni kushauriana wao kwa wao, na wanatoa katika yale tuliyowaruzuku.

39. Na wale ambao wanapofanyiwa jeuri hujitetea.

40. Na malipo ya ubaya ni ubaya ulio sawa nao, lakini anayesamehe na kusuluhisha, basi malipo yake ni juu ya Mwenyeezi Mungu bila shakayeye hawapendi madhalimu.

41. Na yule anayejilipizia kisasi baada ya kudhulumiwa, hao hakuna njia ya kulaumiwa.

42. Basi lawama iko juu ya wale tu wanaodhulumu watu na wakawafanyia jeuri katika ardhi pasipo haki, hao ndio watakaopata adhabu yenye kuumiza.

43. Na anayesubiri na kusamehe, bila shaka hilo ni katika mambo makubwa.

44. Na anayepotezwa na Mwenyeezi Mungu basi hana mlinzi baada yake. Na utawaona madhalimu watakapoiona adhabu, watasema: Je, iko njia ya kurudi?

45. Na utawaona wanapelekwa (motoni) wamekuwa wanyonge kwa dhila, wanatazama kwa mtazamo wa kificho. Na walioamini watasema: Kwa hakika wapatao khasara ni wale waliokhasirisha nafsi zao na watu wao siku ya Kiyama. Tahadharini! bila shaka madhalimu watakuwa katika adhabu ya kudumu.

46. Wala hawatakuwa na viongozi wa kuwasaidia kinyume cha Mwenyeezi Mungu. na ambaye Mwenyeezi Mungu amempoteza, basi hana njia yoyote (ya kusalimika).

47. Mwitikieni Mola wenu kabla ya kufika siku isiyoepukika itokayo kwa Mwenyeezi Mungu, siku hiyo hamtakuwa na pa kukimbilia wala hamtakuwa na (njia ya) kukataa.

48. Na wakipuuza, basi hatukukupeleka uwe mwenye kuwalinda, si juu yako ila kufikisha tu. Na kwa hakika tunapomuonjesha mwanadamu rehema kutoka kwetu huifurahia, na kama ikiwafikia dhara kwa sababu ya yale iliyotanguliza mikono yao, ndipo Mwanadamu anakufuru.

49. Ufalme wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyeezi Mungu huumba apendavyo, humpa amtakaye watoto wa kike nahumpa amtakaye watoto wa kiume.

50. Au huwachanganya (watoto) wa kiume na wa kike, na humfanya tasa amtakae hakika yeye ni Mjuzi, Mwenye uwezo.

51. Na haikuwa kwa mtu yeyote kwamba Mwenyeezi Mungu aseme naye ila kwa ufunuo au kwa nyuma ya pazia au humtuma Mjumbe naye humfunulia kwa idhini yake apendavyo, bila shaka yeye ndiye aliye juu Mwenye hekima.

52. Na hivyo ndivyo tulivyokufunulia Wahyi kwa amri yetu, ulikuwa hujui Kitabu ni nini wala imani (ni nini) lakini tumekifanya (kitabu hiki) ni nuru kwa (nuru) hiyo tunamuongoza tumtakae katika waja wetu. Na kwa hakika wewe unaongoza kwenye njia iliyonyooka.

53. Njia ya Mwenyeezi Mungu ambaye ni vyake vilivyomo mbinguni na ardhini. Jueni! mambo yote yatarudi kwa Mwenyeezi Mungu.

[1] Aya 13

 MWENYEEZI MUNGU ALIVYOJITAMBULISHA KWA MANABII WAKE

NABII IBRAHIM: "Abramu alipokuwa mtu wa miaka tisini na kenda, BWANA akamtokea Abramu. akamwambia: Mimi ni Mungu Mwenyezi, uende mbele yangu ukawe mkamilifu.'' Mwanzo 17:1.

NABII YAKOBO: "Mungu akamtokea tena, aliporudi kutoka padanaramu, akambariki Mungu akamwambia; Jina lako ni Yakobo, hutaitwa tena Yakobo lakini Israeli litakuwa jina lako, akamwita jina lake Israeli. Mungu Akamwambia: Mimi ni Mungu Mwenyezi. uzidi ukaongezeke." Mwanzo 35:9-11.

NABII MUSA: “Kisha Mungu akasema na Musa. akamwambia: Mimi ni Yehova, nami nilimtokea Ibrahimu, na Isaka. na Yakobo, kama Mungu Mwenyezi, bali kwa jina langu Yehova sikujulikana kwao." Kutoka 6:2-3.

NABII DAUDI: "BWANA, Mungu wa majeshi, ni nani aliyehodari kama Wewe, Ee Yahu," Zaburi 89:8.

NABII ISA (Yesu): "Wala mimi simo tena ulimwenguni, lakini hawa wamo ulimwenguni, nami naja kwako, Baba mtakatifu, kwa jina lako ulilonipa uwalinde hawa, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo." Yohana 17:11.

"Yesu akamwambia: Usinishike, sijakwenda bado juu kwa Baba, Lakini nenda kwa ndugu zangu uwaambie: Nakwenda juu kwa Baba yangu na Baba yenu, Mungu wangu na Mungu wenu." Yohana 20:17.

"Yesu akamjibu: Ya kwanza ndiyo hii, sikiliza Israeli! Bwana Mungu wetu, ndiye peke yake Bwana." Marko 12:29.

NABII MUHAMMAD S.A.W: "Jua ya kwamba: Hakuna aabudiwaye ila ALLAH (Mwenyeezi Mungu) tu." Qur'an 47:19.

Mwenyeezi Mungu s.w amejitambulisha kwa Nabii Ibrahimu kwa jina la Mungu Mwenyezi. Kwa Nabii Yakobo amejitambulisha kwa jina la Mungu Mwenyezi. Kwa Nabii Musa amejitambulisha kwa jina la Yehova. Kwa Nabii Daudi amejitambulisha kwa jina la Yahu. Kwa Nabii Issa (Yesu) amejitambulisha kwa jina la Baba Mtakatifu, Baba, Bwana. Na, kwa Nabii wa mwisho Muhammad s.a.w amejitambulisha kwa jina la ALLAH.


[2] Aya 23

 QARABA ZA MTUME WAPENDWE

Iliposhuka Aya hii, Mtume s.a.w aliulizwa; Ni nani qaraba zako hawa ambao sisi imetulazimu kuwapenda? Mtume s.a.w akasema; Ali na Fatima na watoto wao (Hasan na Husein a.s).

Taz: Alburhan fyitafsiril Qur'an  J.4  Uk. 122

Almizan fyitafsiril Qur'an           J.18 Uk. 53

 Tafsirus Saafi                            J.4  Uk. 373

Tafsirul Kashshafi                      J.3  Uk. 467

 Ruuhul Maany                          J.25 Uk. 49

Albahrul Muhiit                         J.9  Uk. 335

 Fat-hul Qadiir                           J.4  Uk. 764

 Ruuhul Bayaani                        J.8  Uk. 311

Amesema Imam Shaafii;

"Enyi watu wa nyumba ya Mtume, kupendwa kwenu ni faradhi (lazima) kutoka kwa Mwenyeezi Mungu katika Qur'an ameteremsha (42:23) inatosha kwenu kuwa ni heshima kubwa kwamba nyinyi, yeyote asiyewatakia rehema hana swala."

"Wakasema, Umekuwa rafidhi (shia') nikajibu: Hapana, urafidhi si dini yang'u wala imani yangu. Isipokuwa nimemtawalisha pasipo shaka, Imani bora na Muongozi mwema. Ikiwa kumpenda Wasii (Imam Ali) ni urafidhi, basi mimi ni rafidhi mkubwa katika waja."