37 SUURA SAAFFAAT

Sura hii imeteremshwa Makka, na ina Aya 182

Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

1. Naapa kwa (Malaika) wajipangao safu.

2. Tena kwa wale wazuiao sana.

3. Kisha kwa wale wasomao mawaidha.

4. Kwa hakika Mungu wenu ni Mmoja tu.

5. Mola wa mbingu na ardhi na yaliyomo kati yake, na ni Mola wa mashariki zote. (na magharibi zote).

6. Kwa hakika sisi tumeipamba mbingu ya karibu kwa pambo la nyota.

7. Na kuilinda na kila shetani asi.

8. Wasiweze kuusikiliza mkutano mtukufu, na wanafukuzwa toka kila upande.

9. Kwa kusukumwa, na wanayo adhabu yenye kudumu.

10. Isipokuwa anayenyakua kitu kidogo mara humfuata kimondo kinachong'ara.

11. Na waulize: Je, wao ni wenye umbo gumu zaidi au wale tuliowaumba? Bila shaka sisi tuliwaumba kwa udongo unaonata.

12. Bali unastaajabu, na wao wanafanya mzaha.

13. Na wanapokumbushwa hawakumbuki.

14. Na wanapouona Muujiza hufanya mzaha.

15. Na wanasema: Hayakuwa haya ila ni uchawi ulio dhahiri.

16. Je, tutakapokufa na kuwa udongo na mifupa kweli tutafufuliwa.

17. Hata Babu zetu wa Zamani?

18. Sema: Naam, na nyinyi mtafedheheka.

19. Na kwa hakika litakuwa kemeo moja tu, mara wataona.

20. Na watasema: Ole wetu! hii ndiyo siku ya malipo!

21. Hii ndiyo siku ya hukumu ambayo mlikuwa mkiikadhibisha.

22. Wakusanyeni wale waliodhulumu na wenzi wao na wale waliokuwa wakiwaabudu.

23. Badala ya Mwenyeezi Mungu, na waongozeni kwenye njia ya Jahannanm.

24. Na wasimamisheni, hakika wao wataulizwa.

25. Mmekuwaje hamjisaidii?

26. Lakini siku hiyo watataka amani,

27. Nao wataelekeana wakiulizana.

28. Watasema: Kwa hakika nyinyi mlikuwa mkitujia upande wa kulia.

29. Watasema: Bali nyinyi hamkuwa waumini.

30. Na hatukuwa na mamlaka juu yenu, bali nyinyi mlikuwa waasi.

31. Basi hukumu ya Mola wetu imetuhakiki, bila shaka tutaionja.

32. Tulikupotezeni kwa sababu sisi tulikuwa wapotovu.

3.3. Basi wao kwa hakika siku hiyo watakuwa katika adhabu wakishirikiana.

34. Hiwo ndivyo tunavyofanya na waovu.

35. Hakika wao walipokuwa wakiambiwa: Hakuna aabudiwaye isipokuwa Mwenyeezi Mungu tu, wakijivuna.

36. Na husema: Je, tuiache miungu yetu kwa ajili ya mshairi mwenda wazimu?

37. Bali ameleta haki na amewasadikisha waliotumwa.

38. Hakika nyinyi lazima mtaionja adhabu yenye kuumiza.

39. Wala hamtalipwa ila yale mliyokuwa mkiyafanya.

40. Isipokuwa waja wa Mwenyeezi Mungu waliosafishwa.

41. Hao ndio watapata riziki maalumu.

42. Matunda na wao wataheshimiwa.

43. Katika Bustani zenye neema.

44. Juu ya vitanda vya fahari wakikabiliana.

45. Wakizungushiwa kikombe chenye (kinywaji) safi.

46. Cheupe chenye ladha kwa wanywao.

47. Hakina. madhara, wala hakiwaleweshi.

48. Na pamoja nao watakuwa wanawake wenye macho mazuri matulivu.

49. Hao wanawake kama mayai yaliyohifadhiwa.

50. Tena wataelekeana wao kwa wao wakiulizana.

51. Atasema msemaji miongoni mwao: Hakika nilikuwa na rafiki.

52. Aliyesema: Je, wewe ni katika wale wanaosadikisha?

53. Je, tutakapokufa na tutakuwa udongo na mifupa tutahukumiwa?

54. Atasema: Je, mtachungulia?

55. Basi akachungulia na akamuona katikati ya Jahannam.

56. Naye atasema: Wallahi ulikuwa karibu kuniangamiza.

57. Na lau kuwa si neema ya Mola wangu, bila shaka ningelikuwa miongoni mwa waliohudhurishwa.

58. Je, sisi ni wenye kufa?

59. Ila kifo chetu cha kwanza, wala hatutaadhibiwa.

60. Bila shaka huku ndiko kufuzu kukubwa.

61. Basi wafanyao wafanye sawa na mfano huu.

62. Je, karibisho la namna hii ni bora au mti wa zakkum?

63. Kwa hakika sisi tumeufanya jaribio kwa madhalimu.

64. Hakika huo ni mti unaoota kati kati ya Jahannam.

65. Matunda yake ni kama vichwa vya mashetani.

66. Bila shaka wao watakula katika huo, na kwa huo watajaza matumbo.

67. Kisha bila shaka watapewa juu ya huo mchanganyiko wa maji ya moto.

68. Halafu, kwa hakika marudio yao yatakuwa kwenye Jahannam.

69. Hakika wao waliwakuta baba zao wakipotea.

70. Na wao wanaendeshwa kasi katika nyayo zao.

71. Na bila shaka walikwisha potea kabla yao watu wengi wa zamani.

72. Na hakika tulipeleka Waonyaji kati yao.

73. Basi tazama ulikuwaje mwisho wa wale walioonywa?

74. Isipokuwa waja wa Mwenyeezi Mungu waliosafishwa.

75. Na kwa hakika Nuhu alituita, basi ni waitikiaji wema tulioje sisi!

76. Na tulimuokoa yeye na watu wake katika msiba mkubwa.

77. Na tuliwajaalia kizazi chake wawe ndio wenye kubaki.

78. Na tukamwachia (sifa) katika watu wa baadaye.

79. Amani kwa Nuhu ulimwenguni kote.

80. Kwa hakika hivyo ndivyo tunavyo walipa wenye kufanya wema.

81. Kwa hakika yeye alikuwa katika waja wetu wenye kuamini.

82. Kisha wengine tukawagharikisha.

83. Na hakika Ibrahimu alikuwa katika kundi lake.

84. Alipomfikia Mola wake kwa moyo safi.

85. Alipomwambia baba yake na watu wake: Mnaabudu nini?

86. Je, kwa uongo tu, mnataka miungu mingine badala ya Mwenyeezi Mungu?

87. Basi ni nini fikra yenu juu ya Mola wa walimwengu?

88. Kisha akatazama mtazamo katika nyota.

89. Na akasema: Hakika mimi mgonjwa.

90. Nao wakamwacha, wakampa kisogo.

91. Basi alikwenda kwa siri kwa miungu yao na akasema: Je, nyinyi hamli?

92. Mmekuwaje hamsemi?

93. Kisha akawageukia kuwapiga kwa mkono wa kulia.

94. Basi (watu) wakamwendea upesi.

95. Akasema: Je, mnaviabudu mnavyo vichonga?

96. Hali Mwenyeezi Mungu ndiye aliyekuumbeni nyinyi na mnavyovifanya.

97. Wakasema: Mjengeeni jengo kisha mtupeni motoni.

98. Basi walitaka kumfanyia hila lakini tukawafanya kuwa dhaifu.

99. Na (Ibrahimu) akasema: Nakwenda kwa Mola wangu, ndiye atakayeniongoza.

100. Ee Mola wangu! nipe (mtoto) miongoni mwa watendao mema.

101. Ndipo tukampa khabari njema ya mwana mpole.

102. Basi alipofikia (makamu ya) kufanya juhudi pamoja naye, akamwambia: Ewe mwanangu! hakika nimeona katika ndoto kuwa ninakuchinja, basi fikiri unaonaje? Akasema: Ewe Baba yangu fanya unayoamrishwa, utanikuta inshaallah miongoni mwa wanao subiri.[1]

103. Basi wote wawili walipojisalimisha na akamlaza kifudi fudi.

104. Mara tukamwita: Ewe Ibrahimu!

105. Umekwisha sadikisha ndoto, kwa hakika hivyo ndivyo tunavyowalipa wenye kutenda mema.

106. Bila shaka [jambo) hili ni jaribio lililo dhahiri.

107. Na tukamkomboa kwa mnyama wa kuchinjwa mtukufu.

108. Na tukamuachia (sifa) kwa (watu) wa baadaye.

109. Amani kwa Ibrahimu.

110. Hivyo ndivyo tunavyowalipa watendao mema.

111. Bila shaka yeye alikuwa miongoni mwa waja wetu walioamini.

112. Na tukambashiria (kumzaa) Isihaka Nabii miongoni mwa watu wema.

113. Na tukambarikia yeye na Isihaka, na katika kizazi chao yuko atendaye mema na mwenye kujidhulumu nafsi yake wazi wazi.

114. Na kwa hakika tuliwafanyia ihsani Musa na Harun.

115. Na tukawaokoa wao na watu wao katika taabu kubwa.

116. Na tukawasaidia, basi wakawa washindi.

117. Nao wawili tukawapa Kitabu kibainishacho.

118. Na tukawaongoza katika njia iliyo nyooka.

119. Kisha tukawaachia (sifa) katika watu wa baadaye.

120. Amani kwa Musa na Harun.

121. Bila shaka hivyo ndivyo tunavyowalipa wenye kufanya mema.

122. Kwa hakika wao walikuwa miongoni mwa waja wetu wenye kuamini.

123. Na hakika Ilyasa alikuwa miongoni mwa waliotumwa.

124. Alipowaambia watu wake: Je, hamuogopi?

125. Je, mnamuomba Ba'ala (sanamu) na mnamwacha aliye Mbora wa waumbaji.

126. Mwenyeezi Mungu Mola wenu na Mola wa baba zenu wa mwanzo?

127. Lakini wakamkadhibisha, basi bila shaka watahudhurishwa.

128. Isipokuwa waja wa Mwenyeezi Mungu waliosafishwa.

129. Na tumemwachia (sifa) kwa watu wa mwisho.

130. Amani kwa Ilyasa.

131. Bila shaka hivyo ndivyo tunavyowalipa wanaofanya wema.

132. Kwa hakika yeye alikuwa miongoni mwa waja wetu walioamini.

133. Na kwa hakika Luti alikuwa miongoni mwa waliotumwa.

134. (Kumbukeni) tulipomuokoa yeye na watu wake wote.

135. Isipokuwa mwanamke mkongwe katika wale waliobaki nyuma.

136. Kisha wengine tukawaangamiza.

137. Na kwa hakika nyinyi mnawapitia wakati wa asubuhi.

138. Na usiku (pia) basi je, hamfahamu.

139. Na hakika Yunus alikuwa miongoni mwa waliotumwa.

140. (Kumbukeni) alipokimbia katika jahazi iliyosheheni.

141. Na wakapiga kura, basi akawa miongoni mwa walioshindwa.

142. Mara samaki alimmeza hali yakuwa mwenye kulaumiwa.

143. Na ingelikuwa hakuwa katika wanaomtakasa Mwenyeezi Mungu.

144. Lazima angelikaa tumboni mwake mpaka siku watakayofufuliwa.

145. Lakini tukamtupa ufukoni hali ya kuwa mgonjwa.

146. Na tukamuoteshea mmea wa mung'unya.

147. Na tulimpeleka kwa (watu) laki moja au zaidi.

148. Basi waliamini na tukawastarehesha kwa muda.

149. Na waulize: Je, kwa Mola wako ni watoto wa kike na kwa wao wenyewe watoto wa kiume?

150. Je, tumewaumba Malaika kuwa wanawake nao wakashuhudia?

151. Sikilizeni! Kwa hakika wao wanasema kwa uongo wao.

152. Mwenyeezi Mungu amezaa, na hakika wao bila shaka ni waongo.

153. Je, amechagua watoto wa kike kuliko wa kiume?

154. Mmekuwaje, mnahukumu namna gani.

155. Je, hamkumbuki?

136. Au mmepata dalili iliyo wazi?

157. Basi leteni kitabu chenu kama mnasema kweli.

158. Na wameweka nasaba baina yake na majinni, na majinni wamekwisha jua hakika wao lazima watahudhurishwa.

159. Mwenyeezi Mungu Yu mbali na sifa wanazompa.

160. Isipokuwa waja wa Mwenyeezi Mungu waliosafishwa.

161. Basi bila shaka nyinyi na mnaowaabudu.

162. Hamuwezi kuwapoteza.

163. Isipokuwa yule atakayeingia Motoni.

164. Na (wamesema) hakuna yeyote miongoni mwetu ila anapo mahala pake khasa.

165. Na kwa hakika sisi ndio tujipangao safu.

166. Na hakika sisi ndio tunaomtukuza.

167. Na hakika walikuwa wakisema.

168. Tungelikuwa na kumbukumbu ya (watu) wa zamani.

169. Lazima tungelikuwa waja wa Mwenyeezi Mungu waliosafishwa.

170. Lakini wakamkataa, basi karibuni watajua.

171.Na bila shaka neno letu limekwisha tangulia kwa waja wetu waliotumwa.

172. Kwa hakika hao ndio watakaosaidiwa.

173. Na hakika jeshi letu ndilo litakalo shinda.

174. Basi waache kwa muda kidogo.

175. Na waonyeshe, nao hivi karibuni wataona.

176. Je, wanaihimiza adhabu yetu?

177. Basi (adhabu) itakaposhuka uwanjani kwao, ndipo itakuwa asubuhi mbaya kwa wale walioonywa.

178. Na waache kwa muda kidogo.

179. Na uone, nao hivi karibuni wataona.

180. Ameepukana Mola wako, Mola Mwenye enzi na yale wanayomsifu.

181. Na amani juu ya wale waliotumwa.

182. Na kila sifa njema ni ya Mwenyeezi Mungu, Mola wa walimwengu.


[1] Aya 102

Tamko la asli tulilolifasiri kwa: "Nimeona" "ARAA" na maana yake ni, "Naona" hii inaitwa: Istia'ratut tabaiyyah.