27. SUURATUN NAML

Sura hii imeteremshwa Makka, na ina  Aya 93

Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu

1. Twaa Syn. Hizo ni Aya za Qur'an na Kitabu kinacho bainisha.

2. Muongozo na khabari njema kwa wenye kuamini.

3. Ambao wanasimamisha swala na kutoa zaka nao wana yakini na Akhera

4. Kwa hakika wale wasioiamini Akhera tumewapambia vitendo vyao, lakini wana hangaika ovyo.

5. Hao ndio watakaopata adhabu mbaya na wao katika Akhera ndio wenye kupata khasara.

6. Na kwa hakika wewe unafundishwa Qur'an inayotokana kwa Mwenye hekima, Mwenye ujuzi.

7. (Kumbuka) Musa alipowaambia watu wake: Hakika nimeona moto, sasa hivi nitakuleteeni khabari au nitakuleteeni kijinga kiwakacho ili mpate kuota.

8. Basi alipoufikia, ikanadiwa kuwa: Amebarikiwa aliyomo katika moto na aliyoko pembeni mwake, na ametukuka Mwenyeezi Mungu, Mola wa walimwengu.

9. Ewe Musa! hakika mimi ndiye Mwenyeezi Mungu Mwenye nguvu, Mwenye hekima.

10. Na itupe fimbo yako, lakini alipoiona ikiyumba kama nyoka akageuka kurudi nyuma wala hakungoja: Ewe Musa! usiogope, bila shaka Mimi mbele yangu hawaogopi Mitume.

11. Ila aliyedhulumu kisha akabadilisha wema baada ya ubaya, basi kwa hakika Mimi ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.

12. Na ingiza mkono wako kifuani mwako utatoka mweupe pasipo ubaya, ni katika Miujiza tisa kwa Firaun na watu wake, hakika wao ni watu wenye kuvunja amri.

13. Basi ilipowafikia Miujiza yetu ionyeshayo, wakasema: Huu ni uchawi dhahiri.

14. Na wakaikataa hali nafsi zao zina yakini nayo, kwa dhulma na kujivuna, basi angalia ulikuwaje mwisho wa wenye kufanya ufisadi.

15. Na bila shaka tuliwapa Daudi na Suleiman elimu, na wakasema: Kila sifa njema ni ya Mwenyeezi Mungu, aliyetufadhili kuliko wengi katika waja wake wenye kuamini.

 16. Na Suleiman alimrithi Daudi na akasema: Enyi watu! tumefundishwa usemi wa ndege na tumepewa kila kitu, hakika hii ndiyo fadhili (iliyo) dhahiri.

17. Na alikusanyiwa Suleiman majeshi yake kutoka katika majinni na watu na ndege, nayo yakawekwa makundi makundi.

18. Hata walipofika katika bonde la Namli (wadudu chungu) akasema mdudu chungu: Enyi wadudu chungu! ingieni majumbani mwenu, asikupondeni Suleiman na majeshi yake, hali hawatambui.

19. Basi akatabasamu akiichekea kauli yake, na akasema: Ee Mola wangu! nipe nguvu nishukuru neema yako uliyonineemesha mimi na wazazi wangu na nipate kufanya vitendo vizuri uvipendavyo, na uniingize kwa rehema yako katika waja wako wema.

20. Na akawakagua ndege na akasema: Imekuwaje mbona simuoni Hud-Hudi au amekuwa miongoni mwa wasiokuwapo?

21. Lazima nitamuadhibu adhabu kali au nitamchinja, au ataniletea hoja iliyo wazi.

22. Basi hakukaa sana mara (Hud-Hud akafika) akasema: Nimegundua usilogundua, na ninakujia kutoka Sabaa na khabari zenye yakini.

23. Hakika nimekuta mwanamke anaye watawala naye amepewa kila kitu na anayo enzi kubwa.

24. Nimemkuta yeye na watu wake wakilisujudia jua badala ya Mwenyeezi Mungu, na shetani amewapambia vitendo vyao na akawazuilia njia, kwa hiyo hawakuongoka.

 20. Mbona hawamsujudii Mwenyeezi Mungu ambaye huyatoa yaliyofichikana katika mbingu na ardhi na huyajua mnayoyaficha na mnayoyadhihirisha.

26. Mwenyeezi Mungu, hapana aabudiwaye ila yeye tu, Mola wa Enzi kubwa.

27. Akasema (Suleiman) Tutatazama kama umesema kweli au u katika waongo.

28. Nenda na barua yangu hii na uwafikishie, kisha uwaache, na utazame watarudisha nini?

29. (Malkia) akasema: Enyi wakuu (wa baraza!) Hakika nimeletewa baruatukufu.

30. Hakika imetoka kwa Suleiman, nayo ni kwa jina la Mwenyeezi Mungu, mwingi wa rehema Mwenye kurehemu.

31. Kwamba msinifanyie jeuri na fikeni kwangu hali yakuwa mmekwisha kusilimu.

32. (Malkia) akasema: Enyi wakuu! nipeni shauri katikajambo langu, maana sikati shauri lolote mpaka mhudhurie.

33. Wakasema: Sisi ni wenye nguvu na ni wenye vita vikali, na hukumu ni juu yako, basi tazama ni nini unaamrisha.

34. (Malkia) akasema: Hakika wafalme wanapouingia mji, wanauharibu na wanawafanya watukufu wake kuwa dhalili hivyo ndivyo wanavyofanya.[1]

35. Na mimi ninawapelekea zawadi, nami nitangoja watakayorudi nayo wajumbe.

36. Basi alipofika (mjumbe) kwa Suleiman akasema (Suleiman): Je, nyinyi mnanisaidia kwa mali? lakini aliyonipa Mwenyeezi Mungu ni bora kuliko aliyokupeni lakini nyinyi mnaifurahia zawadi yenu.

37. Rudi (nayo) kwao, lazima tutawaendea na majeshi wasiyoweza kuyakabili na bila shaka tutawafukuza humo wakidhalilika hali wamekuwa wanyonge.

38. (Suleiman) akasema: Enyi wakuu wa baraza! Ni nani atakayeniletea kiti chake cha enzi kabla hawajafika kwangu, hali ya kuwa wamekwisha kusilimu?

39. Akasema Afriti katika majinni: Mimi nitakuletea hicho kabla hujasimama kutoka mahala pako, na mimi bila shaka ninazo nguvu za hayo, (na) mwaminifu.

40. Akasema yule aliyekuwa na elimu ya Kitabu: Mimi nitakuletea hicho kabla ya kupepesa jicho lako. Basi alipokiona kimewekwa mbele yake, akasema: Haya ni kwa fadhili za Mola wangu, ili anijaribu nitashukuru au nitakufuru? Na anayeshukuru, basi anashukuru kwa ajili ya nafsi yake na anayekufuru, kwa hakika Mola wangu ni Mkwasi, Mkarimu.

41. (Suleiman) Akasema: Kibadilini kiti chake cha enzi, tutaona kama ataongoka au atakuwa miongoni mwa wale wasioongoka.

42. Basi (Malkia) alipofika, akawaambia: Je, kiti chako cha enzi ni kama hiki? Akasema: kama ndicho hasa, nasi tulipewa elimu (ya Utume wako) kabla ya kuona Muujiza huu na tulikuwa wenye kunyenyekea.

43. Na (Suleiman) akamkataza yale aliyokuwa akiabudu kinyume cha Mwenyeezi Mungu, bila shaka (malkia) alikuwa katika watu makafiri.

44. Akaambiwa liingie jumba. Lakini alipoliona, akalidhani kuwa eneo la maji na akapandisha nguo mpaka katika miundi yake. (Suleirnan) akasema:

Hakika hilo ni jumba lililosakafiwa kwa vioo! Akasema (malkia): “Mola wangu! hakika nimedhulumu nafsi yangu na (sasa) najisalimisha pamoja na Suleiman kwa Mola wa walimwengu.”

45. Na bila shaka tuliwapelekea kina Thamudi ndugu yao Saleh, akawaambia:

Muabuduni Mwenyeezi Mungu. Basi mara wakawa makundi mawili wakigombana.

46. Akasema: Enyi watu wangu! kwanini mnauhimiza ubaya kabla ya wema? mbona hamuombi msamaha kwa Mwenyeezi Mungu ili mrehemewe?

47. Wakasema: Tumepata bahati mbaya kwa sababu yako na kwa sababu ya wale walio pamoja nawe. Akasema: Bahati yenu mbaya iko kwa Mwenyeezi Mungu lakini nyinyi ni watu mnaojaribiwa.

48. Na walikuwamo mjini watu tisa wakifanya matata katika ardhi wala hawakusuluhisha.

49. Wakasema: Apianeni kwa Mwenyeezi Mungu (kuwa) Tutamshambulia usiku yeye na watu wake, kisha kwa hakika tutamwambia mrithi wake, sisi hatukuona maangamio ya watu wake, na bila shaka sisi ni wa kweli.

50. Na wakafanya hila, nasi pia tukafanya hila hali hawatambui.

51. Basi angalia ulivyokuwa mwisho wa hila zao, hakika tuliwaangamiza pamoja na watu wao wote.

52. Basi hizo ni nyumba zao zilizoanguka kwa sababu walidhulumu, bila shaka katika hayo mna mazingatio kwa watu wanaojua.

53. Na tukawaokoa wale walioamini na waliokuwa wakimcha (Mwenyeezi Mungu).

54. Na Luti alipowaambia watu wake: Je, mnaufanya ubaya na hali mnaona.

55. Je, nyinyi mnawaingilia wanaume kwa matamanio mabaya badala ya wanawake? Bali nyinyi ni watu mnaofanya ujinga.

56. Basi halikuwa jawabu la watu wake ila kusema: Wafukuzeni wafuasi wa Luti katika mji wenu, bila shaka wao ni watu wanaojitakasa.

57. Kwa hiyo tukamuokoa yeye na wafuasi wake ila mkewe, tukamkadiria katika wakaao nyuma.

58. Na tukawanyeshea mvua, ni mbaya mno mvua hiyo ya wale walioonywa.

59. Sema: Kila sifa njema ni ya Mwenyeezi Mungu, na amani iwashukie waja wake ambao aliwachagua. Je, Mwenyeezi Mungu ni bora au wanaowashirikisha?

60. Au ni nani aliyeziumba mbingu na ardhi, na akakuteremshieni maji kutoka mbinguni, na kwa hayo tukaziotesha bustani zenye kupendeza? Nyinyi hamna uwezo wa kuiotesha miti yake. Je, yupo mungu pamoja na Mwenyeezi Mungu? Bali hao ni watu waliopotoka.

61. Au ni nani aliyeifanya ardhi kuwa mahala pa kustarehe na akaweka ndani yake mito na akaiwekea milima, na akaweka kizuizi kati ya bahari mbili? Je yuko mungu pamoja na Mwenyeezi Mungu? Bali wengi wao hawajui.

62. Au ni nani anayemjibu aliyedhikika amuombapo na kuondoa dhiki, na kukufanyeni wenye kuendesha dunia? Je yuko, mungu pamoja na Mwenyeezi Mungu? Ni kidogo mnayoyakumbuka.

63. Au ni nani anayekuongozeni katika giza la bara na bahari, na ni nani azipelekaye pepo kutoa khabari njema kabla ya rehema zake? Je, yuko mungu pamoja na Mwenyeezi Mungu? Mwenyeezi Mungu ametukuka juu ya wale wanaowashirikisha.

64. Au ni nani anayeanzisha kiumbe kisha anakirudisha, na ni nani anayekuruzukuni kutoka mbinguni na ardhini? Je, yuko mungu pamoja na Mwenyeezi Mungu? Sema: Leteni dalili zenu ikiwa mnasema kweli.

65. Sema; Hakuna aliyoko katika mbingu na ardhi ajuaye yasiyoonekana ila Mwenyeezi Mungu tu, nao hawajui ni lini watafufuliwa.

66. Lakini imekwisha elimu yao juu ya Akhera, bali wao wamo katika shaka nayo, bali wao ni vipofu nayo.

67. Na wale waliokufuru wakasema: Je, tutakapokuwa udongo sisi na baba zetu, je, tutatolewa?

68. Bila shaka haya tuliahidiwa sisi na baba zetu zamani, haya siyo ila ni visa vya watu wa kale.

69. Sema: Nendeni katika ardhi na muone jinsi ulivyokuwa mwisho wa wale waovu.

70. Wala usiwahuzunikie, wala usiwe katika dhiki kwa sababu ya hila wazifanyazo.

71. Na wanasema: Ahadi hii itatokea lini ikiwa mnasema kweli?

72. Sema: Bila shaka iko karibu kukufikieni sehemu ya yale mnayoyahimiza.

73. Na kwa hakika Mola wako ni Mwenye fadhili kwa watu, lakini wengi wao hawashukuru.

74. Na kwa hakika Mola wako anayajua yanayoficha vifua vyao na wanayoyadhihirisha.

75. Na hakuna siri katika mbingu na ardhi ila imo katika Kitabu kibainishacho.

76. Bila shaka Qur'an hii inawaeleza wana wa Israeli mengi ambayo kwa hayo wanakhitilafiana.

77. Na kwa hakika hiyo ni muongozo na rehema kwa wenye kuamini.

78. Hakika Mola wako atawakatia baina yao hukumu yake, naye ni Mwenye nguvu, Mjuzi.

79. Basi tegemea kwa Mwenyeezi Mungu hakika wewe uko juu ya haki iliyo wazi.

80. Kwa hakika huwezi kuwasikilizisha wafu, wala kuwasikilizisha viziwi mwito, wanapogeuka kurudi nyuma.

81. Wala huwezi kuwaongoza vipofu katika upotovu wao. Huwezi kumsikilizisha isipokuwa yule anayeziamini Aya zetu, basi hao ndio watii.

82. Na kauli itakapowathibitikia tutawatolea mnyama katika ardhi atakaye wasemeza kwa sababu watu walikuwa hawaziamini dalili zetu.

83. Na siku tutakapokusanya katika kila umma kundi miongoni mwa wale wanaokadhibisha dalili zetu, nao watawekwa mafungu mafungu.

84. Hata watakapofika, atasema: Je, nyinyi mlizikadhibisha Aya zangu pasipo kuzijua vyema? Au mlikuwa mkifanya nini?

85. Na itawathibitikia kauli kwa sababu walidhulumu, nao hawatasema.

86. Je, hawaoni kwamba tumeuumba usiku ili watulie humo, na mchana uangazao? kwa hakika katika hayo mna mazingatio kwa watu wenye kuamini.

87. Na siku litakapopulizwa parapanda, ndipo watahangaika waliomo mbinguni na waliomo ardhini ila yule Mwenyeezi Mungu amtakaye, na wote watamfikia hali ya kuwa madhalili.

88. Na utaona milima utaidhania imeganda, nayo itapita mpito wa mawingu ndio sanaa ya Mwenyeezi Mungu aliyekitengeneza kila kitu, bila shaka yeye anazo khabari za mnayoyatenda.

89. Atakayeleta mema, basi atapata mema kuliko hayo, nao katika mahangaiko ya siku hiyo watasalimika.

90. Na watakaoleta ubaya, basi zitaangushwa nyuso zao Motoni, hamtalipwa isipokuwa yale mliyokuwa mkiyatenda.

91. Bila shaka nimeamrishwa nimwabudu Mola wa mji huu tu ambaye ameutukuza, na ni vyake vitu vyote, na nimeamrishwa niwe miongoni mwa wanaonyenyekea.

92. Na kwamba nisome Qur'an. Na mwenye kuongoka, basi ameongoka kwa (faida ya) nafsi yake tu, na aliyepotea basi sema: Hakika mimi ni miongoni mwa Waonyaji tu.

93. Na sema: Kila sifa njema ni ya Mwenyeezi Mungu (ambaye) karibuni atakuonyesheni dalili zake na mtazifahamu, wala Mola wako haghafiliki na hayo mnayoyafanya.


[1] Aya 34

 HABARI ZA WAOVU:

Iliposemwa: "Hakika wafalme wanapouingia mji, wanauharibu na wanawafanya watukufu wake kuwa dhalili."

Tunapozungumzia juu ya watawala, ni muhimu kutaja ijapokuwa kwa ufupi  yaliyotokea huko nyuma katika miaka ya arobaini Hijria:

Muawia alipoandaa kumpeleka Mughira bin Shuuba kuwa gavana wake katika Mkoa wa Kuufa, mwaka wa arobaini na moja Hijria, alimwita akamwambia:

"Kwa hakika nilitaka kukuusia mambo mengi sana, lakini nitakuachia wewe na akili yako. Na sitaacha kukuusia jambo moja, usiache Kumtukana Ali na kumkashifu, na kumhurumia Uthman na kumuombea msamaha. Na kuwatia aibu watu wa Ali na kuwatenga mbali."

Taz: Tarekhut Tabari: J.4  Uk. 188

           Tarekh Ibn Athir: J.3 Uk. 234

Kupitia agizo hili, Imam Ali (a.s) alilaniwa kwa muda wa miaka mingi sana. Wafuasi wa Ahlul Bait (a.s) kwa jumla walishambuliwa kwa kutukanwa na kwa kuuliwa kila inapopatikana fursa hiyo.

Katika mwaka wa hamsini na sita Hijria, Muawiya alianza kumwandaa mwanawe Yazid kushika utawala mahala pake. Akawajenga watu watakaofanya kampeni hii. Katika Mkoa wa Kuufa akaweko Mughira bin Shuuba, Basra akaweko Ziyad.

Kisha Muawiya akaandika barua kwa Marwan bin Alhakam kuwa: "Kwa hakika mimi umri wangu umekwisha kukua, na hali yangu imedhoofu, nachelea (kuzuka) mgongano katika umma baada yangu, na nimekwishaona kuwa niwachagulie atakaekaa mahala pangu baada yangu. Na sikupenda kuamua lolote pasipo ya kushauriana na wewe. Kwa hiyo, watangazie hili, na unijulishe mtu ambaye atakupinga." Marwan akawatangazia watu wote shauri hili, na watu wote wakaafiki isipokuwa watu wanne walipinga waziwazi, nao ni: Husein bin Ali (a.s), Abdur Rahman bin Abibakr, Abdullah bin Umar na Abdullah bin Zubeir. Muawiya akaitisha mkutano, na akamwambia Dhahhak bin Qays Alfihry kuwa: Watakapokutana watu, mimi nitazungumza, nikisha, wewe simama umpendekeze Yazid kushika nafasi yangu, na uniombe kwa kusisitiza nikubali pendekezo lako. Kikao kilipokamilika, waalikwa wote walipoketi nafasi zao, Muawiya akatoa hutuba fupi ya kawaida akaketi. Ndipo Dhahhak bin Qays Alfihry akasimama akasifu:

Utukufu wa Islam na heshima ya Ukhalifa na haki zake, akaonyesha Aya inayoamrisha kumtii Mwenyeezi Mungu na kumtii Mtume, na kuwatii watawala. Qur'an 4:59.

Kisha akamtaja Yazid na utukufu wake na elimu yake kwa mambo ya siasa, akatamka kuwa: Anampendekeza Yazid kuwa Khalifa atakaeshika mahala pa baba yake Muawiya. Akasema: Ewe Amiirul muuminim (Muawiya): Hili ni jambo la lazima kwa watu wote kumpata mtawala atakaeshika mahala pako baada yako. Na tumechunguza kwa undani kumpata anayesitahiki nafasi hii tumemuona Yazid mtoto wa amiirul muummiin ni mwenye muongozo mzuri na mwenendo safi, naye ndiye ni mbora wetu kwa elimu na upole.

Basi mtawalishe mahala pako, na utuwekee alama tutakayoegemea na kutulia katika kivuli chake baada yako.” Akasimama Amr bin Said al-Ashdaq akasema kama aliyosema Dhahhak.

Kisha akasimama Yazid bin Al-Muq-nai al-Adhary akasema: "Huyu ndiye amiirul muuminiin, akionyesha kwa Muawiya. Ikiwa atakufa, basi ni huyu, akionyesha kwa Yazid. Na atakaekataa basi ni huu, akaonyesha upanga wake." Muawiya akamuuliza Ahnaf bin Qays: Unasemaje? Ahnaf akasema:

"Tunakuogopeni ikiwa tutasema kweli, na tunamuogopa Mwenyeezi Mungu ikiwa tutasema uongo. Na wewe amiirul muuminiin unamjua zaidi Yazid katika (mwenendo wake) usiku na mchana, na (katika) faragha zake na uwazi wake, na ndani yake na nje yake. Basi ikiwa unamjua anaridhaa ya Mwenyeezi Mungu na ya umma, basi usishauri chochote jambo hili. Na kama unamjua kinyume na (sifa) hiyo, basi usimpe dunia na wewe waelekea Akhera. Sisi hatuna jingine ila kusema: Tumesikia na tumetii.”

Taz: Tarekh Ibn Athir J.3  Uk. 251

Iliposemwa: “Nakhaafukum in swadaqna, wanakhaafu llaha in kadhabna.” yaani, “Tunakuogopeni ikiwa tutasema kweli, na tunamuogopa Mwenyeezi Mungu ikiwa tutasema uongo.” Tarehe imeshuhudia watu walioadhibiwa na wengine kuuliwa kikatili! Chukua mfano: Muhammad bin Abibakr At-Taymy, Abdur Rahman bin Hassan Al-Anzy, Hujr bin Adiyy Al-Kindy na wenzake. Hawa ni baadhi ya waliompinga Muawiya waziwazi, matokeo yalikuwaje Abdur Rahman alipelekwa kwa Ziyad, na akamwamuru amuue kikatili, Ziyad akamzika akiwa hai!

Taz: Tarekhut Tabari: J.4  Uk. 206

Tarekh Ibn Athir: J.3  Uk. 241-242

Hujr bin Adiyy Al- Kindy na wenzake, walipigizwa chini wakafungwa na kuunguzwa chuma!

Taz: Tarekh Ibn Athir: J.3  Uk. 236

Muawiya aliagiza askari wake kumkamata Muhammad bin Abibakr At-Taymy, akatiwa katika kiriba kisha akawashwa moto mpaka akafa!

Taz: Tarekhut Tabari: J.4  Uk. 79

Tarekh Ibn Athir: J.3  Uk. 180

Haya ni baadhi ya matokeo ya wale waliompinga Muawiya na haya ndiyo maf-huum ya maneno ya Ahnaf bin Qays aliyomwambia Muawiya kuwa:

"Nakhaafukum in swadaqna," yaani, Tunakuogopeni ikiwa tutasema kweli." Wale waliomwambia kweli, umeyaona yaliyowafika. Hii ndiyo siasa ya banu Umayya ambayo leo ndiyo inayoongoza duniani, kama yanavyo onyeshwa matukio ya kitarekh ndani ya tafsiri hii.

Baada ya vita vya Nahrawan kumalizika, Muawiya bin Abi Sufyan aliandaa jeshi lililoongozwa na Busru bin Artaat. Na Dhahhak bin Qays alfihry naye akakusanya jeshi jingine kubwa, akaunganisha pamoja na lile la Busru.

Muawiya akayaamuru majeshi hayo kwenda katika miji ili kuwaua wafuasi wa Ahlul Bait (a.s). Jeshi likaenda Madina, huko likaua watu wengi, na likafanya fisadi kubwa. Kisha  jeshi likaingia Makka likaua wafuasi wengi wa Ahlul Bait (a.s).

Taz: Annasaihul Kaafiya: Uk. 65-67

Alipokaribia kufa, Muawiya alimuusia mwanawe Yazid kuwa: Apeleke jeshi Madina. Yazid alipeleka jeshi likiongozwa na Muslim bin Uqba likaingia Madina, watu wengi waliuliwa, wanawake wengi wakanajisiwa!

Taz: Albidayatu Wannihaya: J.6  Uk. 262

Annasai, alikuwa Imam wa Hadithi katika zama zake, na kitabu chake ni mojawapo ya sihahi sita kwa Masunni. Alipoandika kitabu: “Alkhasais” kilichotaja ubora wa Imam Ali (a.s) aliandika: “Nilipofika Damashq na nikawaona wapinzani wengi wa Ali, nikaandika kitabu nikitaraji kuwa watakapokisoma Mwenyeezi Mungu atawaongoza.” Akaulizwa: “Kwa nini hakuandika ubora wa Muawiya?” Annasai akajibu: Ubora gani zaidi ya kuchinja watu? Akashambuliwa ndani ya Msikiti kwa kupigwa, akatolewa nje akatupwa katika kijiji cha Ramala akafa huko!

Taz: Albidayatu Wannihaya: J.ll Uk. 140-141

Mwaka wa sitini na moja, Imam Husein bin Ali (a.s) aliuliwa na majeshi ya Yazid bin Muawiya!

Taz:   Tarekhut Tabari: J.4  Uk. 301

Tarekh Ibn Athir: J.4  Uk. 46

Katika uchaguzi wa kwanza huko Zanzibar, uliofanyika mwezi wa sita 1957. Watu sita walisimama katika uchaguzi huo kupigania kuingia katika Baraza

la kutunga sheria (Legco). Majimbo manne yalikuwa kwa ajili ya Unguja na mawili Pemba. Matokeo ya uchaguzi huo ni kuwa: Chama cha Afro-Shirazi kilipata viti vitatu Unguja. Zanzibar Nationalist Party haikupata kiti hata kimoja. Kile kiti kimoja cha mjini Unguja alikipata Bwana Chodhry, mwakilishi wa chama cha Waislamu. Na vile viti viwili vya Pemba, kimoja alikipata Sheikh Muhammad Shamte, na cha pili alikipata Bwana Ali Sharif. Wote hawa wawili waliosimama huko Pemba walisimama kama watu binafsi.

Katika uchaguzi wa pili, uliofanyika Januari 1961 ulikuwa ni wa kugombea viti 22. Matokeo yake yalikuwa hivi:

Afro-Shiraz Party walipata viti kumi.

Zanzibar Nationalist Party walipata viti tisa.

Zanzibar and Pemba Peoples' Party walipata viti vitatu Jumla viti 22.

Kwa matokeo hayo, hakukuwa na chama kilichoweza kuunda serikali peke yake bila ya kushirikisha na chama kingine. Na hata baada ya kushirikiana matokeo yalikwenda sare. Kwa hivyo, ilibidi kuunda serikali ya muda tu wa miezi sita na baada ya hapo ufanywe uchaguzi mwingine tena. Waziri Kiongozi wa serikali hiyo ya muda aliwekwa Muingereza Bwana P.A.P. Robertson..

Katika uchaguzi wa tatu uliofanywa tarehe 1-6-1961 ulikuwa kwa kugombea viti ishirini na vitatu, kwa kushiriki vyama vya siasa kama ifuatavyo:

Zanzibar and Pemba Peoples Party (ZPPP) walishirikiana na Zanzibar Na-tionalist Party (ZNP) Matokeo ya uchaguzi huo yalikuwa hivi:

ZPPP + ZNP walipata viti 13. ASP walipata viti 10 kwahiyo, ZPPP na ZNP walishinda kwa viti vitatu.

Baada ya matokeo hayo, kulifanywa fujo nyingi kiasi wanachama wa ZNP na ZPPP kupigwa magongo, visu na mapanga katika sehemu za mjini na mashamba, khasa katika kijiji cha Bambi, ambako watoto wadogo wa shule walitiwa katika tanuri la kuchomea mbata na kuchomwa mpaka wakafa. Afro Shirazi Party baada ya kushika wao serikali kwa mavamizi ya tarehe 12-1-1964 waliwapa tunza wanakijiji hiki kwa kuwajengea majumba ya mawe ya ghorofa.

Zanzibar ilipata serikali ya ndani tarehe 24-6-1963, baada ya muda mfupi ulifuatia uchaguzi wa nne wa tarehe 8-7-1963 ambao uliandaliwa kwa kufikia Zanzibar kupewa uhuru wake ili kutokana na ukoloni wa Waingereza.

Walikabidhiwa uhuru wa nchi baada ya miezi sita ya kuunda serikali, yaani tarehe 10-12-1963.

Na baadaya siku 33 za uhuru, serikali hiyo ilipinduliwa katika tarehe 12-1-1964.

Taz: Zanzibar Kinyang'anyiro na Utumwa Uk. 85-142

Serikali ya ukoloni wa Waingereza hapo mwanzoni, haikushughulikia elimu Katika Zanzibar kwa nia safi. Ilikuwa kwa nia ya kuupenyeza na kuuanzisha Ukristo. Zanzibar ikijulikana wazi kwamba ni nchi ya Kiislaamu, zaidi ya asilimia 95 katika mia ya wakazi wake ni Waislaamu. Kulikuwa na haja gani ya kuanzisha elimu kwa njia za makanisa? Kulikuwa na ubaya gani kumuachia uhuru wake kuishi katika mazingira ya nchi yake ambayo zaidi ya asilimia 95 katika mia ya wakazi wake ni Waislaamu?

Rooman Catholic Mission ilianza Zanzibar katika mwezi wa Disemba 1860. Aliyeianzisha ni Bishop wa St. Denis Reunion, na katika mwaka uliofuata 1861 M. Fava (Vicar-General) alianzisha shule ya msingi (Elementary School) na shule ya kazi za mkono (Industrial School). Pamoja na shule hizi ilikuwepo shule nyingine ya R.C.M. ikiitwa Roman Catholic Mission African Urban School.

Hapajakuwa na sababu ya manufaa kwa Waislaamu ya kufanywa hivi katika nchi ambayo watu wake wengi sana ni Waislaamu. Lakini lengo la chini kwa chini lilikuwa si kuwapa elimu wananchi, bali kuendeleza mbele Ukristo.

Mwaka 1907, serikali ikiwa chini ya Uingereza, iliona haina budi ila kukubali kuanzisha rasmi mipango ya elimu Zanzibar. Serikali ya Misri ilikubali kumtoa bwana Rivers-Smith kuja Zanzibar kuanzisha mpango wa elimu.

Katika mwaka 1908, alitayarisha mpango wa Idara ya Elimu na kufunguliwa kwa shule za watoto wanaume Zanzibar na Pemba. Masomo yake yalikuwa kujifunza lughaya Kiingereza, Kiarabu, Hesabu, Jiografia, Qur'an na Dini. Katika mbinu za kuwavunja moyo watu kichinichini ili wasipeleke watoto wao shule, kulizushwa vitisho vya matumizi ya herufi za kizungu katika masomo ya shuleni. Kwa karne nyingi, watu wa Zanzibar na taqriban Mwambao kwa jumla, walikuwa wakitumia khati zinazotumiwa katika Qur'an na masomo ya dini yao ya Kiislaamu. Lugha yote ya Kiswahili, mashairi yote na tenzi zote, yakiandikwa na kusomwa kwa Lugha ya Kiswahili kwa kutumia khati hizo zinazo tumika katika kuandika Qur'an, na ambazo ndizo walizozowea kuzitumia tangu ianze dini ya Kiislaamu kwa ghafla, katika kuanzishwa shule za misheni, ikaambiwa mfumo huo haufai na usitumike tena, na badala yake, ukachukuliwa ule wa herufi za kizungu ziitwazo "Ro-man Script" unaotumika makanisani na ukawa ndiyo wa kufundisha watoto kusoma na kuandika mashuleni.

Anasema Mwenyeezi Mungu kuwa: “Hakika wafalme (watawala) wanapouingia mji, wanauharibu na wanawafanya watukufu wake kuwa dhalili.”

Taz: Zanzibar Kinyang'anyiro na Utumwa Uk. 68-69 Katika qadhia ya Tanganyika tumekwishaieleza katika Sura ya nne (Annisaa).

katika mlango wa: “Nafasi ya Mujahid katika Uislaamu.” Lakusisitizwa hapa ni kwamba: Haya yaliyojiri katika nchi tulizojaribu kutaja matukio yake ya kitarekh, hayakuanguka yenyewe kwa bahati mbaya. Hapana! tena Hapana! Bali ni mambo yaliyoandaliwa na kupangwa na binadarnu walio na akili timamu. Ili kupindua yale waliyokuwa nayo watukufu wa miji hiyo, na kuweka itikadi na tamaduni zao mahala pake! Anasema Mwenyeezi Mungu kuwa: “Na hawatakuwa radhi juu yako Mayahudi wala Wakristo mpaka ufuate mila yao.” 2:120.

Wala hawataacha kupigana nanyi mpaka wawatoe katika dini yenu kama wakiweza. 2:217.

HATUA ZA KUCHUKULIWA

Baada ya hali hii kushika hatamu, watukufu wa nchi (Waislaamu) wakapinduliwa na kudhalilishwa na wafalme (watawala). Ni suluhisho gani liwe ili kurudisha uhuru na heshima waliyokuwa nayo? Jawabu ya swali hili ni lile tukio la kitarekh lililotokea kwa Nabii Musa (a.s) na kaumu yake. Anasema Mwenyeezi Mungu kuwa: “Musa akawaambia kaumu yake”: “Ombeni msaada kwa Mwenyeezi Mungu na vumilieni. Hakika ardhi ni ya Mwenyeezi Mungu atamrithisha amtakaye katika waja wake, na mwisho (mwema) ni kwa wamchao”. 7:128.

Huu ndio mfumo wa Nabii Musa (a.s) alio wawekea kaumu yake, ili kupambana na ukandamizaji wa Firaun, na akafafanua sharti zitakazowezesha kumshinda adui. Akawakumbusha ya kwamba: Ikiwa watatumia nguzo nne, basi lazima adui watamshinda:

(a) Awepo Musa (Kiongozi).

(b) Kumtegemea Mwenyeezi Mungu tu peke yake.

(c) Uvumilivu.

(d) Kumcha Mwenyeezi Mungu.

Sharti hizi za ushindi katika kaumu ya Nabii Musa kwa adui yao, hazikuwa kwa wao peke yao, la, bali kwa kila taifa linalotaka kushinda dhidi ya adui yake, hapana budi kushikamana na nguzo nne hizi.

Firaun ni kiumbe muovu na jeuri sana, Mwenyeezi Mungu anataja habari zake:

“Na hakika Firaun alikuwa jeuri katika nchi, na kwa hakika yeye alikuwa miongoni mwa wapitao kiasi”. 10:83.

“Hakika Firaun alitakabari katika ardhi na akawafanya watu wa huko makundi makundi”. 28:4.

“Na Firaun akasema: Enyi wakuu! Simjui kwa ajili yenu mungu asiyekuwa mimi.” 28:38.

“Akasema (F'iraun): Mimi ndiye Mola wenu mkubwa.” 79:24.

Katika nguzo nne za ushindi, imesemwa: “Awepo Musa” Maana yake, Awepo Kiongozi madhubuti atakaesimamia Sharia ya Mwenyeezi Mungu (s.w).

Na iliposemwa: “Kumtegemea Mwenyeezi Mungu tu peke yake.” Mana yake, Mambo yao yote yarejeshwe kwa Mwenyeezi Mungu tu.

Iliposemwa: “Uvumilivu” Mana yake, kuhimili masaaib kunakofungamana na ujasiri mkubwa.”

Na iliposemwa: “Kumcha Mwenyeezi Mungu” Mana yake, Mwislaamu Shujaa mwenye kuonyesha tafsir ya Sharia ya Mwenyeezi Mungu, kwa matendo ya maisha yake ya kila siku. Ndiko kumcha Mwenyeezi Mungu.