26 SUURATUSH SHUA'RAA

Sura hii imeterenishwa Makka,  ina  Aya 227

Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

1. Twaa Syn Mym.

2. Hizo ni Aya za Kitabu kinacho bainisha.

3. Huenda utaangamiza nafsi yako kwa sababu hawawi waumini.

4. Tungependa tungewateremshia kutoka mbinguni Muujiza, na shingo zao ziwe zenye kuinamia.

5. Wala hauwafikii ukumbusho mpya utokao kwa Mwenyeezi Mungu Mwingi wa rehema ila hujitenga mbali nao.

6. Basi kwa hakika wamekadhibisha, kwa hiyo karibuni zitawafikia khabari za yale waliyokuwa wakiyafanyia mzaha.

7. Je, hawakuiona ardhi, mimea mingapi tumeiotesha humo ya kila namna nzuri?

8. Bila shaka katika hayo iko dalili, lakini wengi wao si wenye kuamini.

9. Na hakika Mola wako yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.

10. Na Mola wako alipomwita Musa, kwamba; Nenda kwa watu madhalimu.

11. Watu wa Firaun, hawaogopi?

12. Akasema; Mola wangu! hakika mimi naogopa kuwa watanikadhibisha.

13. Na kifua changu, kinadhikika, na ulimi wangu hautamki vyema, basi mtumie ujumbe Harun.

14. Nao wanalo kosa, (kisasi) kwangu basi naogopa (wasije) kuniuwa.

15. Akasema: Siyo, basi nendeni na Miujiza yetu, hakika Sisi tu pamoja nanyi, tunasikia.

16. Basi mwendeeni Firaun na mwambieni: Kwa hakika sisi ni Mitume wa Mola wa walimwengu wote.

17. (Tumetumwa) ya kwamba uwapeleke pamoja nasi wana wa Israeli.

18. (Firaun) akasema: Je, hatukukulea Sisi (ulipokuwa) mtoto na ukakaa kwetu miaka (mingi) ya umri wako?

19. Na ulifanya kitendo chako kile ulichofanya na ukawa miongoni mwa wasioshukuru.

20. (Musa) akasema: Nilifanya hayo, hapo nilipokuwa miongoni mwa wale wasioelewa.

21. Basi nikakukimbieni nilipo kuogopeni na Mola wangu akanipa hukumu na akanijaalia miongoni mwa Mitume.

22. Na hiyo ndiyo neema ya kunisumbulia (na) wewe umewatia utumwani wana wa Israeli?

23. Firaun akasema; Na nani Mola wa walimwengu wote?

24. (Musa) akasema: Muumba wa mbingu na ardhi na vilivyomo kati yake, ikiwa nyinyi ni wenye yakini.

25. (Firaun) akawaambia waliomzunguka: Je, hamsikii?

26. (Musa) akasema: Mola wenu na Mola wa baba zenu wa kwanza.

27. (Firaun) akasema: Bila shaka Mtume wenu aliyetumwa kwenu ni mwenda wazimu,

28. (Musa) akasema: (Yeye ni) Mola wa mashariki na magharibi na vilivyomo kati yake, ikiwa mnafahamu.

29. (Firaun) akasema: Kama ukishikilia kuwa kuna mungu mwingine badala yangu lazima nitakuweka miongoni mwa waliofungwa.

30. Akasema: Je, Ijapokuwa nitakuletea kitu kilicho wazi?

31. Akasema: Kilete ukiwa ni miongoni mwa wasemao kweli.

32. Basi akaitupa fimbo yake mara ikawa nyoka dhahiri.

33. Na akatoa mkono wake, na mara ukawa mweupe kwa watazamao.

34. (Firaun) akasema: Kuwaambia wakuu waliomzunguka: Kwa hakika huyu ni mchawi ajuae sana.

35. Anataka kukutoeni katika nchi yenu kwa uchawi wake, basi mna shauri gani?

36. Wakasema: Mpe muda yeye na nduguye na uwatume katika miji wakusanyao (watu).

37. Watakuletea kila mchawi mkubwa ajuaye.

38. Basi walikusanywa wachawi kwa wakati hasa wa siku maalumu.

39. Na wakaambiwa watu: Mmekwisha kukusanyika?

40. Huenda tutawafuata wachawi wakiwa ndio watakaoshinda.

41. Basi walipofika wachawi, wakamwambia Firaun: Je, tutapata malipo

tukiwa sisi ndio tulioshinda?

42. Akasema: Ndio, na pia mtakuwa miongoni mwa wale waliowekwa karibu.

43. Musa akawaambia: Tupeni mnavyotaka kuvitupa.

44. Basi wakatupa kamba zao na fimbo zao, na wakasema: Kwa nguvu za Firaun, kwa hakika sisi ndio wenye kushinda.

45. Kisha Musa akatupa fimbo yake, nayo mara ikavimeza walivyovizusha.

46. Ndipo wachawi wakainamishwa kusujudu.

47. Wakasema: Tunamwamini Mola wa walimwengu wote.

48. Mola wa Musa na Harun.

49. (Firaun) akasema: Je, mmemwamini kabla sijawaruhusuni? Bila shaka yeye ni mkubwa wenu ambaye amekufundisheni uchawi, basi hakika nyinyi karibuni mtajua. Lazima nitaikata mikono yenu na miguu yenu kwa kubadilisha na lazima nitakusulubuni nyote.

50. Wakasema: Haidhuru, hakika sisi (sote) tutarejea kwa Mola wetu.

51. Bila shaka sisi tunatumai ya kwamba Mola wetu atatusamehe makosa yetu, maana sisi tumekuwa wa kwanza wa wenye kuamini.

52. Na tulimpelekea Wahyi Musa, kwamba nenda na watu wangu wakati wa usiku, bila shaka mtafuatwa.

53. Basi Firaun akawatuma wakusanyao watu katika miji.

54. Hakika hawa ni kikosi kidogo.

55. Na bila shaka hao ndio wanaotukasirisha.

56. Na hakika sisi ni wengi wenye kuchukua hadhari.

57. Basi tukawatoa katika mabustani na chemchem.

58. Na (katika) makhazina na mahala pazuri.

59. Hivyo ndivyo, na tukawarithisha wana wa Israeli.

60, Kisha wakawafuata lilipotoka jua.

61. Basi yalipoonana majeshi mawili, watu wa Musa wakasema: Hakika tumepatikana.

62. (Musa) akasema: La, kwa hakika Mola wangu yu pamoja nami, bila shaka ataniongoza.

63. Mara tulimpelekea Wahyi Musa: Piga bahari kwa fimbo yako. Mara ikatengana, na kila sehemu ikawa kama mwamba mkubwa.

64. Na tukawaleta pale karibu wengine.

65. Na tukamuokoa Musa na wale waliokuwa pamoja naye wote.

66. Kisha tukawagharikisha wengine.

67. Hakika katika hayo mna mazingatio, lakini wengi wao si wenye kuamini.

68. Na kwa hakika Mola wako ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.

69. Na wasomee khabari za Ibrahimu.

70. Alipomwambia baba yake na kaumu yake: Mnaabudu nini?

71. Wakasema: Tunaabudu masanamu, nasi tutaendelea kuyafuata.

72. Akasema: Je, yanakusikieni mnapoyaita?

73. Au yanakufaeni au yanakudhuruni?

74. Wakasema: Lakini tumewakuta baba zetu wakifanya hivi hivi.

75. Akasema: Je, mmekiona mnachokiabudu?

76. Nyinyi na baba zenu waliotangulia?

77. Bila shaka hao ni adui zangu isipokuwa Mola wa walimwengu.

78. Ambaye ameniumba, naye ananiongoza.

79. Naye ndiye anayenilisha na kuninywesha.

80. Na ninapougua, basi yeye ananiponya.

81. Na ambaye atanifisha kisha atanihuisha.

82. Na ndiye ninayemtumaini kunisamehe makosa yangu siku ya malipo.

83. Mola wangu! Nipe hukumu na niunge pamoja na watendao mema.

84. Na unijaalie kutajwa kwa wema katika watu wa baadaye.

85. Na unijaalie katika warithi wa Bustani za neema.

86. Na umsamehe baba yangu bila shaka yeye ni miongoni mwa waliopotea.

87. Wala usinifedheheshe siku watakayofufuliwa.

88. Siku ambayo haitafaa mali wala watoto.

89. Isipokuwa mwenye kuja kwa Mwenyeezi Mungu na moyo safi.

90. Na Pepo itasogezwa karibu kwa wacha Mungu.

91. Na Jahannam itadhihirishwa kwa waasi.

92. Na wataambiwa; Wako wapi mliokuwa mkiwaabudu.

93. Badala ya Mwenyeezi Mungu, je, wanaweza kukusaidieni na kujisaidia wenyewe?

94. Basi watatupwa humo wao na waasi (wengine).

95. Na majeshi ya Iblis wote.

96. Watasema: Na hali wakigombana humo.

97. Wallahi, kwa hakika tulikuwa katika upotovu wazi wazi.

98. Tulipokuwa tukikufanyeni sawa na Muumba wa walimwengu wote.

99. Na hawakutupoteza ila wale waovu.

100. Basi hatuna waombezi.

101. Wala rafiki wa dhati.

102. Basi kama tungelikuwa na marejeo tungekuwa miongoni mwa waumini.

103. Bila shaka katika hayo mna mazingatio, lakini wengi wao si wenye kuamini.

104. Na bila shaka Mola wako ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.

105. Watu wa Nuhu waliwakadhibisha Mitume.

106. Alipowaambia ndugu yao Nuhu: Je, Hamumchi Mungu?

107. Hakika mimi kwenu ni Mtume mwaminifu.

108. Basi mcheni Mwenyeezi Mungu na nitiini.

109. Na sikuombeni juu yake malipo, malipo yangu hayapo ila kwa Mola wa

walimwengu wote.

110. Basi mcheni Mwenyeezi Mungu na nitiini.

111. Wakasema: Je, tukuamini wewe hali wanyonge ndio wanakufuata?

112. Akasema: Nayajuaje waliyokuwa wakiyafanya?

113. Hesabu yao haiko ila kwa Mola wangu tu, laiti mngetambua.

114. Wala mimi si wakuwafukuza waumini.

115. Mimi si yeyote ila ni muonyaji dhahiri.

116. Wakasema: Kama hutaacha ewe Nuhu bila shaka utapigwa mawe.

117. Akasema: Mola wangu! bila shaka kaumu yangu wamenikadhibisha.

118. Basi hukumu baina yangu na wao, hukumu (nzuri) na uniokoe mimi na walio pamoja nami, walioamini.

119. Kwa hiyo tukamuokoa yeye na waliokuwa pamoja naye katika jahazi iliyo sheheni.

120. Kisha tukawagharikisha baadaye walio baki.

121. Hakika katika hayo mna mazingatio, lakini wengi wao hawakuwa wenye kuamini.

122. Na bila shaka Mola wako ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.

123. Kina Adi waliwakadhibisha Mitume.

124. Alipowaambia ndugu yao, Hudi: Je, Hamuimchi Mungu?

125. Bila shaka mimi kwenu ni Mtume mwaminifu.

126. Basi mcheni Mwenyeezi Mungu na nitiini.

127. Wala sikuombeni juu yake malipo, malipo yangu hayako ila kwa Mola wa walimwengu.

128. Je, mnajenga juu ya kila mnyanyuko kumbusho la kufanyia upuuzi?

129. Na mnajijengea ngome ili mkae milele.

130. Na mnaposhambulia mnashambulia kwa jeuri.

131. Basi mcheni Mwenyeezi Mungu na nitiini.

132. Na mcheni ambaye amekupeni haya mnayoyajua.

133. Amekupeni wanyama na watoto wanaume.

134. Na mabustani na chemchem.

135. Hakika ninakukhofieni adhabu ya siku kubwa.

136. Wakasema: Ni mamoja kwetu ukitupa mawaidha au kutokuwa miongoni mwa watoao mawaidha.

137. Haya si chochote ila ni tabia za watu wa kale.

138. Wala sisi hatutaadhibiwa.

139. Basi wakamkadhibisha, na tukawahilikisha, bila shaka katika hayo mna mazingatio, lakini wengi wao hawakuwa wenye kuamini.

140. Na kwa hakika Mola wako ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.

141. KinaThamudi waliwakadhibisha Mitume.

142. Alipowaambia ndugu yao Saleh,je Hamumchi Mungu?

14.3. Bila shaka mimi kwenu ni Mtume mwaminifu.

144. Basi mcheni Mwenyeezi Mungu na nitiini.

145. Wala sikuombeni malipo juu yake, malipo yangu hayako ila kwa Mola wa walimwengu.

146. Je, mtaachwa salama katika haya yaliyopo hapa.

147. Katika mabustani na chemchem.

148. Na mimea na mitende yenye makole yaliyoiva.

149. Na mnachonga milimani majumba kwa maarifa.

150. Basi mcheni Mwenyeezi Mungu na nitiini.

151. Wala msitii amri za wale maasi.

152. Ambao wanafanya uharibifu katika ardhi wala hawaitengenezi.

153. Wakasema: Hakika wewe ni miongoni mwa waliorogwa.

154. Wewe si chochote ila ni mtu kama sisi, basi lete Muujiza ikiwa ni miongoni mwa wasemao kweli.

155. Akasema: Huyu ngamia jike awe na zamu yake ya kunywa, na nyinyi muwe na zamu yenu ya kunywa katika siku maalum.

106. Wala msimguse kwa ubaya isije ikakushikeni adhabu ya siku kubwa.

157. Lakini wao walimuua na wakawa wenye kujuta.

158. Basi adhabu ikawashika, bila shaka katika hayo mna mazingatio, lakini wengi wao hawakuwa wenye kuamini.

159. Na hakika Mola wako ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.

160. Watu wa Luti waliwakadhibisha Mitume.

161. Alipowaambia ndugu yao, Luti: Je, Hamumchi Mungu?

162. Hakika mimi kwenu ni Mtume mwaminifu.

163. Basi mcheni Mwenyeezi Mungu na nitiini.

164. Wala sikuombeni malipo juu yake, malipo yangu hayako ila kwa Mola wa walimwengu.

165. Je, mnawaingilia wanaume katika viumbe.

166. Na mnawaacha aliokuumbieni Mola wenu katika wake zenu? Kweli nyinyi watu mnaoruka mipaka.

167. Wakasema: Kama usipoacha wewe Luti, lazima utakuwa miongoni mwa wanaofukuzwa.

168. Akasema: Kwa hakika mimi ni katika wale wanaochukia sana matendo yenu.

169. Mola wangu! niokoe mimi na watu wangu katika yale wanayoyafanya.

170. Basi tukamuokoa yeye na watu wake wote.

171. Isipokuwa kikongwe katika waliokaa nyuma.

172. Kisha tukawaangamiza wengine.

173. Na tukawanyeshea mvua, basi ni mbaya mvua ya walioonywa.

174. Hakika katika hayo mna mazingatio, lakini wengi wao hawakuwa wenye kuamini.

175. Na hakika Mola wako ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.

176. Watu wa mwituni waliwakadhibisha Mitume.

177. Alipowaambia Shua'yb: Je, Hamumchi Mungu?

178. Hakika mimi kwenu ni Mtume mwaminifu.

179. Basi mcheni Mwenyeezi Mungu na nitiini.

180. Wala sikuombeni malipo juu yake, malipo yangu hayako ila kwa Mola wa walimwengu.

181. Kijazeni kipimo sawa sawa wala msiwe miongoni mwa wapunguzao.

182. Na pimeni kwa mizani iliyo sawa.

183. Wala msiwapunguzie watu vitu vyao, wala msitembee katika ardhi mkifisidi.

184. Na mcheni aliyekuumbeni nyinyi na mataifa yaliyotangulia.

185. Wakasema: Hakika wewe ni miongoni mwa waliorogwa.

186. Na wewe hukuwa ila ni mtu kama sisi, na kwa hakika tunakuona ni miongoni mwa waongo.

187. Basi tuangushie kipande cha mbingu ikiwa ni miongoni mwa wasemao kweli.

188. Akasema: Mola wangu anajua sana mnayoyatenda.

189. Lakini wakamkadhibisha, basi ikawashika adhabu ya siku ya kivuli. Bila shaka hiyo ilikuwa adhabu ya siku kubwa.

190. Hakika katika hayo mna mazingatio, lakini wengi wao hawakuwa wenye kuamini.

191. Na kwa hakika Mola wako ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.

192. Na bila shaka hii (Qur'an) ni mteremsho wa Mola wa walimwengu wote.

193. Ameiteremsha Roho (Jibril) mwaminifu.

194. Juu ya moyo wako, ili uwe miongoni mwa waonyaji.

195. Kwa ulimi wa Kiarabu wazi wazi.

196. Na kwa hakika hayo yamo katika Vitabu vya kale.

197. Je, haikuwa alama kwao kwamba wanayajua wanachuoni wa wana wa Israel?

198. Na lau tungeliiteremsha juu ya mmoja wa wasio waarabu.

199. Na akawasomea, wasingelikuwa wenye kuamini.

200. Hivyo ndivyo tulivyoiingiza (kufru) katika nyoyo za waovu.

201. Hawataiamini mpaka waone adhabu iumizayo.

202. Basi itawafikia kwa ghafla hali hawatambui.

203. Na watasema: Je, sisi tutapewa muda?

204. Basi je, wanaihimiza adhabu yetu?

205. Unaonaje kama tukiwastarehesha kwa miaka.

206. Kisha yakawafikia waliyokuwa wakiahidiwa.

207. Yatawafaa nini yale waliyostareheshewa?

208. Wala hatukuangamiza mji wowote ila ulikuwa na Waonyaji.

209. (Kuwa) ni ukumbusho, wala hatukuwa madhalimu.

210. Wala mashetani hawakuteremka nayo.

211. Wala haiwapasi na tena hawawezi.

212. Bila shaka wao wamezuiliwa kusikia.

213. Basi usimuombe mungu mwingine pamoja na Mwenyeezi Mungu ukawa miongoni mwa wanaoadhibiwa.

214. Na uwaonye jamaa zako waliokaribu.[1]

215. Nauinamishe bawa lako kwa yule anayekufuata katika wale walioamini.

216. Nakama wakikuasi, basi sema: Mimi ni mbali na hayo mnayoyafanya.

217. Na umtegemee Mwenye nguvu, Mwenye rehema.

218. Ambaye anakuona unaposimama.

219. Na mageuko yako katika wale wanaosujudu.

220. Hakika yeye ndiye Mwenye kusikia, Mwenye kujua.

221. Je, nikuambieni ambao mashetani wanawateremkia?

222. Wanateremka juu ya kila mzushi mkubwa, mwenye dhambi.

223. Wanampelekea yale wanayoyasikia na wengi wao ni waongo.

224, Na watungaji mashairi, ni wapotovu ndio wanawafuata.

225. Je, huoni kwamba wao wanahangaika katika kila bonde.

226. Na kwamba wao wanasema wasiyoyatenda?

227. Ila wale walioamini na kufanya vitendo vizuri, na kumtaja Mwenyeezi Mungu kwa wingi, na wakajitetea wanapodhulumiwa. Na karibuni wafanyao dhulma watajua ni mgeuko wa namna gani watakao geuka.


[1] Aya 214

MTUME  AMTANGAZA ALI KUWA KHALIFA WAKE

Iliposhuka Aya hii, Mtume s.a.w aliwaita jamaa zake akawaambia:

"Enyi Bani Abdil Muttalibi! Hakika mimi wallahi simjui kijana yeyote katika Waarabu, aliyewaletea watu wake, jambo bora kabisa kuliko nililokuleteeni mimi. Hakika mimi nimekuleteeni kheri ya dunia na ya Akhera na ameniamrisha (Mwenyeezi Mungu) nikuiteni kwake, basi nani kati yenu atakayenisaidia jambo hili ili awe ndugu yangu na wasii wangu na khalifa wangu kwenu? Watu wote wakanyamaza, nikasema (Ali): mimi ewe Nabii wa Mwenyeezi Mungu! nitakuwa waziri wako, Pale pale akanishika shingo yangu, kisha akasema: Hakika huyu ni ndugu yangu, na wasii wangu, na khalifa wangu kwenu, kwa hiyo msikilizeni na mtiini."

Taz: Tarekhut Tabari: J.2  Uk. 63

Tarekh Ibn Athir: J.2  Uk. 62-63

Tafsirul Khazin: J.5  Uk. 127

Assiratul Halabiyya: J.l  Uk.311

 Sabilun Najaati: Uk.113

Kwa hiyo, Ali bin Abi Talib, ni Wasii na khalifa wa Mtume s.a.w kwa Waislamu. Maana ya "WASII" ni mtu anayesimamia kuendesha mambo ya mtu. Kwa kuwa Ali ni Wasii wa Mtume s.a.w maana yake, Ali atasimamia na kuendesha mambo ya Waislaamu baada ya Mtume s.a.w.

Maana ya "KHALIFA" ni mtu anaye kuja kukaa mahala pa mtu baada yake. Kwa kuwa Ali ni Khalifa wa Mtume s.a.w maana yake, Ali atashika mahala pa Mtume s.a.w baada yake.