22 SUURATUL HAJJ

Sura hii imeteremshwa Madina na ina Aya 78

Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

1. Enyi watu! mcheni Mola wenu, hakika tetemeko la Kiyama ni jambo kubwa.

2. Siku mtakapokiona (Kiyama) kila mwanamke anyonyeshaye atamsahau amnyonyeshaye, na kila mwenye mimba ataizaa mimba yake, na utawaona watu wamelewa, kumbe hawakulewa, lakini ni adhabu ya Mwenyeezi Mungu iliyo kali.

3. Na katika watu yuko anayebishana juu ya Mwenyeezi Mungu pasipo elimu, na anamfuata kila shetani asi.

4. Ameandikiwa ya kwamba atakayemfanya (shetani) kuwa kiongozi, basi kwa hakika yeye atampoteza na kumpeleka kwenye adhabu ya Moto uwakao,

5. Enyi watu! Ikiwa nyinyi mna shaka ya kufufuliwa basi kwa hakika tulikuumbeni kwa udongo, kisha kwa manii kisha kwa pande la damu, kisha kwa kipande cha nyama kilichoumbika na kisichoumbika, ili tukubainishieni, nasi tunakikalisha matumboni tunachokitaka mpaka muda uliowekwa, (utimie) kisha tunakutoweni kwa hali ya utoto, kisha (tunakuleeni) ili mfikie baleghe yenu. Na katika nyinyi yuko anayefishwa, na katika nyinyi yuko anayerudishwa kwenye umri dhalili hata asijue chochote baada ya kujua. Na unaiona ardhi kavu lakini tunapoyateremsha maji juu yake inastawi na kurutubika na kuotesha kila namna ya mimea mizuri.

6. Hayo ni kwa sababu Mwenyeezi Mungu ndiye haki, na kwamba yeye huwahuisha wafu, na kwamba yeye ni Mwenye uwezo juu ya kila kitu.

7. Na kwa hakika Kiyama kitakuja hapana shaka ndani yake, na kwa hakika Mwenyeezi Mungu atawafufua walio makaburini.

8. Na katika watu yuko anayejadili juu ya Mwenyeezi Mungu bila elimu wala muongozo wala kitabu chenye nuru.

9. Ageuzaye shingo yake ili kupoteza (watu) katika njia ya Mwenyeezi Mungu atapata fedheha duniani na tutamuonjesha siku ya Kiyama adhabu ya kuungua.

10. Hayo ni kwa sababu ya yale iliyotanguliza mikono yako miwili, na bila shaka Mwenyeezi Mungu si dhalimu kwa waja.

11. Na katika watu yuko anayemwabudu Mwenyeezi Mungu ukingoni, basi kama ikimfikia kheri hutulia kwayo, na kama ukimfikia msukosuko hugeuza uso wake. Amepata khasara ya dunia na Akhera, hiyo ndiyo khasara dhahiri.

12. Anaomba badala ya Mwenyeezi Mungu, kile kisichomdhuru wala kisichomfaa, huo ndio upotovu ulio mbali.

13. Wanamuomba yule ambaye bila shaka dhara yake iko karibu zaidi kuliko nafuu yake, kwa hakika (huyo) ni mlinzi mbaya na ni rafiki mbaya.

14, Bila shaka Mwenyeezi Mungu atawaingiza wale walioamini na kufanya vitendo vizuri katika Bustani zipitazo mito chini yake, kwa hakika Mwenyeezi Mungu hufanya atakavyo.

15. Anayedhaniya kwamba Mwenyeezi Mungu hatamnusuru (Mtume) katika dunia na akhera, basi afunge kitanzi juu kisha ajinyonge, na aone je, hila yake yaweza kuyaondoa yale yaliyomghadhibisha?

16. Na hivyo ndivyo tuliiteremsha (Qur'an) kuwa ni Aya zilizo wazi, na bila shaka Mwenyeezi Mungu humuongoza anayetaka.

17. Hakika wale walioamini na ambao ni Mayahudi na Wasabai na Wakristo na Majusi na wale washirikishao, bila shaka Mwenyeezi Mungu atawapambanua baina yao siku ya Kiyama, hakika Mwenyeezi Mungu ni Shahidi juu ya kila kitu.

18. Je, huoni kwamba Mwenyeezi Mungu kinamsujudia kila kilichomo mbinguni na kilichomo ardhini na jua na mwezi na nyota na milima na miti na wanyama na wengi miongoni mwa watu? Na wengi imewalazimu adhabu, na anayefedheheshwa na Mwenyeezi Mungu hana wa kumheshimu basi hakuna ampaye heshima, bila shaka Mwenyeezi Mungu hufanya apendayo.

19. Hawa mahasimu wawili waliohasimiana kwa ajili ya Mola wao, lakini wale waliokufuru wamekatiwa nguo za moto, yatamiminwa juu ya vichwa vyao maji yachemkayo.

20. Kwa (maji) hayo vitayayushwa vilivyomo matumboni mwao na ngozi.

21. Na kwa ajili yao (yatakuwapo) marungu ya chuma.

22. Kila mara watakapotaka kutoka humo kwa sababu ya uchungu, watarudishwa humo na kuambiwa: lonjeni adhabu ya kuungua.

23. Hakika Mwenyeezi Mungu atawaingiza wale walioamini na kufanya vitendo vizuri (katika) Bustani zipitazo mito chini yake, humo watavishwa bangili za dhahabu, na lulu na mavazi yao humo yatakuwa ya hariri.

24. Na kuongozwa kwenye maneno mazuri na kuongozwa kwenye njia ya Mwenye kuhimidiwa.

25. Hakika wale waliokufuru na kuwazuilia (wengine) njia ya Mwenyeezi Mungu na Msikiti Mtukufu ambao tumeufanya kwa ajili ya watu wote sawa sawa kwa wakaao humo na wageni, na atakayetaka kufanya upotovu humo kwa dhulma tutamuonjesha adhabu yenye kuumiza.

26. Na (Kumbuka) tulipomkalisha Ibrahimu mahala penye Nyumba, kwamba usinishirikishe na chochote na uisafishe Nyumba yangu kwa ajili ya waizungukao na wasimamao na wainamao na wasujudao.

27. Na utangaze kwa watu habari za Hija watakujia (wengine) kwa miguu na (wengine) juu ya kila mnyama wakija toka kila njia ya mbali.

28. Ili washuhudie manufaa yao na kulitaja jina la Mwenyeezi Mungu katika siku zinazojulikana juu ya yale aliyowaruzuku, nao ni wanyama wenye miguu minne, na kuleni katika wanyama hao na mlisheni mwenye shida, fakiri.

29. Kisha wajisafishe taka zao, na watimize nadhiri zao, na waizunguke Nyumba ya kale.

30. Hivyo ndivyo, na anayevitukuza vitu vitakatifu vya Mwenyeezi Mungu basi hiyo ni kheri kwake, mbele ya Mola wake. Na mmehalalishiwa wanyama isipokuwa wale mnaosomewa, basi jiepusheni na uchafu wa masanamu na jiepusheni na usemi wa uongo.

31. Kwa kumtakasia (imani) Mwenyeezi Mungu bila kumshirikisha, na anayemshirikisha Mwenyeezi Mungu basi ni kama kwamba ameporomoka kutoka mbinguni, kisha ndege wakamnyakua au upepo ukamtupa mahala pa mbali.

32. Hivyo ndivyo, na anayeziheshimu alama za Mwenyeezi Mungu basi hayo ni katika unyenyekevu wa nyoyo.

33. Katika hayo yamo manufaa kwa ajili yenu mpaka muda maalumu, kisha mahala pa kuchinjiwa kwake ni kwenye Nyumba ya kale.

34. Na kila umma tumewafanyia mahala pa kuchinjia mihanga ya ibada ili walitaje jina la Mwenyeezi Mungu juu ya vile walivyo ruzukiwa katika wanyama wenye miguu minne, basi Mungu wenu ni Mungu Mmoja kwa hiyo mnyenyekeeni kwake, na waambie khabari njema wanyenyekevu.

35. Ambao anapotajwa Mwenyeezi Mungu nyoyo zao hutetemeka, na wanaovumilia juu ya yale yanayowapata na wanaoshika swala na katika vile tulivyowaruzuku wanatoa.

36. Na ngamia (wa sadaka) tumekufanyieni kuwa katika alama za Mwenyeezi Mungu kwao mnayo kheri, basi litajeni jina la Mwenyeezi Mungu juu yao wasimamapo safu safu, Na waangukapo ubavu, basi kuleni katika hao na mlishe (fukara) aliyekinai na aombaye. Hivyo ndivyo tumewatiisha kwa ajili yenu ili mpate kushukuru.

37. Nyama zao hazimfikii Mwenyeezi Mungu wala damu zao, lakini unamfikia ucha Mungu wenu. Hivyo ndivyo amewatiisha kwenu, ili mumtukuze Mwenyeezi Mungu kwa sababu amekuongozeni, na wape khabari njema wafanyao mema.

38. Hakika Mwenyeezi Mungu huwalinda wale walioamini, bila shaka Mwenyeezi Mungu hampendi kila haini, asiye shukuru.

39. Imeruhusiwa (kupigana) kwa wale wanaopigwa, kwa sababu wamedhulumiwa, na kwa hakika Mwenyeezi Mungu anao uwezo wa kuwasaidia.

40. Ambao wametolewa majumbani mwao pasipo haki ila kwa sababu wanasema Mola wetu ni Mwenyeezi Mungu. Na kama Mwenyeezi Mungu asingeliwakinga watu baadhi yao kwa wengine, bila shaka yangelivunjwa mahekalu na makanisa, na masinagogi, na misikiti ambamo jina la Mwenyeezi Mungu hutajwa kwa wingi. Na bila shaka Mwenyeezi Mungu humsaidia yule anayemsaidia Yeye. Hakika Mwenyeezi Mungu ni Mwenye nguvu Mtukufu.

42. Wale Ambao tukiwapa madaraka katika nchi husimamisha swala na hutoa Zaka na huamrisha yaliyo mema na hukataza yaliyo mabaya, na kwa Mwenyeezi Mungu ndiko mwisho wa mambo.

42. Na kama wakikukadhibisha basi walikadhibisha kabla yao watu wa Nuhu na Adi na Thamudi.

43. Na watu wa Ibrahimu na watu wa Luti.

44. Na watu wa Madyan, na Musa (pia) alikadhibishwa lakini niliwana muda makafiri kisha nikawaadhibu, basi ilikuwaje adhabu yangu!

45. Basi ni miji mingapi tuliiangamiza iliyokuwa ikidhulumu ikaanguka juu ya mapaa yake, na visima vingapi vilivyoachwa na majumba (yaliyokuwa) madhubuti?

46. Je, hawatembei katika ardhi ili wapate nyoyo (akili) za kufahamia, au masikio ya kusikilia? Kwa hakika macho hayakupofuka, bali nyoyo ambazo zimo vifuani ndizo zinazopofuka.

47. Na wanakuhimiza ulete adhabu lakini Mwenyeezi Mungu hatavunja ahadi yake na kwa hakika siku moja kwa Mola wako ni kama miaka elfu mnayoihesabu.

48. Na miji mingapi niliyoipa muda na hali ilikuwa ikidhulumu? kisha nikaitia mkononi? na kwangu ndiko marudio.

49. Sema: Enyi watu! Bila shaka mimi kwa ajili yenu ni muonyaji niliye dhahiri.

50. Basi wale walioamini na wakafanya vitendo vizuri watapata msamaha riziki yenye heshima.

51. Na wale wanaojitahidi kuzipinga Aya zetu hao ndio watu wa Motoni.

52. Na hatukumtuma kabla yako Mtume wala Nabii ila anaposoma, shetani alitia (fitina) katika masomo yake. Lakini Mwenyeezi Mungu huondoa anayoyatia shetani, kisha Mwenyeezi Mungu huzimakinisha Aya zake, na Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye hekima.

53. Ili alifanye lile analotia shetani kuwa ni fitna kwa wale wenye maradhi nyoyoni mwao na ambao nyoyo zao ni ngumu, na bila shaka madhalimu wamo katika uhalifu wa mbali.

54. Na ili wajue wale waliopewa elimu ya kwamba hiyo ni haki iliyotokana kwa Mola wako na waiamini, na zinyenyekee kwake nyoyo zao. Na kwa hakika Mwenyeezi Mungu ndiye awaongozaye wale walioamini kwenye njia iliyonyooka.

55. Na wataendelea wale waliokufuru kuwa katika wasi wasi kwa hilo mpaka Kiyama kiwafikie kwa ghafla, au iwafikie adhabu ya siku isiyokuwa na kheri.

56. Ufalme siku hiyo utakuwa wa Mwenyeezi Mungu, atahukumu baina yao. Basi wale walioamini na wakafanya vitendo vizuri watakuwa katika Bustani zenye neema.

57. Na wale waliokufuru na kuzikadhibisha Aya zetu basi hao watapata adhabu yenye kufedhehesha.

58. Na wale waliohama katika njia ya Mwenyeezi Mungu kisha wakauawa au wakafa, bila shaka Mwenyeezi Mungu atawaruzuku riziki njema, na hakika Mwenyeezi Mungu ni Mbora wa wanaoruzuku.

59. Lazima atawaingiza, mahala watakapoparidhia, na bila shaka Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi, Mpole.

60. Hivyo ndivyo, na ajilipizaye kisasi sawa na dhara aliyotiwa, kisha akadhulumiwa, bila shaka Mwenyeezi Mungu atamsaidia, hakika Mwenyeezi Mungu ni Mwingi wa msamaha, Mwingi wa maghufira.

61. Hayo ni kwa sababu Mwenyeezi Mungu huingiza usiku katika mchana, na huingiza mchana katika usiku, na kwamba Mwenyeezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.

62. Hayo ni kwa sababu Mwenyeezi Mungu ndiye Haki, na kwamba wale wanaowaabudu badala yake ni baatil, na kwamba Mwenyeezi Mungu ndiye aliye Juu, Mkubwa.

63. Je, Huoni kwamba Mwenyeezi Mungu huteremsha maji kutoka mawinguni na ardhi inakuwa kijani. Hakika Mwenyeezi Mungu ni Mwenye kujua yaliyofichikana na Mwenye kujua yaliyo dhahiri.

64. Ni vyake vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini, na hakika Mwenyeezi Mungu ni Mkwasi, Mwenye kusifiwa.

65. Je, huoni kwamba Mwenyeezi Mungu amevitiisha kwa ajili yenu vilivyo ardhini, na majahazi yanayopita baharini kwa amri yake, na ameishikilia mbingu isianguke juu ya ardhi ila kwa idhini yake. Kwa hakika Mwenyeezi Mung kawa watu ni Mpole, Mwenye kurehemu.

66. Naye ndiye aliyekuhuisheni kisha akakufisheni, kisha atakufufueni, hakika mwanadamu ni mwenye kukufuru sana.

67. Kila umma tumeujaalia kawaida ya ibada wanayoishika, basi wasikugombeze katika jambo hili, na uite kwa Mola wako, bila shaka wewe uko juu ya muongozo ulio sawa.

68. Na kama wakijadiliana nawe, basi waambie: Mwenyeezi Mungu anajua sana mnayoyatenda.

69. Mwenyeezi Mungu atahukumu baina yenu siku ya Kiyama katika yale mliyokuwa mkikhitilafiana.

70. Je, hujui kuwa Mwenyeezi Mungu anajua yaliyoko mbinguni na ardhini? Bila shaka hayo yamo Kitabuni, hakika hayo kwa Mwenyeezi Mungu ni mepesi.

71. Na wanawaabudu badala ya Mwenyeezi Mungu (miungu) ambao (Mwenyeezi Mungu) hakuteremsha dalili kwao, na ambavyo hawana ujuzi navyo, na madhalimu hawatakuwa na msaidizi.

72. Na wanaposomewa Aya zetu zilizo wazi, utaona chuki juu ya nyuso za wale waliokufuru, wanakaribia kuwashambulia wale wanaowasomea Aya zetu. Sema je, nikuambieni yaliyo mabaya zaidi kuliko hayo? Ni Moto Mwenyeezi Mungu aliowaahidia wale waliokufuru na ni marudio mabaya.

73. Enyi watu! umepigwa mfano, basi usikilizeni: Hakika wale mnaowaomba badala ya Mwenyeezi Mungu hawawezi kuumba inzi japo wakikusanyika kwa jambo hili, na kama inzi akiwanyang'anya chochote hawawezi kukipata kwake, amedhoofika atakaye na anayetakiwa.

74. Hawakumuadhimisha Mwenyeezi Mungu kama anavyostahiki kuadhimishwa. Hakika Mwenyeezi Mungu bila shaka ni Mwenye nguvu, Mwenye kushinda.

75. Mwenveezi Mungu huchagua Wajumbe miongoni mwa Malaika na miongoni mwa watu,kwa hakika Mwenyeezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.

76. Anajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao, na kwa Mwenyeezi Mungu ndiko yatarejeshwa mambo.

77. Enyi mlioamini! rukuuni na sujuduni na mwabuduni Mola wenu na fanyeni mema ili mpate kufaulu.

78. Na ipiganieni (dini ya) Mwenyeezi Mungu kama inavyostahiki. Yeye amekuchagueni wala hakuweka juu yenu uzito katika dini, (nayo) ni mila ya baba yenu Ibrahimu, yeye aliyekuiteni Waislamu tangu zamani na katika Qur'an hii, ili awe Mtume shahidi yenu na nyinyi muwe mashahidi juu ya watu kwa hiyo simamisheni swala na toeni zaka na shikamaneni kwa ajili ya Mwenyeezi Mungu. Yeye ndiye Mola wenu, basi ni Mola mwema alioje, na Msaidizi mwema alioje!