19. SURA MARYAM

Sura hii imeteremshwa Makka, na  ina Aya

Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

1. Kaaf Haa Yaa 'Ayn Swaad.

2. (Huu) ni ukumbusho wa rehema ya Mola wako kwa mja wake Zakaria.

3. Alipomuomba Mola wake kwa maombi ya siri.

4. Akasema: Mola wangu! bila shaka mfupa wangu umekuwa dhaifu na kichwa kinang'aa kwa mvi wala sikuwa mwenye bahati mbaya, Mola wangu kwa kukuomba.

5. Na hakika mimi nawahofia jamaa zangu baada yangu, na mke wangu ni tasa, basi nipe mrithi kutoka kwako.

6. Atakayenirithi na awarithi ukoo wa Yaakub na umfanye Mola wangu! Mwenye kuridhisha.

7. Ewe Zakaria! Hakika tunakupa khabari njema ya mtoto,jina lake Yahya, Hatujapata kumpa jina hilo yeyote kabla yake.

8. Akasema: Mola wangu! nitapataje mtoto hali mke wangu ni tasa na mimi nimekwisha fikia uzee wa kupita kiasi.

9. Akasema: Ni kama hivyo amesema Mola wako: Haya ni rahisi kwangu, na kwa hakika nilikuumba zamani nawe hukuwa chochote.

10. Akasema: Mola wangu! nifanyie dalili akasema; Dalili yako ni kwamba hutasema na watu kwa siku tatu (na) hali ni mzima.

11. Basi akawatokea watu wake kutoka mihirabuni na akawaashiria kuwa mtukuzeni (Mwenyeezi Mungu) asubuhi na jioni.

12. Ewe Yahya! shika Kitabu kwa nguvu, na tukampa hekima angali mtoto.

13. Na huruma kutoka kwetu, na utakaso na akawa mcha Mungu.

14. Na mwema kwa wazazi wake, wala hakuwa jeuri, muasi.

15. Na amani iko juu yake siku aliyozaliwa na siku atakayofariki, na siku atakayofufuliwa hai.

16. Na mtaje Maryam Kitabuni alipojitenga na jamaa zake, (akaenda) mahala upande wa mashariki.

17. na akaweka pazia kujikinga nao, kisha tukampeleka Malaika wetu aliyejimithilisha kwake (kama) mtu kamili.

18. (Maryam) akasema: Hakika mimi najikinga kwa Mwingi wa rehema aniepushe nawe, ikiwa unamuogopa (Mwenyeezi Mungu).

19. (Malaika) akasema: Hakika mimi ni mjumbe wa Mola wako, ili nikupe mwana mtakatifu,

20. Akasema: Ninawezaje kupata mtoto hali hajanigusa mwanamume yeyote wala mimi si asherati.

21. (Malaika) akasema: Ni kama hivyo, Mola wako amesema; Haya ni rahisi kwangu, Na ili tumfanye Muujiza kwa watu na rehema itokayo kwetu, na ni jambo limekwisha hukumiwa.

22. Basi akachukua mimba yake, na akaondoka naye mpaka mahala pa mbali.

23. Kisha uchungu ukampeleka penye shina la mtende, akasema: Laiti ningekufa kabla ya haya, na ningekuwa niliyesahaulika kabisa.

24. Mara ikamfikia sauti kutoka chini yake: Usihuzunike, hakika Mola wako ameweka kijito chini yako.

25, Na litikise kwako shina la mtende, litakuangushia tende nzuri, zilizoiva,

26. Basi ule na unywe na uburudishe macho, na kama ukimwona mtu yeyote useme; Hakika mimi nimeweka nadhiri kwa Mwingi wa rehema ya kufunga swaumu, kwa hiyo leo sitasema na mtu.

27. Kisha akampeleka kwa jamaa zake akimbeba. Wakasema: Ewe Maryam! hakika umeleta kitu cha ajabu.

28. Ewe dada ya Harun! baba yako hakuwa mtu mbaya wala mama yako hakuwa asherati.

29. Ndipo akaashiria kwake, wakasema: Tuzungumzeje na mdogo yumo katika mlezi?

30. Akasema: Hakika mimi ni mja wa Mwenyeezi Mungu, amenipa Kitabu na amenifanya Nabii.

31. Na amenifanya mbarikiwa popote nilipo, na ameniusia swala na zaka maadamu ningali hai.

32. Na kumfanyia mema mama yangu wala hakunifanya niwe jeuri, muovu.

33. Na amani ikojuu yangu siku niliyozaliwa na siku nitakayokufa, na siku nitakayofufuliwa kuwa hai.

34. Huyo ndiye Isa bin Maryam, ndiyo kauli ya haki ambayo wanaifanyia shaka.

35. Haiwi kwa Mwenyeezi Mungu kufanya mtoto, ametakasika, anapolitaka jambo basi huliambia; Kuwa nalo huwa.

36. Na hakika Mwenyeezi Mungu ni Mola wangu na Mola wenu, basi muabuduni, hii ni njia iliyonyooka.

37. Lakini makundi yakakhitilafiana wao kwa wao, basi ole kwa wale waliokufuru kwa kuhudhuria siku iliyokuu.

38. Watasikia na wataona vizuri vilioje siku watakayotufikia, lakini madhalimu siku hiyo watakuwa katika upotovu ulio dhahiri.

39. Na uwaonye siku ya majuto shauri litakapokatwa, nao wamo katika usahaulifu wala hawaamini.

40. Bila shaka sisi tutairithi ardhi na walioko juu yake, na kwetu watarejeshwa.

41. Na mtaje Ibrahimu katika Kitabu kwani yeye alikuwa mkweli sana, Nabii.

42. Alipomwambia baba yake: Ewe baba yangu! kwa nini unamuabudu asiyesikia na asiyeona wala asiyekufaa chochote.

43. Ewe baba yangu! kwa hakika imenifikia elimu isiyokufikia basi nifuate nitakuongoza njia iliyo sawa.

44. Ewe baba yangu! usimwabudu shetani hakika shetani ni muasi kwa Rahmani.

45. Ewe baba yangu! hakika mimi naogopa kwamba itakugusa adhabu kutoka kwa Rahmani, hivyo utakuwa rafiki ya shetani.

46. Akasema: je, unaichukia miungu yangu, ewe Ibrahim? kama huachi lazima nitakupiga mawe na uniondokelee mbali kwa muda.

47. (Ibrahim) akasema: Amani iwe juu yako, nitakuombea msamaha kwa Mola wangu, kwani yeye ananihurumia sana.

48. Na mimi najitenga nanyi na mnayoyaabudu kinyume cha Mwenyeezi Mungu, na nitamuomba Mola wangu. Huenda nisiwe mwenye kukosa bahati kwa kumuomba Mola wangu.

49. Basi alipojitenga nao na wanayoyaabudu kinyume cha Mwenyeezi Mungu, tukampa Isihaka na Yaakub, na kila mmoja tukamfanya Nabii.

50. Na tukawapa rehema zetu, na tukawafanyia sifa za kweli tukufu.

51. Na mtaje Musa katika Kitabu, hakika yeye alikuwa mwenye kusafishwa, na alikuwa Mtume, Nabii.

52. Na tukamwita upande wa kulia wa mlima, na tukamsogeza kuzungumza naye kwa siri.

53. Nasi tukampa katika rehema zetu nduguye Harun, Nabii.

54. Na mtaje katika Kitabu Ismail kwani yeye alikuwa mkweli wa ahadi, na alikuwa Mtume Nabii.

55. Na alikuwa akiwaamrisha watu wake swala na zaka na alikuwa maridhawa mbele ya Mola wake.

56. Na mtaje Idrisa katika Kitabu, kwani yeye alikuwa mkweli sana, Nabii.

57. Na tulimuinua daraja ya juu kabisa.

58. Hao ndio aliowaneemesha Mwenyeezi Mungu, miongoni mwa Manabii, katika kizasi cha Adamu, na katika kizazi cha wale tuliowachukua pamoja na Nuhu, na katika kizazi cha Ibrahimu na Israeli, na katika wale tuliowaongoza na kuwachagua. Wanaposomewa Aya za Rahman huanguka wakasujudu na kulia.

59. Lakini wakafuatia baada yao watoto wabaya, wakapuuza swala na wakafuata matamanio mabaya kwa hiyo watakutana na adhabu kali.

60. Isipokuwa anayetubu na kuamini na kufanya yaliyo mema basi hao wataingia Peponi wala hawatadhulumiwa chochote.

61. Pepo za milele ambazo Mwingi wa rehema amewaahidi waja wake zilizo katika siri bila shaka ahadi yake ni yenye kufika.

62. Hawatasikia humo upuuzi ila amani, na humo watapata riziki zao asubuhi na jioni,

63. Hiyo ndiyo Pepo tutakayomrithisha katika waja wetu yule ambaye ni mcha Mungu.

64, Wala hatuteremki ila kwa amri ya Mola wako, anayo yaliyoko mbele yetu na yaliyoko nyuma yetu na yaliyomo katikati ya hayo, na Mola wako si Mwenye kusahau.

65. Mola wa mbingu na ardhi na vilivyomo kati yake, basi muabudu yeye na udumu katika ibada yake, Je unamjua (mwingine) mwenye jina (kama) lake.

66. Na mwanadamu husema: Je, nitakapokuwa nimekufa, kweli nitafufuliwa kuwa hai?

67. Je mwanadamu hakumbuki kwamba tulimuumba kabla hali hakuwa chochote?

68. Basi kwa kiapo cha Mola lazima tutawakusanya wao pamoja na mashetani, kisha bila shaka tutawahudhurisha pembezoni mwa Jahannam wakiangukia magoti.

69. Kisha bila shaka tutawatoa katika kila taifa wale miongoni mwao waliomuasi zaidi Mwingi wa rehema.

70. Tena hakika sisi tunawafahamu sana wanaostahili zaidi kuunguzwa humo.

71. Wala hakuna yeyote katika nyinyi ila ni mwenye kuifikia. Ni wajibu wa Mola wako uliokwisha hukumiwa.

72. Kisha tutawaokoa wale wamchao (Mungu) na tutawaacha wale madhalimu humo wamepiga magoti.

73. Na wanaposomewa Aya zetu zilizo wazi, husema wale waliokufuru kuwaambia walioamini: Lipi katika makundi mawili lina makao mema na lenye watu walio watukufu?

74. Na vizazi vingapi tumeviangamiza kabla yao vilivyokuwa na vifaa vizuri mno na virembo zaidi?

75. Sema: Aliye katika upotovu basi Mwingi wa rehema atampa muda mpaka wayaone waliyoonywa, ikiwa ni adhabu au ikiwa ni ile saa. Ndipo watajua ni nani mwenye makao mabaya na mwenye askari dhaifu.

76. Na Mwenyeezi Mungu huwazidishia uongofu wale walio ongoka, navitendo vizuri vibakiavyo ni bora katika malipo mbele ya Mola wako na bora katika matokeo.

77. Je, umemuona yule aliyezikataa Aya zetu na akasema: Kwa hakika nitapewa mali na watoto.

78. Je, amepata khabari za ghaibu au amechukua ahadi kwa Mwingi wa reherna?

79. Siyo, Tunaandika anayoyasema, na tutamzidishia muda katika adhabu.

80. Na tutamrithi anayoyasema, na atatufika peke yake.

81. Na walifanya waungu badala ya Mwenyeezi Mungu ili wawe nguvu kwao.

82. Siyo, watakataa ibada yao na watakuwa makhasimu zao.

83. Je, huoni kuwa tumewatuma mashetani juu ya makafiri wanaowachochea sana?

84. Basi usiwafanyie haraka hakika sisi tunawahesabia idadi (ya siku zao).

85. Siku tutakayowakusanya wacha Mungu kuwapeleka kwa Rahmani kuwa ni wageni.

86. Na tutawaswaga waovu kwenye Jahannam hali wana kiu.

87. Hawatakuwa na mamlaka ya kufanya uombezi ila yule aliyeshika ahadi kwa Rahmani.

88. Nao husema: Rahmani amejifanyia mtoto.

89. Bila Shaka mmeleta jambo lichukizalo.

90. Zinakaribia mbingu kupasuka kwa (tamko) hilo na ardhi kupasuka na milima kuanguka vipande vipande.

91. Kwa kule kudai kuwa Rahmani ana mtoto.

92. Wala haiwi kwa Rahmani kuwa na mtoto.

93. Hakika yeyote aliyomo mbinguni na ardhini ila atafika kwa Rahmani hali ni mtumwa.

94. Kwa hakika amewadhibiti na amewahesabu sawa sawa.

95. Na kila mmoja wao atamfikia siku ya Kiyama peke yake.

96. Hakika wale walioamini na kufanya vitendo vizuri Rahmani atawafanyia mapenzi.

97. Na hakika tumeirahisisha (Qur'an) kwa lugha yako ili uwabashirie kwayo wanaomcha (Mungu) na uwaonye kwayo watu wabishi.

98. Na vizazi vingapi tumeviangamiza kabla yao? Je, unawaona hata mmoja wao au kusikia shindo lao?