18. SUURATUL – KAHF

Sura hii imeteremshwa Makka,   na ina Aya 110.

Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

1. Kila sifa njema ni ya Mwenyeezi Mungu ambaye amemteremshia mja wake Kitabu, wala hakukifanyia tenge.

2. Kimetengenea vizuri, ili kiwaonye watu adhabu kali itokayo kwake, na kiwape khabari njema wenye kuamini ambao wanafanya vitendo vizuri, kwamba watapata malipo mema.

3. Wakae humo milele.

4. Na kiwaonye wale wanaosema: Mwenyeezi Mungu amejifanyia mtoto.

5. Wao hawana elimu ya (jambo) hili, wala baba zao, ni neno kubwa litokalo katika vinywa vyao, hawasemi ila uongo tu.

6. Basi huenda utajiangamiza nafsi yako kwa kusikitikia hali yao ikiwa hawayaamini mazungumzo haya!

7. Kwa hakika tumevifanya vilivyokojuu ya ardhi viwe mapambo yake, ili tuwajaribu ni nani katika wao mwenye vitendo vizuri zaidi.

8. Na hakika sisi ndio tunaofanya vilivyoko juu yake kuwa ardhi kame.

9, Je, unafikiri kwamba watu wa pangoni na (wenye khabari) zilizoandikwa walikuwa ajabu katika hoja zetu?

10. Vijana hao walipokimbilia katika pango na wakasema Mola wetu! utupe rehema kutoka kwako, na ututengenezee muongozo katika jambo letu.

11. Basi tukaziba masikio yao katika pango kwa muda wa miaka mingi.

12. Kisha tukawafufua ili tujue ni lipi katika makundi mawili litakalohesabu sawa sawa muda waliokaa.

13. Sisi tunakusimulia khabari zao kwa kweli. Hakika wao ni vijana walio mwamini Mola wao, nasi tukawazidisha katika muongozo.

14. Na tukaziimarisha nyovo zao waliposimama na wakasema: Mola wetu ni Mola wa mbingu na ardhi, kabisa hatutamuabudu mungu mwingine badala Yake, bila shaka tutakuwa tumesema ubaya uliopitiliza.

15. Hawa watu wetu wamefanya waungu badala Yake. Kwa nini hawaleti juu yao dalili bayana? Basi ni nani dhalim mkubwa kuliko yule amzuliae Mwenyeezi Mungu uwongo.

16. Na mlipokuwa mmejitenga nao na vile wanavyoviabudu badala ya Mwenyeezi Mungu, basi kimbilieni pangoni, Mola wenu atakufungulieni katika rehema zake na atakufanyieni wepesi katika mambo yenu.

17. Na unaliona jua linapopanda linapita mbali na pango lao upande wa kulia, na linapokucha linawakata upande wa kushoto, nao wamo katika uwazi wa pango. Hizo ni katika Ishara za Mwenyeezi Mungu ambaye Mwenyeezi Mungu anamuongoza, basi yeye ndiye aliyeongoka, na anayempoteza, basi hutampatia mlinzi (wala) kiongozi (wa kumuongoza).

18. Na unawadhani wako macho na hali wamelala, na tunawageuza upande wa kulia na upande wa kushoto. Na mbwa wao kanyoosha mikono yake kizingitini, kama ungewaona, lazima ungegeuka kuwakimbia, na bila shaka ungejazwa khofu juu vao.

19. Na kama hivyo tuliwafufua ili waulizane baina yao. Akasema msemaji katika wao: Mmekaa muda gani? wakasema: Tumekaa siku moja au sehemu ya siku (wengine) wakasema Mola wenu anajua zaidi muda mliokaa; Basi mtumeni mmoja wenu pamoja na fedha yenu hii aende mjini, na akatazame chakula (chake) kipi ni kizuri zaidi kisha awaleteeni chakula katika hicho. Na afanye mambo haya kwa busara wala asikutajeni kabisa kwa yeyote.

20. Kwani wao wakikujueni mlipo watakupigeni mawe au watakurudisheni katika dini yao, na hapo hamtafaulu kabisa.

21. Na hivyo tukawatambulisha kwa watu ili wapate kujua kwamba ahadi ya Mwenyeezi Mungu ni ya kweli, na kwamba Kiyama hakina shaka. (Na kumbukeni) walipozozana baina yao juu ya jambo lao, na wakasema; Jengeni jengo juu yao, Mola wao anawajua sana wakasema wale walioshinda katika shauri lao: Lazima sisi tutajenga Msikiti juu yao.

22. (Wengine) watasema: Walikuwa watatu, wanne wao ni mbwa wao, na (wengine) wanasema: walikuwa watano, wasita wao ni mbwa wao, kwa kusikia yasiyoonekana. Na (wengine) wanasema: walikuwa saba, na wanane wao ni mbwa wao. Sema: Mola wangu ndiye ajuaye sawa sawa hesabu yao, hakuna anayewajua isipokuwa wachache tu. Basi usibishane juu yao ila kwa mabishano yanayoshinda, wala usiulize khabari zao kwa yeyote.

23. Wala usiseme kabisa juu ya jambo lolote: Hakika mimi nitalifanya kesho.

24. Isipokuwa Mwenyeezi Mungu apende. Na mkumbuke Mola wako unaposahau, na sema: Hakika Mola wangu ataniongoza (njia) iliyo karibu zaidi na muongozo kuliko hii.

25. Na walikaa katika pango lao miaka mia tatu na wakazidisha (miaka) tisa.

26. Sema: Mwenyeezi Mungu anajua sana muda waliokaa. Ni zake siri za mbingu na ardhi, ndiye aonaye sana na asikiaye sana wao hawana mlinzi badala yake, wala yeye hamshirikishi yeyote katika hukumu yake.

27. Na usome yaliyofunuliwa kwako katika Kitabu cha Mola wako, hakuna awezaye kubadilisha maneno yake nawe hutapata kimbilio kinyume chake.

28. Na ujiweke pamoja na wale wanaomuabudu Mola wao asubuhi na jioni wakitaka radhi yake, wala macho yako yasiwaruke, kwa kutaka mapambo ya maisha ya dunia. Wala usimtii ambaye tumeughafilisha moyo wake asitukumbuke, naye akafuata matamanio yake, na mambo yake yamepita kiasi.

29. Na sema: Ukweli umetoka kwa Mola wenu, basi anayependa akubali, na anayependa basi akatae. Hakika tumewaandalia madhalimu Moto ambao kuta zake zitawazunguka. Na wakiomba msaada, watasaidiwa kwa maji kama shaba iliyoyeyuka, yatakayoziunguza nyuso, kinywaji kibaya kilioje, na mahala pabaya palioje.

30. Hakika wale walioamini na kufanya vitendo vizuri, hakika sisi hatupotezi malipo ya yule anayefanya vitendo vizuri.

31. Hao watapata Bustani za milele, zinazopita mito chini yao, humo watapambwa bangili za dhahabu na watavaa nguo za kijani za hariri laini na za hariri nzito, wanaegemea humo juu ya vitanda vilivyopambwa. Ni malipo mazuri yaliyoje, na mahala bora palioje.

32. Na wapigie mfano wa watu wawili: Mmoja wao tulimpa bustani mbili za mizabibu na tukazizungushia mitende, na pia katikati yake tukatia shamba la nafaka.

33. Hizo bustani mbili zilizaa matunda yao wala hazikupunguza chochote, na ndani yake tukapitisha mto.

34. Na akawa na mali (mengine pia) Basi akamwambia swahibu yake hali akibishana naye: Mimi nina mali nyingi kuliko wewe na (nina) nguvu zaidi kwa wafuasi.

35. Na akaingia bustani yake hali ya kujidhulumu nafsi yake. Akasema: sidhani kabisa kuwa hii itaharibika.

36. Wala sidhani kuwa Kiyama kitatokea, na kama nikirudishwa kwa Mola wangu, lazima nitakuta kikao chema kuliko hiki.

37. Swahibu yake akamwambia hali ya kubishana naye: Je, umemkufuru yule aliyekuumba kwa udongo, tena kwa tone la manii, kisha akakufanva :mtu kamili?

38. Lakini (mimi naamini) yeye Mwenyeezi Mungu ndiye Mola wangu, wala simshirikishi Mola wangu na yeyote.

39. Na ulipoingia katika bustani yako mbona hukusem apendayo Mwenyeezi Mungu (ndiyo huwa) nguvu haipatikani ila kwa Mwenyeezi Mungu tu. Ikiwa unaniona mimi ninayo mali kidogo na watoto wachache kuliko wewe.

40. Basi huenda Mola wangu akanipa kilicho bora  kuliko bustani yako na kuipelekea mapigo ya radi kutoka mbinguni na ikawa ardhi tupu inayoteleza.

41. Au maji yake yawe yenye kuzama hata usiweze kuyatafuta.

42. Na mali yake yakaangamizwa na akawa anapindua pindua viganja vyake kwa ajili ya alichokigharamia, nayo imeanguka juu ya mapaa yake, na akasema: Laiti nisingelimshirikisha Mola wangu na yeyote.

43. Wala hakuwa na kundi la kumsaidia kinyume na Mwenyeezi Mungu wala mwenyewe hakuweza kujisaidia.

44. Huko ufalme ni wa Mwenyeezi Mungu, Mkweli, yeye ni Mbora kwa malipo na Mbora kwa kuleta matokeo.

45. Na wapigie mfano wa maisha ya dunia ni kama maji tunayoyateremsha kutoka mawinguni, na yakachanganyika na mimea ya ardhi, kisha ikawa. majani makavu yaliyo katikakatika ambapo upepo huyasambaza. Na Mwenyeezi Mungu ana uwezo juu ya kila kitu.

46. Mali na watoto ni pambo la maisha ya dunia. Na vitendo vizuri vibakiavyo ndivyo bora mbele ya Mola wako kwa malipo na tumaini bora.

47. Na siku tutakayoipitisha milima, na utaiona ardhi iwazi, nasi tutawafufua wala hatutamuacha (hata) mmoja katika wao.

48. Na watahudhurishwa mbele ya Mola wako kwa safu, (kisha waambiwe);

bila shaka mmetufikia kama tulivyokuumbeni mara ya kwanza. Lakini mlidhani kuwa hatukukuwekeeni miadi.

49. Na daftari itawekwa (mbele yao) ndipo utawaona waovu wanaogopa kwa sababu ya yale yaliyomo, na watasema: Ole wetu! namna gani daftari hili haliachi dogo wala kubwa ila inalihesabu. Na watakuta waliyoyafanya yamehudhurishwa, na Mola wako hamdhulumu yeyote.

50. Na (kumbukeni) tulipowaambia Malaika: Mtiini Adamu, basi wakamtii isipokuwa Iblis, alikuwa miongoni mwa majinni, na akavunja amri ya Mola wake, Je, mnamfanya yeye na kizazi chake kuwa viongozi badala yangu, hali wao ni maadui zenu? Ni ovu mno badala hii kwa wenye kudhulumu.

51. Sikuwashuhudisha kuumbwa kwa mbingu na ardhi wala kuumbwa kwa nafsi zao, wala sikuwafanya wapotezao kuwa wasaidizi (wangu).

52. Na (kumbukeni) siku atakayosema (Mwenyeezi Mungu) Waiteni washirika wangu ambao mlidai (kuwa washirika wangu) basi watawaita, lakini hawatawaitikia, na kati yao tutatia kinga.

53. Na waovu watauona Moto, na watajua kwamba karibu wao wataingia humo, wala hawatapata pa kuepukia.

54. Na bila shaka tumewaelezea watu namna kwa namna katika Qur'an hii kila mfano, lakini mwanadamu amezidi kila kitu kwa ubishi.

55. Na haikuwazuia watu kuamini ulipowafikia muongozo na kuomba msamaha kwa Mola wao isipokuwa wanangoja iwafikie hali ya watu wa kwanza au adhabu iwafikie ana kwa ana.

56. Na hatuwaleti Mitume ila wawe watoaji wa khabari njema na waonyaji. Na wale waliokufuru wanashindana kwa uongo ili kwa mambo hayo waibatilishe haki, na wanazifanya Aya zangu na yale waliyoonywa kuwa ni mzaha.

57. Na ni nani dhalimu mkubwa kuliko yule anaye kumbushwa Aya za Mola wake lakini anazipuuza, na akayasahau iliyotanguliza mikono yake? Hakika sisi tumetia nyoyoni mwao vifuniko wasije kuifahamu, na katika masikio yao (tumetia) uzito, na ukiwaita kwenye muongozo hawakubali kabisa kuongoka.

58. Na Mola wako ndiye Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu, kama angewatesa kwa sababu ya yale waliyoyachuma, bila shaka angewapa adhabu upesi upesi, lakini wanayo miadi ambayo hawatapata kimbilio kuepukana nayo.

59. Na miji hiyo, tuliwaangamiza walipodhulumu na tukawawekea miadi ya maangamio yao.

60. Na (Kumbukeni) Musa alipomwambia kijana wake: Sitasimama mpaka nifike penye maungano ya bahari mbili au niendelee karne na karne.

61. Basi walipofika wote wawili (mahala) zinapoungana, wakamsahau samaki wao, naye akashika njia yake baharini kwa upesi.

62. Na walipofika mbele, (Musa) akamwambia kijana wake: Tupe chakula chetu cha mchana, maana tumepata uchovu katika safari yetu hii.

63. Akasema: Unaona! pale tulipopumzika katika mlima, basi hapo nimemsahau yule samaki, na hakuna aliyenisahaulisha isipokuwa shetani, nisikumbuke, naye akashika njia yake baharini kwa namna ya ajabu.

64. (Musa) akasema: Hapo ndipo tulipokuwa tunapataka. Basi wakarudi nyuma kwa kufuata nyayo zao.

65. Basi wakamkuta mja katika waja wetu, tuliyempa reherna kutoka kwetu, na tuliyemuelimisha elimu kutoka kwetu.

66. Musa akamwambia: Je, nikufuate ili unifundishe katika ule muongozo uliofundishwa?

67. Akasema: Hakika wewe huwezi kuvumilia kuwa pamoja nami.

68. Na utawezaje kuvumilia yale usiyoyajua hakika yake?

69. Akasema: Akipenda Mwenyeezi Mungu, utaniona mvumilivu, wala sita asi amri yako.

70. Akasema: Basi kama utanifuata, usiniulize juu ya chochote, mpaka mimi nianze kukuambia.

71. Basi wote wawili wakaondoka, hata walipopanda jahazi (yule mtu) akaitoboa. (Musa) akasema: Je, umeitoboa ili uwazamishe waliomo? Hakika umefanya jambo baya.

72. Akasema: Je, sikusema kuwa hakika wewe huwezi kuvumilia kuwa pamoja nami?

73. (Musa) akasema: Usinichukulie kwa kule kusahau kwangu, wala usinitie katika taabu kwa jambo langu (hili).

74. Basi wote wawili wakaendelea hata wakamkuta kijana na (yule mtu) akamuua. (Musa) akasema: Je, umemuua mtu asiye na kosa wala hakumuua mtu? Bila shaka umefanya jambo baya.

75. (Yule mtu) Akasema, je sikukuambia hakika wewe huwezi kuvumilia kuwa pamoja nami?

76. (Musa) akasema: Nikikuuliza juu ya chochote baada ya haya, basi usinifanye swahibu, maana umekwisha pata udhuru kwangu.

77. Basi wakaendelea hata walipowafikia watu wa mji, wakawaomba wenyeji wake chakula, lakini wakakataa kuwakaribisha. Wakakuta humo ukuta unataka kuanguka na (yule mtu) akausimamisha. (Musa) akasema kama ungetaka, bila shaka ungeichukulia (kazi hii) malipo.

78. (Yule mtu) Akasema: Huku ndiko kufarikiana baina ya mimi na wewe, (hivi sasa) nitakuambia hakika ya yale ambayo hukuweza kuyavumilia.

79. Ama ile jahazi, ilikuwa ya masikini wafanyao kazi baharini, na nilitaka kuiharibu, na nyuma yao alikuwako mfalme anakamata majahazi yote.

80. Na ama yule kijana, basi wazazi wake walikuwa waumini, na tukakhofia kwamba asije akawapelekea katika uasi na ukafiri.

81. Basi tulitaka Mola wao awabadilishie (mtoto) aliye bora kuliko yeye kwa kutakasika na aliye karibu zaidi kwa huruma.

82. Na ama ukuta, basi ulikuwa wa watoto wawili mayatima mjini, na chini yake kulikuwa khazina yao, na baba yao alikuwa mwema kwa hiyo Mola wako alitaka wafikie baleghe yao, na waiitolee khazina yao. Ni rehema kutoka kwa Mola wako, nami sikulifanya kwa amri yangu, hiyo ndiyo hakika ya yale ambayo hukuweza kuyavumilia.

83. Nawanakuuliza khabari za Dhul Qarnayn, sema: Nitakusomeeni baadhi ya hadithi yake.

84. Hakika sisi tulimtia nguvu katika ardhi, na tukampa niia za kupatia kila kitu.

85. Ndipo akaifuata njia.

86. Mpaka alipofika machweo ya Jua, akaliona linatua katika chemchem iliyovurugika na pale akawakuta watu tukasema: Ewe Dhul Qarnayn! waadhibu au wafanyie wema.

87. Akasema: Ama anayedhulumu basi tutamuadhibu, kisha atarudishwa kwa Mola wake, naye atamuadhibu adhabu mbaya.

88. Na yule mwenye kuamini na kufanya vitendo vizuri atapata malipo mema nasi tutamanyia lililo jepesi katika amri yetu.

89. Kisha akaifuata njia.

90. Hata alipofika matokeo yajua, aliliona linawatokea watu tusiowawekea pazia la kuwakinga nalo.

91. Ni kama hivyo, na tulikuwa tunazijua vizuri khabari zilizokuwa pamoja naye.

92. Kisha akaifuata njia.

93. Hata alipofika kati kati ya milima miwili, akakuta nyuma yake watu ambao hawakuwa wanafahamu lolote.

94. Wakasema: Ewe Dhul Qarnayn! HakikaYaajuju na Maajuju wanafanya uharibifu katika ardhi, basi je, tukupe malipo ili utujengee ngome (itakayotenga) baina yetu na wao?

95. Akasema: Yale ambayo Mola wangu amenimakinishia ni bora, lakini nisaidieni kwa nguvu, nitaweka boma baina yenu na wao.

96. Nileteeni vipande vya chuma, hata alipoijaza nafasi katikati ya milima miwili akasema: Pulizeni (moto) mpaka alipokifanya kile chuma kama moto, akasema: Nileteeni shaba iliyoyayuka niimwage juu yake.

97. Basi (Yaajuju na Maajuju) hawakuweza kuukwea wala hawakuweza kuutoboa.

98 Akasema: Hii ni rehema itokayo kwa Mola wangu, na itakapofika ahadi ya Mola wangu, atauvunjavunja, na ahadi ya Mola wangu ni kweli.

99. Na tutawaacha baadhi yao siku hiyo wakiwasonga wengine, na litapulizwa baragumu, ndipo tutawakusanya wote pamoja.

100. Na tutaileta Jahannam siku hiyo mbele ya makafiri ana kwa ana.

101. Ambao macho yao yalikuwa katika pazia yasijali mawaidha yangu, na walikuwa hawawezi kusikia.

102. Je wale waliokufuru wanadhani kuwa kuwafanya waja wangu kuwa viongozi badala yangu. Hakika sisi tumeiandaa Jahannam iwe mahala pa kuteremkia makafiri.

103. Sema: Je, tukuambieni wenye khasara zaidi kwa vitendo.

104. Ambao bidii yao imepotea katika maisha ya dunia, nao wanafikiri kwamba wanafanya vitendo vizuri.

105. Hao ndio waliozikataa hoja za Mola wao na kukutana naye. Kwa hiyo vitendo vyao vimeharibika, wala hatutawasimamishia mizani siku ya Kiyama.

106. Hiyo Jahannam ni malipo yao kwa sababu walikufuru na kuzifanyia kejeli Aya zangu na Mitume wangu.

107. Kwa hakika walioamini na kufanya vitendo vizuri makazi yao yatakuwa Pepo za Firdaws.

108. Watakaa humo milele, hawatataka mabadiliko kutoka humo.

109. Sema: Kama bahari ingelikuwa wino kwa (kuyaandika) maneno ya Mola wangu, bila shaka bahari ingelikwisha kabla ya kwisha maneno ya Mola wangu, hata kama tungelileta (bahari) kama hiyo kuongezea.

110. Waambie: Bila shaka mimi ni binadamu kama nyinyi, ninaletewa Wahyi kwamba Mungu wenu ni Mungu Mmoja tu. Basi anayetumaini kukutana na Mola wake na afanye vitendo vizuri wala asimshirikishe yeyote katika ibada ya Mola wake.