SUURATUR RAA'DI

Sura hii imeteremshwa Madina, na ina Aya 43

Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu

1. Alif Lam Mym Ra. Hizo ni Aya za Kitabu. Na uliyoteremshiwa kutoka kwa Mola wako ni haki, lakini watu wengi hawaamini.

2. Mwenyeezi Mungu ndiye aliyeziinua mbingu bila ya nguzo mnazoziona kisha akakamilisha (uumbaji) katika Arshi, na akalitiisha (kwenu) jua na mwezi, kila kimoj/a kinaendelea mpaka rnuda ulio wekwa. Yeye ndiye anayeliendesha (kila) jambo, anazipambanua Aya ili mpate yakini ya kukutana na Mola wenu.

3. Naye ndiye aliyeitandaza ardhi na akaweka humo majabali na mito. Na kila matunda akafanya humo viwili viwili dume na jike, huufunika usiku juu ya mchana, hakika katika hayo zimo dalili kwa watu wenye kufikiri.

4. Na katika ardhi mna vipande vilivyokaribiana, na bustani za mizabibu na mimea (mingine) na mitende ichipuayo katika shina moja na isiyochipua, katika shina moja. Vyote vinanyweshwelezwa kwa maji yale yale, na tunavifanya bora baadhi yake kuliko vingine katika kula, hakika katika hayo mnadalili kwa watu wanaofahamu.

5. Na kama ukistaajabu basi cha ajabu ni usemi wao: Je, tutakapokuwa mchanga, kweli tutakuwa katika umbo jipya? Hao ndio waliomkufuru Mola wao, na hao ndio wenye minyororo katika shingo zao, na hao ndio watu wa Motoni, humo watakaa milele.

6. Na wanakuhimiza (ulete) mabaya kabla ya mema, hali zimekwisha pita adhabu za kupigiwa mfano kabla yao. Na hakika Mola wako ni Mwenye msamaha kwa watu juu ya dhulma yao, na hakika Mola wako ni Mkali wa kuadhibu.

7. Na wanasema wale waliokufuru, mbona hakuteremshiwa dalili kutoka kwa Mola wake? Hakika wewe ni muonyaji tu, na kila kaumu ina Kiongozi.

8. Mwenyeezi Mungu anajua abebacho kila mwanamke, na yanavyoviharibu rnatumbo na yanavyovizidisha. Na kila kitu kiko kwake kwa kipimo.

9. Mjuzi wa siri na dhahiri, Mkuu aliye juu.

10. Ni sawa (kwake) anayeficha kauli miongoni mwenu na anayeidhihirisha na ajifichaye usiku na aendaye mchana.

11. (Kila mtu) anakundi (la Malaika) mbele yake na nyuma yake, wanamlinda kwa amri ya Mwenyeezi Mungu. Hakika Mwenyeezi Mungu habadili yaliyoko kwa watu mpaka wabadili yaliyomo katika nafsi zao. Na Mwenyeezi Mungu anapowatakia watu adhabu, basi hakuna cha kuzuia wala hawana mlinzi yeyote badala yake.

12. Yeye ndiye ambaye anayekuonyesheni umeme kwa khofu na tamaa, na huyaleta mawingu mazito.

13. Na radi inamsabihi kwa sifa zake na Malaika (humsabihi) kwa kumuogopa, na hupelekea mapigo ya radi na kumpiga nayo amtakaye, nao wanabishana juu ya Mwenyeezi Mungu hali yeye ni Mkali wa kuadhibu.

14. Kwake ndiyo maombi ya haki, na wale wanaowaomba badala yake hawawajibu chochote, isipokuwa kama yule anyooshaye mikono yake miwili kwenye maji ili yafikie kinywani mwake, lakini hayakifikii. Na hayako maombi ya makafiri ila katika upotovu.

15. Na viliomo mbinguni na katika ardhi vinamsujudia Mwenyeezi Mungu tu vikitaka visitake. Na (pia) vivuli vyao asubuhi najioni.

16. Sema: Ni nani Mola wa mbingu na ardhi? sema: Ni Mwenyeezi Mungu. Sema je, mnafanya viongozi badala yake, ambao hawamiliki kwa ajili nafsi zao nafuu wala dhara? sema: Je wanaweza kuwa sawa kipofu na aonaye? Au vinaweza kuwa sawa giza na nuru? Au wamemfanyia Mwenyeezi Mungu washirika ambao wameumba kama kuumba kwake, kwa hiyo viumbe (vya pande mbili) vimefanana kwao? sema: Mwenyeezi Mungu ndiye Muumbaji wa kila kitu naye ni Mmoja, Mwenye nguvu.

17. Ameteremsha maji kutoka mawinguni na mabonde yakapitisha maji kwa kadiri yake, na mafuriko ya maji yakachukua mapovu yaliyo juu ya maji. Na katika vile wanavyo yeyusha katika moto kwa kutaka mapambo au vyombo vingine, (huja) povu mfano wake. Hivyo ndivyo Mwenyeezi Mungu anavyotoa mfano wa haki na batili. Basi lile povu linapita kama takataka, lakini vile vinavyowafaa watu vinakaa katika ardhi. Hivyo ndivyo Mwenyeezi Mungu anavyopiga mifano.

18. Watapata wema wale waliomwitikia Mola wao. Na wale wasiomwitikia, hata kama wangelikuwa na vilivyomo ardhini (na vingine) kama hivyo pamoja navyo, bila shaka wangelivitoa kujikombolea. Hao watakuwa na hesabu mbaya, na makao yao ni Jahannam, na ni mahala pabaya palioje!

19. Je, anayejua kuwa yaliyo teremshwa kwako kutoka kwa Mola wako ni haki, ni kama aliye kipofu? wenye akili tu ndio wanaozingatia.

20. Ambao hutimiza ahadi ya Mwenyeezi Mungu wala hawavunji mapatano.

21. Na ambao huyaunga aliyoamuru Mwenyeezi Mungu yaungwe, na humuogopa Mola wao, na huiogopa hesabu kubwa.

22. Na ambao husubiri kwa kutaka radhi ya Mola wao, na wakasimamisha swala na wakatoa katika vile tulivyo wapa, kwa siri na dhahiri, na wakayaondoa maovu kwa mema, hao ndio watakaopata malipo (mema) ya nyumba (ya Akhera).

23. Bustani za milele, wataziingia wao na waliofanya wema miongoni mwao baba zao na wake zao na kizazi chao na Malaika watawaingilia katika kila mlango.

24. Amani juu yenu, kwa sababu mlisubiri, basi ni mema yaliyoje matokeo ya nyumba (ya Akhera).

25. Na wale wanaovunja ahadi ya Mwenyeezi Mungu baada ya kuifunga, na wanakata aliyoyaamuru Mwenyeezi Mungu yaungwe, na wanafanya uharibifu katika ardhi, hao ndio watapata laana, watapata nyumba mbaya.

26. Mwenyeezi Mungu hukunjua riziki kwa amtakaye na hukunja. Na wamefurahia maisha ya dunia, hali maisha ya dunia mbele ya Akhera si kitu ila ni starehe ndogo tu.

27. Na wanasema wale waliokufuru: Kwa nini hakuteremshiwa Muujiza kutoka kwa Mola wake? Sema: Hakika Mwenyeezi Mungu humpoteza ambaye anataka na humuongoza anayetaka kurejea kwake.

28. Wale walioamini na zikatulia nyoyo zao kwa kumkumbuka Mwenyeezi Mungu, sikilizeni! kwa kumkumbuka Mwenyeezi Mungu, nyoyo hutulia.

29. Wale walioamini na kufanya vitendo vizuri raha itakuwa yao, na marejeo mema.

30. Hivyo ndivyo tumekuleta katika watu ambao wamekwisha pita kabla yao watu wengine, ili uwasomee tunayokufunulia, na wao wanamkufuru Rahmani sema: yeye ndiye Mola wangu, hakuna aabudiwaye ila Yeye tu. Nimemtegemea na marejeo yangu ni kwake.

31. Na kama ingelikuwako Qur'an ndiyo inayoendeshewa milima, na kupasuliwa ardhi, na kusemeshewa wafu, (basi ingelikuwa Qur'ani hii). Bali mambo yote ni ya Mwenyeezi Mungu, Je, hawajajua walioamini kuwa Mwenyeezi Mungu angelipenda bila shaka angeliwaongoza watu wote? Wala msiba hautaacha kuwafikia wale waliokufuru kwa sababu ya yale waliyoyafanya au utashuka karibu na nyumba yao mpaka ifike ahadi ya Mwenyeezi Mungu, hakika Mwenyeezi Mungu havunji miadi.

32. Na kwa hakika Mitume walifanyiwa mzaha kabla yako, lakini niliwapa nafasi wale waliokufuru, kisha nikawakamata basi ilikuwaje adhabu (yangu).

33. Je aliye msimamizi juu ya kila nafsi kwa yale iliyoyachuma, na wakamfanyia Mwenyeezi Mungu washirika sema: Watajeni. Au mtamwambia asiyo yajua katika ardhi au ni maneno matupu? Bali wamepambiwa walio kufuru hila zao na wakazuiliwa njia (ya haki). Na ambaye Mwenyeezi Mungu amempoteza hana wa kumuongoza.

34. Wanayo adhabu katika maisha ya dunia na bila shaka adhabu ya Akhera ni ngumu zaidi wala hawatakuwa na wa kuwalinda kwa Mwenyeezi Mungu.

35. Mfano wa Pepo waliyoahidiwa wamchao, chini yake inapita mito. Matunda yake ni ya daima na pia kivuli chake, huo ndio mwisho wa wale wamchao Mwenyeezi Mungu na mwisho wa makafiri ni Moto.

36. Na wale tuliowapa Kitabu wanafurahia uliyoteremshiwa na katika makundi (mengine) wako wanaoyakataa baadhi yake sema: Nimeamrishwa kumwabudu Mwenyeezi Mungu tu wala nisimshirikishe, kuendea kwake ndio ninaita na kwake ni marejeo yangu.

37. Na hivyo tumeiteremsha hukumu iliyo wazi, na kama ukifuata matamanio yao baada ya kukufikia elimu hutakuwa na kiongozi wala mlinzi mbele ya Mwenyeezi Mungu.

38. Na bila shaka tuliwapeleka Mitume kabla yako, na tukawapa wake na watoto na haiyumkini kwa Mtume kuleta Muujiza isipokuwa kwa idhini ya Mwenyeezi Mungu, kila muda unayo hukumu.

39. Mwenyeezi Mungu hufuta ayatakayo na huimarisha (ayatakayo) na asili ya hukumu iko kwake.

40. Na kama tukikuonyesha baadhi ya tuliyowaahidi, au tukikufisha, basi juu yako ni kufikisha tu, na juu yetu ni kuhesabu.

41. Je hawakuona kuwa tunaifikia ardhi tukiipunguza mipaka yake? Na Mwenyeezi Mungu huhukumu, hakuna wa kuibadili hukumu yake, naye ni Mwepesi wa kuhesabu.

42. Na wamekwisha fanya vitimbi wale waliokuwa kabla yao lakini vitimbi vyote ni vya Mwenyeezi Mungu, anajua inayoyachuma kila nafsi, na makafiri watajua ni ya nani nyumba ya mwisho (Akhera).

43. Na wanasema waliokufuru: Wewe si Mtume. Sema: Mwenyeezi Mungu anatosha kuwa shahidi baina yangu na baina yenu, na (pia) yule mwenye elimu ya Kitabu.