10.SUURA YUUNUS

Sura hii imeteremshwa Makaa,  Aya 109

Kwa jina la Mwenyeezi Munga, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

1. Aliflam Raa. Hizo ni Aya za Kitabu chenye hekima.

2. Je, ni ajabu kwa watu kwarnba tumemfunulia mtu miongoni mwao kuwa: Waonye watu na wape walioamini khabari njema kwamba watakuwa na daraja kamili mbele ya Mola wao? Makafiri wakasema; Hakika huyu bila shaka ni mchawi dhahiri.

3. Hakika Mola wenu ni Mwenyeezi Mungu ambaye ameziumba mbingu na ardhi katika nyakati sita, kisha ukakamilika (uumbaii wake) katika Arshi. Anaendesha (kila) jambo, hakuna muombezi ila baada ya idhini yake. Huyo ndiye Mwenyeezi Mungu, Mola wenu, basi muabuduni, je hamkumbuki?

4. Kwake ndiyo marejeo yenu nyote, ahadi ya Mwenyeezi Mungu ni ya kweli. Hakika yeye ndiye huanzisha kiumbe kisha hukirudisha ili awalipe walioamini na kufanya vitendo vizuri kwa uadilifu. Na waliokufuru, (wao) watapata kinywaji cha maji yanayochemka na adhabu yenye kuumiza kwa sababu walikuwa wakikataa.

5. Yeye ndiye aliyefanya jua kuwa mwanga na mwezi kuwa nuru, na akaupimia vituo ili mjue idadi ya miaka na hesabu. Mwenyeezi Mungu hakuviumba hivyo ila kwa haki, anapambanua Aya (nyingi) kwa watu wanaojua.

6. Hakika katika mfuatano wa usiku na mchana na alivyoviumba Mwenyeezi Mungu katika mbingu na ardhi kuna dalili kwa watu wanao mcha Mwenyeezi Mungu.

7. Hakika wale wasiotumaini kukutana nasi, na wamekuwa radhi na maisha ya dunia na kutulia kwa hayo, na wale wanaoghafilika na Aya zetu.

8. Hao makazi yao ni Motoni kwa sababu ya yale waliyokuwa wakiyachuma.

9. Hakika wale walioamini na kufanya vitendo vizuri, Mola wao atawaongoza kwa sababu ya imani yao. Itapita mito chini yao katika Mabustani yenye neema.

10. Ibada yao humo itakuwa: Utakatifu ni wako, ewe Mwenyeezi Mungu, na maamkiano yao humo yatakuwa: Salaamun. Na maombi yao ya mwisho yatakuwa kila sifa njema ni ya Mwenyeezi Mungu Mola wa viumbe wote.

11. Na kama Mwenyeezi Mungu angeliwapa watu shari haraka kama, wanavyojihimizia kheri, bila shaka wangelitimiziwa muda wao. Lakini tunawaacha wale wasiotumaini mkutano wetu katika upotovu wao wakihangaika.

12. Na dhara inapomgusa mtu hutuomba (anapolala) ubavu, au hali ya kukaa au kusimaina lakini tunapomuondolea dhara yake hupita kama kwamba hakutuomba tumuondolee dhara iliyompata. Hivyo ndivyo wamepambiwa wapitao mipaka yale waliyokuwa wakiyatenda.

13. Na bila shaka tumekwisha viangamiza vizazi kabla yenu walipodhulumu, na waliwafikia Mitume wao kwa hoja wazi wazi, na hawakuwa wenye kuamini, hivyo ndivyo tunavyowalipa watu waovu.

14. Kisha tukakufanyeni nyinyi ndio wenye kushika mahala (pao) baada yao katika ardhi ili tuone jinsi mtakavyotenda.

14. Na wanaposomewa Aya zetu zilizo wazi, wale wasiotumaini kukutana na Sisi husema; Lete Qur'an isiyokuwa hii, au ibadilishe. Waambie: Siwezi kuibadilisha kwa hiari ya nafsi yangu, sifuati ila ninayofunuliwa kwa Wahyi. Hakika mimi naogopa nikimuasi Mola wangu, adhabu ya siku iliyo kuu.

16. Sema: Kama Mwenyeezi Mungu angelitaka nisingelikusomeeni hii (Qur'an) wala asingelikujulisheni hiyo (Qur'an). Na hakika nimekwisha kaa kati yenu umri (mrefu) kabla yake, je hamfahamu?

17. Basi ni nani dhalimu zaidi kuliko yule anaemtungia Mwenyeezi Mungu uwongo au akadhibishaye Aya zake? Hakika waovu hawafaulu

 18. Nao wanaabudu kinyume cha Mwenyeezi Mungu wasiowadhuru wala kuwanufaisha, na wanasema hawa ndio waombezi wetu mbele ya Mwenyeezi Mungu. Sema; Je, mtamwambia Mwenyeezi Mungu asiyoyajua katika mbingu wala katika ardhi? Ameepukana na upungufu na ametukuka na hao wanaowashirikisha.

19. Wala watu hawakuwa ila kundi moja tu, lakini wakakhitilafiana. Na kama si neno lililotangulia kutoka kwa Mola wako, bila shaka (shauri) lingekwisha katwa baina yao katika yale waliyokhitilafiana.

20. Na wakasema: Kwa nini haukuteremshwa Muujiza juu yake kutoka kwa Mola wake? Basi waambie; Hakika mambo ya ghaibu ni ya Mwenyeezi Mungu tu, kwa hiyo ngojeni, kwa hakika mimi  ni pamoja nanyi katika wenye kuungojea.

21. Na tunapowaonjesha watu rehema baada ya shida kuwagusa, huanza kuzitungia hila Aya zetu. Sema: Mwenyeezi Mungu ni Mwepesi zaidi wa kutunga hila, hakika wajumbe wetu wanaandika hila mnazozitunga.

22. Yeye ndiye anayekuendesheni katika bara na bahari, hata mnapokuwa katika majahazi na yanakwenda nao kwa upepo mzuri na wakafurahi nao, mara upepo mkali unayafikia na mawimbi yanawajia kutoka kila upande, na wanaanza kufikiri kwamba wametinguwa, (ndipo) wanamuomba Mwenyeezi Mungu kwa kumtakasia utii, (wakisema): Ukituokoa katika haya bila shaka tutakuwa miongoni mwa wenye kushukuru.

23. Iakini anapowaokoa, mara wanafanya maasi katika ardhi pasipo haki. enyi watu! Hakika uasi wenu utakudhuruni wenyewe tu. Ni starehe ya : maisha ya dunia, kisha marejeo yenu yatakuwa Kwetu, ndipo tutakuambieni yale mliyokuwa mkiyafanya.

24. Hakika mfano wa maisha ya dunia ni kama maji tuliyoyateremsha kutoka mawinguni, kisha mimea ya ardhini wanayokula watu na wanyama ikachanganyika pamoja, hata ardhi ilipokamilisha uzuri wake na ikapambika na wenyeji wake wakadhani kuwa wana nguvu juu yake, amri yetu ikaifikia usiku au mchana na tukaifanya imefyekwa, kama kwamba jana haikuwepo. Hivyo ndivyo tunavyozieleza Aya kwa watu wanaofikiri.

25. Na Mwenyeezi Mungu anaita kwenye Nyumba ya amani, na humuongoza anaetaka kwenye njia iliyonyooka.

26. Wale waliofanya wema watapata wema na zaidi, na vumbi halitawafunika nyuso zao wala udhalili, hao ndio watu wa Peponi, humo watakaa milele.

27. Na wale waliochuma maovu, malipo ya uovu ni kama huo, na udhalili utawafunika. hawatakuwa na wa kuwalinda na Mwenyeezi Mungu, kama kwamba nyuso zao zimefudikizwa vipande vya usiku wenye giza, hao ndio watu wa Motoni, humo watakaa milele.

28. Na (wakumbushe) siku, tutakapowakusanya wote, kisha tutawaambia wale walioshirikisha: (Simameni) mahala penu nyinyi na washirika wenu, kisha tutawatenga baina yao, na washirika wao watasema: Nyinyi hamkuwa mkituabudu sisi.

29. Basi Mwenyeezi Mungu anatosha kuwa shahidi baina yetu na baina yenu, hakika sisi tulikuwa hatuna khabari ya ibada yenu.

30. Huko kila mtu atayajua aliyoyatanguliza, na watarudishwa kwa Mwenyeezi Mungu, Mola wao wa haki, na yatawapotea yale waliyokuwa wakiyatunga.

31. Sema: Ni nani anayekuruzukuni kutoka mbinguni na ardhini? Au ni nani anaemiliki kusikia na kuona? Na ni nani anayemtoa hai kutoka maiti, na akamtoa mfu katika uzima? na ni nani atengenezaye mambo yote? Basi watasema: Ni Mwenyeezi Mungu. Waambie basi: Je hamumchi Mwenyeezi Mungu?

32. Basi huyo ndiye Mwenyeezi Mungu, Mola wenu wa haki, tena ni nini baada ya haki isipokuwa upotovu? basi mnageuzwa wapi?

33. Hivyo ndivyo ilivyothibiti kauli ya Mola wako juu ya wale walioasi, kwamba wao hawaamini.

34. Sema: Je, yuko katika washirika wenu anayeanzisha kiumbe, kisha akakirejesha? Sema: Mwenyeezi Mungu ndiye aanzishaye kiumbe kisha akakirejesha, basi mnageuzwa wapi?

35. Sema: Je, yuko katika washirika wenu aongozae kwenye haki? Sema: Mwenyeezi Mungu ndiye aongozae kwenye haki. Basi je, aongozae kwenye haki anastahiki zaidi kufuatwa au ni yule asiyeongoka isipokuwa aongozwe? Basi mmekuwaje? mnahukumu vipi?

36. Na wengi wao hawafuati ila dhana tu hakika dhana haifai hata kidogo mbele ya haki, hakika Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi wa yote wanayoyatenda.

37. Na haiwezekani hii Qur'an kuwa imezuliwa (na) haitoki kwa Mwenyeezi Mungu. Lakini inasadikisha yaliyotangulia, na ni maelezo ya Kitabu, haina shaka, imetoka kwa Mola wa viurnbe wote.

38. Je, wanasema ameitunga? Sema: Basi leteni sura moja mfano wake na muwaite muwezao asiyekuwa Mwenyeezi Mungu ikiwa nyinyi mnasema kweli.

39. Bali wameyakadhibisha wasiyoyajua elimu yake, wala hakika yake haijawafikia. Hivyo ndivyo walivyo kadhibisha waliokuwa kabla yao basi kaangalie namna ulivyokuwa mwisho wa madhalimu.

40. Na miongoni mwao yuko anayeiamini, na miongoni mwao yuko asiyeamini. Na Mola wako anawajua sana waharibifu.

41. Na kama wakikukadhibisha, basi sema: Mimi nina amali yangu na nyinyi mna amali yenu. Nyinyi hampasiwi na ninayoyatenda, wala mimi sipasiwi na mnayoyatenda.

42. Na wako miongoni mwao wanaokusikiliza, je, wewe unaweza kuwasikilizisha viziwi ingawa hawafahamu?

43. Na wako miongoni mwao wanaokutazama, je wewe unaweza kuwaongoza vipofu ingawa hawaoni?

44. Hakika Mwenyeezi Mungu hawadhulumu watu chochote, lakini watu wanajidhulumu wenyewe.

45. Na (wakumbushe) siku atakayowakusanya (wataona) kama kwamba hawakukaa (duniani) ila saa moja tu ya mchana, watajuana wao kwa wao. Hakika wamekwisha pata hasara wale walioukadhibisha mkutano wa Mwenyeezi Mungu, wala hawakuwa wenye kuongoka.

46. Na kama tukikuonyesha baadhi ya yale tunayowaonya au tukufishe, basi marejeo yao ni kwetu, kisha Mwenyeezi Mungu ni shahidi juu ya yale wanayoyatenda.

47. Na kila umma una Mtume, basi anapofika Mtume wao, inahukumiwa baina yao kwa uadilifu, nao hawadhulumiwi.

48. Na wanasema: Lini ahadi hii kama mnasema kweli?

49. Sema: Similiki kwa ajili ya nafsi yangu dhara wala nafuu, isipokuwa apendavyo Mwenyeezi Mungu. Kila umrna una muda unapofika muda wao, basi hawakawii saa moja wala hawatangulii.

50. Sema; Mnaonaje kama ikikufikieni adhabu yake usiku au mchana, sehemu gani (ya adhabu) wanaihimiza waovu?

51. Je ikisha tokea mtaiamini? Je, sasa! na hali mlikuwa mkiihimiza.

52. Kisha waliodhulumu wataambiwa: onjeni adhabu ya kudumu Hamtalipwa ila kwa yale mliyokuwa mkiyachuma.

53. Na wanakuuliza: Je, ni kweli hiyo? Sema: Ndiyo naapa kwa Mola wangu hivo ni kweli, nanyi hamuwezi kumshinda.

54. Na kama kila mtu aliyedhulumu angelikuwa na (yote) yaliyomo ardhini, bila shaka angeyatoa kujikomboa. Na watakapoiona adhabu wataficha majuto, na itahukumiwa baina yao kwa uadilifu nao hawatadhulumiwa.

55. Sikilizeni! bila shaka vilivyomo katika mbingu na ardhi ni vya Mwenyeezi Mungu sikilizeni! hakika ahadi ya Mwenyeezi Mungu ni ya haki, lakini wengi wao hawajui.

56. Yeye ndiye anayehuisha na anayefisha, na kwake mtarejeshwa

57. Enyi watu! Hakika yamekufikieni mawaidha kutoka kwa Mola wenu, na poza ya yale yaliyomo vifuani, na muongozo na rehema kwa wenye kuamini.

58. Sema: Kwa fadhili za Mwenyeezi Mungu na kwa rehema zake, basi wafurahi, hiyo ni bora kuliko wanavyovikusanya.

59. Sema: Je, mnaonaje riziki alizokuteremshieni Mwenyeezi Mungu kisha mkafanya katika hizo haramu na halali? Sema: Je, Mwenyeezi Mungu amekuruhusuni au mnamzulia Mwenyeezi Mungu uongo?

60. Na ni nini dhana ya wale wanaomzulia Mwenyeezi Mungu uongo juu ya siku ya Kiyama? Hakika Mwenyeezi Mungu ndiye Mwenye kuwafadhiii watu lakini wengi wao hawashukuru.

61. Na hushughuliki katika jambo lolote, wala husomi humo katika Qur'an, wala hamfanyi kitendo chochote, isipokuwa sisi tunakuwa mashahidi juu yenu mnapoyaingia kwa juhudi. Wala hakifichikani kwa Mola wako kitu chochote kilicho sawa na uzito wa chembe katika ardhi wala katika mbingu, wala kidogo kuliko hicho wala kikubwa, isipokuwa kimo katika Kitabu kielezacho.

62. Sikilizeni! hakika vipenzi vya Mwenyeezi Mungu hawana khofu wala wao hawahuzuniki.

63. (Hao ndio) ambao wameamini na wakawa wanamcha Mwenyeezi Mungu.

64 Wao wana bishara njema katika maisha ya dunia na katika Akhera. Hakuna mabadiliko katika maneno ya Mwenyeezi Mungu. Huko ndiko kufuzu

kukubwa.

65. Wala isikuhuzunishe kauli yao hakika utukufu wote ni wa Mwenyeczi Mungu Yeye ni Mwenye kusikia Mjuzi.

66. Sikilizeni! bila shaka vilivyomo katika mbingu na vilivyomo katika ardhi ni vya Mwenyeezi Mungu. Na wale wanaoabudu wasiokuwa Mwenyeezi Mungu, hawafuati washirikina bali wanafuata dhana tu, nao hawasemi ila uongo tu.

67. Yeye ndiye aliyekufanyieni usiku ili humo mtulie, na mchana ung'aao, hakika katika haya zimo dalili kwa watu wanaosikia.

68. Wanasema: Mwenyeezi Mungu amejifanyia mtoto! ameepukana (na hayo) yeye anajitosheleza. Ni vyake vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini, nyinyi hamna dalili kwa hayo Je, mnasema juu ya Mwenyeezi Mungu msiyoyajua?

69. Waambie: Wale wanaomzulia Mwenyeezi Mungu uongo hawatafaulu.

70. Ni starehe (chache) katika dunia, kisha kwetu ni marejeo yao, kisha tutawaonjesha adhabu kali kwa sababu walikuwa wakikufuru.

71. Na wasomee khabari za Nuhu alipowaambia watu wake: Enyi watu wangu! ikiwa cheo changu na kukumbusha kwangu Aya za Mwenyeezi Mungu yanakuchukizeni, basi mimi nategemea kwa Mwenyeezi Mungu, nanyi kusanyeni mambo yenu na washirika wenu, tena shauri lenu lisifichike kwenu, kisha mpitishe kwangu wala msinipe nafasi.

72. Lakini mkikataa, basi siwaombeni ujira, ujira wangu hauko ila kwa Menyeezi Mungu, na nimeamrisha niwe miongoni mwa wanaojisalimisha.

73. Lakini wakamkadhibisha, na tukamuokoa yeye na waliokuwa naye katika jahazi, na tukawafanya waliobakia na tukawazamisha wale waliozikadhibisha Aya zetu. Basi angalia jinsi ulivyokuwa mwisho wa wale walio onywa.

74. Kisha tukawapeleka Mitume baada yake kwa watu wao, nao wakawafikia kwa hoja wazi wazi, lakini hawakuwa wenye kuamini waliyoyakadhibisha zamani. Hivyo ndivyo tunavyopiga mihuri juu ya nyoyo za watu wanaopita mipaka.

75. Kisha baada ya hao tukawatuma Musa na Haruni kwa Firaun na wakuu wake kwa hoja zetu, lakini wakajivuna, nao walikuwa watu waovu.

76. Basi ilipowafikia haki kutoka kwetu, wakasema: Bila shaka huu ndio uchawi dhahiri.

77. Akasema Musa: Je, mnasema (hivi) Juu ya haki ilipokufikieni? Je, huu ni uchawi na wachawi hawafaulu.

78. Wakasema; je, umetujia ili utuondoe katika yale tuliyowakuta nayo baba zetu, na ili ukubwa uwe wenu wawili katika nchi'? na sisi hatuwezi kukuamini.

79. Na Firaun akasema: Nileteeni kila mchawi hodari.

80. Basi walipokuja wachawi, Musa akawaambia: Tupeni mnavyotaka kuvitupa.

81. Na walipotupa, Musa akasema: Mliyoleta ni uchawi, hakika Mwenyeezi Mungu ataubatilisha hakika Mwenyeezi Mungu hafanikishi vitendo vya waharibifu.

82. Na Mwenyeezi Mungu ataihakikisha haki kwa maneno yake ingawa watachukia waovu.

83. Basi hawakumuamini Musa isipokuwa baadhi ya vijana wa kaumu yake, kwa sababu ya kumuogopa Firaun na wakuu wao ili asiwatese. Na hakika Firaun alikuwa jeuri katika nchi, na kwa hakika yeye alikuwa miongoni mwa wapitao kiasi.

84. Na Musa akasema: Enyi kaumu yangu! ikiwa nyinyi mmemwamini Mwenyeezi Mungu basi tegemeeni kwake, kama nyinyi mmetii.

85. Basi wakasema: Tunamtegemea Mwenyeezi Mungu Mola wetu! usitufanye jaribio kwa watu madhalimu.

86. Na utuokoe kwa rehema yako katika watu makafiri.

87. Na tukampelekea Wahyi Musa na ndugu yake: Watengenezeeni majumba watu wenu katika mji na zifanyeni nyumba zenu Misikiti na simamisheni swala na wape khabari njema wenye kuamini.

88. Na Musa akasema: Mola wetu! wewe umempa Firaun na wakuu wake mapambo na mali nyingi katika maisha ya dunia, Mola wetu! hivyo wanapoteza watu katika njia yako. Mola wetu! ziangamize mali zao na zishambulie nyoyo zao, maana hawataamini mpaka waione adhabu yenye kuumimiza.

89. (Mwenyeezi Mungu) akasema: Maombi yenu yarnekubaliwa, basi kuweni imara wala msifuate njia ya wale wasiojua.

90. Na tukawapitisha wana wa Israeli katika bahari, lakini Firaun na majeshi yake wakawafuata kwa dhulma na uadui hata ilipomfikia kuzama, akasema: Naamini kwamba hakuna aabudiwaye ila yule wanayemwamini wana wa Israeli, nami ni miongoni mwa wanaotii.

91. Je, sasa! hali uliasi zamani na ukawa miongoni mwa waharibifu.

92. Basi leo tutakuokoa kwa (kuuweka) mwili wako ili uwe dalili kwa ajili ya wa nyuma yako. Na kwa kweli watu wengi wameghafilika na Aya zetu.

93. Na bila shaka tuliwaweka wana wa Israeli makazi mazuri, na tukawaruzuku katika vitu vizuri, nao hawakukhitilafiana mpaka ilipowafikia elimu. Hakika Mola wako atahukumu kati yao siku ya Kiyama katika yale waliyokuwa wakikhitilafiana.

94. Na kama unayo shaka juu ya hayo tuliyokuteremshia, basi waulize wale wasomao Kitabu kabla yao. bila shaka haki imekwisha kukufikia kutoka kwa Mola wako, kwa hiyo usiwe miongoni mwa wafanyao shaka.

95. Wala usiwe miongoni mwa wale wanaozikadhibisha Aya za Mwenyeezi Mungu, usije ukawa miongoni mwa wenye khasara.

96. Hakika wale ambao neno la Mola wako limekwisha thibitika juu yao, hawataamini.

97. Ijapo kuwa kila hoja itawafikia mpaka waone adhabu yenye kuumiza.

98. Basi mbona haukuwako mji ulioamini na imani yake ikaufaa, isipokuwa watu wa Yunus. Walipoamini tuliwaondolea adhabu ya fedheha katika maisha ya dunia na tukawastarehesha kwa muda.

99. Na kama angelitaka Mola wako, bila shaka wangeliamini wole waliomo katika ardhi. Basi je, wewe utawalazimisha watu hawa wawe waumini?

100. Na hakuna mtu anayeweza kuamini isipokuwa kwa idhini ya Mwenyeezi Mungu. Na huweka uchafu juu ya wale ambao hawatumii akili.

101. Sema: Tazameni ni nini yanayotokea katika mbingu na ardhi, na dalili (zote hizi) na maonyo hayawafai watu wasioamini.

102. Basi hawangoji ila mfano wa siku za watu waliopita kabla yao. Sema: Basi ngojeni, mimi pia ni pamoja nanyi katika wenye kungojea.

103. Kisha tukawaokoa Mitume wetu na wale walioamini. Ndio kama hivyo, inatustahiki kuwaokoa Waumini.

104. Sema: Enyi watu! ikiwa nyinyi mnayoshaka katika dini yangu, basi mimi siwaabudu wale mnaowaabudu badala ya Mwenyeezi Mungu, bali ninamuabudu Mwenyeezi Mungu ambaye anayekufisheni na nimeamrishwa niwe miongoni mwa wenye kuainini.

105. Na kwamba elekeza uso wako kwenye dini kwa nia safi, wala usiwe miongoni mwa washirikina.

106 Wala usiabudu badala ya Mwenyeezi Mungu ambao hawakufai wala hawakudhuru, na ukifanya (hivyo), basi hakika utakuwa miongoni mwa madhalimu.

107. Na kama Mwenyeezi Mungu akikugusisha dhara, basi hakuna yeyote awezaye kuiondoa isipokuwa yeye tu, na kama akikutakia kheri, basi hakuna awezaye kurudisha fadhili zake. Huzifikisha kwa amtakaye katika waja wake, naye ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.

108. Sema: Enyi watu! imekwisha wafikieni Haki kutoka kwa Mola wenu, basi anayeongoka, bila shaka anaongoka kwa faida ya nafsi yake, na anayepotea, basi hakika anapotea kwa hasara ya nafsi yake, na mimi si mlinzi juu yenu.

109. Na ufuate yanayofunuliwa kwako, na uvumilie mpaka Mwenyeezi Mungu atoe hukumu naye ndiye Mbora wa mahakimu.