1,2,3,4. Ewe uliye jigubika kwa maguo! Inuka hapo kitandani, na uwahadharishe watu na adhabu ya Mwenyezi Mungu, ikiwa hawaamini. Na mkusudie Mola wako Mlezi makhsusi kwa kumtukuza. Na safisha nguo zako kwa maji kuzitoa najisi.

Rudi kwenye Sura

5,6,7. Na iache adhabu, yaani kuwa daima mwenye kujitenga na yanayo pelekea kupata adhabu. Wala usimpe mtu yeyote kwa kutumai kupata zaidi kwake katika kile unacho mpa;  na kwa ajili ya kumridhi Mola wako Mlezi subiri na stahamili juu ya maamrisho na makatazo, na kila jambo la juhudi na mashaka.

Rudi kwenye Sura

8,9,10. Na litakapo pulizwa barugumu, huo ndio wakati wa siku ya shida kwa makafiri, wala si wepesi kwao kujitoa na majadiliano ya hisabu, na vitisho vyenginevyo.

Rudi kwenye Sura

11,12,13,14,15. Niache peke yangu na huyo niliye muumba. Kwani hakika Mimi ninatosha kukukifia mambo yake. Nimemjaalia mali yaliyo kunjuliwa yaliyo enea, yasio tindikia, na wana wanao tokea hadharani naye, na nikamkunjulia cheo na ukubwa kwa ukunjufu ulio timia. Kisha tena anatumai nimzidishie mali na wana na cheo bila ya shukrani yoyote!

Rudi kwenye Sura

16,17. Kuivunja hiyo tamaa yake, tunasema kwamba kwa kuwa yeye  alikuwa akiikaadhibisha Qur'ani kwa inda, tutamgubika kwa adhabu yenye mashaka, wala hataweza kuikwepa.

Rudi kwenye Sura

18,19,20. Hakika yeye amejifikiria nafsi yake, na akajitengenezea ya kuyasema ya kuitia ila Qur'ani, basi kwa hivyo amestahiki kuangamia huko. Vipi alivyo jiandalia kutia ila hiyo! Kisha akastahiki maangamizo hayo. Vipi alivyo jiandalia kutia ila hiyo!

Rudi kwenye Sura

21,22,23,24. Kisha akaziangalia nyuso za watu. Kisha akakunja uso wake, na akazidi kuukunja, kisha akaipa mgongo haki na akajivuna kuwa ati haitambui, na akasema: Haya si chochote ila ni uchawi ulio nukuliwa kutokana na watu wa kale.

Rudi kwenye Sura

25. Maneno haya si chochote ila ni maneno ya viumbe aliyo jifundisha Muhammad, na akadai kuwa ati yametoka kwa Mwenyezi Mungu.

Rudi kwenye Sura

26,27,28,29,30. Nitamtia Motoni aungue humo. Na nini kitakujuvya hiyo Jahannamu ni nini?  Haibakishi nyama wala haisazi fupa ila italiunguza tu, ngozi ibabuke iwe nyeusi. Juu yake wako kumi na tisa wanao angalia kazi yake, na kuwaadhibu waliomo.

Rudi kwenye Sura

31. Na hatukuwafanya walinzi wa Motoni ila ni Malaika, na wala hatukuifanya idadi yao ya kumi na tisa ila kuwapa mtihani walio kufuru wapate yakini walio pewa Kitabu (yaani Biblia, Mayahudi na Wakristo) kwamba inayo sema Qur'ani juu ya walinzi wa Motoni ni kweli tupu itokayo kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, kwa kuwa hayo yanakubaliana na vinavyo sema vitabu vyao; na ili walio muamini Muhammad ipate kuzidi Imani yao.  Na wala wasiyatilie shaka hayo walio pewa Kitabu na Waumini. Na wenye maradhi ya unaafiki katika nyoyo zao na makafiri waseme: Mwenyezi Mungu anataka nini kwa idadi hii ya ajabu? Kwa mfano kama huu ulio tajwa, wa kupoteza na kuongoa, ndio Mwenyezi Mungu huwapoteza makafiri na huwaongoa Waumini. Na hapana anaye wajua askari wa Mola wako Mlezi, jinsi walivyo kuwa wengi mno, ila Yeye Subhanahu wa Taala. Na huo Moto si chochote ila ni kumbusho na kitisho kwa binaadamu.

Rudi kwenye Sura

32,33,34,35,36. Kuzidi kumhadharisha anaye onywa naye asiogope, ninaapa kwa mwezi na usiku unapo ondoka, na kwa asubuhi inapo angaza na kuchomoza, kwamba huu Moto ni moja katika vitisho vikubwa kabisa vya kuonya na kukhofisha.

Rudi kwenye Sura

37. Ni onyo kwa binaadamu kwa atakaye kuja mbele katika nyinyi kutenda kheri, au kubaki nyuma asitende.

Rudi kwenye Sura

38,39. Kila nafsi itashikwa kwa iliyo yatenda, ila Waislamu walio zigomboa shingo zao kwa ut'iifu.

Rudi kwenye Sura

40,41,42. Hao watakuwa katika Mabustani ya Peponi, ambayo hayawezekani kusifika. Wataulizana wao kwa wao khabari za wakosefu, wakiuliza hali zao nini kilicho watia Motoni?

Rudi kwenye Sura

43,44,45,46,47. Waseme: Hatukuwa miongoni mwa wenye kusali kama wasalivyo Waislamu. Wala hatukuwa tukiwalisha masikini kama Waislamu walivyo kuwa wakilisha. Na tulikuwa tukijisoza na kuzama katika upotovu na mazungumzo ya uwongo pamoja na hao walio kuwa wakiporojoka. Na tulikuwa tukiikadhibisha Siku ya Hisabu, mpaka ikatujia yakini, yaani mauti.

Rudi kwenye Sura

48. Basi hao hakuto waokoa kuombewa msamaha na waombezi, wakiwa ni Malaika, au Manabii, au watu wema.

Rudi kwenye Sura

49. Basi wana nini hata wanajitenga na mawaidha ya Qur'ani?

Rudi kwenye Sura

50,51. Hao hakika wamekuwa  kama punda wanao toka mbio kumkimbia anaye wafukuza.

Rudi kwenye Sura

52. Bali kila mmoja wao anataka apewe ukurasa unao toka mbinguni uwazi ulio funguliwa unao thibitisha ukweli wa Mtume s.a.w. (yaani kama shahada ya Ujumbe wake kwao!)

Rudi kwenye Sura

53. Juu ya kuzidi kuwaonya kwa hayo wayatakayo bali hawaikhofu Akhera, na wakapuuza mawaidha, na wakavumbua mbinu mbali mbali za kutaka miujiza na Ishara.

Rudi kwenye Sura

54,55. Ni hakika isiyo na shaka kuwa Qur'ani ni mawaidha na ukumbusho wa kutosha kufikisha Ujumbe. Mwenye kutaka kukumbuka wala asisahau basi na atende.
Rudi kwenye Sura

56. Na wala hawatakumbuka ila Mwenyezi Mungu atake Mwenyewe, kwani Yeye ndiye anaye stahiki kuogopwa, na Yeye ndiye wa kumsamehe mwenye kumcha.

Rudi kwenye Sura