1,2,3. Hakika Sisi tumekupa, ewe Muhammad, FAT-H'I, Ushindi mkubwa unao onekana wazi kwa Haki kuishinda baat'ili, kweli kuushinda uwongo, ili Mwenyezi Mungu akughufirie yaliyo tangulia katika yanayo hisabika kwa mwenye cheo kama chako kuwa ni dhambi, na pia yanayo kuja baada yake. Na ili atimize neema zake juu yako kwa kuenea wito wako, na akuthibitishe kwenye Njia ya Mwenyezi Mungu Iliyo Nyooka. Na Mwenyezi Mungu akunusuru na maadui wa Utume wako kwa nusura yenye nguvu za kushinda

Rudi kwenye Sura

4. Yeye ndiye aliye teremsha utulivu katika nyoyo za Waumini ili wazidi kuwa na yakini juu ya yakini yao. Na ni Mwenyezi Mungu peke yake ndiye mwenye majeshi ya katika mbingu na ardhi. Huendesha mambo yake apendavyo. Na Mwenyezi Mungu amevizunguka vitu vyote kwa ujuzi wake. Ana hikima isiyo na ukomo katika kuendesha kila kitu.

Rudi kwenye Sura

5,6. Ili Mwenyezi Mungu awaingize Waumini wanaume na Waumini wanawake katika Mabustani, yaani Pepo, zipitiwazo na mito ndani yake, wadumu humo daima dawamu, na awafutie makosa yao. Na malipo hayo kwa Mwenyezi Mungu ndio kufuzu kulio fika ukomo kwa utukufu wake. Na ili awatie adhabu wanaafiki wanaume na wanaafiki wanawake, na wanaume wanao mshirikisha Mwenyezi Mungu na wengineo, na washirikina wa kike, wanao mdhania Mwenyezi Mungu dhana mbovu, ya kuwa ati hatamnusuru Mtume wake. Ni juu yao peke yao ndio yatawaangukia mageuko maovu, wala hawawezi kuyakimbia. Mwenyezi Mungu amewaghadhibikia, na amewafukuza kwenye rehema yake, na amewatengenezea Jahannamu kwa ajili ya kuwaadhibu, na huo ndio mwisho mbaya.

Rudi kwenye Sura

7. Na Mwenyezi Mungu anayo majeshi ya mbinguni na katika ardhi. Anaendesha mambo yake kwa hikima yake kama atakavyo. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kushinda kila kitu, Mwenye hikima isiyo na mwisho katika kupanga kila kitu.

Rudi kwenye Sura

8. Ewe Muhammad! Hakika Sisi tumekutuma uwe Shahidi juu ya umma wako na pia juu ya kaumu zilizo tangulia, na uwe Mbashiri kuwapa khabari njema wachamngu kuwa watapata malipo mema, na uwe Mwonyaji kwa watendao maasi kuwa watapata adhabu mbaya.

Rudi kwenye Sura

9. Ili nyinyi, mlio tumiwa Mtume,  mpate kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na mumnusuru Mwenyezi Mungu kwa kuinusuru Dini yake, na mumtukuze kwa taadhima na utukufu, na mumtakase na kila lisilo muelekea, asubuhi na jioni.

Rudi kwenye Sura

10. Hakika wanao kuahidi kuwa watafanya kama wawezalo kukunusuru, kwa hakika wanamuahidi Mwenyezi Mungu. Nguvu za Mwenyezi Mungu ziko pamoja nawe juu ya nguvu zao. Basi atakaye vunja ahadi yake baada ya kwisha itoa, basi madhara yake hayatarudia ila juu ya nafsi yake. Na mwenye kutimiza ahadi aliyo muahidi Mwenyezi Mungu, kwa kutimiza kufungamana nawe, Mwenyezi Mungu atamlipa thawabu za hadi ya mwisho wa ukubwa.

Rudi kwenye Sura

11. Watakwambia hao walio wekwa nyuma na unaafiki wao katika wakaazi wa majangwani, utapo rejea kutoka safarini: Yametushughulisha mali yetu na ahali zetu hata hatukuweza kutoka nawe. Basi tuombee maghfira. Wanasema hayo kwa ndimi zao yasiyo kuwamo katika nyoyo zao. Sema kuwajibu: Nani anaye weza kukufanyieni chochote kukulindeni na hukumu ya Mwenyezi Mungu, pindi akitaka kukudhuruni, au akitaka kukufaeni? Bali Mwenyezi Mungu amevizunguka vyote mtendavyo kwa ujuzi wake.

Rudi kwenye Sura

12. Bali nyinyi mlidhani kwamba Mtume na Waumini hawatarejea kabisa kwa watu wao baada ya vita vyao. Ndio maana mkabaki nyuma, na mkadanganyika na hiyo dhana katika nyoyo zenu. Na mkadhania dhana mbovu katika mambo yenu yote. Na Mwenyezi Mungu alikwisha jua kuwa nyinyi ni watu walio angamia, wenye kustahiki ghadhabu zake.

Rudi kwenye Sura

13. Na asiye muamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi Sisi tumewatengenezea makafiri Moto unao waka kwa nguvu.

Rudi kwenye Sura

14. Na Mwenyezi Mungu peke yake ndiye mwenye ufalme wa mbinguni na katika ardhi, anaupanga kwa mpango wa Mwenye uweza, Mwenye hikima. Humsamehe madhambi amtakaye, na humuadhibu kwa hikima yake amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mkuu wa kusamehe, Mkunjufu wa rehema.

Rudi kwenye Sura

15. Watasema hawa wakaazi wa majangwani walio wekwa nyuma na unaafiki wasitoke nawe: Mkenda kuchukua ngawira, aliyo kuahidini Mwenyezi Mungu kuzichukua, twacheni tukufuateni. Hao wanataka kuigeuza ile ahadi ya Mwenyezi Mungu juu ya ngawira hizo aliyo wapa walio toka na Mtume kwenda Hudaibiya. Ewe Muhammad! Waambie: Hamtatufuata. Hukumu kama hiyo ya kuzuia kufuata Mwenyezi Mungu aliihukumia kabla ya hapo kwa mintarafu ya ngawira kwa walio toka kwenda vitani pamoja na Mtume wake. Wao watasema: Mwenyezi Mungu hakukuamrisheni hayo, bali nyinyi mnatuhusudu tu, hamtaki tushirikiane nanyi. Bali watu hawa, kwa  haya wayasemayo, hawafahamu sharia za Mwenyezi Mungu ila kwa fahamu chache.

Rudi kwenye Sura

16. Waambie walio baki nyuma wasitoke katika watu wa majangwani: Mtakuja takiwa kwenda pigana na watu wa kali wa vita. Ikiwa mtaitikia wito huo basi hapo Mwenyezi Mungu atakupeni ngawira nyingi katika dunia, na thawabu katika Akhera. Na mkikataa kama mlivyo kwisha kataa kabla, basi  Mwenyezi Mungu atakuadhibuni kwa adhabu ya mwisho wa uchungu.

Rudi kwenye Sura

17. Kipofu hapati dhambi kuacha kwenda pigana na makafiri, wala kiguru hapati dhambi, wala mgonjwa hapati dhambi kadhaalika. Kwani hao hawajiwezi. Na mwenye kumt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake katika kila anacho amrisha na kukataza, atamtia katika Mabustani ya Peponi yenye wasaa, yapitayo mito kati yake. Na mwenye kuacha kumt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi Yeye atamuadhibu adhabu iliyo chungu hadi.

Rudi kwenye Sura

18,19. Mwenyezi Mungu amewapa radhi Waumini walipo kuahidi kwa kujitolea chini ya mti. Yeye alijua yaliomo katika nyoyo zao, ya ikhlasi na kuutimiliza Ujumbe wako. Basi akawateremshia utulivu, na kwa ajili ya ukweli wao katika kukuunga mkono na kutimiza sulhu aliwapa nguvu hapo hapo, na ngawira nyingi alizo waahidi kuwa watazipata. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kushinda kila kitu, Mwenye hikima ya mwisho katika kila analo lihukumia.

Rudi kwenye Sura

20,21. Mwenyezi Mungu amekuahidini ngawira nyingi mtakazo chukua katika wakati ulio kadiriwa kwa hayo. Basi akakuleteeni haraka haraka. Na hayo ndiyo hizo ngawira alizo kuahidini. Na akakukingeni na madhara ya watu juu yenu. Na ili hayo yawe ni Ishara kwa Waumini juu ya ukweli wa ahadi ya Mwenyezi Mungu kwao, na akuongozeni kwenye Njia Iliyo Nyooka, kwa kumt'ii Yeye na kumfuata Mtume wake. Na ngawira nyengine ambazo mlikuwa hamjazipata Mwenyezi Mungu amekupeni ushindi wa kuzipata. Na Mwenyezi Mungu ana uwezo ulio timia juu ya kila kitu.

Rudi kwenye Sura

22. Na lau makafiri wa Makka wangeli pigana nanyi, na wasifanye ile sulhu nanyi, basi wangeli toka mbio kwa kushindwa, kwa kukuogopeni, na tena hapo wasinge pata mlinzi wowote wa kuwatawalia mambo yao, wala mtu wa kuwanusuru.

Rudi kwenye Sura

23. Mwenyezi Mungu ameendesha mambo yake kwa mwendo kama alio uendesha zamani kwa viumbe vyake - navyo ni kuwa khatima njema ni ya Mitume wake na Waumini. Wala hutakuta mabadiliko katika mwendo wa Mwenyezi Mungu.

Rudi kwenye Sura

24. Na huyo ni Mwenyezi Mungu pekee, ndiye aliye izuia mikono ya makafiri isikudhuruni katika vita vyao kati ya Makka. Na baada yake akakupeni uwezo wa kuwashinda. Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyaona yote myatendayo.

Rudi kwenye Sura

25,26. Watu wa Makka ndio walio kufuru na wakakuzuilieni msiingie katika Msikiti Mtakatifu, na wakawazuilia dhabihu wanyama wa kutoa mhanga mlio wachunga na kuwafunga kwa ajili ya kutoa dhahiya, wasifike pahala pao pa kuchinjiwa. Na lau kuwa si ubaya wa kuwasibu Waumini wanaume na wanawake kati ya makafiri wa Makka, ambao hamwajui, mkawauwa bila ya kuwajua, na mkapata a'ri na hizaya kwa ajili ya kuwauwa, basi tungeli kusalitisheni nao mkapambana nao. Na kuzuiliwa huko ni kwa ajili ya kuwa Mwenyezi Mungu apate kuwaingiza katika ulinzi wake Waumini walio baina yao, na walio silimu miongoni mwa makafiri. Lau kuwa wanatambulikana Waumini basi tungeli waadhibu walio shikilia ukafiri kati yao adhabu ya ukomo wa uchungu, pale wale walio kufuru walipo fanya katika nyoyo zao dharau za kijahiliya basi Mwenyezi Mungu akateremsha utulivu juu ya Mtume wake na juu ya Waumini, na akawalazimisha neno la kujikinga na ushirikina na adhabu. Na wao walikuwa ni wenye kustahiki na kuelekea hayo, na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua kila kitu.

Rudi kwenye Sura

27. Ameitimiza Mwenyezi Mungu kwa  Mtume wake  ile ndoto ya Mtume kwa kuingia Msikiti Mtakatifu kwa hakika. Ninaapa: Hapana shaka mtaingia katika Msikiti Mtakatifu, Mwenyezi Mungu akipenda, nanyi mmesalimika na maadui zenu, na huku ni wenye kunyoa na kupunguza nywele zenu, na bila ya khofu. Mwenyezi Mungu Subhanahu anaijua kheri msiyo ijua kwa kukuchelewesheni kuingia Msikiti Mtakatifu. Basi amekujaalieni kabla ya kuingia kwenu mpate Ushindi karibuni.

Rudi kwenye Sura

28. Yeye ndiye Mwenyezi Mungu aliye mtuma Mtume wake na uwongozi ulio wazi, na Dini ya Kiislamu, ili itukuke juu ya dini zote. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa ni Shahidi wa hayo.

Rudi kwenye Sura

29. Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na Masahaba wake walio pamoja naye, ni wakali na wenye nguvu kwa makafiri, na wanarehemeana na kuoneana huruma wenyewe kwa wenyewe. Unawaona wakirukuu na kusujudu sana, wakiomba kwa hivyo thawabu kubwa kwa Mwenyezi Mungu, na radhi za kuenea. Alama yao ni unyenyekevu wao katika nyuso zao kutokana na kuathirika kwa Sala nyingi. Hiyo ndiyo sifa yao kubwa katika Taurati. Na sifa yao katika Injili ni kama mmea ulio chipua ukapata nguvu, ukageuka kutokana na udhaifu ukawa mgumu, ukasimama sawa sawa kwenye shina lake. Ukawafurahisha wakulima kwa nguvu zake. Basi Waumini ni hali kadhaalika, ili Mwenyezi Mungu awakasirishe makafiri kwa nguvu zao. Mwenyezi Mungu amewaahidi walio amini na wakatenda mema katika wao maghfira ya kuwafutia madhambi yao yote, na thawabu kubwa mno. (Katika Injili ya Marko 4.26-28 imeandikwa: "Ufalme wa Mungu, mfano wake ni kama mtu aliyemwaga mbegu juu ya nchi; akawa akilala na kuondoka usiku na mchana, nayo mbegu ikamea na kukua, asivyojua yeye. Maana nchi huzaa wenyewe; kwanza jani, tena suke, tena ngano pevu katika suke." Katika Hesabu 16.22 ambacho ni sehemu ya Taurati kwa mujibu wa Biblia imeandikwa kuwa Musa na Haruni walisali kwa kusujudu. Humo inasemwa: "Nao wakapomoka kifudifudi, wakasema, Ee Mungu..." Na katika Injili ya Mathayo 26.39 inatajwa pia kuwa Yesu pia alisali kwa kusujudu: "Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifulifuli, akaomba.." Hivyo ndivyo wasalivyo Waislamu.)

Rudi kwenye Sura