1. H'a, Mim, (H.M.)  Harufi mbili katika harufi za Alifbete zinazo anzia Sura hii kwa mpango wa Qur'ani katika baadhi ya Sura, kuashiria kwamba hii Qur'ani imeundwa na maneno hayo hayo wanayo yatumia wanaadamu. Nayo juu ya hivyo imewashinda kuleta mfano wake.

Rudi kwenye Sura

2,3. Hii Qur'ani imeteremshwa kutokana na Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu, Mwenye kushinda, Mwenye kuvizunguka vitu vyote kwa ujuzi wake, naye ni Mwenye kupokea toba ya wenye kutubia, na Mkali wa kuadhibu, Mwenye neema nyingi; hapana wa kuabudiwa kwa haki isipo kuwa Yeye peke yake. Ni kwake Yeye peke yake ndio marejeo na mafikio.

Rudi kwenye Sura

4. Hawazibishi Ishara za Mwenyezi Mungu zenye kuonyesha dalili zake ila walio makafiri. Basi yasikukhadae huko kutanga tanga kwao katika nchi ukadhani kuwa Mwenyezi Mungu kawasahilishia mambo yao juu ya ukafiri wao.

Rudi kwenye Sura

5. Kabla ya hawa walikufuru kaumu ya Nuhu, na makundi mengine yaliyo jumuika kuwapinga Mitume baada ya kaumu yake Nuhu. Na hao wakawa na pupa ya kumletea shari Mtume wao wamtie nguvuni, na wakawa wanajadiliana katika upotovu usio kuwa na ukweli wowote, ili kwa upinzani wao wapate kuipindua haki iliyo kwisha thibiti. Basi Mimi nikawashika, nikawatia katika adhabu ya kuwang'olea mbali. Hebu angalia ilikuwaje adhabu yangu juu yao!

Rudi kwenye Sura

6. Na kila lilipo thibiti neno la adhabu juu ya mataifa yaliyo wakadhibisha Manabii wao, basi kadhaalika lilithibiti neno la Mola wako Mlezi juu ya hao wanao kukanusha wewe, ewe Muhammad, kwani hao ni watu wa Motoni, kwa kuwa wamekhiari ukafiri kuliko Imani.

Rudi kwenye Sura

7. Malaika wanao beba A'rshi, na wenye kuizunguka, wanamtakasa Mwenye kumiliki mambo yao na Mlezi wao, wanamtakasa kutokana na kila upungufu, kwa mtakaso ulio lingana na sifa zake. Na wanamuamini, na wanamwomba maghfira awaghufirie Waumini, huku wakisema: Ewe Mola wetu Mlezi! Rehema yako imeenea kila kitu, na Ujuzi wako umezunguka kila kitu, basi yasamehe makosa ya walio rejea kwako, na wakaifuata Njia yako, na waepushe na adhabu ya Motoni.

Rudi kwenye Sura

8. Na Malaika hawa husema: Ewe Mola wetu Mlezi! Waingize Waumini katika Mabustani ya Milele ulio waahidi kwa ndimi za Mitume wako, na pia waingize pamoja nao walio wema katika wazazi wao, na wake zao, na dhuriya zao. Hakika wewe peke yako ndiye Mwenye kushinda, wala hushindiki; Mwenye hikima usiye kosa.

Rudi kwenye Sura

9. Na husema katika dua zao: Waepushe Waumini malipo ya madhambi yao, na unaye muepusha Wewe na malipo ya madhambi yake Siku ya Malipo basi hakika ndio umemrehemu kwa fadhila yako. Kuepushwa na malipo ya madhambi ndio ushindi ulio fikilia ukomo mkubwa mno.

Rudi kwenye Sura

10. Hakika walio kufuru watanadiwa waambiwe: Bila ya shaka chuki ya Mwenyezi Mungu na bughdha yake kwenu ni kubwa kuliko chuki zenu wenyewe zilizo kupelekeeni mkapata adhabu pale mlipo itiwa kwenda kwenye Imani mara kwa mara nanyi mkakimbilia kwenye ukafiri.

Rudi kwenye Sura

11. Makafiri watasema: Mola wetu Mlezi! Umetufishe vifo viwili, kifo kimoja katika uhai wetu wa duniani, na kifo kingine katika uhai wetu wa Barzakh, (1) yaani kaburini. Na ukatuhuisha mara mbili, mara moja ndiyo ya uhai wetu wa duniani, na mara ya pili ni wakati wa kufufuliwa kutoka makaburini. Basi, hebu, ipo njia ya kutoka kwetu kwenye adhabu?
(1) Na huenda yakaonyesha uhai wa Barzakh, ambao ni uhai makhsusi hatuujui hakika yake, aliyo yataja Mwenyezi Mungu Mtukufu katika kauli yake juu ya watu wa Firauni: "Moto wanadhihirishiwa asubuhi na jioni; na siku itapo fika Saa ya Kiyama patanenwa: Waingizeni watu wa Firauni katika adhabu kali kabisa." Na kauli yake Mtukufu: "Wala usiwadhanie wale walio uliwa katika Njia ya Mwenyezi Mungu kuwa ni maiti. Bali ni wahai, wanaruzukiwa kwa Mola wao Mlezi."

Rudi kwenye Sura

12. Hiyo ni adhabu mliyo nayo. Kwani mwendo wenu duniani ni kuwa akitajwa Mwenyezi Mungu peke yake nyinyi mnakufuru, na pindi akishirikishwa na mwenginewe ndio mnaamini. Na ikiwa huu ndio mwendo wenu basi mnastahiki kweli malipo ya ushirikina wenu. Basi hukumu ni ya Mwenyezi Mungu Mtukufu Mkuu ambaye humlipa aliye kufuru kwa anavyo stahiki.

Rudi kwenye Sura

13. Mwenyezi Mungu ambaye anakuonyesheni dalili za uweza wake, basi anakuteremshieni kwa maslaha yenu maji kutoka mbinguni ambayo ni sababu ya riziki zenu. Na hapana anaye waidhika kwa haya ila mwenye kurejea akazifikiria Ishara za Mwenyezi Mungu.

Rudi kwenye Sura

14. Basi muabuduni Mwenyezi Mungu mkimsafia Yeye ibada, na hata walau wakiichukia makafiri ibada yenu na ikhlasi yenu.

Rudi kwenye Sura

15,16. Mwenyezi Mungu, Mwenye vyeo vya juu, Mwenye A'rshi, huteremsha Wahyi kwa hukumu yake na amri yake juu ya anaye mteuwa katika waja wake, ili awaonye watu adhabu ya kwenda kinyume na Mitume Siku ya kukutana viumbe vyote, Siku ya Hisabu watapo tokeza watu wazi, hapana lifichikanalo kwa Mwenyezi Mungu, watakuwa wakijisikilizanisha wao kwa wao wito unao tisha: Ufalme wa nani leo? Na jawabu ya kukata: Wa Mwenyezi Mungu, Mmoja, Mwenye kutengeka kwa hikima, Aliye pita mipaka kwa nguvu zake!

Rudi kwenye Sura

17. Leo tunailipa kila nafsi kwa iliyo tenda. Hapana dhulma leo kwa kupunguziwa ujira au kuzidishiwa mateso. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwepesi kuhisabu kwake, basi hachelewi na wakati wake.

Rudi kwenye Sura

18. Ewe Muhammad! Waonye, Siku ya Kiyama ipo karibu. Siku zitakapo kuwa nyoyo zipo kooni kwa wingi wa khofu, zimejaa majonzi, haziwezi hata kuyaelezea. Walio jidhulumu nafsi zao kwa ukafiri hawatakuwa na jamaa wala mwombezi wa kuwat'ii katika amri yao.

Rudi kwenye Sura

19. Na Yeye Subhanahu analijua jicho linalo khuni, na siri zilizo fichikana vifuani.

Rudi kwenye Sura

20. Na Mwenyezi Mungu anahukumu kwa uadilifu, na hao miungu ya uwongo wanayo iomba badala ya Mwenyezi Mungu haihukumu chochote, kwa kuwa haiwezi kitu. Hakika Mwenyezi Mungu peke yake ndiye Mwenye kuvizunguka vyote vinavyo sikia na vinavyo ona.

Rudi kwenye Sura

21. Kwani hao washirikina wamekaa kitako tu wala hawatembei katika ardhi wakaiona vipi ilikuwa hali ya mataifa yaliyo kuwa kabla yao? Walikuwa wana nguvu kuliko wao na walijenga zaidi kuliko hawa, nao Mwenyezi Mungu aliwang'olea mbali kwa madhambi yao, wala hawakuwa na mlinzi wa kuwalinda na adhabu ya Mwenyezi Mungu.

Rudi kwenye Sura

22. Na adhabu hiyo iliwateremkia kwa sababu ilikuwa Watume wao wakiwajia na dalili zilizo wazi, nao wakazikataa, basi Mwenyezi Mungu akafanya haraka kuwapelekea adhabu ya kuwang'oa. Hakika Yeye ana nguvu kubwa mno, na amefikilia ukomo katika kuadhibu.

Rudi kwenye Sura

23,24. Ninaapa kuwa tulimtuma Musa na miujiza yetu na ushahidi wenye uthibitisho ulio wazi kumpelekea Firauni na Hamana na Qaruni, wakasema: Huyu ni mchawi kwa hiyo anayo dai kuwa ni miujiza, na amepita mipaka kwa uwongo katika madai yake kuwa yeye ni Mtume aliye toka kwa Mola wake Mlezi!

Rudi kwenye Sura

25. Musa alipo waletea Haki kutoka kwetu, Firauni na wafuasi wake walio kuwa pamoja naye walisema: Wauweni watoto wa kiume wa hao walio amini pamoja naye, na waachilieni wahai binti zao! Na vitimbi vya makafiri haiwi ila kuondoka, na kuangamia, na kupotea.

Rudi kwenye Sura

26. Na Firauni akasema: Nachilieni nimuuwe Musa, naye naamwite huyo Mola wake Mlezi amwokoe kwangu! Hakika mimi nakhofia asije  huyu akaigeuza dini yenu, enyi watu wangu, au akaeneza fitna katika nchi.

Rudi kwenye Sura

27. Na Musa akamwambia Firauni na watu wake: Hakika mimi nimejilinda na Mwenye kumiliki mambo yangu ambaye ndiye aliye nilea, na ndiye Mwenye kumiliki mambo yenu pia, na Mwenye kukuleeni nyinyi kwa neema zake na hisani zake, nimejilinda na kila anaye jivuna na kutakabari, asiye iamini Siku ya Hisabu.

Rudi kwenye Sura

28. Akasema mtu mmoja Muumini anaye ficha Imani yake katika watu wa Firauni, akiwasemeza watu wake: Mnataka kumuuwa mtu kwa sababu anasema: Mungu wangu ninaye muabudu ni Mwenyezi Mungu, naye amekuleteeni  dalili zilizo wazi zinazo tokana na Mwenye kumiliki mambo yenu na Mlezi wenu? Na akiwa yeye mwongo, basi uwongo wake ni juu yake yeye peke yake, balaa ya uwongo wake itamwangukia mwenyewe. Na akiwa ni mkweli baadhi ya adhabu anazo tutahadharisha nazo zitakuteremkieni nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu hamwafikishi njia ya uwokovu mwenye kupita mipaka, aliye mwongo mno.

Rudi kwenye Sura

29. Enyi watu wangu! Leo nyinyi mnao ufalme, na ni watu wa juu katika nchi ya Misri, wala hapana mwenginewe. Lakini ni nani atakaye kukingeni na adhabu ya Mwenyezi Mungu pindi ikitujia? Firauni akasema: Sikwambiini rai ila ambayo mimi mwenyewe ninayo itakidi. Na sikuongozeni kwa rai hii ila njia ya uwongofu.

Rudi kwenye Sura

30,31. Akasema yule mtu aliye amini katika watu wa Firauni: Enyi watu wangu! Hakika mimi nakukhofieni isikufikieni siku kama ile siku walipo jikusanya watu makundi mbali mbali kuwapinga Mitume wao, mfano  wa ada ya kaumu Nuhu, na ya A'di, na ya Thamudi, na mataifa mengine yaliyo kuja baada yao. Wala Mwenyezi Mungu hataki kuwadhulumu waja wake.

Rudi kwenye Sura

32,33. Na enyi watu wangu! Mimi nakukhofieni siku viumbe watapo pigiana makelele, siku mtapo kimbia kurudi nyuma, hapana wa kukukingeni na Mwenyezi Mungu. Na mwenye kuachiliwa na Mwenyezi Mungu kupotea - kwa kuwa anamjua kuwa amekhiari upotovu kuliko uwongofu - basi hatokuwa na mwongozi wa kumwongoa.

Rudi kwenye Sura

34. Ninaapa! Bila ya shaka alikwisha kujieni Yusuf na Ishara zilizo wazi. Nanyi hamkuacha kuwa na shaka na hayo aliyo kuja nayo kwenu, mpaka alipo kwisha kufa mkasema: Mwenyezi Mungu hatoleta tena Mtume mwengine baada ya Yusuf. Mfano wa upotovu kama huu mbaya Mwenyezi Mungu humwacha kupotea yule aliye pindukia mipaka, mwingi wa mashaka na wasiwasi.

Rudi kwenye Sura

35. Wanao bishana juu ya Ishara za Mwenyezi Mungu bila ushahidi wowote ulio wajia, humkirihisha mno na kumchukiza Mwenyezi Mungu na Waumini kwa yale majadiliano waliyo yatilia muhuri. Mfano wa muhuri huu Mwenyezi Mungu anaupiga juu ya kila moyo ulio takabari juu ya viumbe wenzake, na ukataka kuwatawala.

Rudi kwenye Sura

36,37. Na Firauni akasema: Ewe Hamana! Nijengee jengo refu nifikilie njia za mbinguni nipate kumwona huyo Mungu wa Musa. Na mimi nina hakika huyu ni mwongo kwa anavyo jidai kuwa yeye ati ni Mtume. Mfano wa pumbao la uwongo kama hivi Firauni alipambiwa uovu wa vitendo vyake, hata akaviona mwenyewe kuwa ni vizuri, na akazuilika na njia ya haki kwa kukhiari mwenyewe njia ya upotovu. Na havikuwa vitimbi vya Firauni ila katika upotovu tu.

Rudi kwenye Sura

38. Na akasema yule aliye amini katika watu wa Firauni: Enyi watu wangu! Nifuateni mimi, nitakuongozeni njia njema!

Rudi kwenye Sura

39. Enyi watu wangu! Haya maisha ya duniani si chochote ila ni kama starehe ya muda ya mwenye kupanda kipando, inakwisha upesi. Na makaazi ya Akhera, hayo tu peke yake, ndiyo makaazi ya kudumu.

Rudi kwenye Sura

40. Mwenye kutenda uovu duniani hatolipwa kwa uovu huo huko Akhera ila kwa mfano wake. Na mwenye kutenda wema, akiwa mwanamume au mwanamke, naye ni Muumini, basi hao wataingia Peponi watakapo ruzukiwa bila ya kipimo cha kuhisabiwa na wenye kuhisabu.

Rudi kwenye Sura

41,42. Na enyi watu wangu! Kwani mimi nina nini? Mimi nakuiteni mfuate njia za kuokoka, na nyinyi mnaniita niingie Motoni! Mnaniita nimkufuru Mwenyezi Mungu kwa kumshirikisha Yeye na vitu nisivyo vijua, na hali mimi nakuitieni mwende kwa Mwenye Nguvu asiye shindwa, Mwingi wa kusamehe madhambi!

Rudi kwenye Sura

43. Bila ya shaka yoyote huyo mungu mnaye niitia nimuabudu hana wito wowote unao stahiki kuitikiwa la duniani wala Akhera. Na hakika marejeo yetu sote ni kwa Mwenyezi Mungu, na wenye kupita mipaka ndio watu wa Motoni, wala si Waumini walio kaa sawa.

Rudi kwenye Sura

44. Basi watakuja jua ukweli wa niliyo kuambieni, na mimi namtegemezea mambo yangu Mwenyezi Mungu. Hakika jicho la Mwenyezi Mungu limewaenea waja wake wote, na Yeye ni Mwenye kuwalipa kwa vitendo vyao.

Rudi kwenye Sura

45,46. Mwenyezi Mungu akamlinda yule Muumini katika watu wa Firauni mateso ya vitimbi vyao, na ikawazunguka watu wa Firauni adhabu mbaya, nayo ni Moto wanao uingia asubuhi na jioni. Haya ni ya duniani na wapo katika ulimwengu wa Barzakh, kaburini. Na Siku ya Kiyama, atasema Mwenyezi Mungu: Waingizeni watu wa Firauni kwenye adhabu iliyo kali kabisa!

Rudi kwenye Sura

47. Ewe Muhammad! Watajie pale wanapo zozana watu wa Motoni humo, wakawa walio kuwa wanyonge, nao ni wafuasi, wakiwaambia wanao takabari, nao ni maraisi: "Sisi tulikuwa duniani ni wafuasi wenu, basi je, hamtuchukulii baadhi ya adhabu ya moto?"

Rudi kwenye Sura

48. Na walio takabari waseme: "Hakika sote sisi tumo humu, sisi na nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu amehukumu kwa haki baina ya waja. Basi kila mmoja wetu amepata adhabu aliyo hukumiwa juu yake."

Rudi kwenye Sura

49. Watasema walio Motoni, wanyonge na wakuu, kuwaambia walinzi wa Jahannamu wakiwaomba msaada: Muombeni Mungu wenu atupunguzie japo siku moja tupumzike na adhabu.

Rudi kwenye Sura

50. Walinzi wa Jahannamu watawaambia kwa kuwahizi: Kwani hamkunabihika kwa yaliyo kuwa mkiteremshiwa, na hali walikuwa wakikujieni Mitume na ushahidi ulio wazi? Na watasema watu wa Motoni: Kwani? Walitujia Mitume na sisi tukawakadhibisha. Walinzi wakasema: Ikiwa mambo ni hivyo, basi waombeni nyinyi! Lakini madua ya makafiri hayana ila kupotea bure.

Rudi kwenye Sura

51. Hakika Sisi bila ya shaka tunawanusuru Mitume wetu na Waumini katika maisha ya duniani kwa kulipiza juu ya maadui wao, na kusimamisha hoja juu yao; na Siku ya Kiyama watasimama Mashahidi washuhudie kwamba Mitume wamefikisha Ujumbe wao, na washuhudie kwamba makafiri waliukadhibisha.

Rudi kwenye Sura

52. Siku ambayo madhaalimu hautawafaa udhuru wao kwa yale waliyo yakosa kuyatenda duniani. Nao watapata laana, yaani watafukuzwa kwenye rehema, na watapata makaazi maovu kabisa.

Rudi kwenye Sura

53,54. Naapa kwamba tulimpa Musa cha kuongoa kwendea Haki, na tukawarithisha Wana wa Israili Taurati yenye kuongoa na yenye kuwakumbusha wenye akili zilio nzima.

Rudi kwenye Sura

55. Ikiwa umejua tuliyo kusimulia, basi subiri, ewe Muhammad, kwa maudhi yanayo kupata. Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ya kukunusuru wewe na kuwanusuru Waumini ni kweli isiyo geuka. Na taka maghfira kutoka kwa Mola wako Mlezi kwa hayo ambayo kwa mnasaba wako  wewe huhisabiwa kuwa ni dhambi. Na mtakase Mola wako Mlezi na kila upungufu kwa mtakaso unao ambatana na kumsifu jioni na asubuhi.

Rudi kwenye Sura

56. Hakika hao wanao jadili katika dalili za Mwenyezi Mungu bila ya hoja iliyo tokana naye Yeye Mtukufu, hamna vifuani mwao ila kutaka uluwa, ubora, wasiifuate Haki, wala huko kutaka kwao uluwa, ubora,  hakuwafikishii walitakalo. Basi wewe iombe Hifadhi kutokana na Mwenyezi Mungu; kwani Yeye hakika ni Mwenye kuenea kila kitu kusikia kwake na kuona kwake.

Rudi kwenye Sura

57. Ninaapa: Bila ya shaka kuziumba mbingu na ardhi ni jambo kubwa zaidi kuliko kuwaumba watu. Lakini wengi wa watu wameitupa ilimu, wakawa hawaamini kufufuliwa juu ya kukubali kwao kwamba Yeye ndiye Muumba mbingu na ardhi.

Rudi kwenye Sura

58. Na hawawi sawa, kipofu asiyo iona Haki, na mwenye kuijua. Wala hawawi sawa wema wenye kuamini na wakatenda mema, na muovu wa itikadi na vitendo. Ni kwa uchache, uchache mno, ndio mnakumbuka, enyi watu!

Rudi kwenye Sura

59. Hakika Kiyama kitakuja tu, hapana shaka yoyote. Na lakini wengi wa watu hawasadiki.

Rudi kwenye Sura

60. Na anasema Muumba wenu na Mwenye kumiliki mambo yenu yote: Niombeni nami nitakupeni! Hakika wale wanao takabari hata wakakataa kuniomba wataingia Jahannamu nao ni madhalili wanyonge.

Rudi kwenye Sura

61. Mwenyezi Mungu peke yake ndiye aliye kujaalieni usiku mpate kutua ndani yake mpumzike na kazi, na mchana wenye mwangaza mpate kufanya kazi ndani yake. Hakika Mwenyezi Mungu bila ya shaka ni Mwenye fadhila kuu juu ya watu. Lakini watu wengi hawamshukuru juu ya neema zake.

Rudi kwenye Sura

62. Huyo Mwenye kukuneemesheni kwa neema hizi tukufu ndiye Mwenyezi Mungu, Mwenye kumiliki mambo yenu, Muumba wa kila kitu, hapana wa kuabudiwa kwa haki ila Yeye. Basi mtaelekea wapi kwa ibada mkimwacha Yeye?

Rudi kwenye Sura

63. Mfano wa kukengeuka huku kuiacha Haki kuendea upotovu, walikengeuka walio kuwa kabla yenu. Wakazikanya Ishara za Mwenyezi Mungu na wakazikataa.

Rudi kwenye Sura

64. Ni Mwenyezi Mungu peke yake ndiye aliye kufanyieni ardhi iwe ni pahala panapo silihi maisha yenu, na mbingu zikawa ni jengo lilio shikamana. Na akakadiria kukuumbeni nyinyi, akazitengeneza sura zenu, na akakujaalieni na umbo zuri lilio nyooka. Na akakuruzukuni katika vitu vya halali mnavyo viona vitamu.  Mneemesha huyo kwa neema hizi ndiye Mwenyezi Mungu Mola wenu Mlezi. Basi ametukuka Mwenyezi Mungu Mwenye kuumiliki ulimwengu wote, na Mwenye kuulea.

Rudi kwenye Sura

65. Yeye pekee Mwenye uhai wa daima dawamu, hapana wa kuabudiwa kwa Haki ila Yeye. Basi muelekeeni Yeye kwa kumuomba, mkimsafia ibada Yeye. Sifa njema zote ni haki iliyo thibiti kwa Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa viumbe vyote.
 

Rudi kwenye Sura

66. Ewe Mtume! Sema: Hakika mimi nimekatazwa kuiabudu miungu mnayo iabudu nyinyi badala ya Mwenyezi Mungu, zilipo nijia hoja kutoka kwa Mola wangu Mlezi, na nikaamrishwa nimfuate Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa walimwengu wote katika mambo yangu  yote.

Rudi kwenye Sura

67. Mwenyezi Mungu, peke yake, ndiye aliye kuumbeni, enyi wanaadamu, kutokana na udongo, kisha akaugeuza udongo ukawa tone la manii, kisha akalifanya tone la manii kuwa pande la damu iliyo gandana, kisha akakutoeni kwenye matumbo ya mama zenu kuwa ni watoto wachanga. Kisha akaukuza umri wenu mpaka mkakamilika nguvu zenu na akili, tena ukawa mrefu umri wenu mpaka mkawa wazee. Na wako kati yenu wanao kufa kabla ya kufikia ujana au uzee. Na Mwenyezi Mungu akakuumbeni kwa namna hii ili mfikilie wakati maalumu kwake Yeye, nao ni wakati wa kufufuliwa; na kwa ajili mpate kupima na kufahamu hikima na mazingatio katika mageuzi haya.
"Yeye ndiye aliye kuumbeni kwa udongo, kisha kwa tone la manii, kisha kwa pande la damu..n.k."
Maoni juu ya "Tone la manii", "pande la damu" na "pande la nyama" yamo katika Aya 7,8 na 9 Sura Assajda; Aya 12, 13 na 14 Sura Al-Muuminuna; Aya 67 Sura Ghaafir; 5 Sura Al-Hajj. Neno Nut'fa katika lugha hutumika kwa maana ya manii ya mwanamume.
Tukirejea kwenye Aya Tukufu (75.37) "Je! Hakuwa tone la manii lilio shushiwa?" inadhihiri kuwa makusudi kwa "tone la manii" ni sehemu makhsusi ya manii. Na ilimu ya sayansi imevumbua kuwa makusudi ya sehemu hiyo ni kile kijidudu kinacho shushiwa, ambacho kinacho chukuliwa na maji yanayo shushwa, na kidudu hicho "Sperm" ambacho kikiingia kwenye kijiyai (Buwaydha Kiarabu au  Ovum  kwa Kizungu), cha mwanamke ndio huumbika mtoto.
Al-A'laqah katika maana zake kilugha ni damu iliyo ganda, au inayo tiririka iliyo nyekundu mno. Na ki-sayansi maana yake ni Khalaya, au Cells za Embryo (Mtoto ndani ya tumbo la mama) lilio gandamana (ta-a'llaqa) na ukuta wa tumbo la uzazi baada ya kwisha ingiana kidudu cha ume na yai la uke, na ikapatikana Khalaya moja ambayo ikagawika ikawa Khalaya kadhaa wa kadhaa zinazo endea kwenye ukuta wa tumbo la uzazi, kwenda kujibandika na huzua  hapo kumwagika damu.
Al-mudhghah huyo ni mtoto katika mageuzi yake baada ya kutoka kuwa  Al-a'laqah, yaani baada ya kwisha shikamana na ukuta wa tumbo la uzazi na kuviringana bila ya sura maalumu, na huzungukwa na vifuniko, na hubaki katika hali hiyo wiki chache hivi mpaka yafanyike mafupa. Na Mudhghah ambayo imefasiriwa kama pande la nyama ina khalaya zenye umbo maalumu, na hizo ndizo zinakuwa mtoto,  na khalaya zisio kuwa na umbo maalumu, na hizi huzunguka sehemu ile iliyo timia umbo lake, na kazi yake ni kulinda na kutoa chakula.
Mafupa: Ilimu ya mimba Gynaecology imethibitisha karibuni kuwa mafupa yanadhihiri katika t'abaka ya katikati katika Khalaya za Mudhghah baada ya kutoka kiwango cha kugawanyika Khalaya za viungo.    

Rudi kwenye Sura

68. Mwenyezi Mungu ndiye anaye huisha na kufisha. Akitaka jambo lolote kulidhihirisha katika kuwepo basi huliambia: Kuwa! Na huwa bila ya taakhira.

Rudi kwenye Sura

69. Je! Huwaangalii hao wanao zozana katika Ishara za Mwenyezi Mungu zilio wazi, vipi walivyo geuzwa nadhari yao katika hizo, na wanaendelea kushikilia ule ule upotovu wao walio nao?

Rudi kwenye Sura

70,71,72,73,74. Walio ikadhibisha Qur'ani na Ujumbe tulio watumia Mitume wetu, Ufunuo wote, watakuja jua matokeo ya kukanusha kwao zitapo kuwa pingu na minyororo zipo shingoni mwao, wakibururwa kwazo katika maji yaliyo fikia ukomo wa moto, tena baadae watupwe Motoni waokwe kwenye joto lake. Kisha waambiwe kwa kuwakejeli na kuwahizi: Wako wapi hao miungu yenu mliyo kuwa mkiiabudu badala ya Mwenyezi Mungu? Watasema makafiri: Wametupotea. Bali kwa hakika sisi hatukuwa hapo zamani duniani tukiabudu chochote. Katika mfano wa upotovu mbaya kama huu ndio Mwenyezi  Mungu anawawacha makafiri waipotee Njia ya Haki kwa kujua kwake kwamba hao wamekhiari upotovu kuliko uwongofu.

Rudi kwenye Sura

75,76. Makafiri wataambiwa: Adhabu hiyo ni kwa sababu ya mlivyo kuwa katika dunia mkifurahi katika nchi kwa jambo lisilo stahiki kufurahikiwa, na kwa sababu ya kufurahikia kwenu kwa maudhi yaliyo kuwa yakiwasibu Manabii wa Mwenyezi Mungu na vipenzi vyake. Basi ingieni kwenye  milango ya Jahannamu, ambako mmekadiriwa mkae daima dawamu. Pahala paovu kabisa pa kukaa wenye kujivuna ni Jahannamu.

Rudi kwenye Sura

77. Subiri, ewe Muhammad! Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu kwako ya kwamba atawaadhibu maadui wako, ni kweli isiyo na shaka yoyote. Na adhabu itawafikia tu, ama wakati wa uhai wako au wakati watapo rejea wao kwetu!  Wakiacha baadhi ya adhabu tunayo wahadharisha nayo katika uhai wako, basi. Na ikiwa tutakufisha, basi watarejea kwetu. Nasi tutawahisabia waliyo kuwa wakiyatenda.

Rudi kwenye Sura

78. Ninaapa: Bila ya shaka tuliwatuma Mitume wengi kabla yako wewe. Wengine tumekuzungumzia khabari zao, na wengine hatukukuzungumzia khabari zao. Wala haikuwa Mtume yeyote kuleta muujiza ila kwa apendavyo Mwenyezi Mungu na kutaka kwake. Hawezi kuleta kwa nafsi yake tu, wala kwa watakavyo watu wake. Na inapo kuja amri ya Mwenyezi Mungu ya kuleta adhabu duniani au Akhera wanahukumiwa kwa uadilifu. Na wakati huo wapotovu huwa ndio wenye kukhasiri.

Rudi kwenye Sura

79. Mwenyezi Mungu ndiye aliye kudhalilishieni ngamia, mpate kuwapanda wengine, na wengine muwale.

Rudi kwenye Sura

80. Na mnapata kwao manufaa mengi, mbali ya kuwapanda na kuwala; na ili mpate kufikilia haja zenu mnazo zishughulikia nafsi zenu, kama kuburura mizigo na kuibeba, na kadhaalika. Na juu ya ngamia, ambaye ni katika nyama hoa, na juu ya marikebu, mnajipakia nyinyi wenyewe na mizigo yenu.

Rudi kwenye Sura

81. Mwenyezi Mungu anakuonyesheni dalili zake, basi hebu nambieni dalili gani katika hizo mnazo zikataa? Na hizo dalili zenyewe ziwazi, hawezi kuzikataa yeyote mwenye akili hata kidogo.

Rudi kwenye Sura

82. Je! Kwani hao watu wamekaa tu, hawazunguki ulimwenguni wakaona ulikuwaje mwisho wa wale walio kuwa kabla yao, walivyo hilikishwa na wakaangamizwa? Hao walio kabla yao walikuwa wengi kwa kuwahisabu kuliko wao, na walikuwa na nguvu na waliathiri kwa majenzi na maendeleo kushinda wao. Hapana kilicho wakinga na adhabu ya Mwenyezi Mungu katika hayo waliyo yachuma,  si mali wala nguvu, wala utawala.

Rudi kwenye Sura

83. Basi Mitume wao walipo wajia mataifa haya kwa sharia na miujiza iliyo kuwa wazi, hayo mataifa yalifurahi na kujitapa kwa kuwa wao ati wana ilimu za dunia, na wakawafanyia maskhara Mitume. Ikawateremkia adhabu waliyo wakhubiria Mitume, na hali wao wakiwakejeli.

Rudi kwenye Sura

84. Mataifa haya yalipo ona adhabu imekuwa kali walisema: Tumemsadiki Mwenyezi Mungu pekee, na tumewakataa miungu ambao kwa sababu yao tulikuwa washirikina.

Rudi kwenye Sura

85. Imani yao haikuwafaa kitu wakati walipo kwisha ona ukali wa adhabu yetu. Mwenyezi Mungu alikwenda mwendo ule ule aliyo kuwa akienda nao waja wake, nao ni kutokukubali Imani wakati wa kuteremka adhabu. Na makafiri ndio walio khasiri wakati wa kuteremka adhabu.

Rudi kwenye Sura