1. Naapa kwa mataifa katika viumbe vyangu, walio jipanga wenyewe kwa safu zilio sawa katika msimamo wa ibada na ut'iifu.
Rudi kwenye Sura

2. Na kwa wanao zuia wanao pindukia mipaka kwa mzuio mkali, nidhamu ibakie, na ulimwengu uhifadhiwe.
Rudi kwenye Sura

3. Na kwa wenye kusoma Aya, na wanamdhukuru Mwenyezi Mungu kwa dhikri ya Tasbihi, Kumtakasa, na Kumhimidi, kumsifu.
Rudi kwenye Sura

4. Hakika Mungu wenu anaye faa kuabudiwa bila ya shaka ni Mmoja tu. Hana mshirika wake, kwa dhati, wala kitendo, wala sifa.
Rudi kwenye Sura

5. Yeye - peke yake - ndiye Muumba mbingu na ardhi na viliomo baina yao, na ndiye Mwenye kupanga mambo, na ndiye Mwenye kutawala mashariki za kila chenye mashariki.
Mwenyezi Mungu ndiye Muumba mbingu saba na viliomo baina yao, navyo ni hivyo vyombo vya mbinguni na nyota zake. Naye ndiye Mwenye kusimamisha, Mwenye kulinda vile vile juu ya mwahali zinapo chomozea jua na nyota zote. Na Yeye ndiye anaye vionyesha hivyo kila  siku katika pahala huko upeo wa macho, kila siku pahala mbali na vilipo dhihiri siku iliyo tangulia. Na hayo ni kwa mwendo wa mpango wa jua maalumu kwa inavyo zunguka dunia juu ya msumari-kati wake kutoka magharibi kwendea mashariki kila siku na wakati huo huo inavyo lizunguka jua katika njia yake katika falaki.
Na jua na nyota huonekana na wakaazi wa ardhi kila siku kama zinachomoza mwahala mbali mbali. Na kila ardhi ikigeuza mahala pake katika safari yake katika mbingu linaonekana jua linachomoza pahala pengine. Ukiliangalia jua kwa utulivu kuanzia mwishoni wa mwezi wa Machi, yaani linapo kuwa jua lipo kati ya mstari wa Ikweta mwanzo wa musimu wa Rabii, yaani Spring, kwa nusu ya kaskazini ya dunia, utaliona linachomoza pahala katika mashariki juu ya upeo wa macho. Kwa mwenye kupeleleza kila siku ikipita ataona kuchomoza kwake kunajongelea kaskazini. Na mwishoni mwa mwezi wa Juni utaona linachomozea mwisho wa kukaribia kaskazini. Kisha baada ya hapo utaliona jua linarejea linafuata kugeuka kule kule mpaka mwisho wa Septemba (wakati wa kuwa sawa wakati wa Khariif yaani Autumn) utaliona jua linachomoza pale pale lilipo chomoza mwanzo wa Machi. Kisha litaendelea kuelekea kusini kuchomoza kwake mpaka mwisho wa Desemba linakuwa linachomoza karibu kabisa na kusini. Baada ya hapo huanza tena kurejea kuelekea kaskazini mpaka limalize safari yake ya kufika kati sawa katika Rabii ya pili. Na safari hii yote inachukua siku 365 na robo siku. Na inaonekana kuwa nyota nazo zinachomoza mwahala mbali mbali katika upeo wa macho inapo kuwa dunia imo katika safari yake ya mbinguni, na khasa nyota za buruji (au vituo) 12 vinavyo pitiwa na jua katika mwendo wake wa mwaka.
Rudi kwenye Sura

6. Sisi tumeipamba hii mbingu ya karibu na watu wa duniani kwa mapambo, nayo ni hizo nyota zinazong'ara, zenye ukubwa mbali mbali, na mwahala pao mbali mbali kwenye anga la ulimwengu kama ionekanavyo kwa macho.
Rudi kwenye Sura

7. Na tukaihifadhi hiyo mbingu na kila shetani jabari aliye a'si.
Rudi kwenye Sura

8. Hao majabari wa kishetani hawawezi kusikiliza yanayo pita katika ulimwengu wa Malaika. Na wao hupopolewa kwa kila kinacho faa cha kuwazuia.
Rudi kwenye Sura

9. Hufukuzwa hao kwa nguvu wasifikilie kuweza kusikiliza khabari za mbinguni. Na Akhera watapata adhabu kali ya kudumu.
Rudi kwenye Sura

10. Isipo kuwa anaye lipata neno moja hivi katika khabari za mbinguni kwa kuibia. Na huyo naye tunamwandama kwa mwenge wa moto unao murika anga kwa mwangaza wake, ukamuunguzilia mbali.
Rudi kwenye Sura

11. Ewe Nabii! Hebu waulize hao wanao kanya kufufuliwa wanao ona hayawi hayo: Je! Kwani kuwaumba wao hawa ni kugumu zaidi au kuziumba mbingu, na ardhi, na nyota, na vyenginevyo, tulivyo viumba Sisi?
Rudi kwenye Sura

12. Hakika Sisi tumewaumba wao kutokana na udongo unao gandana. Basi kwa nini wanaona ajabu kurejezwa tena wao?
Rudi kwenye Sura

13. Na wanapo kabiliwa kwa dalili za uweza wa Mwenyezi Mungu kufufua, hata hawazishughulikii wakanufaika kwa hizo dalili.
Rudi kwenye Sura

14. Na wanapo ona ushahidi wa kuonyesha uweza wa Mwenyezi Mungu huitana wapate kupita mipaka katika kumkejeli.
Rudi kwenye Sura

15. Na makafiri husema juu ya Ishara zinazo onyesha uweza wa Mwenyezi Mungu: Haya tunayo yaona si chochote ila ni uchawi tu.
Rudi kwenye Sura

16. Hivyo sisi tukisha kufa tukawa udongo na mafupa tutatolewa tena makaburini kwetu tuwe wahai?
Rudi kwenye Sura

17. Sisi tuwe wahai, na pia watafufuliwa baba zetu wa zamani walio kufa kabla yetu, na wakapotea, na wakateketea?
Rudi kwenye Sura

18. Ewe Nabii! Waambie: Ndio mtafufuliwa nyote, nanyi ni madhalili na wanyonge.
Rudi kwenye Sura

19. Kwani hakika kufufuliwa ni Ukelele mmoja tu, mara wote watakuwa wahai wakiyaona waliyo ahidiwa.
Rudi kwenye Sura

20. Na washirikina watasema: Ee msiba wetu huu! Hii ndiyo Siku ya Hisabu na Malipo kwa a'mali zilio tendwa!
Rudi kwenye Sura

21. Watajibiwa: Hii ndiyo Siku ya Hukumu na kufarikisha vitendo, mliyo kuwa mkiikadhibisha.
Rudi kwenye Sura

22,23. Enyi Malaika wangu! Wakusanyeni walio jidhulumu nafsi zao kwa kufuru, pamoja na wake zao wa kikafiri, na miungu yao waliyo kuwa wakiiabudu badala ya Mwenyezi Mungu, yakiwa masanamu au watu, na waonyesheni njia ya kwendea  Motoni waingie humo.
Rudi kwenye Sura

24. Na wazuieni hapo hapo; kwani wao hakika watahojiwa juu ya imani zao na vitendo vyao.
Rudi kwenye Sura

25. Enyi washirikina! Mna nini? Mbona hamsaidiani kama mlivyo kuwa mkisaidiana nyinyi kwa nyinyi duniani?
Rudi kwenye Sura

26. Leo hii hawasaidiani, bali leo wanaongozwa tu, wamekwisha salimu amri.
Rudi kwenye Sura

27. Watakuwa wakikabiliana kulaumiana na kusutana, na wakiulizana khabari za mwisho wao muovu.
Rudi kwenye Sura

28. Wanyonge watawaambia walio jipa ukubwa: Nyinyi mlikuwa mkitujia upande tulio udhania ni wa kheri na mafanikio, ili mtugeuze njia tuache Haki twende kwenye upotovu.
Rudi kwenye Sura

29. Watasema walio jipa ukubwa: Sisi hatukukugeuzeni njia, lakini nyinyi wenyewe mliikataa Imani, na mkaipuuza kwa khiari yenu.
Rudi kwenye Sura

30. Na sisi hatukuwa na madaraka juu yenu hata tuweze kukunyang'anyeni uweza wenu wa kukhiari. Bali nyinyi wenyewe mlikuwa watu mlio iacha Haki.
Rudi kwenye Sura

31. Basi neno la Mola wetu Mlezi limethibiti juu yetu. Hakika hapana shaka sisi tutaionja adhabu ya Siku ya Kiyama.
Rudi kwenye Sura

32. Tukakuiteni kwenye maasi na upotovu na nyinyi mkaitikia wito wetu. Kazi yetu ni kufanya hila ya kuwaita watu wafuate upotovu tulio nao. Basi hatuna lawama.
Rudi kwenye Sura

33. Kwani hakika wafuasi na wenye kufuatwa wote watashiriki pamoja katika adhabu ya Siku ya Kiyama.
Rudi kwenye Sura

34. Hakika mfano wa adhabu hiyo Sisi tunawapa wale walio fanya makosa katika Haki ya Mwenyezi Mungu kwa ushirikina na kutenda maasi.
Rudi kwenye Sura

35. Hakika watu hao walikuwa wakiambiwa: La ilaha illa 'Llah, Hapana mungu ila Mwenyezi Mungu tu, wakakataa kukiri kwa kiburi na majivuno.
Rudi kwenye Sura

36. Na husema: Sisi tuache kuabudu miungu yetu kwa kufuata kauli ya mtunga mashairi aliye zugwa asiye kuwa na akili?
Rudi kwenye Sura

37. Bali Mtume wao amewaletea Tawhidi, Imani ya Mwenyezi Mungu Mmoja, ambayo ndiyo wito wa Mitume wote, naye akasadikisha kwa hivyo wito wa hao Mitume.
Rudi kwenye Sura

38. Enyi washirikina! Hakika nyinyi hapana shaka mtaionja adhabu kali ya Akhera.
Rudi kwenye Sura

39. Na hamtapata malipo Akhera ila malipo ya vitendo vyenu vya duniani.
Rudi kwenye Sura

40. Ila waja wangu walio safika; hao hawataionja adhabu kwa sababu wao ni watu wa Imani na ut'iifu.
Rudi kwenye Sura

41. Hawa watu wa ikhlasi watapata Akhera riziki maalumu kwa Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye Sura

42. Matunda ya namna mbali mbali. Nao watastareheshwa na kutukuzwa,
Rudi kwenye Sura

43. Katika Bustani zenye neema.
Rudi kwenye Sura

44. Wakikaa humo juu ya viti wakikabiliana.
Rudi kwenye Sura

45. Watawazungukia watoto na chombo chenye kinywaji kilicho toka kwenye chemchem zisio katika.
Rudi kwenye Sura

46. Kinywaji chenyewe ni cheupe kinapo changanywa, na kitamu kwa wenye kukinywa.
Rudi kwenye Sura

47. Hakiwaumizi kichwa na kuwaletea ghururi, wala kwa kukinywa hicho haiwapotei akili yao kidogo kidogo, yaani hakileweshi.
Rudi kwenye Sura

48. Na watu hawa wat'iifu walioko Peponi watakuwa nao mahuruleini walio safi, wema, macho yao hayawatazami ila waume zao tu, basi hawayatafuti matamanio maovu, jicho la mwema haliangalii ila mema.
Rudi kwenye Sura

49. Hao wanawake wenye macho ya staha ni kama mayai ya mbuni, yaliyo hifadhiwa na mbawa zake. Basi hayaguswi na mikono, wala hayapati vumbi.
Rudi kwenye Sura

50. Hao watu wema watakuwa wakiingia kuulizana hali, na walikuwaje duniani?
Rudi kwenye Sura

51. Hapo mmoja wao atasema: Mimi nalikuwa na rafiki katika washirikina, akijadiliana nami katika mambo ya Dini na yaliyo kuja katika Qur'ani.
Rudi kwenye Sura

52. Akisema: Ati wewe ni katika hao wanao sadiki kuwa kupo kufufuliwa na kuhisabiwa na kulipwa baada ya kufa?
Rudi kwenye Sura

53. Ati baada ya kwisha teketea, tukawa udongo na mafupa, tutakuja kuwa hai mara nyengine, tuhisabiwe na tulipwe kwa vitendo tulivyo kwisha vitenda?
Rudi kwenye Sura

54. Muumini awaambie wenzie alio kaa nao: Enyi watu wa Peponi, mnawaona watu wa Motoni nipate kumwona rafiki yangu?
Rudi kwenye Sura

55. Jicho lake lipige duru kuelekea Motoni, na huko amwone sahibu yake wa zamani yuko katikati akiadhibika kwa Moto.
Rudi kwenye Sura

56. Akimwona aseme: Wallahi! Ulikaribia kule duniani kunihilikisha lau ningeli kufuata katika ukafiri wako na maasiya yako!
Rudi kwenye Sura

57. Na lau kuwa si neema ya Mola wangu Mlezi kwa hidaya yake na kuniwezesha kwake nikamuamini Mwenyezi Mungu na kufufuka, basi ningeli kuwa mfano wako wewe katika walio hudhurishwa katika hiyo adhabu.
Rudi kwenye Sura

58,59. Je! Sisi tutakaa milele tukineemeka katika Pepo, wala hatufi kabisa isipo kuwa kule kufa kwetu mara ya kwanza duniani, na wala hatuadhibiwi baada ya kwisha ingia Peponi?
Rudi kwenye Sura

60. Hakika haya aliyo tupa Mwenyezi Mungu katika ukarimu wa Peponi bila ya shaka ndiyo kufuzu kukubwa, na kuvuka kukuu na hiyo adhabu tuliyo kuwa tunatahadhari nayo tangu duniani.
Rudi kwenye Sura

61. Ili wapate ukarimu wa Akhera kama walio bahatika kuupata Waumini, basi nawafanye kazi duniani hao wafanyao kazi, ili wapate kama walio pata wao.
Rudi kwenye Sura

62. Je! Hiyo riziki maalumu iliyo andaliwa kwa sababu ya watu wa Peponi ni bora, au mti wa Zaqqum ulio andaliwa kwa ajili ya watu wa Motoni?
Rudi kwenye Sura

63. Hakika Sisi tumeujaalia mti huu uwe ni mtihani na adhabu ya Akhera kwa ajili ya washirikina.
Rudi kwenye Sura

64. Hakika huo ni mti ulioko katikati ya Jahannamu, umekulia huko Motoni, na umeumbwa kutokana na huko huko.
Rudi kwenye Sura

65. Matunda yake mabaya kuyatazama, yana sura ya kukirihisha, macho hayapendi kuyatazama, kama vichwa vya mashetani ambavyo kwa hakika watu hawajaviona, lakini mtu humpitikia tu katika dhana jinsi ya ubaya wake.
Rudi kwenye Sura

66. Na wao watakuwa wanakula matunda ya mti huo, na wajaze matumbo yao kwayo. Kwani hawanacho kinginecho cha kukila.
Rudi kwenye Sura

67. Kisha washirikina hao juu ya kula mti wa Zaqqum watapewa maji yaliyo changanywa, yamoto, ya kuwababua nyuso zao, na kukatakata matumbo yao.
Rudi kwenye Sura

68. Tena mwisho wao ni Motoni. Wao watakuwa katika adhabu ya milele. Wataletwa kutoka Motoni waje kula mti wa Zaqqum kisha wanyweshe kinywaji hicho, na tena warejeshwe mahala pao katika Jahannamu.
Rudi kwenye Sura

69,70. Wao waliwakuta baba zao wamepotoka, na wao wakafanya haraka kufuata zile zile nyayo za baba zao. Wakawa mbioni kwendea njia yao, wakifuata tu wala hawachungui, kama walio timuliwa na wakihimizwa wende mbio mbio kuwafuata hao baba zao bila ya kupima wala kuzingatia.
Rudi kwenye Sura

71. Na hakika walipotea njia ya sawa na njia ya Imani wengi katika mataifa yaliyo kwisha tangulia kabla ya hawa washirikina wa Makka.
Rudi kwenye Sura

72. Na bila ya shaka Sisi tuliyatumia Mitume hayo mataifa yaliyo tangulia ili wawaonye na wawahadharishe na adhabu ya Mwenyezi Mungu, nao wakawakadhibisha.
Rudi kwenye Sura

73. Basi angalia, ewe uliye jaaliwa kuangalia, ulikuwaje mwisho wa walio onywa na Mitume? Bila ya shaka waliteketezwa, wakawa ni mazingatio kwa watu.
Rudi kwenye Sura

74. Lakini walikuwapo Waumini ambao aliwakhitari Mwenyezi Mungu wamuabudu Yeye, ili wapate fadhila za ukarimu wake. Basi hao walizipata thawabu zake, na wakaepukana na adhabu yake.
Rudi kwenye Sura

75. Na hakika Nuhu alitwita alipo kwisha kata tamaa na watu wake, basi na Sisi tukawa ni wabora wa kuitikia wito wake, tulipo muitikia ombi lake, na tukawaangamiza watu wake kwa tofani.
Rudi kwenye Sura

76. Na tukamwokoa Nuhu na walio amini pamoja naye, wasizame na kuteketea kwa tofani.
Rudi kwenye Sura

77. Tukawajaalia vizazi vya Nuhu ndio walio bakia katika ardhi baada ya kuteketea watu wake.
Rudi kwenye Sura

78. Na tukamwachilia Nuhu kutajwa kwa wema na watu walio kuja baada yake wakimdhukuru mpaka Siku ya Kiyama.
Rudi kwenye Sura

79. Maamkio ya Salama na Amani kumuamkia Nuhu kutokana na Malaika, na watu, na majini.
Rudi kwenye Sura

80. Hakika Sisi huwalipa walio tenda mema mfano wa haya. Basi aliingia katika Jihadi kulinyanyua Neno letu, na akavumilia maudhi kwa ajili yetu.
Rudi kwenye Sura

81. Hakika yeye ni miongoni mwa waja wetu walio tuamini, na wakatimiza ahadi yetu, na wakaufikisha Ujumbe wetu.
Rudi kwenye Sura

82. Kisha tukawazamisha wenginewe katika makafiri wa kaumu yake.
Rudi kwenye Sura

83. Na hakika bila ya shaka Ibrahim alikuwa akifuata ile ile njia yake na mwenendo wake katika kuitia Tawhidi, Imani ya Mwenyezi Mungu Mmmoja, na kumuamini Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye Sura

84. Alipo mkabili Mola wake Mlezi kwa moyo ulio kuwa nadhifu hauna ushirikina, umemsafia ibada Yeye tu.
Rudi kwenye Sura

85. Alipo chukia kuwa baba yake na watu wake wanaabudu masanamu, akawaambia: Ni nini haya masanamu mnayo yaabudu?
Rudi kwenye Sura

86. Si mnazua uwongo tu ulio wazi kwa haya myatendayo, kwa kuwa mnamuabudu asiye kuwa Mwenyezi Mungu? Na si mnataka kuzua uzushi huu bila ya udhuru wowote ila kupenda kwenu tu?
Rudi kwenye Sura

87. Mnamdhania nini huyo ambaye ndiye Mwenye haki ya kuabudiwa kwa kuwa Yeye ndiye Muumba walimwengu wote, mtapo kutana naye na hali nyinyi mmemfanyia washirika wenginewe katika ibada?
Rudi kwenye Sura

88. Basi akazitupia jicho nyota kuzitazama ili apate kuona dalili ya Muumba ulimwengu. Akaziona zinageuka, zinabadilika.
Rudi kwenye Sura

89. Akajikhofia nafsi yake asiwe ana upotovu na maradhi ya itikadi.
Rudi kwenye Sura

90. Watu wake wakamwachilia mbali, na wakapuuza maneno yake.
Rudi kwenye Sura

91. Akayaendea kwa haraka yale masanamu kwa kificho, na akayapa chakula ambacho wale washirikina walikiweka mbele yao ili nao wapate baraka yao kwa mujibu wa madai yao. Akasema kwa maskhara na kejeli: Mbona hamli?
Rudi kwenye Sura

92. Mna nini hata mmeshindwa kusema lolote, hata ndio au sio?
Rudi kwenye Sura

93. Akayaingilia yale masanamu kuyapiga kwa mkono wa kulia, kwa kuwa ndio wenye nguvu, akayabomoa.
Rudi kwenye Sura

94. Walipo baini kwamba kuvunjwa miungu yao ni kwa kitendo cha Ibrahim, basi walimkimbilia ili wamtese kwa alivyo watendea miungu yao.
Rudi kwenye Sura

95. Ibrahim akawaambia kwa kuwahizi: Hivyo nyinyi mnaabudu mawe mliyo yachonga nyinyi wenyewe kwa mikono yenu? Akili zenu zimekwenda wapi?
Rudi kwenye Sura

96. Na Mwenyezi Mungu ndiye aliye kuumbeni, na akayaumba hata hayo masanamu mnayo yaunda kwa mikono yenu. Basi Yeye peke yake ndiye Mwenye kustahiki kuabudiwa.
Rudi kwenye Sura

97. Hoja ilipo wapata wale wanao abudu masanamu, wakaona hawana ila waingie kutumia nguvu; wakaazimia kumchoma moto.  Basi waliambizana: Mjengeeni jengo, na mlijaze moto, na mtupeni katikati yake!
Rudi kwenye Sura

98. Kwa haya walikusudia kumteketeza, lakini Mwenyezi Mungu alimwokoa na ule moto baada ya wao kwisha mtumbukiza humo. Hadhi yake ikawa juu kwa utukufu ule, na Mwenyezi Mungu akawafanya wao ndio watu wa chini.
Rudi kwenye Sura

99. Ibrahim alipo kata tamaa nao, kuwa hawaamini tena, alisema: Mimi ninahama kwendea pahala alipo niamrisha Mola wangu Mlezi nende. Mola wangu Mlezi atanihidi aniongoze mpaka nifike pahala pa utulivu, penye amani, na nchi nzuri.
Rudi kwenye Sura

100. Ewe Mola wangu Mlezi! Nipe dhuriya walio wema wa vitendo, wasimamie hii kazi ya wito kuwaitia watu kwako Wewe, baada yangu.
Rudi kwenye Sura

101. Malaika wakampa bishara ya kwamba atapata mwana atakaye pambwa kwa akili na upole.
Rudi kwenye Sura

102. Akazaliwa huyo mwana, na alipo kuwa kijana wa kwenda naye baba yake katika kutafuta haja za maisha, Ibrahim alipewa mtihani kwa ndoto aliyo iota. Ibrahim akasema: Ewe mwanangu! Hakika mimi nimeona usingizini ufunuo kutokana na Mwenyezi Mungu ananitaka nikuchinje! Basi wewe tazama unaonaje? Yule mwana mwema alisema: Ewe baba yangu! Tekeleza amri ya Mola wako Mlezi. Utaniona mimi katika wanao subiri, Inshallah!
Rudi kwenye Sura

103. Yule baba na mwanawe walipo iridhia hukumu ya Mwenyezi Mungu, na akamweka juu ya fungu la mchanga na akamlaza juu yake, kipaji chake kikawa juu ya ardhi, akawa tayari kumchinja.
Rudi kwenye Sura

104,105. Na Mwenyezi Mungu akajua umadhubuti wa Ibrahim na mwanawe katika majaribio, Mwenyezi Mungu alimwita Ibrahim kwa wito wa kirafiki: Ewe Ibrahim! Hakika umeuitikia kwa utulivu huo ufunuo wa ndoto, na wala hukusitasita katika kufuata amri. Basi haya yanakutosha. Sisi tunakupunguzia haya majaribio yetu kuwa ni malipo kwa wema wako, kama tunavyo walipa walio wema kwa wema wao.
Rudi kwenye Sura

106. Hakika majaribio haya tuliyo mjaribia Ibrahim na mwanawe bila ya shaka ni majaribio yaliyo dhihirisha undani wa Imani yao na yakini yao kwa Mola Mlezi wa walimwengu.
Rudi kwenye Sura

107. Na tukamkomboa kwa mhanga wenye cheo kikubwa, kwa kuwa hayo ni kwa amri ya Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye Sura

108. Na tukaacha atajike kwa sifa nzuri katika ndimi za walio kuja baada yake.
Rudi kwenye Sura

109. Maamkio ya amani na salama kwa Ibrahim!
Rudi kwenye Sura

110. Mfano wa malipo kama haya ya kuwakinga na balaa ndivyo tunavyo walipa walio wema katika kufuata amri za Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye Sura

111. Hakika Ibrahim ni katika waja wetu wanao ifuata Haki.
Rudi kwenye Sura

112. Na kwa amri yetu, Malaika walimbashiria kuwa ataruzukiwa mwana, Is-haqa juu ya kukata tamaa na kuwa mkewe ni tasa. Na kwamba yeye hakika atakuwa Nabii miongoni mwa walio wema.
Rudi kwenye Sura

113. Nasi tukamtunukia yeye na mwanawe baraka na kheri duniani na Akhera. Na miongoni mwa vizazi vyao watatokea watakao jifanyia wema nafsi zao kwa Imani na ut'iifu, na watakao jidhulumu kwa upotovu wa ukafiri na maasi.
Rudi kwenye Sura

114. Na bila ya shaka tuliwaneemesha Musa na Haruni kwa kuwapa Unabii na neema kubwa kubwa.
Rudi kwenye Sura

115. Na tukawaokoa wao na watu wao kutokana na dhiki kubwa iliyo kuwa iwashukie kutokana na Firauni na kaumu yake.
Rudi kwenye Sura

116. Na Sisi tukawanusuru na adui zao, wakawa wao ndio wenye kushinda.
Rudi kwenye Sura

117. Na tukampa Musa na Haruni Kitabu kilicho wazi chenye kubainisha hukumu za Dini, nacho ni Taurati.
Rudi kwenye Sura

118. Na tukawaongoza waifuate Njia iliyo sawa.
Rudi kwenye Sura

119. Na tukabakisha sifa njema za kutajika wote wawili hao kwa watu wengineo walio kuja baada yao.
Rudi kwenye Sura

120. Maamkio ya Amani na Salama kwa Musa na Haruni.
Rudi kwenye Sura

121. Hakika mfano wa malipo tuliyo mjazi Musa na Haruni ndivyo tunavyo wajazi wote walio wema.
Rudi kwenye Sura

122. Hakika wawili hao ni katika waja wetu wenye kuifuata Haki.
Rudi kwenye Sura

123. Na hakika Ilyas ni katika hao tulio watuma kwenda waongoa watu wao.
Rudi kwenye Sura

124. Ilyas alipo waambia watu wake, nao walikuwa wakiyaabudu masanamu yao: Je! Mnaendelea juu ya makosa yenu, na wala hamumkhofu Mwenyezi Mungu mkajikinga na adhabu yake?
Rudi kwenye Sura

125. Mnaliabudu sanamu linalo itwa Baa'li, na mkaacha kumuabudu Mwenyezi Mungu aliye uumba ulimwengu na akaufanya mzuri uumbaji wake?
Rudi kwenye Sura

126. Mwenyezi Mungu amekuumbeni na amekuhifadhini nyinyi na baba zenu wa zamani. Yeye basi ndiye Mwenye haki ya kuabudiwa.
Rudi kwenye Sura

127. Lakini walimkadhibisha, basi jaza yao ni kuhudhurishwa kwenye Moto Siku ya Kiyama.
Rudi kwenye Sura

128. Isipo kuwa waja wa Mwenyezi Mungu walio safisha Imani yao. Hao basi ndio wenye kufuzu.
Rudi kwenye Sura

129. Na tukamjaalia awe anatajwa kwa wema na ndimi za walio kuja baada yake.
Rudi kwenye Sura

130. Salamu juu ya Ilyasi, au juu yake yeye na watu wake, kwa kuwa kawashinda.
Rudi kwenye Sura

131. Hakika mfano wa malipo tuliyo mlipa Ilyas tunamlipa kila aliye mwema kwa sababu ya wema wake.
Rudi kwenye Sura

132. Hakika Ilyas ni katika waja wetu walio amini.
Rudi kwenye Sura

133. Na hakika Lut'i ni katika Mitume tulio watuma ili afikishe Ujumbe wetu kwa watu.
Rudi kwenye Sura

134. Kwa hakika Sisi tumemwokoa yeye na ahali zake wote kutokana na adhabu iliyo wasibu watu wake.
Rudi kwenye Sura

135. Ila mkewe mkongwe. Yeye bila ya shaka aliteketea pamoja na walio teketea.
Rudi kwenye Sura

136. Kisha tukawaangamiza wote isipo kuwa Lut'i na walio muamini.
Rudi kwenye Sura

137,138. Na hakika nyinyi, watu wa Makka, mnayapitia majumba ya hao kaumu Lut'i katika safari zenu za kwendea Sham asubuhi au usiku. Je!  Mmepotelewa na akili zenu hata hamwezi kuzingatia yaliyo wapitia hao kuwa ni malipo ya ukanushaji wao?
Rudi kwenye Sura

139. Na hakika Yunus ni miongoni mwa tulio watuma wawafikishie Ujumbe wetu watu.
Rudi kwenye Sura

140,141. Alipo wahama watu wake bila ya amri ya Mola wake Mlezi, akaliendea jahazi ambalo lilio kwisha sheheni pomoni, akalipanda. Jahazi likapatikana na mambo ikawajibikia lazima mmoja katika abiria atoswe kupunguza shehena yake. Kura ikamuangukia Yunus, akashindwa kwa kura. Akatoswa baharini kwa mujibu wa ada yao zama zile.
Rudi kwenye Sura

142. Samaki akammeza, naye hakika alistahiki lawama kwa kuikimbia kazi yake ya Daa'wa, Wito, kuwaitia watu wafuate Haki, na kuacha kuwasubiria wale walio kwenda kinyume naye..
Rudi kwenye Sura

143,144. Na lau kuwa Yunus hakuwa katika wanao mtakasa Mwenyezi Mungu, wanao dumu kumdhukuru, angeli kufa ndani ya samaki, wala asingeli toka humo mpaka siku ya kufufuliwa.
Rudi kwenye Sura

145. Tukamtupa pahali patupu kwenye nchi pasipo kuwa na miti wala majumba, naye ni mgonjwa kwa yaliyo mpata.
Yaliyo mtokea Sayyidna Yunus a.s. ni muujiza. Lakini nayo si muhali kutokea mtu kumezwa na samaki, na akabakia yuhai ndani yake kwa muda fulani. Mawili yaweza kuwa -
* Kwanza, ni kuwa huyo samaki ni namna asiye kuwa na meno katika kabila ya nyangumi wakubwa kabisa, kama nyangumi wanao onekana sana katika Bahari ya Kati (Mediterranean). Urefu wake huweza kufika Mita 20. Alibaki Yunus katika mpandikizi wa kinywa chake huyo nyangumi mpaka alipo mtema kwenye ufukwe mtupu, kwani koo ya nyangumi ni nyembamba hawezi kupita mtu.
* Pili, yaweza kuwa huyo samaki ni namna ya wenye meno pia, kama nyangumi wa ambari, na ambaye pia urefu wake hufika mita 20. Hawa mara kadhaa wa kadhaa huonekana katika Bahari ya Kati. Nyangumi hao yawezekana kwa kawaida kuwameza wanyama wakubwa wanao pita  urefu wa mita tatu.
Rudi kwenye Sura

146. Tukauotesha mmea wa kutambaa, usio simama juu ya kigogo, ukamfunika na kumkinga na madhara ya hali ya hewa.
Rudi kwenye Sura

147. Hata alipo pata nafuu kutokana na yaliyo msibu, tukamtuma awaendee watu wengi. Wanasema walio waona kuwa wanapata laki moja au zaidi.
Rudi kwenye Sura

148. Wakauwitikia wito wake, nasi tukawakunjulia neema zetu kwa muda maalumu.
Rudi kwenye Sura

149. Ewe Nabii! Waulize watu wako: Ati Mwenyezi Mungu aliye kuumba ana watoto wa kike kinyume na wao; na wao ndio wana watoto wanaume  kinyuma na Yeye?
Rudi kwenye Sura

150. Ati tumewaumba Malaika kuwa ni wanawake, na wao hao makafiri waliona kwa macho yao kuumba kwao, na ndio wakasimulia walio yaona?
Rudi kwenye Sura

151,152. Ewe mwenye kusikia! Yazingatie maneno yao. Hakika wao kwa uwongo wao wanasema: Mwenyezi Mungu amezaa! Na hali Yeye ametakasika na upungufu kama huo wa kuwa mzazi au kuzaliwa. Na hakika bila ya shaka hao ni waongo kwa usemi huo, kwa ushahidi wa dalili nyingi za Upweke wake.
Rudi kwenye Sura

153. Ati Yeye amejichagulia mwenyewe mabinti ambao kwa madai yenu ndio mnawachukia kuliko watoto wa kiume ambao mnawapenda, na hali Yeye ndiye Mwenye kuwaumba wote,  watoto wa kike na wa kiume?
Rudi kwenye Sura

154. Ni nini lilio kusibuni hata mkakata hukumu bila ya ushahidi? Vipi mnahukumu hivyo na hali ni upotovu ulio wazi?
Rudi kwenye Sura

155. Je! Mmesahau dalili za uweza wake na kutakasika kwake, ndio msikumbuke mpaka mkaingia katika upotovu?
Rudi kwenye Sura

156. Hebu nyinyi mnazo nguvu za ushahidi wa kubainisha wa kuthibitisha hayo mnayo yadai?
Rudi kwenye Sura

157. Basi leteni hoja zenu, ikiwa mnazo hoja za katika Kitabu cha mbinguni, kama nyinyi ni wakweli katika hayo myasemayo na mnayo yahukumia.
Rudi kwenye Sura

158. Wakashikilia katika itikadi zao, na wakazua baina ya Mwenyezi Mungu na majini, ambao hawawaoni,  kuwa ati yapo makhusiano ya nasaba. Na bila ya shaka hao majini walikwisha jua kuwa makafiri watahudhurishwa mbele ya Mwenyezi Mungu ili wapate malipo yao yasiyo kimbilika.
Rudi kwenye Sura

159. Mwenyezi Mungu Mtukufu ametakasika na hizo sifa za kuemewa na za upungufu wanazo mzulia kuwa anazo.
Rudi kwenye Sura

160. Lakini waja wa Mwenyezi Mungu walio khitariwa wakasafishwa  hawana makosa ya huo uzushi wa makafiri.
Rudi kwenye Sura

161,162,163. Enyi makafiri! Hakika nyinyi, na hao mnao waabudu badala ya Mwenyezi Mungu - Nyinyi kwa kuwaabudu kwenu badala yake Yeye, hamtampoteza yeyote kwa upotovu wenu. Isipo kuwa yule ambaye tangu hapo Mwenyezi Mungu Mtukufu anamjua ni katika watu wa Motoni, na huko ataingia.
Rudi kwenye Sura

164. Na Malaika kuwania kuwa wao ni waja wa Mwenyezi Mungu, wakasema: Hapana yeyote katika sisi ila ana cheo chake maalumu katika ujuzi, na ibada, na wala hakikiuki hicho.
Rudi kwenye Sura

165. Na sisi tumejipanga safu wenyewe katika misimamo ya kutumika daima.
Rudi kwenye Sura

166. Na hakika sisi bila ya shaka yoyote ndio wenye kumtakasa Mwenyezi Mungu na kila lisilo kuwa na maelekeo naye katika kila hali.
Rudi kwenye Sura

167,168,169. Na walikuwapo makafiri wa Makka kabla ya kuteuliwa Mtume s.a.w. ambao wakisema: Lau kuwa sisi tungeli kuwa na Kitabu kama Vitabu vya watu wa zamani, yaani kama Taurati na Injili, nasi bila ya shaka tungeli kuwa waja wa Mwenyezi Mungu wenye kumsafia ibada Yeye.
Rudi kwenye Sura

170. Na Kitabu kikawajia, nao wakakikataa. Basi watakuja jua nini matokeo ya kukataa kwao.
Rudi kwenye Sura

171,172. Ninaapa! Hukumu yetu kwa Mitume tulio watuma imekwisha tolewa mbele, ya kwamba ushindi na matokeo mema ni yao wao dhidi ya makafiri.
Rudi kwenye Sura

173. Na kwamba wafuasi wetu na wasaidizi wetu ndio peke yao watakao washinda walio kengeuka.
Rudi kwenye Sura

174. Basi waachilie mbali, nawe ngoja mpaka wakati ujao. Kwani Sisi tutakupa wewe matokeo mema, na manusura, na ushindi.
Rudi kwenye Sura

175. Nawe watazame, na uangalie vyema adhabu gani na mateso yatakayo wapata kwa kwenda kinyume nawe na kukukadhibisha. Basi watakuja ona kwa macho yao zitakavyo shindwa safu zao, na wataona nusura ya Mwenyezi Mungu inavyo wafikia Waumini.
Rudi kwenye Sura

176. Je! Wamepoteza akili zao nini, hata wakawa wanaihimiza adhabu yetu?
Rudi kwenye Sura

177. Basi adhabu hiyo itakapo teremka kwenye uwanja wao mpana, itakuwa asubuhi ovu kweli hiyo kwa hao walio onywa na adhabu.
Rudi kwenye Sura

178. Na waachilie mbali mpaka mambo yatakapo waishia.
Rudi kwenye Sura

179. Na yaangalie yatakayo wafika wao na yatakayo kufika wewe. Wao watakuja yaona hayo wanayo yahimiza.
Rudi kwenye Sura

180. Mwenyezi Mungu, aliye kuumba wewe na aliye ziumba nguvu na ushindi, ametakasika na huo uzushi wanao muambatisha naye.
Rudi kwenye Sura

181. Na salamu zishuke juu ya Mitume wapenzi walio safika.
Rudi kwenye Sura

182. Na sifa njema ni za Mwenyezi Mungu peke yake, Muumba wa viumbe vyote, na Mwenye kuwaangalia makhaluku wote.
Rudi kwenye Sura