1. Alif Lam Mim - Hizi ni harufi za kutamkwa na zikasikilizana, zilizo letwa ili kubainisha kwamba hii Qur'ani yenye kuwaemea watu kuiiga imetungwa kwa harufi hizi hizi mnazo ziweza kuzitamka vizuri. Na pia ni kwa ajili ya kuwazindua wasikilizaji na wapate kuiangalia Haki.
Rudi kwenye Sura

2. Hivyo watu wanadhani kwamba wataachiliwa tu hivi hivi kwa sababu ya kutamka kwao shahada mbili basi, bila ya kujaribiwa kwa mitihani na shida ili utambulikane ukweli wa Imani yao? La, sivyo hivyo! Bali hapana budi kutiwa mithanini.
Rudi kwenye Sura

3. Na bila ya shaka Mwenyezi Mungu alikwisha zijaribu kaumu zilizo tangulia kwa kuwapa shida na namna  mbali mbali za neema na mitihani, ili yapate kuonekana yale ambayo Yeye anayajua tangu mwanzo, na awatengue baina ya walio kuwa wakweli katika Imani yao, na waongo.
Rudi kwenye Sura

4. Wanadhani wanao mshirikisha Mwenyezi Mungu na wanamuasi kwamba watatuponyoka katika kukimbia kwao kuikimbia adhabu ya Mwenyezi Mungu na malipo yake? Kuhukumu kwao huku ni kuovu mno!
Rudi kwenye Sura

5. Mwenye kuamini kufufuliwa, na akawa anataraji malipo ya Mwenyezi Mungu, na anaikhofu adhabu yake, basi huyo Imani yake ni ya kweli. Basi na aingie kwenye vitendo vyema. Kwani Siku iIliyo ahidiwa itakuja tu, hapana hivi wala hivi. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia maneno ya waja, ni Mwenye kuvijua vitendo vyao. Na atamlipa kila mmoja kwa anavyo stahiki.
Rudi kwenye Sura

6. Na mwenye kuwania jihadi kwa sababu ya kutukuza Neno la Mwenyezi Mungu, na akapambana na nafsi yake ivumilie juu ya ut'iifu, basi malipo ya jihadi yake yatamrudia mwenyewe. Na hakika Mwenyezi Mungu aliye takasika si mhitaji wa ut'iifu wa walimwengu.
Rudi kwenye Sura

7. Na wale walio sifika kwa Imani na wakatenda mema hapana shaka tutawaondolea makosa yao, na tutawasamehe, na tutawalipa bora ya malipo kwa vitendo vyao vyema.
Rudi kwenye Sura

8. Na Mwenyezi Mungu amemuamrisha mwanaadamu afanye ukomo wa uwezo wake kuwafanyia wema wazazi wake na kuwat'ii. Na wakikushikilia kumfanyia shirki Mwenyezi Mungu - na hayo hayakubaliki katika ilimu wala akili - basi usiwat'ii. Na marejeo ya viumbe vyote ni kwa Mwenyezi Mungu, na Yeye atawaeleza waliyo yatenda duniani, na atawalipa kwayo.
Rudi kwenye Sura

9. Na walio msadiki Mwenyezi Mungu na Ujumbe wake, na wakatenda mema, basi hao hapana shaka Mwenyezi Mungu atawaingiza pamoja na walio wema, wapate malipo yao na wayastarehee.
Rudi kwenye Sura

10. Na miongoni mwa watu yupo ambaye husema kwa ulimi wake: Tumeamini. Na akipata dhiki yoyote kwa ajili ya Mwenyezi Mungu hukereka na akafitinika hata katika dini yake. Wala haifikirii adhabu ya Mwenyezi Mungu ya Siku ya Kiyama. Yeye huyo huwa kama kwamba anafanya mateso ya wanaadamu kuwa sawa na adhabu ya Mwenyezi Mungu ya Akhera. Mwenyezi Mungu akiwanusuru Waumini, akawapa ushindi kuwashinda maadui zao na wakapata ngawira, watu hao wanao dhihirisha imani huja wakawaambia Waislamu: Sisi ni wenzenu katika Imani. Basi hebu tupeni nasi fungu letu la ngawira. Wasidhani watu hawa kwamba mambo yao yamefichikana kwa Mwenyezi Mungu, kwani Mwenyezi Mungu anayajua yaliomo vifuani mwa watu, ikiwa unaafiki au Imani.
Rudi kwenye Sura

11. Na hapana shaka Mwenyezi Mungu atawadhihirishia watu yale ambayo Yeye anayajua tangu hapo. Atawatenga mbali mbali baina ya Waumini na wanaafiki. Na kila mmoja atamlipa kwa alilo litenda.
Rudi kwenye Sura

12. Waongozi wa shirki walikuwa wakiwaambia wale walio ingia katika Uislamu kwa usafi wa niya: Kueni kama mlivyo kuwa katika dini yetu. Na fuateni tunayo fuata sisi. Na ikiwa kama huko kutakuwapo kufufuliwa na kuhisabiwa ambako nyinyi mnakuogopa, basi sisi tutakubebeeni madhambi yenu. Hapana mtu atakayembebea mwenzie dhambi zake. Hakika hao makafiri ni waongo tu katika hiyo ahadi yao.
Rudi kwenye Sura

13. Basi makafiri wataibeba wenyewe mizigo yao mizito, na juu ya hiyo watabeba mfano wa mizigo ya wale walio wapoteza na wakawazuia wasiifuate Haki. Na hapana shaka yoyote watahisabiwa Siku ya Kiyama kwa walio kuwa wakiyazua ya uwongo duniani, na watapewa adhabu kwa hayo.
Rudi kwenye Sura

14. Na Mwenyezi Mungu alimtuma Nuhu ende kwa watu wake awaite wafuate Tawhidi, Imani ya Mwenyezi Mungu Mmoja. Akakaa nao miaka mia tisa na khamsini akiwalingania. Nao hawakumuitikia. Mwenyezi Mungu akawazamisha kwa kuwapelekea tufani (kimbunga), nao ni wenye kujidhulumu nafsi zao kwa ukafiri.
Rudi kwenye Sura

15. Mwenyezi Mungu akamtimilizia Nuhu ahadi yake, na akamwokoa yeye na Waumini walio panda naye jahazi. Na akakifanya kisa chao ni funzo kwa walio kuja baadae.
Rudi kwenye Sura

16. Na kumbuka, ewe Mtume, kisa cha Ibrahim, pale alipo wataka watu wake wamuamini Mwenyezi Mungu Mmoja na wamt'ii Yeye, na akawanabihisha kwamba kuamini ni bora kwao kuliko kukanusha, ikiwa wao wana ujuzi na akili.
Rudi kwenye Sura

17. Akawaambia: Nyinyi hamuabudu badala ya Mwenyezi Mungu ila vinyago na masanamu mnayo yaunda kwa mikono yenu. Na mnazua uwongo na mnayaita kuwa miungu. Na haya masanamu mnayo yaabudu badala ya Mwenyezi Mungu hayakufaini wala hayakudhuruni, wala hayawezi kukupatieni riziki. Basi tafuteni riziki kwa Mwenyezi Mungu peke yake, na muabuduni Yeye tu, na mshukuruni Yeye tu kwa neema zake. Kwani kwake Yeye ndio marejeo yenu nyote, naye atakulipeni kwa mujibu wa vitendo vyenu.
Rudi kwenye Sura

18. Na mkishikilia kunikadhibisha mimi basi hamtanidhuru kitu. Kwani bila ya shaka nimekwisha kwambieni kwamba Mitume wa kabla yangu walikanushwa  na kaumu zao, na hawakuwadhuru kitu, bali walijidhuru wenyewe nafsi zao, pale Mwenyezi Mungu alipo waangamiza kwa sababu ya kukadhibisha kwao. Basi Mjumbe hana jukumu lolote ila kufikisha Ujumbe wake kwa kaumu yake kwa uwazi.
Rudi kwenye Sura

19. Hakika wamekwisha ona na wamejua kwamba hakika Mwenyezi Mungu ndiye aliye anzisha uumbaji, na akisha akaurudisha tena. Basi vipi ikawa wanakanusha kufufuliwa Siku ya Akhera kwa ajili ya hisabu na malipo? Hakika kurejesha tena kwa Mwenyezi Mungu ni jambo jepesi zaidi.
Rudi kwenye Sura

20. Ewe Mtume! Waambie hawa wanao kanusha: Tembeeni katika ardhi, na zingatieni vilivyo vitu mbali mbali alivyo viumba Mwenyezi Mungu. Na angalieni mabaki ya waliyo kuwa kabla yenu, baada ya kwisha kufa kwao na majumba yao waliyo yaacha. Na jueni ya kuwa Mwenyezi Mungu kwa kudra yake atayarejesha yote hayo mwishoe kwa kufufua, nako ndiko huko kuumba umbo la baadaye. Hali kadhaalika shani yenu. Hakika Mwenyezi Mungu Subhanahu ni Mwenye kutimia uwezo wake juu ya kila kitu.
"Sema: Tembeeni katika ardhi na tazameni jinsi alivyo anzisha uumbaji; kisha Mwenyezi Mungu ndiye anaye umba umbo la baadaye. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza juu ya kila kitu." Aya hii tukufu inawahimiza wachunguzi wende katika dunia wapate kuvumbua vipi ulianza uumbaji wa vitu, tangu wanyama, na mimea mpaka visio kuwa na uhai. Kwani mabaki ya uumbaji wa mwanzo yamehifadhiwa baina ya tabaka za ardhi na juu yake. Na kwa hivyo ardhi ni daftari lilio sajiliwa ndani yake taarikhi yote ya uumbaji, tangu mwanzo wake mpaka hivi sasa.
Rudi kwenye Sura

21. Mwenyezi Mungu atawaadhibu awatakaye baada ya uumbaji mwingine, na hao ndio wale wenye kukanusha hayo. Na atawarehemu awatakaye, nao ndio Waumini wenye kuyakubali hayo. Na kwake Yeye peke yake ndio marejeo ya viumbe vyote kwa ajili ya hisabu na malipo.
Rudi kwenye Sura

22. Enyi mnao kadhibisha! Nyinyi hamtaweza kuishinda kudra ya Mwenyezi Mungu; sawa sawa mkiwa katika ardhi au katika mbingu. Bali hiyo kudra yake imekuzungukeni nyinyi. Wala nyinyi hamna mlinzi wa kukulindeni na Mwenyezi Mungu, wala msaidizi wa kukuzuilieni adhabu yake.
Rudi kwenye Sura

23. Na wale wanao zikataa dalili za Mwenyezi Mungu zinazo thibitisha upweke wake, na wakawakadhibisha Mitume wake na Vitabu vyake, na wakakanusha kufufuliwa na kuhisabiwa - watu hao hawana tamaa ya kupata rehema ya Mwenyezi Mungu. Na watu hawa watapata adhabu kali yenye kutia uchungu.
Rudi kwenye Sura

24. Na pale Ibrahim alipo waamrisha watu wake wamuabudu Mwenyezi Mungu na waache ile ibada ya masanamu waliyo kuwa nayo, hawakuwa na jawabu yoyote ya kumjibu ila kukakamia katika ukafiri, na kuambizana wenyewe kwa wenyewe: Muuweni, au mchomeni moto! Basi wakamtupa motoni. Lakini Mwenyezi Mungu akaufanya moto uwe baridi na wenye salama kwake. Na akamwokoa nao. Hakika kwa kubwatika vitimbi vyao na kuokoka kwake zipo dalili zilizo wazi kwa watu wanao isadiki Tawhidi (upweke) wa Mwenyezi Mungu na kudra yake.
Rudi kwenye Sura

25. Ibrahim akawaambia watu wake: Kwa nini mnaabudu miungu ya uwongo, na wala hamkatazani, kwa sababu ya mapenzi ya madhambi mliyo yakhiari katika maisha yenu ya dunia? Kisha hali itabadilika Siku ya Kiyama. Huko waongozi watawakataa wafuasi wao. Na wafwasi watawalaani waongozi wao. Na marejeo ya wote ni Motoni. Wala hamtakuwa na msaidizi wa kukuzuilieni msiingie humo.
Rudi kwenye Sura

26. Na alikuwa katika wa mwanzo wa kuitikia wito wa Ibrahim, ni Lut'i. Akasadiki, na kabla yake alikuwa kesha kuwa mwenye kushika Tawhid. Na Ibrahim akasema kwa kut'ii amri ya Mwenyezi Mungu: Mimi ninahama kwendea upande aliyo niamrisha Mola wangu Mlezi nihamie, na nikakae na huko niwaitie watu wamfuate Mwenyezi Mungu. Na Yeye ndiye Mwenye nguvu wa kuweza kunilinda na maadui zangu, Mwenye hikima ambaye haniamrishi ila lilio la kheri.
Rudi kwenye Sura

27. Na Mwenyezi Mungu akamtunukia Ibrahim kwa kumpa mwana, naye ni Is-haq, na kumpa mjukuu, naye ni Yaa'qub. Na akamfanyia ukarimu kwa kumjaalia Unabii katika dhuriya zake, na kuwateremshia Vitabu vya mbinguni, na kwa kumlipa bora ya malipo katika dunia, naye huko Akhera kuwa ni miongoni mwa bora ya watu wema.
Rudi kwenye Sura

28. Na ewe Mtume! Kumbuka pale tulipo mtuma Lut'i kwa kaumu yake, akawataka waishike Tawhidi ya Mwenyezi Mungu na ut'iifu wake. Na akawakataza kitendo kichafu walicho kuwa wakikitenda, ambacho hajapata kukitenda yeyote katika viumbe vya Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye Sura

29. Hakika hayo myatendayo ni maovu na yanahilikisha.  Kwani nyinyi mnawafanya mambo machafu wanaume, na mnaikata njia ya uzazi; na khatima ya hayo ni kutoweka kabisa. Na katika mikutano yenu mnatenda maovu bila ya kumkhofu Mwenyezi Mungu wala kuoneana haya baina yenu. Wala watu wake hawakumsikia, wala hawakuwa na jawabu ya kumpa ila kumfanyia maskhara tu. Na wakamtaka alete upesi hiyo adhabu ya Mwenyezi Mungu aliyo watishia kwayo, ikiwa yeye ni mkweli kwa hayo ayasemayo.
Rudi kwenye Sura

30. Basi Lut'i akamtaka msaada Mwenyezi Mungu kupambana nao, na akamwomba amnusuru juu ya watu wake wenye kufanya fisadi katika nchi.
Rudi kwenye Sura

31. Na walipo kuja Malaika wa Mwenyezi Mungu kwa Ibrahim, a.s. kwa kumbashiria, walisema kwamba wameamrishwa kuwaangamiza watu wa mji huo kwa sababu ya kufisidi kwao na kujidhulumu kwao wenyewe kwa ushirikina na kutenda uchafu.
Rudi kwenye Sura

32. Ibrahim a.s. akawaambia Malaika: Hakika katika huo mji yumo Lut'i. Basi vipi mtawaangamiza hao naye yumo kati yao. Malaika wakamjibu kwamba wao wanajua nani waliomo humo, na kwamba wao kwa hakika watamwokoa Lut'i na ahali zake wasipate adhabu, isipo kuwa mkewe. Yeye huyo atakuwa miongoni mwa watao angamizwa kwa sababu ya ukafiri wake na uovu wake.
Rudi kwenye Sura

33. Walipo ondoka wale Malaika walio tumwa kumuendea Lut'i naye  akawaona, alihuzunika kwa kuwakhofia uadui wa watu wake, na akaemewa asiwe na hila ya kuweza kuwalindai. Wao, basi, wakampoza na wakamwambia: Kabisa usiukhofu uadui wa kaumu yako juu yetu, wala usihuzunike kwa ajili yetu. Kwani sisi hakika tumekuja kuwaangamiza watu wa mji huu, na tutakuokoa wewe na ahali zako. Lakini mkeo atakuwa pamoja na wenye kuangamia.
Rudi kwenye Sura

34. Malaika wakasema: Hakika sisi tumetumwa kutimiliza amri ya Mwenyezi Mungu kwa kuwateremshia watu wa mji huu adhabu itokayo mbinguni kwa sababu ya uchafu wao na ukafiri wao.
Rudi kwenye Sura

35. Na Mwenyezi Mungu akauteketeza mji huu, na akaacha humo mabaki yaliyo wazi, ili yawe ni dalili ya kuonyesha aliyo wafanyia Mwenyezi Mungu, na funzo kwa mwenye kuzingatia.
Rudi kwenye Sura

36. Na Mwenyezi Mungu aliwapelekea watu wa Madyana Mtume kutokana nao wenyewe, naye ni Shuaibu. Akawaita waishike Tawhidi ya Mwenyezi Mungu, na wamuabudu Yeye tu, na waiogope Siku ya Mwisho, na watende vitendo ambavyo kwavyo watumai kupata malipo mema kwa Mwenyezi Mungu, na akawakataza kukimbilia kutenda ufisadi katika nchi.
Rudi kwenye Sura

37. Wakamkanusha na wakamuasi. Basi Mwenyezi Mungu akawaangamiza kwa tetemeko kubwa mno lilio wavunjia majumba yao. Wakawa humo wameanguka maiti.
Rudi kwenye Sura

38. Na ewe Mtume! Watajie hawa walio danganyikiwa kw mali zao na madaraka yao vifo vya A'di na Thamudi  pale tulipo waangamiza. Na yapo yamebakia mabaki ya majumba yao yenye kuonyesha utajiri wao. Na sababu ya kuangamizwa huko ni kwa kuwa Shetani aliwazaini, aliwapambia vitendo vyao viovu, nao wakamfuata. Basi akawaachisha Njia ya Haki ambayo walikuwa wakiijua kwa kufunzwa na Mitume.
Rudi kwenye Sura

39. Na ewe Mtume! Watajie hawa walio ghurika kwa mali yao na madaraka yao, kifo cha Qaruni na Firauni na Hamana na yaliyo wapata katika ada ya Mwenyezi Mungu  kuwahiliki wakanushao. Na Mwenyezi Mungu aliwatumia Musa naye akawa na miujiza iliyo wazi ya kuthibitisha ukweli wake. Lakini wao walimkadhibisha, na wakakataa kumuitikia kwa kiburi chao tu. Na wala wao hawakuweza kuishinda kudra ya Mwenyezi Mungu kwa kuikimbia adhabu yake.
Rudi kwenye Sura

40. Kila kaumu katika kaumu zote zilizo wakadhibisha Mitume wao Mwenyezi Mungu ameziangamiza kwa sababu ya kufuru zao walizo zifanya na maasi yao.  Baadhi ya kaumu hizo Mwenyezi Mungu alizihiliki kwa upepo wa kimbunga ulio wapopoa kwa  mawe. Na baadhi yao waliangamia kwa ukelele wenye kuvuma wenye kuhiliki. Na baadhi yao Mwenyezi Mungu aliwadidimiza katika ardhi. Na baadhi yao aliwazamisha majini.  Wala adhabu hizi hazikuwa ni kudhulumiwa na Mwenyezi Mungu, bali sababu yake ni kwa kufuru yao wenyewe na kutenda maasi kwao.
Rudi kwenye Sura

41. Shani ya hao waongo wenye kumfanya urafiki asiye kuwa Mwenyezi Mungu na kumtegemea asiye faa kutegemewa, ni kama shani ya buibui mwenye kuifanya nyumba ya kumlinda, na hali nyumba yake ndiyo nyumba isiyo faa kabisa kutumika kwa ulinzi. Na lau kuwa hawa waongo  ni watu wa ujuzi na utambuzi wasinge fanya hayo.
"Mfano wa walio wafanya walinzi badala ya Mwenyezi Mungu, ni mfano wa buibui alivyo jitandia nyumba. Na hakika nyumba dhaifu mno kuliko zote ni jumba la buibui, laiti kuwa wanajua.":
Nyumba za buibui anazo jenga kwa ajili ya maskani yake na kwa ajili ya kukamatia mateka wake zimeundwa kwa wembamba mno, kwani hizo ni nyuzi zilizo kuwa hadi ya mwisho wa wembamba, zinashinda wembamba wa hariri. Na kwa hivyo mfumo wake umekuwa ni wa mwisho wa udhaifu kuliko nyumba zote walizo jijengea wanyama kuwa ni makaazi yao.
Rudi kwenye Sura

42. Hakika Mwenyezi Mungu, Subhanahu, anajua vyema upotovu wa kuwaabudu hiyo miungu ya uwongo. Na Yeye Subhanahu ndiye Mwenye kushinda kila kitu, Mwenye hikima katika kuendesha na kuweka sharia.
Rudi kwenye Sura

43. Na mazingatio haya na mifano hii, Mwenyezi Mungu anawatajia watu ili wawaidhike na wazingatie. Na hawazingatii haya ila wenye akili ambao wanapima.
Rudi kwenye Sura

44. Mbali na aliyo yataja Mwenyezi Mungu ya visa na mifano na ishara ipo Ishara moja iliyo wazi kabisa, nayo ni uumbaji wa mbingu na ardhi kwa uwezo na hikima, na kipimo kilicho kamilika, kwa maslaha ya watu. Na katika haya zipo dalili za kweli kwa wenye kuiamini Haki.
Rudi kwenye Sura

45. Ewe Nabii! Soma Kitabu cha Mwenyezi Mungu, wala usiwashughulikie. Na timiza Sala kwa inavyo stahiki. Kwani Sala pamoja na ikhlasi, kwa dhati yake humwachisha, mwenye kuishika, madhambi makubwa na kila maovu yanayo katazwa na Sharia. Na bila ya shaka, kumcha Mwenyezi Mungu, na kumhudhurisha kwa kumkumbuka katika Sala na kwengineko kuna athari kubwa zaidi na thawabu nyingi zaidi. Na Mwenyezi Mungu anayajua mnayo yatenda, yakiwa ya kheri au shari. Naye atakulipeni kwayo.
Rudi kwenye Sura

46. Wala msijadiliane na wanao kukhalifuni katika Mayahudi na Wakristo ila kwa njia yenye uwongofu kabisa, na laini kabisa, na inayo pelekea zaidi kukubalika. Isipo kuwa wale walio pita mpaka katika ubishi, basi hao hapana ubaya mkiwakabili kwa mkazo. Na waambieni mnao jadiliana nao: Sisi tumeiamini Qur'ani tulio teremshiwa sisi, na Taurati na Injili mlizo teremshiwa nyinyi. Na tunaye muabudu sisi, na mnaye muabudu nyinyi, ni mmoja. Na sisi tunamnyenyekea Yeye peke yake.
Rudi kwenye Sura

47. Na kama tulivyo wateremshia vitabu Mitume wa kabla yako, tumekuteremshia wewe hii Qur'ani. Basi wale tulio wapa Kitabu (Biblia) kabla ya Qur'ani, na wakaizingatia na wakaifuata, wanaiamini hii Qur'ani. Na miongoni mwa hawa Waarabu (washirikina) wapo wanao iamini. Na hapana wanao zikataa Ishara zetu - baada ya kudhihiri kwake na kuondoka kila shaka juu yake - ila walio shikilia ukafiri.
Rudi kwenye Sura

48. Wala wewe hukuwa ukisoma kitabu chochote kabla ya Qur'ani. Wala hukuwa ukiandika kwa mkono wako wa kulia. Na lau kuwa wewe ni katika ya wanao soma na kuandika wangetilia shaka watu wapotovu kuwa hiyo Qur'ani haitoki kwa Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye Sura

49. Kitabu hichi si cha kutiliwa shaka, bali hizi ni Ishara zilizo wazi zilizo hifadhiwa katika vifua vya watu ambao Mwenyezi Mungu amewapa ilimu. Na hazikatai Ishara zetu, baada ya kuzijua, ila wenye kuidhulumu Haki na wakazidhulumu nafsi zao.
Rudi kwenye Sura

50. Na makafiri katika majadiliano yao na ukaidi wao walisema: Mbona hakuteremshiwa miujiza ya kuiona kwa macho kama iliyo wateremkia Mitume wa kabla yake?  Waambie: Miujiza yote iko kwa Mwenyezi Mungu. Huiteremsha anapo taka.  Ama mimi nimetumwa kuonya kwa uwazi, sio kuleta hayo mtakayo.
Rudi kwenye Sura

51. Wanataka Ishara  hizo,  nao haiwatoshi wao kuwa Sisi tumekuteremshia hichi Kitabu wanacho somewa? Na huu ndio Muujiza wa kudumu milele na zingapita zama. Hakika kwa kuteremka Kitabu hichi juu yako bila ya shaka ni rehema kwao na kwa vizazi vyote vijavyo baada yao, na ni kumbusho la daima dawamu lenye manufaa kwa watu ambao shani yao ni kuamini wanapo onyeshwa wazi Njia ya Uwongofu.
Rudi kwenye Sura

52. Sema: Yanitosha mimi na yakutosheni nyinyi ya kwamba Mwenyezi Mungu ndiye Shahidi kuwa  mimi nimefikisha niliyo tumwa kwenu. Na hayo ndiyo chanzo cha mambo yangu na mambo yenu. Wala hakifichiki kwake chochote cha mbinguni na duniani. Na walio muabudu asiye kuwa Mwenyezi Mungu, na wakamkataa Mwenyezi Mungu na wasimkhusishe Yeye tu kwa ibada, hao ndio walio nunua ukafiri kwa Imani, na wakasibiwa na khasara iliyo wazi.
Rudi kwenye Sura

53. Na makafiri wanakufanyia ushindani ya kuwa kama unaweza basi waletee kwa haraka hiyo adhabu ulio waonya kuwa itawapata.  Na lau kuwa wakati maalumu haukuwekwa kwa mujibu wa hikima yetu, tungeli waletea kwa haraka hiyo adhabu wanayo ihimiza. Ninaapa itawatokea kwa ghafla, na hali wao hawana khabari.
Rudi kwenye Sura

54. Wanakutaka waletewe upesi adhabu, nayo itawajia tu, hapana hivi wala hivi. Na hakika, Jahannamu imewazunguka makafiri kwa yakini.
Rudi kwenye Sura

55. Siku itapo wafunika adhabu kutoka juu, licha ya kutoka chini, na Malaika aliye wakilishwa kuwaadhibu atapo sema: Onjeni jazaa ya hayo maovu mliyo kuwa mkiyatenda!
Rudi kwenye Sura

56. (Mwenyezi Mungu anasema:) Enyi waja wangu mlio niamini Mimi na Mtume wangu! Hakika ardhi yangu ni kunjufu kwa atakaye kukimbia kutoka katika nchi za shirki. Kimbieni mje kwangu mpate kunisafia Mimi ibada.
Rudi kwenye Sura

57. Kila nafsi itaonja uchungu wa mauti bila ya shaka yoyote. Kisha mtarejea kwetu, na mtakuja lipwa kwa hayo mliyo yatanguliza, ikiwa ya kheri au ya shari.
Rudi kwenye Sura

58,59. Na walio muamini Mwenyezi Mungu na Vitabu vyake na Mitume wake, na wakatenda vitendo vyema, tunaapa kwamba bila ya shaka tutawaweka katika makaazi ya starehe kwenye maghorofa yapitayo mito chini yake. Neema zake haziwakatikii. Ni nzuri mno jazaa hii kuwa ni ujira wa wenye kutenda, wenye kusubiri kwa yanayo wapata kwa ajili ya Mwenyezi Mungu wanapo acha nchi zao na watu wao na mali yao, nao wakimtegemea Mwenyezi Mungu peke yake katika hali zao zote.
Rudi kwenye Sura

60. Na wanyama wengi wanao ishi nanyi katika ardhi ambao, kwa unyonge wao, hawawezi kubeba riziki yao na wakaihamisha kwa ajili ya kuila au kuiweka akiba. Ni Mwenyezi Mungu ndiye ambaye anawatengezea sababu za kuwaruzku na kuwaweka hai. Na Yeye anakutengenezeeni nyinyi sababu za riziki zenu na maisha yenu. Na Yeye ni Mwenye kumiliki kila alicho kiumba kwa kusikia na kukijua.
Rudi kwenye Sura

61. Na ninaapa ukiwauliza washirikina: Nani aliye ziumba mbingu na ardhi, na akalit'iisha jua na mwezi, na akayafanya hayo yawanufaishe watu? Hapana shaka watasema: Kaviumba hivyo Mwenyezi Mungu. Wala hawamtaji mwenginewe. Basi inakuwaje wanaacha kumuamini Mwenyezi Mungu Mmoja Mtukufu, baada ya kukiri kwao huku?
Rudi kwenye Sura

62. Mwenyezi Mungu humkunjulia riziki amtakaye, na humdhikishia amtakaye, kwa mujibu wa inavyo wafikiana na ujuzi wake kwa ajili ya maslaha. Kwani hakika Mwenyezi Mungu amevizunguka vitu vyote kwa ujuzi wake.
Rudi kwenye Sura

63. Ninaapa, lau kuwa utawauliza: Nani anaye teremsha maji kutoka mbinguni, na akaihuisha ardhi kwa mimea baada ya kuwa na ukame? Hapana shaka watasema: Ni Mwenyezi Mungu. Sema: Alhamdu Lillahi, kuwa  wanaikubali Haki. Lakini wengi wao hawafahamu kuwa wenyewe wanajitia katika migongano ya maneno.
Rudi kwenye Sura

64. Na haya maisha ya duniani si chochote ila ni starehe ya muda wenye ukomo. Wanapumbazika walio ghafilika kama wanavyo pumbazika watoto wadogo, na wanacheza kwa muda fulani na kisha wanatawanyika. Na hakika makaazi ya Akhera ndio makaazi ya maisha ya kweli, yaliyo kamilika, yenye kudumu. Na kweli hizi ni zenye kuthibiti, wangeli zitambua hawa lau kuwa ni watu wa kutambua vilivyo.
Rudi kwenye Sura

65. Hao kwa walivyo sifika kwa ushirikina, wakipanda vyombo vya baharini, na wakapata kidogo katika vitisho vyake, humuelekea Mwenyezi Mungu kwa kumwomba kwa ikhlasi ili awaondolee madhara. Na akisha waokoa akawafikisha nchi kavu mara hukimbilia kurejea kwenye ushirikina.
Rudi kwenye Sura

66. Ili wapate kuzikanya neema tulizo wapa, na wapate kunafiika kwa yale yanayo ridhiana na pumbao lao katika maisha haya. Basi watakuja yajua matokeo  ya ukafiri pale watapo iona adhabu iliyo chungu.
Rudi kwenye Sura

67. Makafiri wa Makka wameingia upofu, hawazioni neema za Mwenyezi Mungu alizo wamiminia, wala hawaoni kwamba hakika Sisi tumeufanya mji wao kuwa umehifadhika, haushambuliwi wala hauvamiwi, mtakatifu; watu wake hawatekwi nyara, wala ndani yake havitokei vita. Na hali kote jirani zao watu wananyakuliwa! Hawa wamepofuka hawazioni neema hizi, basi wanasadiki yasiyo na asli yoyote, na wanamkanusha Muhammad na yote aliyo yaleta!
Rudi kwenye Sura

68. Na hapana aliye dhulumu zaidi kuliko yule anaye msingizia Mwenyezi Mungu jambo ambalo hakulitolea sharia, au akaikadhibisha Dini ya Haki inapo mfikilia. Hakika katika Jahannam ndiko kwenye makaazi ya watu hawa madhaalimu, makafiri.
Rudi kwenye Sura

69. Na wale walio fanya ukomo wa juhudi zao, na wakastahamili mashaka kwa sababu ya kuinusuru Dini yetu, hapana shaka tutawazidishia kuwaongoa kuendea kheri na Haki. Na hakika Mwenyezi Mungu bila ya shaka yu pamoja na wale wanao fanya vizuri vitendo vyao; atawasaidia na atawanusuru. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi kuliko wote.
Rudi kwenye Sura