Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

93. SURAT WADH-DHUH'AA

(Imeteremka Makka)

Sura hii imeanza kwa viapo viwili vyenye kueleza nyakati mbili za uchangamfu na za kutulia, ya kwamba kwa hakika Mwenyezi Mungu hakumwacha Mtume wake wala hakumchukia, na kwamba aliyo mtengenezea katika Akhera makao ya juu ni bora zaidi kuliko alio mkirimu duniani. Kisha Subhanahu akaapa kwamba Yeye atampa mpaka aridhike, na yaliyo tangulia ni ushahidi wa yatakayo kuja. Kwani alikuwa yatima, akampatia makaazi; alikuwa amepotea akampa bora ya uwongofu, na alikuwa fakiri akamtajirisha. Kisha Aya zikataka aangaliwe vyema yatima, na asikemewe mwenye kuomba au kuuliza,  na zisimuliwe neema za Mwenyezi Mungu.

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Naapa kwa mchana! *

2. Na kwa usiku unapo tanda! *

3. Mola wako Mlezi hakukuacha, wala hakukasirika nawe. *

4. Na bila ya shaka wakati ujao utakuwa bora kwako kuliko ulio tangulia. *

5. Na Mola wako Mlezi atakupa mpaka uridhike. *

6. Kwani hakukukuta yatima akakupa makaazi? *

7. Na akakukuta umepotea akakuongoa? *

8. Akakukuta mhitaji akakutosheleza? *

9. Basi yatima usimwonee! *

10. Na anaye omba au kuuliza usimkaripie! *

11. Na neema za Mola wako Mlezi zisimlie.  *  


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright © 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani