Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

88. SURAT AL-GHAASHIYAH

(Imeteremka Makka)

Imeanza Sura hii kwa njia ya kutia shauku kuisikiliza hadithi ya Siku ya Kiyama, na hayo mambo yatakayo tokea humo. Inaashiria kwamba watu ni makundi mawili: miongoni mwao wapo ambao hawatapata hishima yoyote kwa watakavyo pokewa na wataingia kwenye Moto mkali. Na wapo watakao ifikia siku hiyo kwa furaha kwa namna ya rehema na radhi zilizo andaliwa kwa ajili yao. Kisha Sura ikaeleza dalili zilizo wazi za uweza wa Mwenyezi Mungu Mtukufu kufufua kutokana na wanavyo ona wenyewe kwa macho yao na wanayo nafiika kwayo katika uhai wao. Na baada ya kuzitaja dalili hizi ikageukia khabari za Mtume s.a.w. kwa kukumbusha kwamba waajibu wake mkubwa kwa mintarafu yao ni wazi, ya kwamba yeye hakutawalishwa juu yao awalazimishe kuamini, na kwamba mwenye kugeuka na akakufuru baada ya waadhi huu ni Mwenyezi Mungu ndiye atakaye mshika kwa dhambi zake, na atamuadhibu kwa adhabu kubwa kabisa, atapo rejea kwake baada ya kufa, kwani marejeo ya wote na kuhisabiwa kwao wote ni kwake Yeye Mwenyezi Mungu.

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Je! Imekufikia khabari ya msiba wa kufudikiza? *

2. Siku hiyo nyuso zitainama, *

3. Zikifanya kazi, nazo taabani. *

4. Ziingie katika Moto unao waka - *

5. Zikinyweshwa kutoka chemchem inayo chemka. *

6. Hawatakuwa na chakula isipo kuwa kichungu chenye miba. *

7. Hakinenepeshi wala hakiondoi njaa. *

8. Siku hiyo nyuso nyengine zitakuwa kunjufu. *

9. Zitakuwa radhi kwa juhudi yao, *

10. Katika Bustani ya juu. *

11. Hawatasikia humo upuuzi. *

12. Humo imo chemchem inayo miminika. *

13. Humo vimo viti vilivyo nyanyuliwa, *

14. Na bilauri zilizo pangwa, *

15. Na matakia safu safu, *

16. Na mazulia yaliyo tandikwa. *

17. Je! Hawamtazami ngamia jinsi alivyo umbwa? *

18. Na mbingu jinsi ilivyo inuliwa? *

19. Na milima jinsi ilivyo thibitishwa? *

20. Na ardhi jinsi ilivyo tandazwa? *

21. Basi kumbusha! Hakika wewe ni Mkumbushaji. *

22. Wewe si mwenye kuwatawalia. *

23. Lakini anaye rudi nyuma na kukataa, *

24. Basi Mwenyezi Mungu atamuadhibu kwa adhabu iliyo kubwa kabisa! *

25. Hakika ni kwetu Sisi ndio marejeo yao. *

26. Kisha hakika ni juu yetu Sisi hisabu yao!  *  


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright © 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani