Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

87. SURAT AL- AA'LAA

(Imeteremka Makka)

Sura hii imeanza kwa kumtakasa huyo aliye umba vitu vyote, na akavifanya vyote sawa kwa kuvishughulikia, na akakadiria kila kitu kwa kinavyo silihi, basi akakiongoza kifikilie hivyo. Na akaotesha malisho ya wanyama, na khalafu akayafanya makavu yaliyo ingia weusi. Kisha Aya zikatoa khabari kwamba Mwenyezi Mungu atamsomesha Mtume wake Qur'ani, naye ataihifadhi, wala hatosahau chochote katika hivyo ila apende Mwenyezi Mungu. Na atamsahilishia kwa wepesi. Kisha Sura inamuamrisha Mtume akumbushe kwa Qur'ani apate kukumbuka mwenye kuogopa, na ajitenge na ukumbusho huyo mwovu atakaye ingia kwenye Moto mkubwa. Na Aya zimetilia mkazo kwamba uwokovu ni wa mwenye kujisafisha, na akalikumbuka jina la Mola wake Mlezi, na akasali. Na Sura imekhitimisha kwa kubaini kwamba yaliyo kuja humu yamethibiti katika Vitabu vya zamani, Vitabu vya Ibrahimu na Musa.

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Litakase jina la Mola wako Mlezi aliye juu kabisa, *

2. Aliye umba, na akaweka sawa, *

3. Na ambaye amekadiria na akaongoa, *

4. Na aliye otesha malisho, *

5. Kisha akayafanya makavu, meusi. *

6. Tutakusomesha wala hutasahau, *

7. Ila akipenda Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye anayajua yaliyo dhaahiri na yaliyo fichikana. *

8. Na tutakusahilishia yawe mepesi. *

9. Basi kumbusha, kama kukumbusha kunafaa. *

10. Atakumbuka mwenye kuogopa. *

11. Na atajitenga mbali nayo mpotovu, *

12. Ambaye atauingia Moto mkubwa. *

13. Tena humo hatakufa wala hawi hai. *

14. Hakika amekwisha fanikiwa aliye jitakasa. *

15. Na akakumbuka jina la Mola wake Mlezi, na akasali. *

16. Lakini nyinyi mnakhiari maisha ya dunia! *

17. Na Akhera ni bora na yenye kudumu zaidi. *

18. Hakika haya yamo katika Vitabu vya mwanzo, *

19. Vitabu vya Ibrahimu na Musa.  *  


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright © 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani