Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

84. SURAT AL-INSHIQAAQ

(Imeteremka Makka)

Sura hii imetaja baadhi ya ishara za Saa ya Kiyama, na kunyenyekea ardhi na mbingu kufuata atakavyo Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na imefahamisha kwamba mtu anachungwa ende akakutane na Mola wake Mlezi, na kwamba vitendo vyake vimeandikwa katika daftari atakalo kuja likuta. Basi mwenye kulipokea kwa mkono wake wa kulia, hisabu yake itakuwa nyepesi. Na mwenye kulipokea kwa mkono wa kushoto atayayatika kuipata adhabu na kuingia Motoni. Tena Mwenyezi Mungu Subhanahu ameapa kwa Ishara ambazo zinashuhudia uweza wake, na ambazo zinaitia imani ya kufufuliwa. Lakini juu ya hayo walio kufuru hawaamini, wala hawaizingatii Qur'ani, wala hawazifuati hukumu zake. Kisha Sura inakhitimisha kwa kuonya kwamba Mwenyezi Mungu anayajua wanayo dhamiria, na kwamba Yeye amekwisha waandalia adhabu iliyo chungu, kama alivyo waandalia Waumini ujira wa daima usio katika.

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1.Itapo chanika mbingu, *

2. Na ikamsikiliza Mola wake Mlezi, na ikapasiwa kumsikiliza, *

3. Na ardhi itakapo tanuliwa, *

4. Na kuvitoa vilivyo kuwa ndani yake, ikawa tupu, *

5. Na ikamsikiliza Mola wake Mlezi, na ikapasiwa kumsikiliza, *

6. Ewe mtu! Hakika wewe unajikusuru kwa juhudi kumwendea Mola wako Mlezi, basi utamkuta. *

7. Ama atakaye pewa daftari lake kwa mkono wa kulia, *

8. Basi huyo atahisabiwa hisabu nyepesi, *

9. Na arudi kwa ahali zake na furaha. *

10. Na ama atakaye pewa daftari lake kwa nyuma ya mgongo wake, *

11. Basi huyo ataomba kuteketea. *

12. Na ataingia Motoni. *

13. Hakika alikuwa furahani kati ya jamaa zake. *

14. Huyo hakika alidhani kuwa hatarejea tena. *

15. Kwani? Hakika Mola wake Mlezi alikuwa akimwona! *

16. Basi ninaapa kwa wekundu wa jua linapo kuchwa, *

17. Na kwa usiku na unavyo vikusanya, *

18. Na kwa mwezi unapo pevuka, *

19. Lazima mtapanda t'abaka kwa t'abaka! *

20. Basi wana nini hawaamini? *

21. Na wanapo somewa Qur'ani hawasujudu? *

22. Bali walio kufuru wanakanusha tu. *

23. Na Mwenyezi Mungu anajua wanayo yadhamiria. *

24. Basi wabashirie adhabu chungu! *

25. Isipo kuwa wale walio amini na wakatenda mema; hao watakuwa na ujira usio malizika.  *  


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright © 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani